Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha Megaliving -By Robin Sharma
Habari msomaji wa jukwaa la jiongeze ufahamu, Ni matumaini yangu unaendelea vizuri katika safari hii ya mafanikio. Katika safari ya mafanikio kujifunza kila wakati ndio njia ya uhakika ya kukufikisha kwenye mafanikio, na ndio lengo la Jiongeze Ufahamu. Katika kuhakikisha kwamba tunajiongeza ufahamu kwelikweli kila wiki tutakua tunashirikishana kwa ufupi mambo 20 niliyojifunza kutoka kwenye kitabu kimoja kati ya 2 ninavyosoma. Wiki hii tutaanza na kujifunza kutoka kwenye kitabu kizuri sana cha Megaliving kilichoandikwa na mwandishi mashuhuri duniani Robin Sharma.
Karibu sana:
1. Mafanikio ya nje yanaazia na mafaniko ya ndani.
2. Kama unataka kuongoza kampuni lazima ujifunze kujiongoza wewe kwanza.
3. Watu wengi ni wafungwa wa maisha yao ya nyuma. Lazima tufike mahali tuachane na kua wafungwa wa maisha yaliyopita ili kuanza maisha mapya mazuri
4. Mawazo yangu ya leo ndio yatakayotengeneza ndoto zangu za kesho.
5. Kitu cha kwanza kuepukana na utumwa wa mawazo, ni uelewa. Kwanza anza kwa kutambua mawazo ambayo yamekua yakikurudisha nyuma. Tafuta karatasi yaandike mambo hayo. Halafu weka mikakati ambayo utaitumia kuondokana na mawazo hayo.
6. Orodha ya ndoto. Andika chini orodha ya ndoto ambazo unatamani zitimie maishani mwako
7. Tumezungukwa na utajiri mwingi tu, na wanaoweza kuupata ni wale tu wanaotambua hilo na kua na fikra chanya ambazo zinawasaidia kuona fursa mbalimbali zinazowapelekea kuupata utajiri huo
8. Usijilinganishe na wengine. Kimbia mbio zako mwenyewe
9. Kinachowatenganisha waliofanikiwa na wasiofanikiwa ni hiki; Waliofanikiwa wanayo njaa au kiu kubwa sana ya kupata wazo jipya na maarifa mapya, wakati wasiofanikiwa wanabweteka na hali walio nayo, hawana kiu ya kujifunza vipya.
10. Wasomaji ni viongozi, utakua kiongozi mkubwa pale tu utakapojijengea tabia ya kujiendeleza wewe binafsi kwa kusoma vitabu vizuri kwenye Nyanja husika.
11. Huwezi kuwa mtu mkubwa katika Nyanja yeyote mpaka umeanza kuhisi kua wewe ni mkubwa
12. Washindi ni watu wenye nidhamu ya hali ya juu
13. Watu wenye mawazo chanya ndio wanao ongoza kila sehemu, kama baishara, uongozi, familia, elimu n.k. Hii ina maana kama una mawazo hasi hutaweza kushindana na mwenye mawazo chanya…
14. Washindi hua wanatengeneza mikakati ya kunufaika kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo, wanahakikisha wanashinda kwa gharama yeyote. Washindi lazima wapate njia tu.
15. Hakuna kitu kinachoweza kumzuia mtu aliyekataa kuzuiliwa.
SOMA; Fursa katika Kilimo cha Bustani
16. Hakuna kinachoweza kumzuia mtu mwenye mtazamo sahihi wa kiakili asiweze kufikia malengo yake, lakini pia hakuna kitu chochote hapa duniani kinachoweza kumsaidia mtu mwenye mtazamo hasi.
17. Malengo ni msingi wa muhimu sana katika maisha. Kama huna malengo huwezi kujua unakokwenda, yaani utaenda kila mahali maana hujui unakotaka kwenda hasa.
18. Kusudi la Maisha ni Maisha yenye kusudi.
19. Vikwazo vinavyokuzuia wewe kupata vile amabavyo ungeweza kuvipata ni vile ulivyojiwekea mwenyewe kwenye mawazo yako.
20. Hata ukimuomba Mungu ufanikiwe kama huta chukua hatua sahau kuhusu kufanikiwa. Wengi wanafikiri wakimuomba Mungu awafanikishe ni kwamba atawateremshia mafanikio toka mbinguni na wao wakiwa wamekaa hapohapo walipo. Kwanza Jua ni nini unataka kisha Muombe Mungu sawa kabisa, lakini chukua hatua zinazostahili.
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana nae kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au email daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
4/15/2015 01:00:00 PM | | 0 Comments
Siri Za Kuwa Mjasiriamali Bora Na Kufikia Mafanikio Makubwa.
Wajasiriamali wengi wamekuwa wakijishughulisha shughuli za uzalishaji kama kutoa huduma au kuuza bidhaa na lengo likiwa kupata mafanikio. Katika kufikia mafanikio makubwa wachache wameweza na wengi wao kutofikia au kukua kwa taratibu. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa katika ujasiriamali kuna vitu ambavyo unatakiwa kuvifahamu na kuthubutu kuvifanya ili kupata mafanikio makubwa. Mambo ambayo yana tija kubwa ni mambo madogo madogo ila yana mchango mkubwa sana katika kufikia mafanikio makubwa.
Hizi ndio siri za mjasiriamali bora ambazo zitapelekea kufikia mafanikio makubwa
Kupenda kitu ambacho unakifanya
Kama unatoa huduma au kuuza bidhaa ni muhimu kuipenda na kuithamini huduma ambayo unaitoa ili uweze kuifanya kwa ubora na kukidhi mahitaji ya wateja wako. Ukipenda kitu ambacho unafanya ni rahisi kukifanya bila kuchoka hata kama unakutana na changamoto kwa kiasi gani. Ukipenda huduma unayoitoa utawapenda wateja wako na kuweza kutoa huduma bora.
SOMA; Wajasiriamali Wenye Mafanikio Hufanya Mambo Haya Matano Kila Siku.
Kuwa mvumilivu na kutokata tamaa
Hakuna jambo ambalo unaweza kulifanya kwa urahisi katika dunia ya leo ambayo imejaa changamoto nyingi na kukatishwa tamaa. Ukiwa mjasiriamali unatakiwa kuwa mvumilivu hasa pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo yako. Ukiwa katika ujasiriamali kuna kipindi unakutana changamoto nyingi ambazo usipokuwa makini unaweza kata tamaa ila changamoto hizi zinapima uwezo wako wa ustahimilivu na kupambana na changamoto. Ukiwa umefanikiwa kutatua changamoto hiyo ndivyo ambavyo utapiga hatua na kufikia mafanikio makubwa.
Kuwa na nidhamu ya pesa
Kama unahitaji kuwa mjasiriamali ambaye anakua kila siku nidhamu ya pesa ni muhimu sana katika msingi wa kukuza biashara yako. Matumizi yako yasizidi au yasiathiri ukuaji wa biashara yako. Ili uweze kukuza biashara yako ukawa na matumizi ya kiasi ambayo yatakuwa rafiki wa ukuaji wa biashara yako. Ili uweze kujua kama biashara yako inakua ni vizuri ukawa na kumbukumbu ya biashara yako kuhusu matumizi na mapato.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Kuanza kufanya biashara hata kwa mtaji mdogo
Watu wengi hasa wenye elimu hupenda kuanza kufanya biashara kwa mtaji mkubwa na kuona tatizo kubwa ambalo linafanya washindwe kujiajiri na kwa kutokuwa na mtaji wa kutosha. Kuna faida kubwa ya kuanza kuifanya biashara kwa mtaji mdogo huku ukiendelea kukua kwa taratibu faida hizo ni a) Unapata uwezo kusimamia biashara kwa madaraja yaani kuanzia chini b) Unapata uwezo wa kuzisimamia pesa c) Unapata uwezo mkubwa wa kupambana na changamoto
Kufanya kazi kwa Bidii na Ubunifu
Hakuna kitu ambacho unaweza fikia mafanikio makubwa kama hautofanya kazi kwa bidii. Unaweza kuwa na mtaji mkubwa kama hufanyi kazi kwa bidii na kwa ubunifu ni kazi bure. Mafanikio makubwa yanahitaji kujitoa na kufanya kazi kuliko ambavyo ulikuwa unafanya kazi mwanzo na ikiwezekana fanya kazi zaidi ya masaa ambayo ulikuwa unafanya mwanzo.
Huduma au bidhaa yako ilenge kuisaidia jamii
Ukitoa huduma ambayo itasaidia kutatua matatizo ya jamii husika ni rahisi kwako kuweza kuliteka soko na kuuza bidhaa yako au huduma katika kiwango cha juu. Kama huduma yako itatua tatizo katika jamii ni rahisi kupata wateja wengi na wewe mjasiriamali kuweza kufikia mafanikio makubwa. Biashara nyingi ambazo zimelenga kutatua matatizo ya jamii zinafanya vizuri katika soko na kuwa na ushindani mdogo kuliko bishara za kuiga toka kwa wengine.
SOMA; Huyu Ni Mjasiriamali Mwenye Hamasa Kubwa sana. Unaweza kujifunza kila kitu kutoka kwake.
Jifunze kila siku
Mjasiriamali unatakiwa kujifunza kuhusu biashara mpya au kujifunza zaidi kuhusu biashara ambayo unaifanya ili uweze kuwa bora zaidi na kuifanya kwa ubora. Katika kujifunza jifunze kwa vitu ambavyo vinalenga kuiboresha biashara yako ili uweze kupata mbinu mpya na kuwa bora zaidi. Kujifunza huku kutakufanya kufanya vitu kwa ubora na kuwa tofauti katika kutoa huduma na kuifanya biashara yako kuwa bora na kuvutia wateja wengi zaidi.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422. http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/15/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO, UJASIRIAMALI | 0 Comments
Hizi Ndizo Sifa Saba Za Kiongozi Bora.
Kila mtu ni kiongozi toka alivyozaliwa, yaani ni kipaji ambacho kila mtu huzaliwa nacho. Kila mtu ana uwezo wa kuwa kiongozi. Kila sehemu katika dunia hii huhitaji kiongozi, labda nikuulize swali, umewahi kuwa kiongozi? Jibu laweza kuwa ndiyo au hapana. Lakini hilo baki nalo kwa sasa. Niseme kwamba kama ukishindwa kuwa kiongozi wa watu wengi, utakuwa kiongozi wa familia yako kama baba au mama. Na kama hata hilo likikushinda basi wewe ni kiongozi wa maisha yako. Kuwa kiongozi wa maisha yako mwenyewe na usiruhusu mtu kuwa kiongozi na mwamuzi wa maisha yako. Kuwa bora au usiwe bora ni juu yako mwenyewe kuamua. Ukitaka kufanya chochote lazima ujifunze kuwa kiongozi bora kwani tayari umezaliwa kiongozi. Hizi ndizo sifa za kiongozi bora wa watu.
SOMA; Mahitaji Manne Ya Mtu Kuwa Kiongozi.
1. Kiongozi lazima awe na maono
Kiongozi ni lazima awe na maono ambayo ni tofauti wengine. Lazima awe na uwezo wa kuona vitu ambavyo watu wengine hawana uwezo kuviona. Ujue pia kuwa kiongozi alishawahi kuongozwa na akawa tofauti na watu wengine kwa kuona ambayo wao wameshindwa kuona.
2. Kiongozi huhitaji heshima
Kiongozi huhitaji heshima kutoka kwa watu wake na hata wa nje. Kiongozi lazima ajiheshimu ili aweze kuheshimiwa. Usilazimishe kuheshimiwa bali tengeneza mazingira ya kuheshimiwa.
SOMA; Nguzo Kuu Ya Uongozi; Tekeleza Kile Unachoahidi.
3. Kiongozi huona picha kubwa
Kiongozi lazima awe na uwezo wa kuona vitu vikubwa, maoni makubwa yaani picha kubwa. Kuna viongozi mfano wa Mwl. Nyerere, Mandela, Martin Luther King jr, Lincoln na wengineo, ni mfano wa viongozi waliokuwa na picha kubwa.
4. Kiongozi hujua ni wakati gani wa kubadili mwelekeo
Kuna wakati kiongozi hulazimika kubadili mwelekeo wa nguvu zake ama sera zake. Kama kiongozi bora kuwa na uwezo huo kutakusaidia sana katika kufanya maamuzi. Ni wakati gani wa kutumia nguvu kubwa, wakati gani utumie nguvu ndogo, wakati gani uache ama wakati gani wa kubadili mwenendo.
5. Kiongozi huweza kuona matatizo yalipo na kutafuta majibu
Kiongozi huweza kuona maeneo yenye matatizo na kuweza kutafuta suluhisho. Kujua tatizo lililopo sehemu ni nusu ya kulitatua. Ni dhahiri kuwa hutaweza kutatua tatizo usilolijua.
SOMA; Viongozi 100 Walioibadili Dunia.
6. Kiongozi lazima ajiamini na kuwa na mtazamo chanya
Kujiamini ni sifa kubwa katika kufanya mambo mengi. Ili uweze kujiamini ni lazima pia uwe na mtazamo chanya. Bila kujiamini na kuwa na mtazamo chanya na wenye kujenga sahau kuwa kiongozi mkubwa na bora. Kuwa na mtazamo chanya na mwenye kujiamini ili uweze kuaminiwa na wale unaowaongoza kwani hakuna mtu anayekubali kuongozwa na mtu asiyejiamini mwenyewe.
7. Kiongozi ni mwajibikaji
Kiongozi bora lazima aweze kuwajibika. Kuwajibika katika kutenda kazi na kusaidia watu. Pia kuwa tayari kung’atuka pale itakapoonekana kuwa umeshindwa kutekeleza matakwa ya watu wako. Kumbuka kuwajibika kwa nafasi yako kama kiongozi hata kama kosa hujalitenda kwako kwani hii itakuongezea sifa na heshima kwa watu wako. Usiwe king’ang’anizi wa madaraka pale utakapoona muda wako umeisha au hutakiwi na wale unaowaongoza.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes ambae ni mjasirimali na mhamasishaji.
Unaweza kuwasiliana na naye kwa : simu: 0712 843030/0753 843030
e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blogu yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.
SOMA; Tabia Tatu Za Viongozi Dhaifu, Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
4/14/2015 07:30:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Sababu Zinazokufanya Wewe Kushindwa Kuthubutu Wazo Lako
Watu wengi wamekuwa na mawazo mazuri sana ya kuthubutu ndoto zao, licha ya kuwa na mawazo mazuri sana ambayo yangeweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu ya leo kuna changamoto au sababu zinazowafanya washindwe kuthubutu ndoto zao. Nazo ni;
1. Woga / Hofu,
Woga au hofu siku zote huja pale mtu anaposhindwa kujiamini kuwa anaweza kufanya jambo fulani katika jamii husika . Hii ni sababu inayowafanya watu wengi kufa na mawazo yao mazuri ,kushindwa kuthubutu wazo zuri alilokuwa nalo pia kushindwa kuwa mbunifu katika kazi, biashara na hali kadhalika woga unamfanya mtu kuendelea kuwa mtumwa wa jambo fulani, kwa nini nasema kuwa mtumwa? Kufanya kitu chochote ambacho hukipendi ni utumwa hivyo basi ukitaka kuwa na mafanikio fanya kile unachopenda. Woga ni mbaya hatupaswi kuupa shukrani
SOMA; Ukweli Kuhusu Maisha Ambao Kila Mtu Anapaswa Kuujua.
2. Kutoamua kufanya Jambo hilo kwa Hamasa na Wakati
Ukishakuwa na wazo la kufanya jambo chanya ambalo litakuletea mabadiliko katika maisha yako anza hapo hapo ulipo usisubiri mpaka hamasa iliyokuwa ndani yako ya kufanya jambo hilo lipotee kabisa, ikishapotea hamasa basi na wazo lako litakufa kwa kushindwa kuthubutu kwa wakati. Usipoteze wakati au muda kwani muda ndiyo rasilimali tuliyopewa sawa sio kwa masikini au tajiri wote tuna muda sawa hakuna upendeleo katika hili.
3. Kuahirisha Mambo (procrastination)
Wengi wanashindwa kufanya mabadiliko katika maisha yao, wanashindwa kuthubutu mawazo yao kila siku kwa sababu ya kuahirisha mambo, tabia hii ya kusema nitafanya badaye ndio inakufanya wewe ushindwe kutimiza ndoto yako kwa wakati.
Mtunzi wa kitabu cha procrastination –Timothy anasema ‘’ ukitaka kufanya jambo Fulani anza kulifanya ‘’ Just start’’. Hivyo basi ili kuondokana na hali ya kuahirisha mambo kila siku anza kulifanya jambo hilo usisubiri itakusaidia kuthubutu ndoto yako .
Mpenzi msomaji wa makala hii ili uweze kufanikiwa na kuthubutu mawazo yako mazuri ambayo ulikuwa nayo au unayo kwa muda mrefu huu ndio muda wa kuthubutu kwa vitendo.
SOMA; Mara Zote Sema Ukweli, Ni Rahisi Kukumbuka.
4. Kuomba Ushauri kwa Watu Walioshindwa
Ukitaka kufanikiwa, kuthubutu mawazo ambayo unayo usiombe ushauri kwa mtu aliyeshindwa kwa sababu atakukatisha tamaa, omba ushauri kwa yule aliyefanikiwa ambaye alikuwa na mawazo mazuri kama uliyonayo wewe akaweza kuthubutu hatimaye kufanikiwa.
5. Kutojifunza kwa Bidii
Mafanikio yoyote yanatokana na kujifunza kwa bidii, kama wazo ni kuhusu biashara fulani jifunze sana kuhusiana na hiyo biashara, utakuwa bora na utaweza kutimiza ndoto yako.
Mtunzi wa kitabu cha The Entrepreneur Mind –Kevin D.Johnson anasema, ili uweze kuwa mjasiriamali bora jifunze sana katika kile unachofanya tumia mbinu ya ‘’Ignorance can be bliss’’ Ujinga utakufanya kuwa na furaha kama ukijifunza.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi,mhamasishaji na majasiriamali unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au barua pepe (Email) deokessy.dk@gmail.com.au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com
SOMA; Usiweke Maanani Unachoambiwa Na Mtu Aliye Kwenye Hali Hizi Tatu.
4/13/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO | 0 Comments
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo Na Kukosa Muda Katika Ulimwengu Huu Wa Utandawazi.
Majukumu mengi sana yameongezeka sasa ukilinganisha na zamani. Kuna wakati watu tunahisi kama masaa yamekuwa yakienda haraka kupita zamani. Usiku ni mfupi na mchana ni mfupi pia. Ukiamka saa mbili basi ujue saa kumi na mbili jioni ipo karibu, saa kumi na mbili ikifika haujakaa vizuri saa nne usiku tayari unahitaji kulala na kesho uamke asubuhi mapema ili uendelee na mikiki mikiki ya maisha. Ukweli ni kwamba masaa ni 24 kama zamani na hakuna hata saa moja iliyopunguzwa na Mungu. Majukumu yamekuwa mengi, kumekua na maendeleo ya kiteknolojia na hivyo ndivyo vinavyofanya siku ,wiki, mwezi hata mwaka kuonekana mfupi na kujikuta hatujatimiza majukumu yetu kama tunavyotarajia.
SOMA; Siri Itakayokuwezesha Kufanya Chochote.
Hebu tupitie ratiba za wengi wetu katika ulimwengu huu wa sasa wa utandawazi,unaamka asubuhi kitu cha kwanza ni kuchukua simu yako ya kisasa (smartphone) na kuangalia ujumbe mfupi whatssap, baadaye telegram, ukimaliza, twitter baadaye kidogo unaingia facebookuonewaliowekapicha na habari mpya. Wakati huo umewasha TV yako ukisikiliza ni jambo lipi jipya limejiri. Bado hujaenda youtube kutafuta video, nyimbo mpya. Hivi kwa mtindo huu siku si itaisha hata hujakumbuka kusali wala kuangalia majukumu yako kijamii na kifamilia? Kwa namna hii ndoto zako utaishia kuota tuu au kupanga mipango bila kuwa na utekelezaji.
SOMA; Hiki Ndio Kitu Muhimu Sana Kwenye Maisha Yako. Na Sio Chakula Au Hewa.
Umeshajiandaa na unataka kufanya jambo la maana unasikia mlio mtu katuma ujumbefacebookunajifariji naangalia hii ya mwisho, unaona habari LULU atoa mpya. Unaingia mtandaoni kuona ni mpya ipi. Katika kuchunguza unaona ni kitu cha kawaida tuu, wakati unafikiri kuendelea na shughuli zako unaona habari nyingine Diamond kapata kashfa (scandal) unajifariji uchungulie dakika moja lakini haiwi hivyo. Unaenda nyingine hadi nyingine mpaka siku inaisha. Ufanye nini sasa? Tuungane pamoja wiki ijayo ili kujua ni namna gani unaweza kupanga majukumu yako vizuri ingawa kuna vitu vingi sana vinavyoweza kusonga ratiba zetu na majukumu yetu na kutufanya tuwe nje ya mstari.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com
4/10/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Fursa katika Kilimo cha Bustani
Habari msomaji wa makala za kilimo katika jukwaa hili la JIONGEZE UFAHAMU. Wiki hii tutajiongezea ufahamu kuhusu kilimo cha bustani kwa ufupi. Ila kwa wiki zinazokuja tutaingia kwa kina na tutaenda hadi kuchambua kilimo cha baadhi ya mazao, kuanzia uzalishaji hadi soko lake.
Karibu kwenye somo:
Kilimo cha bustani ni sekta ndogo iliyopo ndani ya sekta ya kilimo na ndio inayokua kwa kasi zaidi kuliko sekta ndogo yeyote ya kilimo. Tunaposema kilimo cha bustani tunamaanisha kilimo cha mbogamboga, matunda, maua pamoja na viungo (spices). Kilimo cha bustani ni kilimo ambacho kinalimwa na wakulima wadogo kwa asilimia kubwa, japokuwa upo uwekezaji mkubwa na uwekezaji wa kati ambao unakua kwa kasi pia. Ukweli ni kwamba mazao ya bustani ndio mazao yanayotumika sana kuliko mazao mengine. Huwezi kukwepa kutumia mazao ya bustani, haiwezi kupita siku hujatumia tunda, au mbogambogakama nyanya, kitunguu, mboga za majani, au viungo kama tangawizi, mdalasini, hiliki, karafuu, nazi n.k Pamoja na hayo lakini bado kilimo hichi hatujaweza kufikia kile kiwango cha uwezo wetu. Kutokana na rasilimali ardhi na hali ya hewa nzuri Tanzania inao uwezo wa kuzalisha mazao ya bustani mara 10 zaidi ya jirani zetu Kenya lakini pamoja na hayo yote wenzetu wanazalisha na kuuza nje ya nchi mara 10 zaidi yetu. Hii ni kwasababu kwanza wamegundua fursa iliyopo, wakaamua kutumia teknolojia na mbinu za ki leo katika kilimo, pia wanaongeza thamani ya mazao yenyewe kama kuweka katika madaraja na kuweka kwenye vifungashio. Kitu kingine kikubwa ni kwamba wenzetu wako vizuri sana katika masoko, wachangamfu sana katika kujitangaza na wanajua mbinu mbalimbali za kuteka soko kitu ambacho sisi hatuna. Sisi tunasubiri mteja aje atufuate wakati wenzetu wanalifuata soko.
SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo - 2
Kilimo cha Bustani Duniani
Katika dunia kilimo cha bustani kinakua kwa wastani wa 13% kwa mwaka, kikitegemea masoko ya ndani ya nchi, masoko ya kikanda pamoja na masoko ya kimataifa.Masoko makubwa ya mazao ya bustani ni Marekani, Urusi, India, nchi za Falme za Kiarabu pamoja na nchi za Ulaya. Changamoto ya kwenye soko la kimataifa ni kwamba wanazingatia sana ubora, na zipo taasisi kwa ajili ya kuthibitisha ubora tokea ilipozalishwa mpaka zao linapomfikia mlaji. Taasisi hizo ni kama Global GAP, BRC n.k. Changamoto hii imekua ikiwaathiri zaidi wakulima wadogo maana wanashindwa kukidhi viwango, lakini pia wakulima wadogo hawana uzalishaji endelevu. Mfano kama soko la Urusi unatakiwa kupeleka tani 200 za matunda au mboga kila wiki, wakulima wadogo inawawia changamoto maana yeye anafikiria azalishe akivuna ndioaanze tena kuandaa shamba kupanda tena. Wakati anaandaa shamba kwa ajili msimu unaofuata hana cha kuuza. Kwahiyo panahitajika mifumo ya uzalishaji ambayo inaweza kulihudumia soko katika hali endelevu. Pamoja na kwamba ni changamoto lakini kwa wengine imekua fursa, zipo kampuni zilianzishwa kupitia fursa hii, wao wanachokifanya wanatafuta hayo masoko kama ya Ulaya, Afrika kusini na kwingineko, na wanakua na vigezo vinavyohitajika kwenye soko. Halafu wanaingia mikataba na wakulima wadogo, wakulima wanazalisha kampuni inanunua na kwenda kuongeza thamani, kwa kuweka kwenye madaraja, kuweka kwenye vifungashio na wanauza kwenye hayo masoko.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Kilimo cha Bustani Tanzania
Hapa Tanzania kwa miaka mitano iliyopita kilimo cha bustani kimekua kikiongezeka kwa asilimia 6 hadi 10 kwa mwaka. Maeneo ya nyanda za juu kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Manyara) ndiyo yanayoongoza kwa uzalishaji wa mazao mengi ya bustani. Yapo pia maeneo mengineyanayofaa kwa kilimo hichi kama ukanda wa pwani, nyanda za juu kusini (Mbeya na Katavi), Nyanda za ziwa (Mwanza, Geita, Mara, Kagera n.k) pamoja na nyanda za kati (Dodoma - maarufu kwa kilimo cha Zabibu). Ukichunguza kila kanda in uwanja wa ndege hivyo kuwepo kwa fursa ya kuuza nje ya nchi. Kuna viwanja vya ndege kama Songwe - Mbeya, KIA –Kilimanjaro, Uwanja wa ndege Mwanza, Uwanja wa ndege JK Nyerere .
Katika nchi yetu tuna eneo takribani hekta Milioni 44 (44,000,000)ambalo bado halijatumiwa ipasavyo, kati ya hizo hekta milioni 29 (29,000,000) zinafaa kwa umwagiliaji lakini eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta laki mbili tisini elfu tu (290,000) eneo ambalo ni dogo sana ikilinganishwa na uhalisia wa eneo ambalo linafaa kwa umwagiliaji. Hii ni sawa na asilimia moja tu (1%). Hii ina maana asilimia 99 bado halijafanyiwa kazi.
SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.
Mazao mengi ya bustani unaweza kutumia eneo dogo na ukapata faida zaidi ya mara tatu kama ungezalishia mazao ya nafaka katika eneo lenye ukubwa sawa.
Kuona hilo, wahisani wengi wa miradi ya kilimo kwa wakulima wadogo wamejikita zaidi katika kuhamasisha kilimo cha bustani maana ndio kinachoweza kumkomboa mkulima kwa haraka zaidi.
Hii inatupa ishara kwamba kwa mtu anayetaka kuwekeza kwenye kilimo anashauriwa awekeze kwenye kilimo cha bustani.
Hapa chini nimeweka kiunganishi (link)ya tovuti (website) ya moja ya makampuni yanafanya kilimo cha bustani.Kampuni hii inaitwa StakeAgrobaseInt. Ltd (SAIL) na inamilikiwa na Mtanzania mwenzetu. Mwanzilishi wa kampuni hii alikua daktari wa hospitali ya mkoa, yeye aliona fursa akaichangamkia sasa hivi yuko mbali sana.
Stake AgrobaseInt. Ltd (SAIL)http://www.sailfv.com/aboutus.php
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email)daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
Makala Imehaririwa kwa Kiswahili sanifu na Rumishael Peter wasiliana nae kuhariri kitabu au Makala email:rumishaelnjau@gmail.com simu: +255-713-683422http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/09/2015 07:30:00 AM | Labels: KILIMO | 0 Comments
Siri Ya Kutambua Kampuni Nzuri Ya Kuwekeza Ili Upate Faida.
Unapohitaji kufanya uwekezaji katika hisa inatakiwa kutambua kampuni sahihi za kuwekeza mtaji wako ili uweze kukua. Katika kuchagua kampuni sahihi ya kuwekeza unahitajika kuzingatia vitu muhimu ambavyo vitasaidia kujua kampuni hii inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri. Ili uweze kutambua kampuni inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri unatakiwa kuzingatia vitu vifuatavyo ambavyo ni muhimu kuvifahamu.
Ukuaji wa Mauzo (Revenue)
Kampuni ambayo mauzo yake yanaongezeka kila mwaka, hii inaonyesha kwa kiasi gani kampuni hiyo inafanya bidii katika masoko na bidhaa zake zinafanya vizuri katika soko. Ukuaji huu unaashirilia hata uongozi upo makini katika kutekeleza mipango yao kwa umakini. Vile vile ukuaji wa mauzo unaonyesha kwa kiasi gani kampuni hiyo bidhaa yake ilivyo na umuhimu katika matumizi ya watu katika eneo husika.
SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.
Kufahamu ukuaji wa faida ya kampuni
Kampuni ambayo inaukuaji mzuri wa faida kuanzia 20% au 25% kwa mwaka ni nzuri kwa kuwekeza kwa kuwa gawio litakua na kuwavutia wawekezaji wengi zaidi. Vile vile kampuni itapata pesa ya kuwekeza katika fursa nyingine ambazo zitaongeza faida kwa kipindi kijacho. Ukuaji wa faida unaonyesha kwa kiasi gani kampuni ambavyo ipo makini katika kudhibiti matumizi yasiyo ya msingi katika uendeshaji wa kampuni na kupelekea ongezeko la faida.
Ukuaji mzuri wa Gawio
Kampuni ambayo inaukuaji mzuri wa gawio ni ishara kuwa hata ukuaji wa faida ni mzuri. Gawio likiongezeka mwekezaji anapata kipato vile vile huwavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika kampuni hiyo na bei kuongezeka kutokana na ushindani kuwa mkubwa katika soko. Gawio ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wengi kuwekeza katika kampuni yoyote na gawio likikua na ushindani huwa mkubwa katika soko la hisa na kupelekea bei zake kupanda.
SOMA; Tabia Saba Za Watu Wasiokuwa Na Mafanikio.
Ukuaji mdogo wa madeni
Kampuni ambayo ukuaji wake wa madeni ni mdogo au madeni ya kampuni yanapungua huashiria kuwa kampuni hiyo ina mipango madhubuti katika kukuza mauzo na kupunguza madeni ili kupunguza hatari ya kufirisika. Kampuni ambayo madeni yake yanaongezeka kwa kila mwaka na kwa kiwango cha juu hii inaashiria kampuni haifanyi vizuri na kuna hatari ya kushindwa kulipa madeni.
Ukuaji wa bei za hisa za kampuni
Sehemu mojawapo kwa mwekezaji kupata faida kupitia uwekezaji wake kwa kupitia ongezeko la bei za hisa. Bei ya hisa ikiongezeka kwa kiwango kizuri na mwekezaji hupata faida ambayo hutokana na ongezeko la thamani. Kampuni ambayo ina ongezeko la bei kwa 20% au zaidi kwa mwaka ni kampuni nzuri kwa kuwekeza kwa kuwa mwekezaji atapata ongezeko la thamani ya hisa zake katika kiwango kinachorizisha. Katika soko la hisa kuna kampuni ambazo zina ukuaji bei za hisa wa zaidi ya 40% kwa mwaka ambazo ni nzuri kuwekeza kwa mwekezaji.
SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Umuhimu Na Jinsi Ya Kujijengea Tabia Ya Shukrani.
Kufahamu mipango ya Kampuni kwa miaka ijayo
Kampuni ili iweze kufanya vizuri katika soko ni kuwa na mipango mizuri kwa miaka ijayo ili iweze kuendana na mabadiliko yanayotokea. Mwekezaji ataweza kufahamu mipango ya kampuni kwa kuangalia taarifa za mwaka za kampuni (Annual Report) ambapo kampuni huonyesha mipango yao katika kipindi kijacho kama wanahitaji kuongeza bidhaa mpya au kuongeza matawi katika sehemu nyingine au nchi nyingine.
Hivi ni vitu vya msingi kwa mwekezaji kuviangalia unapohitaji kuwekeza katika hisa ili uweze kupata manufaa na kuwekeza kwa faida na kukuza mtaji wako. Tukutane katika makala nyingine ambazo zinakujenegea uwezo zaidi katika kuwekeza katika hisa.
SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.
Ili uweze kupata taarifa za kiswahili zitakozokuwezesha kutamua ukuaji wa mauzo, faida ya kampuni, ukuaji wa bei na mipango ya kampuni tuwasiliane kwa mawasiliano hapo chini.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
4/08/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Huu Ndio Mtaji Mkubwa Ambao Tayari Unao.
Labda niane kwa kueleza kuwa hakuna mtu ambae hana mtaji huo. Mtaji wenyewe unautengeneza mwenyewe kuweza kuwa bora kwani tayari unao. Mtaji wenyewe ni watu. Watu wanaweza kukuwezesha au kukuangusha kutegemea na unavyowatumia. Wanasiasa, walimu, wanasheria, wafanyabiashara huhitaji watu ili kuweza kufanikisha malengo yao. Hakuna kiongozi yeyote wa siasa ambaye amewahi kufanikiwa bila kuwa na watu. Hakuna mfanyabiashara aliyefanikiwa bila kuwa na mtaji wa watu. Ili uweze kufanikiwa ni lazima uweze kuwa na watu wa kufanya nao kazi, kukutia moyo, kukufariji na hata wa kukupa changamoto zitakazokuimarisha.
SOMA; Kila Suluhisho Linatengeneza Tatizo, Chagua Ni Tatizo Gani Unataka.
Ukihitaji mafanikio utahitaji watu ambao utafanya nao kazi, utahitaji watu wa kununua bidhaa zako, utahitaji watu wa kukukopesha, utahitaji watu wa kukufanyia kazi, utahitaji watu wa kukushauri na kwa vyovyote vile huwezi kufanikiwa bila kuwa na watu. Hayati Nelson Mandela aliwahi kusema kwamba ‘’ukitaka kutembea haraka tembea mwenyewe, lakini ukitaka kutembea umbali mrefu basi tembea na watu’’. Jaribu kuutumia msemo huu katika maisha yako ya kawaida na utaona uhalisia wake. Jaribu kujijengea watu wa kukuinua na sio wa kukuangusha. Jaribu kujijengea mtandao bora ambao utakufaa. Ukijenga mtandao mbovu utakuangusha sawa na kujenga nyumba yenye msingi mbovu, Itaanguka siku moja. Je kuna ulazima wa kuwa na watu wengi? Jibu linaweza kuwa ndiyo au hapana. Kuwa na watu wengi wenye lengo la kukuangusha au kukurudisha nyuma si mali kitu. Ni bora kuwa na watu wawili watakaokusaidia. Laini pia kama kuna ulazima wa kuwa na watu wengi jifunze namna ya kuwapata kwa kujifunza kupata na kukaa na watu.
SOMA; Mipango Sio Muhimu Kama Kitu Hiki.
Kwa kuhitimisha nitumie fursa hii kukuambia kuwa na watu halafu usishirikiane nao utaukuwa hujafanya chochote. Jifunze kushirikiana na watu. Usimdharau yeyote bali muheshimu kila mtu kwa nafasi yake kwani hujui atakuja kukufaa lini. Nakushauri pia uondoe watu wanaokuletea mawazo hasi na kukuaminisha kuwa huwezi. Hao watakufanya usifikie malengo yako. Usipende kukaa na watu ambao wataupoteza muda wako kwa vitu visivyokujenga. Bali tumia kila sekunde moja ya masha yako kukujenga na tumia watu waliofanikiwa kuweza kujifunza kutoka kwao.
Nakutakia heri ya pasaka na mapumziko mema ya siku ya kumbukumbu ya Karume. Tukutane wiki ijayo siku ya leo kwa makala nyingine ya kukujenga.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes ambae ni mjasirimali na mhamasishaji. Unaweza kuwasiliana na nae kwa kwa: simu: 0712 843030/0753 843030 e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.
4/07/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO | 0 Comments
Hiki Ndio Kitu Kitakachokuletea Mafanikio Ambacho Tayari Unacho.
Vitu vyote hapa duniani ambavyo tunaviona vilivyotengenezwa na binadamu, vimetokana na mawazo ya mtu, ambayo mawazo hayo yameweza kuleta mapinduzi makubwa hapa duniani. Mpaka leo mimi na wewe tunatumia vitu ambavyo vimetokana na mawazo ya watu .
Ukiwa na wazo au mawazo ya kutengeneza jambo Fulani basi wewe ni tajiri kama ukilifanyia kazi wazo lako kwa vitendo sio kuishia kuongea tu. Watu wote waliofanikiwa hapa duniani walianza kufikiria ,halafu wakapata wazo wakaweza kuthubutu na kuleta matokeo chanya katika jamii. Mfano simu au compyuta unayotumia leo kusoma makala hii yalikuwa ni mawazo ya mtu ambaye aliweza alithubutu kwa vitendo hatimaye akaleta matokeo chanya duniani.
SOMA; BIASHARA LEO; Kwa Nini Watu Hawawaambii Wengine Kuhusu Biashara Yako.
Hivyo basi hata wewe usife na wazo au mawazo yako mazuri uliyokuwa nayo ambayo yanaweza kuleta mabadiliko makubwa sana katika jamii yetu. Acha tabia ya kuhairisha mambo (procrastination) Anza SASA kuthubutu wazo lako na wewe najuwa utakuwa na mawazo mazuri sana ambayo ulikuwa nayo ungetamani kuyathubutu leo.
Ifuatayo ni kanuni ambayo inaonesha namna gani wazo au mawazo yako yanavyofanya kazi na kanuni hii kila mtu anaitumia pengine kwa kujua au kutokujua .
THOUGHTS (T) + FEELINGS (F) +ACTIONS (A) =RESULTS(R)
Ufafanuzi wake ni huu hapa MAWAZO +HISIA+VITENDO =MATOKEO
Kila kitu huwa kinaanza na mawazo ambayo yanazalishwa na akili yako kama tulivyoona hapo juu katika kanuni elekezi , na usemi huu unawezwa kudhihirishwa pia na mtunzi wa kitabu cha Secrets of the Millionaire Mind –T . Harv Eker ambaye alisema hivi ‘’everything begins with your thoughts which are produced by your mind ‘’
SOMA; UKURASA WA 95; Fanya Kwa Kiasi.
Hisia (feelings), baada ya kuwa na wazo au mawazo ya kufanya jambo Fulani, kuna kitu kinakuja ndani yako kama tulivyoona katika kanuni elekezi ambacho kinakusukuma kufanya jambo hilo kwa shauku ,hisia nazo zinazalisha kitu kipya yaani hatua nyingine ya kuthubutu kufanya jambo hilo.
Vitendo (actions),baada ya kuwa na wazo ukapata hisia ya wazo lako hatua inayofuata ni vitendo ambapo hapa sasa ndio unaweza kuthubutu wazo lako na kupelekea hatua nyingine ambayo ni matokeo.
Matokeo (results) hapa ndio hitimisho la wazo lako, baada ya kuwa na wazo,ukapata hisia ya kufanya jambo hilo ukaweza kuthubutu kwa vitendo na hatimaye ukapata matokeo .
SOMA; NENO LA LEO; Mipango Sio Muhimu Kama Kitu Hiki.
Hivyo basi , tumeona kuwa kila kitu huwa kinaanza na mawazo hata wewe unaweza kutengeneza wazo lako zuri leo na kubadili kabisa fikra yako na kuwa na mtazamo chanya unaoweza kubadili maisha yako. Mtunzi wa kitabu cha The Magic of Think Big –David J.Schwartz ,ph.d anasema kuwa binadamu ni zao la mawazo yake mwenyewe , ‘’ A person is a product of his own thoughts’’
‘’ Your mind is a thoughts factory ‘’ – Akili yako ni kiwanda cha mawazo
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi mhamasishaji na mjasiriamali unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe (E-mail) deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea blog yake (tovuti) kwa kujifunza zaidi www.actualizeyourdream.blogspot.com
4/06/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO | 0 Comments
Salamu Za Sikukuu Kutoka AMKA CONSULTANTS Na Mambo Muhimu Kwako Kuzingatia.
Leo ni sikukuu ya pasaka ambapo wakristo wote duniani wanaadhimisha mateso na kufufuka kwa mwokozi wao Yesu Kristo. Vile vile leo ni siku ya mapumziko kwa Watanzania wote.
Kampuni ya AMKA CONSULTANTS ambayo ndio inasimamia mitandao hii AMKA MTANZANIA, KISIMA CHA MAARIFA, MAKIRITA AMANI NA JIONGEZE UFAHAMU inachukua nafasi hii kukutakia wewe mtanzania sikukuu njema na mapumziko mema pia.
Katika sikukuu hii umekuwa na siku nyingi za mapumziko na kusherekea pia. Sherekea sikukuu hizi kwa amani na upendo na kumbuka kwamba kuna maisha baada ya sikukuu hizi.
Pia katika muda huu mrefu wa mapumziko, kumbuka kupata muda wa kufanya jambo ambalo ni muhimu kwako na ambalo hukupata muda wa kulifanya katika siku za kawaida.
AMKA CONSULTANTS itaendelea kuwa nawe katika safari ya kuboresha maisha yako. Lengo letu ni kufanya kazi na watu ambao wapo tayari kuchukua hatua ya kuboresha maisha yao na kuwasaidia kufikia lengo lao hilo. AMKA CONSULTANTS tunajua kwamba unawez akubadili maisha yako kama utakuwa tayari na kama ukipata msaada wetu ambao ni muhimu sana kwako.
Tutaendele akuwa nawe katika kila hatua ya maisha yako, kazi yako na hata biashara yako.
Endelea kutembelea mitandao yetu kila siku ili kujifunza, kuhamasika na kushauriwa. Tunakuahidi kupata huduma bora sana kulingana na mahitaji yako.
Karibu sana tufanye kazi pamoja.
Nawatakia watanzania wote sikukuu njema na mapumziko mema.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Mkurugenzi, AMKA CONSULTANTS.
N;B Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.
4/05/2015 10:00:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Tabia Hizi Zitakusaidia Sana Kufikia Malengo Yako Kwa Haraka - 2
Habari ndugu msomaji wa mtandao huu wa JIONGEZE UFAHAMU. Nina imani ulikua na wiki nzuri. Karibu tena kwenye sehemu hii ya pili ya makala inayokukumbusha juu ya tabia zitakazokusaidia kufikia malengo yako kwa haraka. Wiki iliyopita tuliangalia baadhi ya tabia hizo na wiki hii tutamalizia tabia zilizobaki.
Kama hukusoma makala ya wiki iliyopita unaweza kuisoma hapa; Tabia Hizi Zitakusaidia Sana Kufikia Malengo Yako Kwa Haraka.
5. Heshimu kila mtu.
Usimdharau mtu yeyote unayekutana naye, iwe unamfahamu au haumfahamu. Inawezekana mtu huyo ni njia ya wewe kutimiza malengo yako. Katika utamaduni wa kiafrika heshima ni tabia njema, muheshimu mtu yeyote hata mwenye kipato kidogo kiasi gani. Kila mtu anamchango fulani katika maisha yako ambao kwa namna moja au nyingine mchango huo unakusaidia wewe kukamilisha ndoto zako, kama wewe pia ulivyo na mchango katika kutimiza ndoto za wengine. Iwe ni mfanya usafi, mvulana au msichana wa kazi, mbeba mizigo n.k
SOMA; BIASHARA LEO; Lengo La Biashara Sio Kupata Faida, Bali Ni Hili Hapa.
6. Jenga mahusiano mazuri na watu wote.
Kuna kitu kipya cha kujifunza kwa kila mtu unayekutana naye, iwe unamfahamu au haumfahamu. Watu ni rasilimali muhimu sana katika kufikia malengo yetu. Mtu unayekutana naye anaweza kuwa mteja, mshauri wako katika jambo fulani, unaweza kumtumia mtu kama msaada wa nguvu kazi au mtu anaweza kukupa msaada wa kifedha. Ona kila mtu anavyoweza kukusaidia kufikia malengo yako huku ukitoa msaada kwa wengine ili nao pia wafikie malengo yao.
7. Tafuta rafiki mwenye malengo yanayofanana na yako.
Waswahili wanasema “ndege wenye mbawa zinazofanana huruka pamoja”
Ni rahisi kufikia malengo kama utakaa na watu wenye ndoto na muelekeo kama ulionao. Ni rahisi kusaidiana na kutiana nguvu ili kukamilisha malengo yenu kama wote mnaelekea njia moja. Pia kuwa na marafiki waliofanikiwa katika jambo ambalo nawe pia unatamani kufanisha, hao watakusaidia sana kukupa mbinu za kufikia mafanikio katika lengo lako.
SOMA; NENO LA LEO; Hiki Ndio Chanzo Cha Wivu.
8. Jitahidi kuishi maisha yako na sio kuiga maisha ya wengine.
Waswahili wanasema “miluzi mingi humpoteza mbwa”.
Kila binadamu amepangiwa maisha yake na Mungu na maisha yake hayo hayafanani na maisha ya mtu mwingine yeyote. Usikubali kuishi kama fulani anavyotaka uishi, kumbuka kuwa hakuna anayefanana na wewe zaidi ya wewe mwenyewe. Kutaka kuwa kama fulani, au kuishi namna fulani ili umfurahishe mtu mwingine kutakufanya uumie na wakati mwingine kutofikia viwango ambavyo Mungu amepanga wewe ufikie. Kutamani kwa uzuri maisha ya mwingine ni jambo zuri lakini sio kujaribu kuiga kila kitu chake. Wewe ni wa pekee vile ulivyo. Kubali na fanya mambo yatakayokusaidia kutimiza malengo yako na si malengo ya watu wanaokuzunguka.
SOMA; Utashi, kitu muhimu kwako kufikia mafanikio.
9. Jitahidi kuwa na furaha kila wakati, jivishe tabasamu usoni pako.
Mambo mengi tunayoyafanya vizuri huwa yanafanyika wakati tukiwa na furaha na utulivu wa akili. Hatufanyi vitu vizuri tunapokuwa na chuki,kinyongo na huzuni. Jitahidi kuwa na furaha kila wakati. Epukana na msongo wa mawazo. Ukiwa na akili iliyotulia nirahisi kuona fursa zitakazokusaidia kufikia malengo yako.
Nakutakia maisha yenye furaha.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110/ 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com
4/03/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo - 2
Habari za leo msomaji wa makala za kilimo kwenye Jiongeze Ufahamu, ni matumaini yangu unaendelea mbele na juhudi za kuyafikia mafanikio. Nipende kuwashukuru wote ambao mmekua mkijifunza kupitia jukwaa hili, nimepokea barua pepe (email) kadhaa za ndani ya Tanzania na hata nje ya nchi za watu kukiri kujifunza kutokana na makala za kilimo. Wale ambao mmeniandikia barua pepe kwa ajili ya kupata ushauri, wapo ambao tayari nimeshawajibu ila wapo wengine wiki hii mwishoni nitakua nimewajibu wote waliobakia.Tujikumbushe tu kidogo,wiki iliyopita tulianza kujifunza mambo matano ya muhimu kuyafahamukabla ya kuwekeza kwenye kilimo, na tuliweza kujifunza mambo mawiliambayo ni soko na hali ya hewa inayoruhusu kustawi kwa kilimo ulichokusudia. Leo tutaweza kuyamalizia mambo yaliyobakia. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki iliyopita isome hapa; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo.
Karibu kwenye somo
3. Upatikanajiwa rasili watu (Wafanya kazi)
Ukweli ni kwamba hata ukiwa na kiasi kikubwa cha fedha hutaweza kuwekeza kwenye kilimo kama huna rasilimali watu. Wafanyakazi ni rasilimali muhimu sana kama zilivyo fedha, vifaa, mitambo au mashine za utendaji kazi, ndio maana kulijua hilo kampuni nyingi zimeweka utaratibu wa kutunza rasilimali hii muhimu ya watu. Utakuta kwenye makapuni kuna afisa au meneja rasilimali watu. Ukweli ni kwamba vitendea kazi ulivyo navyo vitaendeshwa na watu. Wafanyakazi ni wa muhimu sana kwenye kilimo kuanzia uwekezaji mdogo hadi mkubwa. Wafanyakazi tunaweza kuwaweka kwenye makundi 2, la kwanza ni la wafanyakazi wa kawaida wale ambao hawana ujuzi wa kitaalamu au vibarua, na kundi lingine ni la wafanyakazi wenye utaalamu au ujuzi fulani hasa wa kilimo.Kama unaanza kuwekeza kwenye kilimo kwa uwekezaji wa chini hutahitaji sana wataalamu kwa kuwaajiri, ila utahitaji kutafuta ushauri wa kitaalamu ambao sio gharama kubwa. Lakini pia utahitaji vibarua ambao watakua wakifanya shughuli za shambani, hapo itategemea na ukubwa wa shamba lako. Ila kama unataka kufanya uwekezaji mkubwa lazima utahitaji hao wataalamu wa kilimo, na sio hao tu utahitaji fani nyingine kama washauri wa fedha, wahasibu, utawala, wataalamu wa sherian.k Kumbuka hapo kwa wafanya kazi, sio alimradi wafanya kazi, unahitaji wafanya kazi wenye kufanya kazi kwa bidii, wenye kujituma sio mpaka wasimamiwe ndio wafanye kazi, wenye hamasa ya kazi, wabunifu na wanaoweza kufuata maelekezo vizuri hata kama sio mtaalamu lakini ana uwezo wa kufuata maelekezo ya kitaalamu. Pia bila kusahau mwajiri lazima ujali wafanya kazi wako maana ni rasilimali inayokuzalishia kipato, lazima ujue wafanyakazi ni zaidi ya hizo mashine au mitambo na fedha.
Katika nchi zinazoendelea rasilimali watu ni rahisi kuipata, gharama yake ni rahisi ukilinganisha na nchi zilizoendelea tayari. Katika nchi zilizoendelea gharama ya kumlipa kibarua au mfanya kazi wa kawaida inakaribia kulingana na gharama ya kulipa mtaalamu mwenye ujuzi katika nchi za kwetu, na ndio maana nchi tajiri zinapendelea kuja kuwekeza huku kwenye nchi zinazoendelea.
SOMA; BIASHARA LEO; Ondoka, Hakuna Aliyekuita Hapa.
4. Upatikanaji wa maji wa uhakika
Wakulima wengi baraniAfrika kilimo chao kinategemea mvua, hivyo mvua isiponyesha uzalishaji unakua matatani. Mabadiliko ya tabia nchi yanapelekea mvua zisiwe za uhakika laikini pia majira ya mvua yanabadilika, mfano kama mvua za masika tulikua tumezoea zinaanza mwezi wa pili lakini kwa sasa zinaanza mwezi wa tatu au wanne. Upatikanaji wa maji kila kukicha unakua ni changamoto. Ikumbukwe kwamba ukame huongoza kusababishanjaa au upungufu wa chakula dunia kote. Katika uwekezaji wa kilimo kitu ambacho unatakiwa uwe na uhakika nacho ni maji ya uhakika, uwe na chanzo cha maji cha uhakika. Ili ufanye kilimo cha kibiashara lazima uwe na uwezo wa kuzalisha mwaka mzima, kama huna maji ya uhakika hutaweza kufanya hivyo. Hapa namaanisha kilimo cha umwagiliaji, zipo njia mbali mbali za umwagiliaji kama njia ya mifereji, umwagiliaji wa matone, umwagiliaji wa maji mfano wa mvua. Lakini katika njia zote njia ya umwagiliaji wa matone ndio nzuri maana inatumia maji machache na pia maji yanakwenda pale mmea ulipoota hivyo hakuna upotevu wa maji. Njia hii ya umwagiliaji wa matone unaweza kufanyika katika mashamba ya wazi au katika nyumba ya kupandia mazao maarufu kama Nyumba ya kijani(greenhouse). Unaweza kuwa na vyanzo tofauti vya maji mfano kutoka mtoni, kuchimba kisima cha chini, kuvuna maji ya mvua n.k. Pia ni vizuri kutengeneza miundombinu ya kutunza maji kama Bwawa ambalo litahifadhi maji. Israel ni moja ya nchi zinazofanya vizuri sana kwenye kilimo cha umwagiliaji,ijapokuwa eneo lake kubwa ni ukame wameweza kuvumbua teknolojia nzuri sana kwenye umwagiliaji. Israel mvua ikinyesha siku tatu tu, wana uwezo wa kupanda na kuvuna mazao yakutumia na kuuza nje ya nchi. Hii ni kwasababu wanayo miundo mbinu mizuri katika kuvuna maji ya mvua na kuyatunza kwa ajili ya kutumia kumwagilia kwa njia ya matone. Kwa Tanzania zipo kampuni kadhaa ambazo zimekua zikifanya biashara ya kuuza vifaa vya umwagiliaji wa matone, moja ya kampuni hiyo ni Balton Tanzania ambayo ni kampuni ya Waisraeli. Kwa Tanzania wapo Arusha na pia wanayo ofisi Dar. Pia wanatoa huduma ya kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji.Kwahiyo kwa kumalizia pointi yetu hii ni kwamba, upatikanaji wa maji ni muhimu sana katika uwekezaji wa kilimo maana kama vile maji ni uhai kwa mwanadamu, vivyo hivyo maji ni uhai kwa mimea.
SOMA; UKURASA WA 91; Utashi, kitu muhimu kwako kufikia mafanikio.
5. Miundombinu pamoja na kufifika kwa eneo la uwekezaji
Hapa tunaangalia miundombinu kama barabara, umeme, mawasiliano ya simu n.k Lazima eneo unalowekeza kilimo chako liwe linafikika, hakikisha barabara iko vizuri na inapitika wakati wote, maana utahitaji kusafirisha kwenda shambani vitendea kazi, pembejeo n.k. Pia wakati wa kuvuna utahitaji kusafirisha kupeleka sokoni. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba eneo likiwa ni gumu kufikika hii itaongeza gharama za uzalishaji na hivyo kupelekea kupunguza faida yako. Hivyo pamoja na kuzingatia vigezo vinne vilivyopita ni lazima kuchagua eneo ambalo linafikika, mawasiliano ya simu yako sawa, pia nishati ya umemena mengineyo.
SOMA; Hiki Ndio Unachohitaji Ili Kugeuza Ndoto Yako Kuwa Uhalisia.
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email) daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
Imehaririwakwa Kiswahili sanifunaRumishael Peter
email:rumishaelnjau@gmail.comsimu:+255-713-683422
http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/02/2015 07:30:00 AM | Labels: KILIMO | 1 Comments
MIAKA MIWILI YA AMKA MTANZANIA; Kwa Nini Ipo Na Itaendelea Kuwepo Na Mambo Mazuri Yanayokuja.
Tarehe 31/03/2013 ilikuwa ndio siku ya kwanza kwa makala ya kwanza kwenda hewani kwenye mtandao huu wa AMKA MTANZANIA. Kipindi hiko wakati naanzisha mtandao huu mambo hayakuwa kama sasa, watu walikuwa na muamko mdogo wa kusoma habari za aina hii na hata kujisomea vitabu. Leo hii miaka miwili tu mbele, mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa sana
Leo hii, miaka miwili baadaya kuanzishwa kwa mtandao huu nimeona ni vyema tukashirikishana kwa nini mtandao huu upo, utaendelea kuwepo na mambo makubwa yanayokuja.
Moja ya makala za mwanzo kabisa kwenye AMKA MTANZANIA;
UTARATIBU WA KUJISOMEA VITABU
USIMLAUMU YEYOTE, ANZA KUJILAUMU WEWE
ZOEZI ZURI LA KUFANYA KILA SIKU
Kwa nini mtandao huu upo?
Miaka miwili kabla ya kuanz akwa mtandao huu, nilikuwa naishi kwenye hadithi nzuri ambayo tumekuwa tukidanganywa. Hadithi kwamba nenda shule, soma kwa bidii, faulu vizuri na utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Nilisoma kwa bidii kweli na kufaulu vizuri sana masomo yangu ya kidato cha sita. Baada ya hapo nilipata nafasi ya kusomea udaktari wa binadamu. Kwa nafasi hii niliamini ndio nimepata tiketi ya maisha mazuri.
Lakini mambo yalibadilika sana baadaya ya kuanza masomo haya ya udaktari. Baada ya kuona kile nitakachokwenda kufanya na mazingira ya kukifanya na hata maisha ya madaktari wengine, sikushawishika sana kama mwanzo kwamba kuwa daktari ndio tiketi ya maisha bora.
Changamoto kubwa zaidi ilitokea mwaka 2011 ambapo nilijikuta nje ya mfumo wa elimu, huku sina degree wala chochote cha kuniwezesha kupata kazi ya kujikimu kwenye maisha yangu. Mbaya zaidi hakuna aliyeweza kunielewa kwenye kipindi hiki kwa sababu kila mtu anayenifahamu aliona nimefanya makosa makubwa sana kwenye maisha, sijui ninachofanya na mengine mengi. Ni hapa ndio nilipoamua kushika hatamu ya maisha yangu. Nilikaa chini na kuamua kwamba kama nitakwenda kufanikiwa kwenye maisha yangu, basi hiyo ni juu yangu. Na nilijiambia kabisa kwamba mafanikio kwenye maisha hayahitaji degree au elimu yoyote kubwa.
Ni baada ya maamuzi haya ndipo niliacha kulalamika na kuanz akuchukua hatua juu ya maisha yangu. Nilitafuta kazi yoyote ninayoweza kufanya ili angalau iniwezeshe kuendelea kuwepo mjini. Nilipata kazi hiyo na sio kwa sababu ya kuwa nimesomea kazi hiyo, au kwa sababu ya kujulikana, bali kwa ushawishi niliokuwa nautoa kwenye maombi ya kazi hiyo.
Baada ya hapa niliamua kujifunza na kuangalia ni kitu gani ninachopendelea kufanya. Nilianza kujifunza mambo yanayohusiana na teknolojia ya habari(IT) ambapo nilijifunza jinsi ya kutengeneza tovuti, blog, programu za kompyuta na vitu vingine vingi. Yote haya sikuwa na darasa la kufundishwa, bali nilitafuta vitabu na kujisomea kisha kufanyia kazi yale ambayo nimeyasoma. Uzuri ni kwamba nilikuwa naona matokeo mazuri kila ninapojifunza na kufanya kitu.
Baada ya mwaka mmoja wa kujifunza vitu vya kitaalamu na pia kujisomea vitabu vyakujijenga na kujihamasisha niliona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yangu. Kwanza nilijikuta katika hali kubwa ya kujiamini, nikiwa na vyanzo mbalimbali vya mapato kutoka kwenye shughuli mbalimbali ambazo nilikuwa naweza kufanya. Ni katika wakati huu ambapo niliona makosa makubwa niliyokuwa nafanya kwenye maisha yangu na jinsi nilivyoweza kuyarekebisha.
Ni wakati huu pia ambapo niliona watu wengi wanafanya makosa haya na kunafanya maisha yao yawe magumu sana. Ndio maana niliona kuna umuhimu wa kuwashirikisha vitu hivi vizuri ambavyo nimefanya kwenye maisha yangu na ninaendelea kuvifanya ili nao waweze kuboresha maisha yao. Hapa ndipo mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ulipozaliwa. Lengo kubwa la mtandao huu ni kumsaidia kila mtanzania ambaye ameamua kushika hatamu ya maisha yake kuweza kufikia malengo na mipango aliyojiwekea kwenye maisha yake.
Kwa nini nimekushirikisha sehemu hiyo ndogo ya maisha yangu na historia ya mtandao huu?
Nimefanya hivi kwa sababu najua kuna kijana wa kitanzania ambaye amemaliza masomo yake ila hajapata ajira. Kijana huyu amekaa nyumbani na hajui afanye nini, kwani hata biashara anasema hana mtaji. Nataka kukuambia wewe kijana mwenzangu kwamba AMKA na uchukue hatamu ya maisha yako, utakapoamua kuamka hakuna linaoshindikana.
Najua kuna mfanyakazi ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu sasa ila haoni kitu kikubwa ambacho amefanya kwenye maisha yake. Maisha yake yamekuwa ya kuamka, kwenda kazini, kurudi nyumbani na kesho pia kufanya hivyo. Kipato anachopata pia hakioni kwa sababu kinaishia kulipa madeni na kulipia gharama za maisha. Nataka kukuambia wewe mtanzania mwenzangu, haijalishi kazi yako ni ya chini kiasi gani, haijalishi umeifanya kw amuda gani, kuna njia nzuri sana za wewe kuweza kuyabadili maisha yako na kuwa bora sana zaidi ya sasa ambapo unayaona yanakwenda tu.
Pia najua kuna mfanyabiashara ambaye amekuwa anafanya biashara zake kwa muda mrefu ila haoni mabadiliko yoyote kwenye biashara hiyo. Au ameanza biashara na kupata hasara hivyo kuamini kwmaba biashara haiwezekani. Napenda kukuambia kwamba kuna mbinu nzuri sana za kufanya biashara zako na kama ukiamua kuzitafuta na kuzifuata maisha yako yatakuwa tofauti sana na yalivyo sasa.
Maisha yoyote ambayo unapitia sasa, hata yawe magumu kiasi gani, unayo nafasi kubwa sana ya kuyabadili wewe mwenyewe. Huna haja ya kulaumu serikali, kulaumu wazazi au kulaumu mtu mwingine yeyote unayefikiri ndio anakuletea maisha hayo magumu. Leo nakuambia kwamba, maisha magumu uliyonayo, yataondolewa na wewe mwenyewe.
Kwa nini AMKA MTANZANIA itaendelea kuwepo.
AMKA MTANZANIA itaendelea kuwepo kwa sababu bado watanzania wengi hawajaamka. Bado watanzania wengi wamekabidhi maisha yao kwa waajiri wao, kwa serikali, kwa jamii na wameruhusu taasisi hizi zifanye maamuzi muhimu kwenye maisha yao. Hii ndio maana wanaona maisha yao yakienda tu na hivyo kuishia kulaumu pale ambapo kile walichotarajia hakijatokea.
Bado watanzania tunahitaji maarifa muhimu sana ya kuweza kuboresha maisha yetu na kufanikiwa zaidi. Sehemu kubwa sana ya watanzania wanafanya mambo kwa mazoea. Wanafanya kazi kwa sababu ndio kazi ambayo wamekuwa wanaifanya kila siku. Wanafanya biashara kwa sababu wamezoea kufanya biashara hiyo. Hii ni sumu kubwa sana ya kufikia mafanikio makubwa kama unavyoweza kuisoma vizuri kwenye kitabu JINSI YA KUFAIDIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA.
Mtandao huu utaendelea kuwepo na kutoa makala na mafunzo mazuri yatakayomwezesha kila aliyeamua kuboresha maisha yake kuweza kufikia lengo hilo.
Mambo mazuri yanayokuja kwenye AMKA CONSULTANTS.
Ilianza AMKA MTANZANIA ambayo ilikuwa na jukumu kubwa la kukupa wewe taarifa muhimu unazohitaji kuwa nazo ili kuboresha maisha yako. Mwaka mmoja baadae ikaja KISIMA CHA MAARIFA ambayo ni sehemu maalumu kwa wale ambao wako tayari kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yao. Kupitia KISIMA CHA MAARIFA watu wanajifunza tabia za mafanikio, mbinu za kufikia mafanikio, biashara na ujasiriamali na hata kupata uchambuzi wa vitabu vizuri. Kupitia KISIMA CHA MAARIFA pia unapata nafasi ya kukutana na watanzania wengine ambao nao wanaelekea kwenye safari ya mafanikio.
Kuna mambo mengi na mazuri ambayo yataendele akukujia kupitia mtandao huu wa AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA. Endelea kutembelea mitandao hii na washirikishe wengi zaidi ili nao wapate mambo haya mazuri.
Kuna kipengele muhimu kitakachokuja kwenye AMKA MTANZANI ambapo tutapata shuhuda za watu mbalimbali ambao maisha yao yamebadilika sana baada ya kujifunza kupitia AMKA MTANZANIA na kuamua kufanyia kazi yale ambayo wamejifunza. Shuhuda zipo nyingi mpaka sasa. Kama na wewe ungependa kuwashirikisha watanzania wenzako ushuhuda mzuri kutokana na uliyojifunza kwenye mtandao huu tafadhali andika maelezo yako kwa kujitambulisha, kueleza ulipotoka, ulipo sana na unapokwenda na jinsi gani AMKA MTANZANIA imekusaidia kisha tuma kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz Tafadhali fanya hivi na utakuwa sehemu ya mabadiliko ya nchi yetu na watanzania wenzetu.
Ufanye nini ili maisha yako kuwa bora ziadi?
Kwanza kabisa chukua maamuzi juu ya maisha yako, jua kama utakwenda kufanikiwa basi ni kwa juhudi zako na hakuna atakayekuletea mafanikio hayo.
Pili amua kujifunza sana kuhusiana na hiko unachofanya na maisha yako kwa ujumla. Jisomee vitabu mbalimbali vinavyotumwa kwenye mtandao huu na endelea kusoma mtandao huu kila siku kwa sababu kila siku kunakuwa na makala nzuri za kukuwezesha kuboresha maisha yako.
Tatu, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, kwa kuwa ndani ya kisima utajifunza mbinu nyingi sana za kukuwezesha kufikia mafanikio na pia utapata nafasi ya kukutana na watanzania wengine ambao wameamua kuchukua hatamu ya maisha yao. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA na weka taarifa zako kisha lipa ada ya uanachama na utapata nafsi ya kupata maarifa hayo adimu. Kuhakikisha unapata mambo yote mazuri lipia ada ya GOLD MEMBER.
Naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana wewe msomaji ambaye umekuwa na mtandao huu mpaka sasa. Ni kwa sababu yako ndio maana mtandao huu umeendelea kukua na kuwafikia wengi zaidi. Umekuwa ukiwashiriksiha wengine habari za mtandao huu na kuwafanya wautembelee pia. Tafadhali endelea kuw abalozi mzuri wa AMKA MTANZANIA na hakikisha kila mtu unayemfahamu naye amefahamu kuhusu mtandao huu ili na yeye autembelee na kujifunza.
Pia niseme kwamba sisi sote tunaendelea na safari ya kujifunza, hakuna anayejua zaidi bali tunajifunza na wakati mwingine tunafanya makosa. Mimi na waandishi wengine wa mtandao huu sio kwamba ndio mabingwa sana kwenye kile tunachoandika, ila tunapenda kujifunz ana kutumia mambo haya na maisha yetu yanakuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda. Na wewe usikose nafasi hii ya kuboresha maisha yako kila siku hata kama ni kidogo kiasi gani.
Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako. Kumbuka kwamba kila kitu kinawezekana kama ukiamua kuchukua hatua. Kama kuna jambo lolote ambalo linakupa changamoto na ungependa kupata ushauri zaidi karibu sana tuwasiliane. Unaweza kupiga simu kwenye namba 0717396253 na tukaona ni jinsi gani tunaweza kusaidiana kwenye jambo hilo.
TULIKUWA PAMOJA, TUPO PAMOJA NA TUTAENDELEA KUWA PAMOJA. Tafadhali tuma makala hii kwa njia ya email kwa watu watano na nicopy(weka email yangu makirita@kisimachamaarifa.co.tz kwenye sehemu ya cc) kwenye email hiyo na nitakutumia zawadi nzuri ya kitabu cha kufaidika na mabadiliko.
4/01/2015 04:00:00 PM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Jinsi ya kuzuia hatari ya kupata hasara kupitia uwekezaji katika hisa
Uwekezaji katika hisa ni kama biashara nyingine unaweza kupata hasara au faida, ila uwekezaji huu ni wa upekee ni jinsi ambavyo unafanyika. Ili uweze kukuza thamani ya pesa yako kupitia uwekezaji katika hisa na kuondoa hatari ya kupoteza pesa yako kuna vitu vya kuzingatia.
Jinsi ya kuzuia hatari ya kupata hasara kupitia uwekezaji katika hisa
1) Wekeza katika kampuni ambayo inafanya vizuri
Ili kuondoa hatari ya kupoteza pesa yako kupitia uwekezaji katika hisa ni kuwekeza katika kampuni ambazo zinafanya vizuri. Kuwekeza kwa kampuni ambazo zinafanya vizuri ni rahisi kukuza mtaji wako na kupata gawio lako. Katika somo lililopita tumeona jinsi ya kuchagua kampuni ambayo inafanya vizuri, kwa hiyo ni vizuri kwa mwekezaji kuwekeza katika kampuni ambayo inafanya vizuri.
SOMA; Kila Sehemu Utakayokwenda Utawakuta Watu Hawa.
2) Wekeza kwa muda mrefu
Unapoamua kuwekeza katika hisa ni vizuri ukawa na malengo ya kuwekeza kwa muda mrefu. Uwekezaji wa muda mrefu una manufaa makubwa kwa mwekezaji na unapunguza hatari ya kupata hasara. Huwezi ukawekeza kwa mwezi mmoja na ukasema wewe ni mwekezaji bali wewe ni mtu ambaye anabahatisha au mtu ambaye ana Bet. Kuonyesha jinsi gani kuwekeza kwa muda mrefu kuna manufaa kuna moja wa msomaji katika blogu yangu ya www.wekezamtanzania.blogspot.com alikiri kuwa alinunua hisa za kampuni ya SWIS mwaka 2013 kwa bei ya shilingi 2000 na mpaka sasa hisa za kampuni ya SWIS zinauzwa kwa shilingi 6,500. Bei ya hisa imeongezeka mara tatu ya bei ya mwanzo, kuwa na malengo ya kuwekeza kwa muda mrefu kuna manufaa makubwa kwa mwekezaji.
SOMA; BIASHARA LEO; Fukuza Wateja Hawa, Ni Mzigo Kwako.
3) Wekeza kampuni zaidi ya moja
Njia nzuri ya kulinda na kukuza uwekezaji wako ni kuwekeza kwenye kampuni zaidi ya moja katika soko la hisa. Ukiwekeza kwenye kampuni tatu au zaidi ikiwa kampuni moja haitofanya vizuri utafidiwa na ukuaji mzuri wa kampuni nyingine katika soko la Hisa. Hii ni njia mojawapo ambayo ina manufaa makubwa kwa mwekezaji. Ikiwa unataka kuwekeza unaweza ukatenga kiasi cha mwezi wa kwanza unanunua hisa katika kampuni ya SWIS, mwezi mwingine unanunua za CRDB na mwezi unaofuata unanunua za TBL. Au unaweza ukagawa kiasa sawa kwa kampuni ambazo umechagua kuwekeza mfano. SWIS 25%, CRDB 25%, TBL 25% na NMB 25% ni asilimia ishirini na tano ya akiba yako ya kuwekeza.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com/0714445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
SOMA; Haya Ndio Matumizi Mazuri Ya Mshahara Wako Ambayo Yatakuletea Furaha Na Mafanikio.
4/01/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Jinsi Ya Kujijengea Uwezo Wa Kujiamini - 2
Ndugu msomaji karibu tena katika mwendelezo wa makala yangu ya namna ya kujijengea uwezo wa kujiamini. Naamini ulifaidika na machache kati ya mengi ambayo niliyaainisha katika juma lililopita. Nakukaribisha tena tuweze kuongeza ufahamu wetu kupitia jukwaa hili la JIONGEZE UFAHAMU.
Kama hukusoma makala ya wiki iliyopita isome kwa kubonyeza hapa; Jinsi Ya Kujijengea Uwezo Wa Kujiamini.
9. Tabasamu
Ninaposema tabasamu simaanishi kucheka bali ni hali ya kuonyesha bashasha usoni. Si tu kwamba kutabasamu kutaonyesha kwamba unajiamini bali pia huonyesha kwamba wewe ni mtu mwenye siha njema na hujasongwa na mawazo. Kutabasamu kutakusaidia kuonyesha kwamba wewe ni mkarimu. Ni rahisi zaidi kuwasiliana na mtu aliyetabasamu kuliko kinyume chake. Mtu kutokutabasamu inatuma ujumbe kwa watu kuwa yawezekana yeye hajiamini, mwoga au ana hasira na wakati mwingine husababisha mawasiliano yao na watu wengine kuwa magumu.
10. Mtazame unayeongea naye.
Hili tatizo la kushindwa kumtazama unayezungumza naye usoni linawakabili watu wengi, pengine mimi na wewe. Kumtazama unayeongea naye usoni huweza kutuma ujumbe kwamba uko makini na unayezungumza naye, unajali anachozungumza na kufurahishwa na mazungumzo yake. Pia huonyesha kwamba wewe unajiamini na siyo mwoga. Kumtazama unayezungumza naye haimaanishi kumkodolea macho muda wote kwani unaweza kumfanya akose kujiamini. Jifunze tabia hii kwani wataalamu husema kwamba macho ni lango la moyo na kupitia machoni unaweza kugundua mengi ikiwemo kujua kwamba yanayozungumzwa na msemaji ni ya kweli au uongo. Kumbuka kila mtu ana tabia ya kuona haya/aibu lakini inakupasa uishinde kwa mazoezi.
SOMA; Sheria Tatu Muhimu Za Kufanikiwa Kwenye Maisha.
11. Jiweke katika hali ya kutoogopwa
Jifunze kujiweka katika hali ya kufanya watu wawe rahisi kuzungumza na wewe. Kuna watu wamejitengenezea mazingira ya kuonyesha kwamba hawako tayari kuzungumza na watu. Watu hawa hujifanya kwamba wanatumia sana simu zao kwa kuongea ama ujumbe mfupi na mengine yanayofanana na hayo. Pia usipende kuzungusha miguu wala mikono yako kwani unatuma ujumbe kwamba hauko tayari kuzungumza. Kumbuka lugha ya alama huzungumza yaliyo ndani mwako hivyo chukua tahadhari. Ulivyo kwa nje inasadifu ulivyo kwa ndani.
12. Fahamu vipaji vyako
Kuna wakati ambao unaweza kujijisikia kukosa thamani. Katika kipindi hiki chukua kalamu na karatasi na uandike kuhusu vipaji vyako na vyote vizuri ulivyowahi kuvifanya. Achana na mabaya ama vitu ambavyo vitakufanya ujidharau. Kumbuka pongezi ulizowahi kupewa na ndugu, jamaa na hata marafiki. Jaribu kusahau mabaya yaliyosemwa juu yako na watu kwani hayana nafasi katika maisha yako. Kumbuka hata ukiwa mfano mbaya watu wengine wanaweza kujifunza kwa mfano wako. Kumbuka kuwa kama vile wewe usivyo mkamilifu ndivyo na watu wengine wasivyo. Fanyia kazi vipaji vyako na punguza au ondoa kabisa mabaya yako na kwa hali hii utakuwa mtu mwenye kujiamini sana. Kumbuka kujiambia kuwa wewe ni mshindi siku zote na acha kujihukumu.
SOMA; Haya Ndio Mambo Matatu Yatakayokuletea Matokeo Ya Kushangaza.
13. Kumbuka ulizaliwa ukijiamini
Unakumbuka ulipokuwa mtoto mchanga? Kipindi hicho ulikuwa mwenye kujiamini na ulifanya vitu uliyoona wewe vinafaa. Ulilia, ulitambaa, ulicheza na mengi kadhalika bila kumwogopa yeyote. Lengo langu kukumbusha haya ni ujue kuwa kutokujiamini kwako kumetokana na kuhukumiwa na watu na kunyooshewa vidole kila ulipokwenda. Lakini lililo jema zaidi ni kwamba kila mtu huja duniani bila kitu na hujifunza vyote hapa duniani. Kama vyote uliweza kujifunza unaweza pia kujifunza kujiamini na kuacha ama kusahau kutokujiamini.
14. Sio tatizo lako peke yako
Kuna msemo unasema kifo cha wengi ni harusi. Msemo huu unakusaidia kujua kuwa kila mtu hukabiliwa na matatizo kama wewe. Tatizo la kujiamini ni la dunia nzima. Kila mtu hukabiliwa na tatizo hili ila wengine wamejifunza kulishinda tatizo hilo na kulificha kwenye macho ya jamii. Kiukweli kila mtu huwa jambo analojiamini kwayo na yapo mengine mengi ambayo wanashindwa kujiamini. La muhimu zaidi acha kujifananisha na watu wengine kwani haya ni maisha yako na hupaswi kuwa sawa na mtu fulani. Hupaswi kuwa sahihi zaidi, mjanja zaidi ama mzuri zaidi bali kuwa mwenye furaha zaidi. Kumbuka kuwa kuweza kujiamini si suala la siku moja na huhitaji muda zaidi. Kuna siku waweza kushindwa lakini usife moyo, jaribu tena na tena.
SOMA; Hizi Ndizo Gharama Unazotakiwa Kuzilipia, Ili Uweze Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako.
15. Saidia wengine
Kusaidia watu wengine kutakuongezea uwezo wa kujiamini zaidi. Saidia pale unapoweza, pongeza panapostahili na punguza kuhukumu wengine. Kama kuna mtu anahitaji msaada wako jaribu kumsaidia hata kama hajakuomba kwani kuna watu wengine ni waoga wa kuomba msaada. Hii itakusaidia kujiamini, kujenga urafiki na pia kufungua milango ya wewe kusaidiwa kwani kadiri unavyotoa ndivyo unavyopokea. Utajisikia vizuri sana pale utakapojua kuwa Fulani kafanikiwa kwa sababu yangu pia.
16. Achana na wanakufanya ukose kujiamini.
Kuna watu katika hii dunia hupenda kuhukumu wengine kwa kila jambo walifanyalo liwe zuri au baya. Watu wa namna hii kaa nao mbali kwani siku zote utakuwa mdogo tu kwao na hutaweza kujiamini. Hawa hutafuta makosa na mapungufu yako siku zote. Kaa nao mbali kama wenye ugonjwa wa ebola lakini si kuwachukia. Chagua marafiki ambao watakufanya ujisikie vizuri katika ubora wako. Tabia na mafanikio yako huchangiwa kwa kiasi kikubwa na watu unatumia nao muda wako mwingi.
SOMA; Haya Ndio Matumizi Mazuri Ya Mshahara Wako Ambayo Yatakuletea Furaha Na Mafanikio.
17. Ongea na watu wageni kwako
Kujiamini ni zaidi ya kusoma ama kujifunza kupitia vitabu na makala, hii ni tabia ambayo hujifunzwa. Jifunze kuongea na watu wageni usoni kwako kwani huwezi kujua ni wapi utawahitaji. Itakuwia vigumu mwanzoni lakini baadaye utazoea kadiri siku zinavyokwenda na kadiri unavyoongea na wageni. Kuongea na watu usiowafahamu pia ni ukarimu.
18. Tegemea mafanikio
Katika kila jambo unalofanya tegemea mafanikio. Watu wengi sana hushindwa jambo kabla ya kulijaribu, kwa maana nyingine hushindwa mchezo nje ya uwanja. Ukitegemea kushindwa hutaweza kulifanya jambo kwa jitihada kwani huwezi kwenda mbali zaidi ya unavyowaza. Hivyo basi katika kujiamini amini pia kwamba inawezekana. Inawezekana anza sasa, usiahirishe kwani kamwe hutafanya ama utafanya katika hali ya taharuki.
Asante kwa kuuungana nami katika makala hii, tupo pamoja.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes ambae ni mjasirimali na mhamasishaji.
Unaweza kuwasiliana na naye kwa: simu: 0712 843030/0753 843030
e-mail: nmyohanes@gmail.com Pia unaweza kutembelea blogu yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.
3/31/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments