Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.

Kuna watu ambao wangetamani kuwa wajasiriamali. Wanapoona mafanikio ya wajasiriamali wakubwa wanatamani sana kama wangekuwa wao.

Hijalishi unatamani kiasi gani kuwa mjasiriamali, tamaa yako tu haitakuwezesha kufikia mafanikio katika ujasiriamali. Ni lazima uwe na misingi ambayo utaisimamia ndio uweze kuona mafanikio makubw akupitia ujasiriamali.

Kwanza ni lazima uondoke kwenye kutamani na uingie kufanya na ukishaingia kufanya uwe tayari kukabiliana na lolote litakalojitokeza mbele yako.

SOMA; Maswali Matatu Muhimu Ya Kujiuliza Kwenye Wazo Lako La Biashara.

Leo hapa UTAJIONGEZA na vitu vitano muhimu vya kufanya unapokuwa tayari kuingia kwenye ujasiriamali.

1. Usianze tena kujishuku.

Ukishaamua kwamba wewe umechagua njia ya ujasiriamali, sahau kuhusu kujishuku na kuanza kuwa na wasi wasi kama kweli utaweza. Kikubwa ni nia yako ya kufikia mafanikio kupitia ujasiriamali. Matatizo, changamoto na vikwazo kila mtu anavipitia. Hivyo acha kuwa na wasi wasi kama utaweza na jitoe kwa asilimia 100 kufanya kile ambacho umeamua kufanya.

Kwenye ujasiriamali hakuna kujaribu, kuna kufanya. Fanya sasa na ondoa wasi wasi na hofu.

SOMA; SIRI YA 20 YA MAFANIKIO; Iendee Dhahabu...

2. Kuwa na mshauri.

Kuna ushauri wa bure ambao unapatikana kila mahali kwenye maisha yetu ya kitanzania. Ushauri kama, biashara fulani inalipa kweli yani, ukianza kuifanya tu, utapata mafanikio makubwa. Ukimuangalia anayekupa ushauri huo nae amesikia kwamba biashara hiyo inalipa.

Sasa hawa sio washauri ambao nakuambia uwe nao. Nakuambia uwe na mshauri ambaye anaelewa ni nini hasa anachokuambia. Mtu ambaye amekuwa kwenye safari ya ujasiriamali na anaujua ugumu wa safari hiyo. Mtu ambaye hatakuwa mnafiki kwako kukuambia mambo ili tu kukupa moyo na kukufurahisha, bali atakuambia ukweli, na ukweli huu utakufanya uweze kutumia mazingira yako vizuri kufikia mafanikio.

SOMA; UKURASA WA 43; Ushauri Wa Bure Una Gharama Kubwa.

3. Jitengenezee utaratibu wako wa kila siku, ambao utauheshimu.

Tofauti ya ujasiriamali na kazi zingine ni kwamba kwenye ujasiriamali wewe unajiongoza mwenyewe. Hakuna atakayekugombeza au kukutishia kukufukuza kazi kama utakuwa mzembe. Na hii ni hatari kubwa sana kwa sababu kama huwezi kujiongoza mwenyewe utashindwa kwenye ujasiriamali.

Njia rahisi ya kuweza kuanza kujiongoza mwenyewe ni kuwa na utaratibu wako wa kila siku ambao utaufuata na kuuheshimu. Ipangilie siku yako kabla hujaianza na weka vipaumbele kwenye malengo na mipango yako kwenye maisha na kupitia ujasiriamali unaofanya.

4. Acha kukaa na watu ambao wanakurusisha nyuma.

Tumeshajadili hili mara nyingi sana kwamba wewe ni wastani wa watu watano ambao wanakuzunguka. Hivyo kama umezungukwa na watu watano ambao hawana malengo yoyote kwenye maisha yako, ni vigumu sana wewe kuweka malengo na kuyasimamia. Hivyo wewe unapoamua kuingia kwenye ujasiriamali usikubali kukaa tena na watu ambao mawazo yao yanakurudisha wewe nyuma. Wewe unajua kwamba kwenye ujasiriamali, hasa wakati wa mwanzo unaweza kujikuta unafanya kazi mpaka masaa 16 au 20 kwa siku, lakini rafiki zako wanataka kila siku jioni mkutane mkipata moja moto na moja baridi, hii hutaiweza wewe kama mjasiriamali, niamini.

SOMA; UKURASA WA 11; Watu Hawa Wanakurudisha Nyuma.

5. Kuza mtandao wako.

Tumesema sana hili pia, haijalishi unajua nini bali unamjua nani. Unapoamua kuingia kwenye ujasiriamali hakikisha kila mtu anayehusika na aina ya ujasiriamali unaofanya anajua kuhusu wewe na kile unachofanya. Angalia watu muhimu ambao unahitaji ushirikiano wao, watafute, angalia ni jinsi gani unaweza kuwasaidia ili nao wakusaidie, kukua zaidi.

Kama unafikiri kwenye ujasiriamali utashinda kwa jeshi la mtu mmoja umepotea njia, ongea na watu wengi uwezavyo, wajue unachofanya na wao watakuunganisha na watu wengi zaidi.

Haya ndio mambo matano muhimu sana ya wewe kufanya pale unapoamua kwamba ujasiriamali ndio maisha yako. Na miaka sio mingi kila mtu atahitaji kuwa mjasiriamali, hivyo ni vyema kama utaanz akujiandaa mapema.

Kwa ushauri wowote kuhusu biashara na ujasiriamali tafadhali tuma email kwenda ushauri@kisimachamaarifa.co.tz

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio kupitia ujasiriamali.

TUPO PAMOJA.

Makirita AMANI 

0 comments: