Dalili Kumi Kwamba Tayari Wewe Ni Kiongozi.

Kwenye makala zilizopita tumeona ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuwa kiongozi. Pamoja na umuhimu huo sio watu wote ni viongozi na sio watu wote wataweza kuwa viongozi. Na hata ambao ni viongozi sio wote ni viongozi bora wanaotoa matokeo mazuri.

Pia tumejifunza kwamba kiongozi anaweza kuzaliwa au kutengenezwa. Kutegemea na mazingira na uhitaji wa mtu, mtu yeyote anaweza kuendeleza tabia za uongozi ndani yake.

Leo tutaona dalili kumi za sifa ya uongozi. Kama wewe una sifa hizi tayari wewe ni kiongozi na unahitaji kujiendeleza zaidi ili kuweza kufanya makubwa zaidi kwenye uongozi wako. Kama huna dalili hizi kuna habari nzuri na mbaya kwako.

Habari mbaya kwako ni kwamba utaendelea kuwa mfuasi maisha yako yote na kwa nafasi kubwa utashindwa kuonesha uwezo wako wa kweli na kuleta tofauti kubwa kwenye jamii yako na dunia kwa ujumla.

Habari nzuri ni kwamba unaweza kujifunza tabia hizi na ukawa kiongozi bora sana. Uzuri ni kwamba kila kitu unaweza kujifunza, ni utayari wako na juhudi zako ndivyo vitakufanya uweze kujua kile unachotaka kujua. Njia bora ya kujifunza uongozi ni kujua vitu na kuvifanyia kazi. Hutakuwa kiongozi kwa kusoma tu hapa, bali soma na utumie yale unayojifunza kwenye maisha yako ya kila siku.

Kwa kifupi sana naomba nitaje dalili kumi zinazoonesha kwamba wewe ni kiongozi. Kwa maelezo zaidi tunaweza kujadiliana kwenye maoni hapo chini.

1. Unapenda kuleta mabadiliko.

2. Una ndoto kubwa sana mpaka wengine wanaona haziwezekani.

3. Husubiri kuambiwa nini cha kufanya,

4. Unapenda kutatua matatizo yanayowasumbua wengine.

5. Hupendi kulalamika au kulaumu wengine.

6. Unajali sana na kukuza mahusiano.

7. Matendo yako na maneno yako vinaendana.

8. Hukubaliani na mifumo isiyo na tija.

9. Uko tayari kukiri makosa na kuomba radhi.

10. Unapenda kujifunza mambo mapya na kuhusu uongozi.

Kama una dalili hizo kumi hongera wewe ni kiongozi. Kama huna usikate tamaa bado una nafasi kubwa ya kujijengea uongozi.

Uongozi unaanza na kuchagua kuwa kiongozi, baada ya hapo unaendelea kujifunza na kupata uzoefu. Karibu kwenye mafunzo ya kuongozi kupitia blog hii. Ili kuhakikisha hukosi mafunzo haya weka email yako hapo juu kwenye blog ili upate makala hizi moja kwa moja kwenye email yako.

TUKO PAMOJA.

Makosa Makubwa Matano Yanayoweza Kukuharibu Wewe Kama Kiongozi.

Ili uweze kufanikiwa kwenye uongozi kuna mambo muhimu unatakiwa kuwa unafanya na pia kuna mambo mengine unatakiwa kuepuka kufanya.

Katika makala zilizopita tumekuwa tukiangalia mambo muhimu ya kufanya ili kuweza kufanikiwa kwenye uongozi. Ili kuwa kiongozi mzuri ni muhimu kuwa na maono, ushawishi, ushirikiano na uadilifu. Kuwa na mpango mikubwa na kuweza kuwashawishi wengine kuifikia ili kuboresha maisha yako ni tabia moja inayoweza kukutengeneza kuwa kiongozi bora.

Pamoja na hayo kuna mambo ukiyafanya unaweza kuharibu sana uongozi wako bila ya kujali umeutengeneza kwa muda gani. Mambo haya yamekuwa yakifanywa na watu wengi na ndio sababu kubwa ya wao kushindwa kuwa viongozi wazuri. Kwa kuwa wewe unajifunza kuwa kiongozi bora, ni muhimu sana ukayajua mambo haya ili usije kuyafanya na ikakugharimu kwenye maisha yako na uongozi wako.

Hapa nitaongelea makosa kubwa matano unayoweza kufanya yakaharibu kabisa uongozi wako. Makosa hayo ni kama ifuatavyo.

1. Kutaka kupendwa badala ya kuheshimika.

Ni rahisi sana kwa kiongozi kutaka watu wampende yeye kutokana na uongozi wake. Ili kutimiza hilo anajikuta anafanya mambo ya kuwafurahisha watu badala ya kufanya mambo yatakayowasaidia watu. Katika uongozi kuna maamuzi unaweza kufanya watu wasikuelewe kwa sababu wewe una maono, baadae mafanikio yanapoonekana watu hukuheshimu sana kama kiongozi. Ila ukitaka kuwafurahisha watu hutoweza kufanya mambo ya kuwasaidia. Usitake kupendwa na watu bali jenga kuheshimiwa na watu kutokana na maamuzi unayofanya yenye manufaa kwenye maisha yao.

2. Kutochukua ushauri na msaada wa wengine.

Kuna wakati kiongozi anaweza kuona yeye yupo juu ya wengine hivyo ushauri wake ndio sahihi. Pia anafikiri hahitaji msaada wowote kutoka kwa anaowaongoza. Hili ni kosa kubwa sana unaloweza kufanya wewe kama kiongozi. Bila ya kujali ngazi yako ya uongozi ni muhimu sana kuchukua ushauri kwa unaowaongoza. Wakati mwingine kuna mawazo mazuri sana kutoka kwa unaowaongoza, pia unaweza kupata msaada mkubwa kutoka kwa unaowaongoza.

3. Kutokujali na kuendeleza vipaji vya wengine.

Watu unaowaongoza wana vipaji na uwezo mkubwa sana. Kazi yako kama kiongozi ni kuendeleza vipaji hivi ili kuwawezesha kufikia malengo makubwa kwenye maisha yao. Kama kiongozi hutothamini vipaji na uwezo wa watu wako itakuwa vigumu sana kwao kukufuata na hii itaathiri uongozi wako.

4. Kushindwa kupanga majukumu vizuri kwa unaowaongoza.

Kama wewe ni kiongozi wa timu au kikundi ambacho kinatakiwa kukamilisha jukumu fulani ni muhimu sana kila mtu kujua jukumu lake ni nini na anawezaje kulitimiza. Kushindwa kupanga na kueleza vizuri majukumu ya kila mtu ni chanzo kikubwa cha kupungua kwa uzalishaji kwenye maeneo mengi ya kazi. Wewe kama kiongozi hakikisha wafuasi wako wanajua majukumu yao na njia za kuyatimiza.

5. Kushindwa kutoa taarifa kwa watu.

Ni muhimu sana kutoa taarifa kwa wale unaowaongoza. Watu wanataka kujua ni mafanikio kiasi gani yamefikiwa na ni changamoto gani zinawarudisha nyuma. Wewe kama kiongozi unajukumu la kutoa taarifa sahihi na kwa muda sahihi kwa watu unaowaongoza. Hii itawafanya kuwa sehemu ya uongozi wako na kuufurahia.

Kama ukiweza kuepuka mambo haya matano, utafanikiwa sana kwenye uongozi wako. Kumbuka ni muhimu sana kwako kuwa kiongozi kwenye maisha yako. Na unaweza kujifunza kuwa kiongozi bora. Weka email yako hapo juu(kwenye blog) ili kupata makala hizi za mafunzo ya uongozi moja kwa moja kwenye email yako.

Karibu sana.

Siri Kumi za Mafanikio Kwenye Uongozi.

Katika watu wengi wanaopewa nafasi za kuongoza kuna wachache sana ambao wanakuwa ni viongozi bora. Wengine wanaishia kuwa tu na majina ya uongozi ila wanashindwa kufanya mambo makubwa kupitia nafasi zao za uongozi.

Mpaka unasoma hapa naamini unataka kuwa kiongozi bora. Ili uweze kupata mafanikio kwenye uongozi, kuna tabia kumi muhimu unatakiwa kuwa nazo na kuziendeleza. Tabia hizo ziko wazi kabisa ila kutokana na watu wengi kutozipa mkazo zimegeuka na kuwa siri kubwa.

Leo tutazungumzia tabia kumi muhimu za kufanikiwa kwenye uongozi. Tabia hizi zinafanya kazi bila ya kujali wewe ni kiongozi wa aina gani. Uwe ni kiongozi usiyekuwa na cheo, kiongozi wa wananchi, kiongozi wa shughuli zako au hata kiongozi wa maisha yako ni vyema ukaanza kutengeneza na kuendeleza tabia hizi.

1. Mfano.

Ili uweze kufanikiwa kama kiongozi ni lazima uwe mfano bora kwa wale unaowaongoza. Utatengeneza mfano mzuri pale ambapo utakuwa unatenda yale unayohubiri. Lazima wewe uwe wa kwanza kuonesha mwendo ili wafuasi wako nao wafuate. Ile kauli kwamba “fuata maneno yangu, usifuate matendo yangu” imesababisha watu wengi sana kushindwa kwenye uongozi. Watu wanapenda kumfuata na kumheshimu mtu ambae anaonesha mfano wa vitendo kwao.

2. Nguvu,

Mafanikio katika uongozi yanategemea sana nguvu ya kiongozi. Naposema nguvu simaanishi nguvu za kimwili pekee bali hata nguvu za kihisia, nguvu za kiakili na nguvu za kiimani. Kiongozi unapokuwa na nguvu hizi inakuwa rahisi kuzitoa kwa wale unaowaongoza.

3. Shauku.

Viongozi wanaofanikiwa sana ni wale wenye shauku kubwa kwenye kazi zao na kwenye maendeleo ya watu wanaowaongoza. Kwa kuwa na shauku kunawafanya wafanye mambo bora zaidi. Pia shauku inaambukizwa mpaka kwa wafuasi.

4. Uvumilivu.

Bila ya uvumilivu huwezi kuwa kiongozi bora, hakuna zaidi ya hapo. Viongozi wengi waliofanikiwa sana walipitia mambo magumu sana kwenye maisha yao. Hata wewe utapitia mambo magumu sana kwenye uongozi wako na maisha yako kwa ujumla. Kuna wakati utashindwa, kuna wakati utakosea sana, tumia nyakati hizi ngumu kujijenga na kuwa imara. Unapovumilia na kuvuka nyakati hizi ngumu unatoa imani kubwa kwa wafuasi wako.

5. Uelewa wa kihisia.

Hisia ni moja ya vitu vinavyoweza kumjenga kiongozi au kumbomoa ndani ya muda mfupi sana. Ili kuwa kiongozi bora ni lazima uzijue hisia zako na ujue ni jinsi gani ya kuzimiliki. Usikubali hisia zako zikutawale mwishowe uanze kufanya mambo yatakayoharibu sifa zako. Pia ni muhimu kuweza kusikiliza na kuelewa hisia za wafuasi wako na kuweza kuwasaidia kupata mtazamo sahihi.

6. Uwezeshaji.

Kiongozi bora ni yule anayewawezesha wafuasi wake kuchukua hatua na kufanya mabadiliko kwenye kazi zao na maisha yao. Katika uwezeshaji kiongozi anawapa watu nguvu na mamlaka ya kufanya mambo ambayo yatakuwa na manufaa kwenye maisha yao. Unapowawezesha watu kuchukua hatua, unawajengea ujasiri ambao baadae utawapelekea kuwa viongozi bora.

7. Ufanisi.

Viongozi bora huwa na ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu yao. Katika ufanisi viongozi huwa na mipango mizuri ambayo itawasaidia kufikia malengo waliyojiwekea. Viongozi bora hufanya jambo sahihi na sio kufanya jambo kwa usahihi. Uongozi bora unapimwa kutokana na majibu anayozalisha kiongozi na sio kwa hotuba nzuri.

8. Kuchukua hatua.

Viongozi bora wanajua ni wapi walipo na pia wanajua ni wapi wanataka kwenda na huchukua hatua mara moja ili kufika wanakotaka kwenda. Hapa ndipo viongozi wanapobadili maono kuwa uhalisia. Kama kiongozi una ahadi na maneno mengi mazuri ila huwezi kuchukua hatua ya kuyatekeleza hufai kuwa kiongozi bali muigizaji.

9. Mafanikio.

Mafanikio ni nguzo muhimu sana kwa viongozi waliofanikiwa. Kiongozi lazima awe amefanikiwa kwenye shughuli zake ili aweze kupata wafuasi wanaotaka kufanikiwa kama yeye. Viongozi bora hupanga kuwa bora kwenye shughuli zao na hivyo kukazana kila siku kutoa majibu yenye ubora.

10. Maadili.

Tabia hii imekuja mwisho ila ilipaswa kuwa ya kwanza kabisa. Huwezi kufanikiwa kwenye uongozi wa aina yeyote ile kama huna maadili. Watu wanapenda kumfuata mtu ambaye anajiheshimu na hivyo kuamini atawaheshimu. Kama kiongozi una skendo chafu ni vigumu sana watu kukupa imani ya kweli kutoka ndani ya mioyo yao. Tatizo kubwa tunalolipata kwenye uongozi hapa Tanzania ni maadili mabovu ya viongozi. Kuwa kiongozi wa mfano kwa kuwa na maadili mazuri kwenye maisha yako.

Kwa kujijengea na kuendeleza sifa hizo kumi utajijenga kama kiongozi wa mfano na mwenye mafanikio makubwa sana. Kumbuka wewe ni kiongozi, hivyo endeleza uongozi wako ili uweze kuwasaidia watu wengi zaidi.

Kama una jambo lolote unaona ni zuri kutushirikisha tafadhali weka maoni yako hapo chini. Kwa kuweka maoni yako hapo chini ni dalili nzuri kwamba unaelekea kuwa kiongozi bora na wa mfano.

Karibu kiongozi tujadiliane yaliyo mema kwenye uongozi.