Njia KUMI Za Kubana Matumizi Yako Mwaka Huu 2015.

Kama kila siku una matatizo ya fedha, na karibu kila mtu ana matatizo haya, huenda kuna mambo mawili unayoyafanya kimakosa sana.

Jambo la kwanza kipato chako ni kidogo.

Jambo la pili matumizi yako yanazidi kipato chako.

Leo tutajadili jambo la pili na siku nyingine tutajadili jambo la kwanza. Hiyo endelea kutembelea mtandao huu wa JIONGEZE UFAHAMU ili uweze kujifunza mambo hayo mazuri ambayo yataboresha maisha yako.

Ili kuweza kurudisha usimamizi mzuri kwenye fedha zako, hatua ya kwanza kabisa ni kubana matumizi. Unaweza kufikiri kwa nini hatujaanza kujadili kuongeza kipato, ila kama utaongez akipato kwa tabia uliyonayo ya matumizi mabovu bado utarudi pale pale.

Leo tubane kwanz ama matumizi halafu kwenye makala ijayo tutaongeza kipato.

Zifuatazo ni njia kumi za kubana matumizi kwa mwaka huu 2015.

1. Tengeneza bajeti. Bajeti yako ni muhimu na ndio itakayokuongoza kwenye matumizi yako ya fedha. Jua kila mwezi utatumia kiasi gani na gawa kwenye wiki na hata siku. Iheshimu bajeti yako.

2. Nunua vitu kwa jumla. Kama ni vitu vinavyohusiana na matumizi muhimu ya nyumbani nunua kwa jumla. Hii itakufanya ununue kwa bei nzuri na pia kuweza kwenda na bajeti yako.

3. Sitisha huduma ambazo hutumii. Kama kuna huduma umejiunga nazo ambazo hutumii sana sitisha. Hii inaweza kuwa malipo ya kuangalia tv, malipo ya kuhudhuria mazoezi, malipo ya gharama za simu na kadhalika.

4. Usinunue vitu hovyo. Ukikutana na mtu anauza nguo hata kama umeipenda kiasi gani usiinunue kama hukuwa na ratiba hizo.

5. Epuka sana mikopo. Kama kitu sio muhimu sana kwao, usiingie kwenye mkopo ili kukipata, mikopo ni mzigo ambao unakupotezea fedha nyingi.

6. Punguza starehe. Punguza kiasi ambacho unatumia kwenye starehe kama kula kwenye hoteli kubwa, kutumia vilevi, kwenda kwenye kumbi za starehe na kadhalika.

7. Nunua vitu vyenye ubora, hata kama ni ghali. Unaweza kufikiri kununua vitu vya bei rahisi ni kubana matumizi ila ukawa ndio unaongeza matumizi zaidi. Nunua kitu chenye ubora hata kama ni bei ghali, utakaa nacho muda mrefu zaidi na hivyo kuepuka kupoteza fedha kwenye kununua mara kwa mara.

8. Nunua vitu ambavyo unavihitaji kweli na sio unavyotamani. Kwa mfano nguo, nusu ya nguo zako hujazivaa mwaka mmoja uliopita. Sasa unanunua nyingine za nini? Acha kupoteza fedha.

9. Andaa vitu unavyoweza kuandaa mwenyewe badala ya kufikiria kununua tu. Pendelea kupika chakula badala ya kununua chakula kilichopikwa.

10. Acha kutaka kuonekana. Usifanye mambo kwa sababu kila mtu anafanya. Usinunue simu mpya kwa sababu kila mtu ana simu mpya. Fanya kitu ambacho unakitaka kweli na sio kwa sababu kila mtu anakifanya.

Tumia mbinu hizi kumi na uanze kupunguza matumizi yako mwaka huu 2015. Katika makala ijayo tutajadili njia kumi za kuongeza kipato chako mwaka 2015.

Kila la kheri.

0 comments: