Haya Ndio Makundi Matatu Ya Watu, Je Wewe Upo Katika Kundi Lipi?



Kuna watu wa aina mbalimbali ambao huwa tunaonana nao na kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kila siku. Watu hawa tunaonana nao barabarani, ndugu katika familia, wafanyakazi wenzetu, waumini wenzetu, marafiki na majirani pia.
Watu hawa haijalishi jinsia ya kiume au ya kike, umri wao au rangi zao, wamegawanyika katika makundi matatu.
Wale wanaoona au wanaosikia unachofanya lakini wasielewe, wale wanasikia unachosema au wanaoona unachofanya wakakukatisha tamaa, na wale wanaoona nakusikia unachofanya wakakutia moyo.
WASIOELEWA
Hawa husikia unachofanya na huwa hawana maoni yoyote juu ya kile kinachoendelea. Hawawezi kukubishia wala kukuunga mkono. Wao husubiri tu kuona hatua inayofuatia. Inawezekana kabisa huwaza juu ya kushinda au kushindwa kwako. Lakini hawawezi kutoa maoni yoyote zaidi ya kusubiri kuona tukio linalofuatia.
WANAOKATISHA TAMAA
Hawa kwa namna moja au nyingine huelewa kile unachofanya , lakini mara nyingi watakuambia maneno ambayo hayakupi moyo wa kuendelea kufanya kile unachokusudia kufanya. Wao hutoa mifano ya watu walioshindwa katika jambo ambalo unalifanya na kukuogopesha kabisa. Mara nyingi watu hawa huwa hawajafinikiwa pia. Hivyo sifa ya watu hawa ni kwamba wao pia hawafamu njia au mbinu zinazoweza kukusaidia kufanikiwa katika kitu unachokifanya, hivyo ushauri watakaokupa unatokana na uzoefu walionao katika vitu walivyowahi kufanya
Mara nyingi watu hawa huamini kuwa wale waliofanikiwa katika eneo hilo walikuwa na bahati au wana uwezo fulani hivi ambao wamepewa na Mungu hivyo si rahisi mtu mwingine kufanikiwa kama wale wenye uwezo huo. Imani yao hiyo ni njia ya wao kujilinda ili kuonyesha kuwa katika juhudi zao hakuna makosa waliyoyafanya ila kuna nguvu tu za ajabu ambazo wengine wanazo na wao hawana ndio zilizotofautisha kufanikiwa kwa wengine na kushindwa kwao.
Ukiwasikiliza na kuwaamini watu hawa lazima utafanana nao na hautaweza kufanya mambo makubwa kwa imani kuwa kuna aina ya watu wamezaliwa kufanya mambo makubwa na wanabahati hiyo.
WANAOTIA MOYO
Watu hawa hukupa mawazo ya matumaini katika jambo ambalo unakusudia kulifanya. Wao hukuelekeza pale unapokosea na kukupa moyo kuongeza juhudi zaidi. Huwa wakweli kama kuna kitu ambacho hufanyi vizuri watakuambia na kukuelekeza namna ya kukiboresha. Au wanaweza kuona kitu ambacho ungefanya vizuri zaidi na wakakuambia kutokana na vipaji walivyoona ndani yako.
Watu hawa mara nyingi huwa ni wale wenye mafanikio na ukikaa na watu hawa kutokana na ushauri wao na mawazo yao utajikuta ukifanana nao na wewe pia kuwa na mafanikio kwani hakuna wakati watakuvunja moyo.
NINI UNATAKIWA UFANYE
Ingawa kuna aina hizi za watu ni vizuri kuamua wewe ungependa kuwa katika kundi gani. Kundi zuri ni hili la kutia moyo kwani kwa kufanya hivi hata wewe mwenyewe huwezi kujikatisha tamaa. Kama unakatisha tama wengine ni vigumu hata wewe kujipa moyo pale mambo yanapokuwa magumu.  Ni vigumu kuendelea mbele hata pale unapokutana na changamoto ndogo.
Ni vizuri kuwa karibu na watu wanaotia moyo na wenye ndoto za kufanikiwa lakini cha kwanza ni wewe kuwa na mawazo chanya , kuwa mvumilivu na kujipa moyo ili kufikia kiwango kile unachotaka katika eneo lolote lile. Kwa kufanya hivyo sio rahisi mtu mwingine akakurudisha nyuma hata kama changamoto zitakuwa nyingi kiasi gani.

Nakutakia utekelezaji mwema wa haya uliyojifunza.
Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com





Jinsi ya Kuwaandaa Kuongoza Viongozi Watarajiwa (Chipukizi)

Habari na karibu ndugu mpenzi msomaji wa blogu hii ya JIONGEZE UFAHAMU. Ni matumaini yetu umekuwa na wiki ya mafanikio sana.
Leo nitazungumzia namna ya kuwaandaa watu wenye sifa za uongozi ambao umewatambua upo nao katika timu yako katika taasisi. Kuwaandaa viongozi hawa watarajiwa kunahusisha wewe ambaye tayari ni kiongozi pamoja na hao viongozi watarajiwa , nah ii inaweza kulinganishwa kwa kiasi Fulani kama unawawapatia mafunzo.

1.     Tengeneza Mahusiano na Viongozi Chipukizi Unaowaandaa
Viongozi chipukizi ambao umeshawatambua unahitaji kuwafahamu, kuwasikiliza historia za maisha yao ili uweze kuwajua zaidi ya vile unavowajua tu kiofisi. Huhitaji kujua kuhusu uwezo au ubora wao tu bali unahitaji pia kujua kuhusu madhaifu yao pia ili uweze kujua namna ya kuwafanya wakamilifu kwa hayo mapungufu uliyoyatambua. Na ukiweza kujenga mahusiano mazuri maanake utafanya wakupende na pia kuongeza nia na kiu kwao kujifunza kutoka kwako

SOMA; Hatua 6 za Kuwalea Viongozi Watarajiwa (Chipukizi)


2.     Washirikishe ndoto yako
Wakati unaendelea kuwafahamu usiwaache wao peke yao tu wakuambie ya kwao, na wewe pia unahitaji kuwashirikisha pi historia ya maisha yako na unahitaji kwenda hatua ya ziada kwa kuwashirikisha ndoto yako kuhusiana na taasisi ambayo unaiongoza. Na hii itawasaidia kujua ni wapi unataka kwenda na hivo kujiunga kujitoa kufuatana nawe mpaka mwisho wa safari yako
3.     Waombe utayari wao kujitoa kiuongozi
Moja ya kiungo muhimu ambacho kinaweza kumfanya kiongozi chipukizi kuwa kiongozi mwenye mafanikio, ni utayari wa kujitolea kiuongozi. Ni muhimu sana kwa hawa viongozi chipukizi unaowaandaa wawe wamejitoa kwa ajili ya uongozi pamoja na taasisi. Na unahitaji kuwaeleza gharama ambayo itawachukua kwa wao kuwa viongozi, na jambo la muhimu ni uwe mkweli kuhusu mambo ambayo watahitaji kuzingatia au kuyajua hata kabla ya hatua yenyewe ya kufanya maamuzi ya kukubali kuweza kujitoa kiuongozi.
4.     Weka malengo kwa ajili ya ukuaji
Viongozi hawa chipukizi wanahitaji kujua malengo yaliyo fasaha ambayo wanatakiwa kuyapigania au kuyafanikisha, nah ii itawasaidia kujua ni nini wnatakiwa kufanya na pia ni vitu gani vinatarajiwa kutoka kwao. Jambo muhimu zaid la kuzingatia ni unapoweka malengo zingatia malengo yawe yako wazi, fasaha na yanayoeleweka. Malengo yawe ni sahihi kwao lakini pia yawe yanaweza kupimika. Baada ya kuyafahamu hayo malengo ni vizuri yawekwe katika maadnishi ili kila mmoja aweze kujitoa kikamilifu katika malengo hayo
5.     Weka mambo ya msingi sawa
Ni muhimu sana kuweka misingi kwa kuwaelewesha majukumu yao na wayafahamu kwa undani. Weka kwa ufasaha mategemeo yako kwao lakini pia na wao wajue vipaumbele ni vipi katika majukumu yao. Na uhakikishe wanaweza kujua tofauti kati ya kazi iliyo ya umuhimu sana na ile kazi yenye umuhimu kiasi.
6.     Mfumo wa ufundishaji unaofaa
Kuna hatua tano muhimu zinazoweza kukupatia matokeo mazuri hasa inapohusisha kuwaandaa kiuongozi viongozi chipukizi
                               i.            Kuwa mfano kwanza kwa kila unachotaka waweze kukifanya
                             ii.            Wafundishi au waelekeze
                          iii.            Simamia maendeleo ya kile unachowaelekeza
                          iv.            Wahamasishe
                             v.            Wape fursa pia ya kutengeneza viongozi kati yao viongozi chipukizi
7.     Simamia maendeleo yao bila kuacha
Ni muhimu ukawa na mikutano iliyo rasmi na isiyo rasmi pia ili kuweza kujua mahitaji, matatizo ambayo wanakumbana nayo pia. Na hii itakusaidia kuwapatia vifaa sahihi zaidi na kuendelea kuwapa ujasiri na kuwahamasisha.

Mwandishi: Goodluck Moshi
Mawasiliano:
Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi
Pia unaweza kutembelea blog yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.

Wajue Watu Hawa Wanaokazana Kukurudisha Nyuma Na Jinsi Ya Kuwashinda.

Kuna watu katika jamii wapo kwa ajili ya kukufanya ushindwe, wapo kusubiri kuona ukiharibikiwa, wanafurahia kupata habari mbaya za kukuhusu, wanakaa kusubiri kuona kwamba umeshindwa kumaliza masomo yako, wanasubiri kuona kwamba hiyo biashara imekushinda, wanasubiri kusikia kuwa umefukuzwa kazi. Lakini tambua hawaishii kutamani hayo tu bali wengi huenda mbali zaidi kwa kuwafuata watu na kuwapa taarifa za mabaya yako hata kama si ya kweli, wengine hata wakisikia mtu anakuongelea vizuri au kukusifia watajitahidi kuonyesha kwamba wewe ni mbaya haustahili sifa hizo, wanaweza kukukosesha hata kazi au mambo mengi ya muhimu.
SOMA; Ukiendelea Na Maisha Haya Watu Watakunyanyasa Sana…
Lakini pia tambua watu hawa wanaweza kuwa ni watu wako wa karibu sana tu, watu wanaokufahamu vyema tu , hivyo wakati mwingine wanakuwa wana uhakika na wanachokisema au kukiongea mbele za watu, wanafurahia kuona mabaya yako yakijulikana nje, wanafurahi kuanika wazi udhaifu wako na wanapofanya hivyo wanasahau kwamba hakuna binadamu aliye mkamilifu, maana kila mwanadamu aliyezaliwa ana madhaifu yake na hata wao kwa kufanya hilo wanasahau kuwa wanaonyesha na kuweka wazi udhaifu wao pia, maana kama wanaweza fanya hayo kwako uliye mtu wao wa karibu je kwa asiye wa karibu hivyo wakati mwingine humfanya hata anayepokea habari hizo kushindwa kuwaamini hata kwa kufanya nao mambo mengine zaidi , maana tayari wanakuwa wameonekana si watu wema.
Kwa kutambua kuwa tuna watu wa aina hiyo, hutakiwi kuwafuatilia sana au kuacha kufanya yale unafanya na kuwaangalia hao na kuwasikiliza. Haijalishi watakuchafua kwa kiasi gani wewe endelea kufanya kile unafanya, ongeza bidii na maarifa katika kufanya hicho unafanya. Nadhani unaufahamu ule msemo unaosema kwamba mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe, hivyo tambua mpaka wakutakie hayo mabaya, mpaka wakufanyie yote hayo tambua kipo kitu cha ziada unacho ambacho wao hawana. Kuna kitu cha thamani wameona ndani yako na wanaona hawawezi kuwa nacho au wanaona kitakufaa sana maishani, hivyo wanatumia kila njia kukufanya ujione mnyonge au uache kufanya hilo jambo. Wanatafuta namna ya kukuhamisha hapo, wanatafuta namna ya kukupoteza ndugu yangu, huenda ni wivu tu unawasumbua , sasa kwanini ukubali au kuruhusu matatizo ya mwingine yakuzuie kuendelea na safari yako? Unajua kwanini unafanya hivyo, unajua kwanini upo hivyo, hiyo inatosha sana, usisubiri kuona kila mtu anakubali unachofanya, usitegemee hilo maana kwanza haliwezi kutokea katika dunia yetu hii, wengi wa watu wamezoea kuona kwamba kuna baadhi ya vitu haviwezi kufanywa na watu wa aina fulani, sasa mtu huyo akiona wewe unafanya hivyo vitu na wakati upo kwenye kundi la wasioweza unafikiri atakuunga mkono? Anaweza kukufanya ushindwe, ujiuone huwezi , anaweza kufanya upoteze dira kama utakuwa hujielewi, kama hujui nini unataka maishani mwako atakupoteza tu. Hivyo wewe kujielewa inakutosha sana.
SOMA; Kitu Pekee Unachoweza Kukidhibiti Kwenye Maisha Yako.
Amua kuishi wewe, kuishi maisha yako, kuishi ndoto yako usisikilize kelele zisizokuhusu, chagua kitu cha kuilisha akili yako, kaa na watu wenye mtazamo sahihi juu ya unachofanya watakupa moyo wa kusonga zaidi, hata pale ambapo huwezi watakutia moyo tu, watatamani kuona unafanikiwa, unaishi ndoto yako, mafanikio yako ni furaha kwao , hawa ndio watu unatakiwa kuwa nao, lakini hao wanaosubiri anguko lako, wanaosubiri uharibikiwe waache hivyo, wamechagua fungu hilo huwezi kuwabadilisha. Ila wanaweza kushangaa jinsi watakavyopoteza muda wao kusubiri anguko lako milele, maana ikiwa unajitambia haitatokea kamwe, maana kelele zao ni kama zinakufanya uzidi kufanikiwa tu maana wewe ndio kwanza unazidi kufanya kazi kwa bidii. Kataa kuwapa sababu ya kucheka, kataa kuwafanya waone walichoksiema kwako ni kweli kwa kukazana kuiishi ndoto yako.
Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu wa Tehama, lakini anaandika makala katika muda wake wa ziada kwa ajili kuelimisha jamii.
Ms.Beatrice Mwaijengo
+255755350772
bberrums@gmail.com

Kitu Kimoja Kinachowatofautisha Waliofanikiwa Na Walioshindwa.

Ndugu msomaji wa Jiongeze Ufahamu nakukaribisha katika Makala yangu ya leo.
Watu wengi wamekuwa wakiota kuhusu mafanikio lakini bahati mbaya ni kwamba wanaofikia mafanikio makubwa ni wachache sana. Waliofanikiwa ni wachache sana kulinganisha na ambao hawajafanikiwa. Kuna watu pia wamekuwa wakiwaza kuhusu njia za mkato za kutoa kufikia mafanikio kama kafara, freemason nk. Lakini ukweli ni kwamba hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa. Kila kitu kina gharama zake ambazo unatakiwa kuzilipia ili ufanikiwe. Gharama za kulipa sio lazima ziwe pesa, hata muda na kujitoa ni gharama kubwa.

SOMA; MUDA–Kitu Chenye Thamani Kubwa Ila Kisichothaminika Na Wengi.
Ngoja nikupeleke moja kwa moja kwenye makala ya leo ya kwamba tatizo hujajipa nafasi. Katika kufikia mafanikio katika maisha ni wajibu wako. Hakuna mtu ambaye atakufikisha kwenye mafanikio kama hujaamua mwenyewe. Ni sawa na kumpeleka punda mtoni anywe maji, kunywa na kutokunywa ni juu yake mwenyewe. Hilo ni sawa na kufanya maamuzi ya maisha yako. Ili kufika huko ni lazima ujipe nafasi. Jipe muda wa kutafakari namna unavyotaka maisha yako yawe baada ya muda fulani. Jenga picha kubwa ambayo wakati mwingine yaweza kuwa ngumu kuifikia. Hii itakufanya ufanye kazi kwa juhudi na maarifa. Tenga muda wa angalau saa zima kutafakari maisha yako na kupanga mipango yako.
Acha kutoa muda kwa watu wengine kwani muda wako ndio maisha yako, ndiyo mafanikio yako pia. Kama muda wako unautumia kuangalia sana filamu, tamthilia, kusoma udaku, kupiga umbea, kutazama sana mpira, mitandao ya kijamii na kadhalika, acha ama punguza kabisa baadhi ya vitu ambavyo sio vya muhimu kwako. Vitu vingi unavyofanya kama vinapoteza muda wako ujue havitaleta mafanikio. Kufanya vitu hivyo nilivyovitaja hapo juu kwa kiwango kikubwa ni sawa na kuwa mtumwa. Vyote unavyovifanya ujue umewapa muda wako watu wengine waweze kufanikiwa.
Kuna mtu mtu mmoja aitwaye TONY GASKINS aliwahi kusema ‘’If you don’t build your dream, someone will hire you to help build theirs’’ (Kama hutaifanyia kazi ndoto yako, watu wengine watakuajiri ili usaidie kufanyia kazi ndoto zao). Ni juu yako kuamua kujenga kwako au kujenga kwa mwenzio. Amua ni kipi unachokitaka, amua leo, amua sasa. Pia acha kuwapa watu kuyatawala maisha yako. Acha kuwapa watu nafasi ya kukufanyia maamuzi. Maisha haya ni yako wewe mwenyewe. Fanya kazi kila siku, jilipe wewe kwanza na kisha wekeza, walipe watu wengine mwishoni na wewe jilipe wa kwanza. Hili litakufanya wewe ufanikiwe. Ukijilipa wa mwisho sahau kuhusu kufanikiwa.
SOMA; Kuna Jambo Moja La Ziada La Kufanya.
Jipe muda wa kujenga afya yako kwani ndio asset uliyo nayo. Ukiwa na afya mbovu hutaweza kufanya kazi wala kuwaza vizuri. Nikisema suala la afya ujue ni neno pana sana. Neno ambalo linajumuisha akili, mwili, mahusiano na kiroho pia. Kama mojawapo kati ya hivyo hakipo sawa huwezi kusema una afya. Tenga muda wa kutosha wa kulala,kumbuka usingizi ni dawa ya akili. Pia tenga muda kila siku wa kufanya mazoezi.

Kumbuka kuwa nafasi ya kufanikiwa ni kubwa sana kama utaamua kujipa muda. Kutenga muda kwa ajili ya maisha yako. Kutenga muda wa kufanya kazi, muda wa kujielimisha na muda wa kujiendeleza. Kumbuka kuwa kujipa muda haimaanishi kwamba uwe mbali na watu wengine wa muhimu kwako kama familia na marafiki. Haimaanishi uache kucheza mchezo unaoupenda wala haimaanishi usipate burudani, la hasha ina maana kwamba ujipe muda wa angalau saa moja katika saa 24 uliyopewa na Mungu. Watu waliofanikiwa wameutumia vizuri muda wao vizuri. Kila mtu ana muda sawa na kila mtu lakini waliofanikiwa wamejipa muda wao, wamejilipa na pia wamefanikiwa.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes
Unaweza kuwasiliana na nae kwa kwa: simu: 0712 843030/0753 843030
e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.

Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu THE ART OF THE START.

Habari rafiki, ni matumaini yangu unaendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu. Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa THE ART OF THE START. Kitabu kimeandikwa na Guy Kawasaki. Kwa ufupi ni kwamba kitabu hiki ni kizuri sana. Kama unayo mpango wa kuanza biashara yeyote hata kuanza kitu chochote, nakwambia kitabu hiki hakijaacha kitu, hupaswi kukosa. Hata wale ambao tayari wapo kwenye biashara kitabu hiki ni zaidi ya “Asset”.

art of start

Kitabu kianelezea mambo mengi sana, kuanzia jinsi ya kutengeneza jina la kampuni yako, jinsi ya kutengeneze mpango biashara (business plan), jinsi ya kupata mtaji kutoka kwa wawekezaji, jinsi ya kuanda presentation, jinsi ya kufanya branding za ukweli, jinsi ya kuwasiliana kwa njia ya email, jinsi ya kuajiri watu wenye uwezo wa kuiinua kampuni yako, jinsi ya kuanzisha ushirikiano wa kibishara (partnering) n.k, hayo ni baadhi tu. Hapa chini nimechukua vitu vichache sana, naona kabisa sijakitendea haki kitabu hiki. Mwishoni nimeweka anwani kwa atakayependa kukipata kitabu hiki nitampatia bure kabisa.

SOMA; Kanuni Sita(6) Muhimu Za Kushinda Tatizo Lolote Unalokutana Nalo.

Karibu tujifunze

1. Katika kutafuta jina la kuipa kampuni unayoanzisha, jaribu kutafuta jina rahisi na fupi ambalo linatamkika vizuri au pia lenye uwezo wa kua kitendo “VERB POTENTIAL." Mfano Google, mtu akitaka kukwambia ukatafute kwenye google, anakwambia …”nenda uka Google. Tengeneza jina ambalo litakua rahisi kutumiwa na watu mbalimbali kama vile wateja, washirika wako pamoja na wawekezaji

2. Ajiri watu wenye uwezo mkubwa kuliko wako na mwenye kuamini kwamba kampuni au shirika lako linaweza kuibadili dunia

3. Kuajiri mtu mwenye uzoefu kutoka kwenye shirika au kampuni kubwa iliyofanikiwa sio kigezo kwamba na kampuni yako inayooanza itafanikiwa. Maana pengine mtu huyo hata hakua na mchango wowote kwenye mafanikio ya shirika hilo lililofanikiwa. Chunguza zaidi

4. Ujasiriamali sio vita. Lengo la biashara yako sio kuua biashara ya mwingine, kuwa chanya.

5. Mjasiriamali sio cheo cha kazi, bali ni hali ya akili/ufahamu wa watu wenye kutaka kuleta mabadiliko

6. Mwanzoni kuelekea kwenye ujasiriamali kila mjasiriamali huogopa. Wewe sio wa kwanza kuogopa, kufanikiwa kwako kutategemea unaikabili vipi hofu hiyo na kuishinda. Bila hivyo utakua mtu wa kusubiri kuanza kesho, na kesho ndo hiyoo unajikuta miaka 60..ukisubiri kesho

7. Wanaofanikiwa sana, hua wana madhaifu makubwa tu. Watu wasio na mapungufu yeyote hua huishia kua watu wa kawaida tu. Maana wale wasiokua na madhaifu huridhika na hali waliyonayo wakiona kua wamekamilika.

8. Shirika au kampuni inafanikiwa kutokana na utekelezaji mzuri na sio mpango mzuri wa biashara. Unaweza kua na business plan nzuri sana, lakini usikufikishe mahali. Hakikisha utekelezaji unakua mzuri.

SOMA; Kitu Pekee Unachoweza Kukidhibiti Kwenye Maisha Yako.

9. Unapofanya ushirikiano wa kibiashara (Business partnership) usifanye ili kufurahisha watu, hakikisha kuna maslahi pande zote (Win-win situation)

10. Haijalishi unajua nini au unamjua nani, bali kinachojalisha ni nani anakujua. Mfano Unaweza ukawa unamjua Reginald mengi, lakini yeye hakujui, uwezekano wa kusaidika ni mdogo.

11. Saidia watu wengi kadri uwezavyo. Msaada wa kweli ni ule ambao unatoa kwa watu ambao hawana uwezo wa kukurudishia msaada baadaye. Na unapomsaidia mtu usitegemee kurudishiwa fadhila, maana ukitegemea kupata kitu baadaye utakua hujasaidia bali unafanya biashara.

12. Unapofanikiwa katika biashara tenga fungu kwa ajili ya kurudisha kwenye jamii, hii ni njia moja wapo ya kujitangaza

13. Sababu kubwa na nzuri ya kuanzisha biashara ni kutengeneza maana, kutengeneza bidhaa au huduma ambazo zitaifanya dunia kua sehemu pazuri zaidi ya mwanzo. Kazi yako ya kwanza ni kuamua ni jinsi gani utakavyo tengeneza maana.

14. Mfumo wa biashara ni muhimu sana. Haijalishi ni biashara kubwa kiasi gani unaanzhisaha, ni lazima uweze kutengeneza njia kutengengeneza pesa. Mfumo mbovu utapelekea biashara kua na maisha mafupi. Katika kufanya hili unahitaji kujiuliza maswali haya muhimu:

· Nani mwenye pesa zako mfukoni mwake?

· Jinsi gani utazichukua pesa hizo kuja mfukoni mwako?

15. Usisubiri mpaka uwe na bidhaa au huduma iliyokamilika kabisa ndio upeleke sokoni, la hasha, muda upo wa kurekebisha kadri siku zinavyokwenda na uhitaji wa soko.

16. Haijalishi umenazaje bali inajaslisha umemalizaje. Unaweza anza vizuri ukamaliziia kwa udhaifu au vibaya, unaweza pia kuanza kwa udhaifu ukamaliza kwa nguvu. Usivunjike moyo unapoanza kitu kwa udogo au kwa hali chini, unayo nafasi ya kufanya mageuzi mbele ya safari.

SOMA; USHAURI; Kuhusu Kujiunga Na Biashara Ya Mtandao(Network Marketing) Na Mambo Muhimu Ya Kuzingatia.

17. Tafuta mshirika wa kibiashara (Business partner). Mabilionea unaowaona kwenye dunia hii hawakuanza peke yao, walitafuta washirika sahihi wa kibiashara. Hata wavumbuzi wakubwa kama Thomas Edison walianza na ni timu nzuri. Unaweza kusema “sasa nikitafuta mtu wa kushirikiana kibiashara si itabidi tugawane mapato yatokanyao na biashara, sasa si bora tu ni miliki mwenyewe kampuni ili chote kiwe changu” . Kumbuka Ni afadhali kumiliki kampuni kubwa kwa aslimia 50, kuliko kumiliki kampuni ndogo kwa asilimia 100.

18. Jikite katika kuwaelewesha wateja wako kwanini wanunue kwako na si kwa washindani wako, wateja wako wanachotaka kujua ni faida gani zaidi ziko kwako, hawajalishwi na jinsi gani unavyotaka kuharibu uhsindani uliopo. Kwa hiyo unapozungumza na wateja wako usilogwe ukaishia kupondea washindani wako, wewe elezea ubora wa bidhaa au huduma unayotoa na uwe specific.

19. Katika kuandaa mpango wa biashara (Business plan) nguvu kubwa weka katika muhtasari mkuu (executive summary) , maana hapo ndipo patapelekea mtu aendelee mbele au aishie hapohapo. Ukweli ni kwamba hata kama mpango biashara wako ni mzuri kiasi gani, ukishindwa kuonyesha hapo mwanzoni ndo basi tena. Hakikisha executive summary inashiba kiasi cha kumshawishi mwekezaji aendelee kupekua kurasa za mbele.

20. Soma kwa bidii sana. Wajasiriamali wa viwango vya dunia (world-class), wansoma sana, kusoma kutafanya uwe mbunifu zaidi ya wengine. Soma tena na tena, usomee tena

Asanteni sana tukutane wiki ijayo. Kama utapenda kupata kitabu hiki cha THE ART OF THE START wasiliana nami. Nitakupatia bure kabisa. Mwisho wa ofa hii ni tarehe 30 May 2015.

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Makundi Matatu (3) Ambayo Hayawezi Kufikia Mafanikio.

Ni haki ya kila mtu hapa duniani kufikia mafanikio makubwa katika nyanja yoyote ile ya maisha kama vile kijamii, kiuchumi, kimwili na kadhalika. Na ili kuwa na mafanikio yoyote lazima uamue. Katika makala yetu ya leo tutajifunza makundi matatu ya watu ambayo ni vigumu sana kwao sana kufikia mafanikio yoyote yale.

HAWAWEZI

Makundi hayo ni kama yafuatayo;

1. Kundi Ambalo Hawataki au Hawahitaji Mafanikio

Mtu mwenyewe au watu wenyewe hawataki au hawahitaji mafanikio au hawana utayari wa kuwa na mafanikio. Kundi hili huwa wanajilinda sana kwa nafsi zao, ni watu ambao ni wagumu na siyo rahisi kuingilika na wana maneno mengi sana ya kujihami kiasi ambacho hawawezi kuvamiwa ovyo.

Kundi hili hawapendi kuingia katika matatizo, hawaishiwi sababu na wanaamini kuwa ukiingia katika mafanikio ni lazima ujiingize katika matatizo. Ni watu ambao hawataki kujifunza, kusumbuliwa ,wanachelewa sana kuamka na kulala upesi, hata akifanya kitu hapendi kukosolewa na wanakuwa wakali sana wanapoulizwa na ukiwaambia waongeze mwendo wako tayari kugeuza na kurudi nyuma au kutafuta njia nyingine ili wasiongozane na wewe na kusumbuliwa katika safari hiyo.

Hivyo basi, watu hawa wameridhika na hali zao za maisha wanaishi kwa imani. Wako tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza katika maisha yao na watu hawa au kundi hili ni vigumu kufikia mafanikio au utajiri.

SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.

2. Kundi Lisilopenda Kujiingiza Katika Hatari

Kundi hili lina mawazo na imani kuwa unapojiingiza katika mafanikio au kuwa na utajiri umejiingiza katika hatari , kuwa katika hali ya kuvamiwavamiwa na majambazi wakati wote au kuingiliwa na wezi kauli yao kuu wanasema ‘’ Hali niliyonayo inatosha sitaki kujiingiza katika hatari’’

Watu hawa ni watafutaji na wanenaji wazuri sana wa kutoa habari za watu ambao wamepatwa na mikasa mikubwa kutokana na utajiri au kutafuta utajiri . Watu hawa hawana ile hali ya kutamani kuwa na mafanikio au utajiri na ndani mwao hali hiyo haipo kabisa.

Hata wakiwa wana uwezo au kipato ndani yao hawana ile tabia ya kuwaza na kutamani mambo makubwa ya mafanikio au utajri watu hawa ifikapo uzeeni hali yao huwa mbaya sana kwa sababu pale mwanzo hakutaka kujiingiza katika hatari ili apate mafanikio.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.

3. Kundi Ambalo Lina Tabia ya Wasiwasi (Hofu na Woga ) Ndani Mwao

Kuna baadhi ya watu ambao ndani mwao wana ile hali ya woga na hofu, ile hali ya kuogopa kila wakati na kila kitu. Ukiwa na hofu huwezi kuthubutu na kuingia katika uwanja wa mapambano kutafuta mafanikio ili upate utajiri .

Kundi hili wana hofu ya shinikizo la mahangaiko. Hawataki na wanaogopa kushikwa na ile hali ya mahangaiko wanajuwa kuwa ili kuingia katika mafanikio kuna hali inayojitokeza bila kutazamia mahangaiko. Ni lazima upambane na uhangaike huku na huku na baadaye mafanikio yatatokea lakini wao wanaendelea kuogopa hali hiyo ya mahangaiko ingawaje hawana chochote kinachowawezesha katika maisha.

Wanaogopa kuteseka, wanaogopa ile hali ya kutowajibika, mafanikio au hali yoyote ya utajiri haiji bila ya kujitesa .

Kwahiyo, katika haya makundi tuliyojifunza leo yapo sana katika jamii yetu iliyotuzunguka. Kama wewe ni miongoni mwa haya makundi matatu tuliyojifunza leo achana na ondoka kabisa katika hali hiyo na chukua hatua leo ya kukufikisha katika kilele cha mafanikio.

Makala hii imendikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

Hii Ndio Siri Ya Kupata Marafiki Bora Watakaokuwezesha Kufikia Malengo Yako.

Habari za leo mpendwa msomaji wa mtandao huu wa JIONGEZE UFAHAMU. Karibu tena kwenye ijumaa nyingine ambayo kwa leo tunaangalia upande wa marafiki na mchango wao katika maisha yetu ya kila siku

Waswahili wanasema nioneshe rafiki zako nami nitakuambia tabia zako. Msemo huu ni wa kweli. Kila mtu ni shahidi wa usemi huu ingawa kuna baadhi hujifariji kwa kusema mimi nina rafiki jambazi lakini mimi si jambazi.

Ukweli ni kwamba tabia za watu ambao ni marafiki hufanana kwa kiwango kikubwa ingawa hazitafanana kwa asilimia mia moja kwakua kila mtu anatofautiana na mwingine kwa namna moja ama nyingine. Kwa mfano mtu anaweza kukutambulisha kwa rafiki yake na kusema ukimuona yeye umeniona mimi. Si kweli kuwa mtu mwingine anaweza kuwa wewe lakini kuna namna fulani au katika maeneo fulani(ambayo ni muhimu sana) mnaendana na sababu hiyo ndiyo iliyoleta ukaribu ndani yenu na kuwafanya muwe marafiki.

SOMA; Kanuni Sita(6) Muhimu Za Kushinda Tatizo Lolote Unalokutana Nalo.

clip_image002

URAFIKI NA MALENGO.

Mara nyingi marafiki zetu wamekua na sehemu kubwa sana ya kutufanya tufikie au tusifikie malengo yetu. Marafiki hawa tunaweza kuwa tumeonana nao mahali pa kazi,masomoni, mahali tunapoishi, sehemu za ibada. N.k

Marafiki wanafaida sana katika malengo yetu ikiwa ni kututia moyo pale tunapokata tamaa, kutushauri, kuturekebisha wakati tunapokosea, kutufariji, kushirikiana nao nyakati za huzuni na furaha na pia marafiki ndiyo hao wanaoweza kuwa mume au mke baadae. Kwa hiyo marafiki wanamchango mkubwa sana katika maisha yetu ya kila siku .

Kuna baadhi ya watu hushindwa kufikia malengo ya maisha yao waliyojiwekea kwasababu tu ya marafiki walionao. Marafiki hawa huwa ukuta wa wao kufanya mambo mazuri na makubwa wanayohitaji kuyafanya. Ni vizuri kuwa makini na kuchunguza vizuri kama maraki tulionao wana chembechembe za mambo ambayo tumeyapa kipaumbele. Kama una rafiki mlevi , mtembezi, anayependa kubishana, mvivu na wewe ukawa na tabia za tofauti na yeye basi urafiki wenu waweza kuingia doa au hapo lazima mmoja abadilike amfuate mwingine ili muweze kuongea lugha zinazofanana.

SOMA; Kitu Pekee Unachoweza Kuwa Na Uhakika Nacho…

Fikiria unapokuwa na ndoto za kufikia mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na uhuru wa kifedha, furaha, mahusiano yenye tija, familia nzuri,afya bora na kuwa muumini mzuri katika dini yako. Halafu ukatafuta rafiki ambaye yeye hatarajii kuboresha eneo lolote lile kama wewe unavyofikiri. Je atakuwa msaada au kikwazo cha wewe kufika pale unapohitaji? Mkiwa kama marafiki mtakuwa mnazungumza nini basi mkikaa pamoja. Kwakua kama unatarajia kuboresha eneo fulani ni vizuri ukawa karibu na mtu aliyefanikiwa katika eneo hilo au ambaye naye pia yuko katika safari ya kuboresha eneo hilo ili ule msukumo ulioko ndani yako usijeondolewa na watu wanokatisha tamaa.

Ni vizuri kufahamu mwelekeo na namna ambavyo rafiki yako anayachukulia maisha, mafanikio,na vipengele vingine ambavyo kwako wewe ni muhimu. Kwa kujua hivyo ni rahisi kumshirikisha rafiki yako ratiba yako ya siku na yeye kukushirikisha yake ili kusiwe na ugomvi na kila mmoja atambue na kuheshimu kitu rafiki yake anachokifanya na kujali muda pia.

SOMA; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015.

Hakikisha kuwa rafiki uliyenaye anakusaidia kufikia malengo yako na wewe pia unamsaidia kufikia malengo yake. Kama rafiki uliyenae ni kikwazo cha wewe kufika unapotaka basi ni vizuri ukaachana nae. Kuna wakati unafika ni lazima ufanye maamuzi magumu ili kuhakikisha kuwa unafikia ndoto zako. Usiachane nae kwa ugomvi. Fuata ratiba zako na umwambie kuhusu ratiba yako akishindwa kuendana na wewe basi yeye mwenyewe ataamua kuachana na wewe. Na hio itakuwa fursa nzuri kwako kuweza kuwa na rafiki ambaye mwelekeo wenu unaendana.

Pia kuna marafiki wengine wazuri sana ambao hawawezi kukuvunja moyo hata siku moja ambao ni vitabu vya uhamasishaji, makala mbalimbali, vitabu vya audio n.k.

Kumbuka watu wanaotuzunguka wana mchango mkubwa katika ukuaji wetu. Hivyo usijitenge kabisa na watu ila ufahamu namna bora ya kushirikiana nao bila kupoteza mwelekeo wako wa maisha.

Nakutakia utekelezaji mwema wa haya uliyojifunza.

Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com