Fursa katika Kilimo cha Bustani

Habari msomaji wa makala za kilimo katika jukwaa hili la JIONGEZE UFAHAMU. Wiki hii tutajiongezea ufahamu kuhusu kilimo cha bustani kwa ufupi. Ila kwa wiki zinazokuja tutaingia kwa kina na tutaenda hadi kuchambua kilimo cha baadhi ya mazao, kuanzia uzalishaji hadi soko lake.

Karibu kwenye somo:

Kilimo cha bustani ni sekta ndogo iliyopo ndani ya sekta ya kilimo na ndio inayokua kwa kasi zaidi kuliko sekta ndogo yeyote ya kilimo. Tunaposema kilimo cha bustani tunamaanisha kilimo cha mbogamboga, matunda, maua pamoja na viungo (spices). Kilimo cha bustani ni kilimo ambacho kinalimwa na wakulima wadogo kwa asilimia kubwa, japokuwa upo uwekezaji mkubwa na uwekezaji wa kati ambao unakua kwa kasi pia. Ukweli ni kwamba mazao ya bustani ndio mazao yanayotumika sana kuliko mazao mengine. Huwezi kukwepa kutumia mazao ya bustani, haiwezi kupita siku hujatumia tunda, au mbogambogakama nyanya, kitunguu, mboga za majani, au viungo kama tangawizi, mdalasini, hiliki, karafuu, nazi n.k Pamoja na hayo lakini bado kilimo hichi hatujaweza kufikia kile kiwango cha uwezo wetu. Kutokana na rasilimali ardhi na hali ya hewa nzuri Tanzania inao uwezo wa kuzalisha mazao ya bustani mara 10 zaidi ya jirani zetu Kenya lakini pamoja na hayo yote wenzetu wanazalisha na kuuza nje ya nchi mara 10 zaidi yetu. Hii ni kwasababu kwanza wamegundua fursa iliyopo, wakaamua kutumia teknolojia na mbinu za ki leo katika kilimo, pia wanaongeza thamani ya mazao yenyewe kama kuweka katika madaraja na kuweka kwenye vifungashio. Kitu kingine kikubwa ni kwamba wenzetu wako vizuri sana katika masoko, wachangamfu sana katika kujitangaza na wanajua mbinu mbalimbali za kuteka soko kitu ambacho sisi hatuna. Sisi tunasubiri mteja aje atufuate wakati wenzetu wanalifuata soko.

SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo - 2

Kilimo cha Bustani Duniani

Katika dunia kilimo cha bustani kinakua kwa wastani wa 13% kwa mwaka, kikitegemea masoko ya ndani ya nchi, masoko ya kikanda pamoja na masoko ya kimataifa.Masoko makubwa ya mazao ya bustani ni Marekani, Urusi, India, nchi za Falme za Kiarabu pamoja na nchi za Ulaya. Changamoto ya kwenye soko la kimataifa ni kwamba wanazingatia sana ubora, na zipo taasisi kwa ajili ya kuthibitisha ubora tokea ilipozalishwa mpaka zao linapomfikia mlaji. Taasisi hizo ni kama Global GAP, BRC n.k. Changamoto hii imekua ikiwaathiri zaidi wakulima wadogo maana wanashindwa kukidhi viwango, lakini pia wakulima wadogo hawana uzalishaji endelevu. Mfano kama soko la Urusi unatakiwa kupeleka tani 200 za matunda au mboga kila wiki, wakulima wadogo inawawia changamoto maana yeye anafikiria azalishe akivuna ndioaanze tena kuandaa shamba kupanda tena. Wakati anaandaa shamba kwa ajili msimu unaofuata hana cha kuuza. Kwahiyo panahitajika mifumo ya uzalishaji ambayo inaweza kulihudumia soko katika hali endelevu. Pamoja na kwamba ni changamoto lakini kwa wengine imekua fursa, zipo kampuni zilianzishwa kupitia fursa hii, wao wanachokifanya wanatafuta hayo masoko kama ya Ulaya, Afrika kusini na kwingineko, na wanakua na vigezo vinavyohitajika kwenye soko. Halafu wanaingia mikataba na wakulima wadogo, wakulima wanazalisha kampuni inanunua na kwenda kuongeza thamani, kwa kuweka kwenye madaraja, kuweka kwenye vifungashio na wanauza kwenye hayo masoko.

SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.

Kilimo cha Bustani Tanzania

Hapa Tanzania kwa miaka mitano iliyopita kilimo cha bustani kimekua kikiongezeka kwa asilimia 6 hadi 10 kwa mwaka. Maeneo ya nyanda za juu kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Manyara) ndiyo yanayoongoza kwa uzalishaji wa mazao mengi ya bustani. Yapo pia maeneo mengineyanayofaa kwa kilimo hichi kama ukanda wa pwani, nyanda za juu kusini (Mbeya na Katavi), Nyanda za ziwa (Mwanza, Geita, Mara, Kagera n.k) pamoja na nyanda za kati (Dodoma - maarufu kwa kilimo cha Zabibu). Ukichunguza kila kanda in uwanja wa ndege hivyo kuwepo kwa fursa ya kuuza nje ya nchi. Kuna viwanja vya ndege kama Songwe - Mbeya, KIA –Kilimanjaro, Uwanja wa ndege Mwanza, Uwanja wa ndege JK Nyerere .

Katika nchi yetu tuna eneo takribani hekta Milioni 44 (44,000,000)ambalo bado halijatumiwa ipasavyo, kati ya hizo hekta milioni 29 (29,000,000) zinafaa kwa umwagiliaji lakini eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta laki mbili tisini elfu tu (290,000) eneo ambalo ni dogo sana ikilinganishwa na uhalisia wa eneo ambalo linafaa kwa umwagiliaji. Hii ni sawa na asilimia moja tu (1%). Hii ina maana asilimia 99 bado halijafanyiwa kazi.

SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.

Mazao mengi ya bustani unaweza kutumia eneo dogo na ukapata faida zaidi ya mara tatu kama ungezalishia mazao ya nafaka katika eneo lenye ukubwa sawa.

Kuona hilo, wahisani wengi wa miradi ya kilimo kwa wakulima wadogo wamejikita zaidi katika kuhamasisha kilimo cha bustani maana ndio kinachoweza kumkomboa mkulima kwa haraka zaidi.

Hii inatupa ishara kwamba kwa mtu anayetaka kuwekeza kwenye kilimo anashauriwa awekeze kwenye kilimo cha bustani.

Hapa chini nimeweka kiunganishi (link)ya tovuti (website) ya moja ya makampuni yanafanya kilimo cha bustani.Kampuni hii inaitwa StakeAgrobaseInt. Ltd (SAIL) na inamilikiwa na Mtanzania mwenzetu. Mwanzilishi wa kampuni hii alikua daktari wa hospitali ya mkoa, yeye aliona fursa akaichangamkia sasa hivi yuko mbali sana.

Stake AgrobaseInt. Ltd (SAIL)http://www.sailfv.com/aboutus.php

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email)daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Makala Imehaririwa kwa Kiswahili sanifu na Rumishael Peter wasiliana nae kuhariri kitabu au Makala email:rumishaelnjau@gmail.com simu: +255-713-683422http://rumishaelnjau.wix.com/editor

0 comments: