Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo - 2

Habari za leo msomaji wa makala za kilimo kwenye Jiongeze Ufahamu, ni matumaini yangu unaendelea mbele na juhudi za kuyafikia mafanikio. Nipende kuwashukuru wote ambao mmekua mkijifunza kupitia jukwaa hili, nimepokea barua pepe (email) kadhaa za ndani ya Tanzania na hata nje ya nchi za watu kukiri kujifunza kutokana na makala za kilimo. Wale ambao mmeniandikia barua pepe kwa ajili ya kupata ushauri, wapo ambao tayari nimeshawajibu ila wapo wengine wiki hii mwishoni nitakua nimewajibu wote waliobakia.Tujikumbushe tu kidogo,wiki iliyopita tulianza kujifunza mambo matano ya muhimu kuyafahamukabla ya kuwekeza kwenye kilimo, na tuliweza kujifunza mambo mawiliambayo ni soko na hali ya hewa inayoruhusu kustawi kwa kilimo ulichokusudia. Leo tutaweza kuyamalizia mambo yaliyobakia. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki iliyopita isome hapa; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo.

Karibu kwenye somo

3. Upatikanajiwa rasili watu (Wafanya kazi)

Ukweli ni kwamba hata ukiwa na kiasi kikubwa cha fedha hutaweza kuwekeza kwenye kilimo kama huna rasilimali watu. Wafanyakazi ni rasilimali muhimu sana kama zilivyo fedha, vifaa, mitambo au mashine za utendaji kazi, ndio maana kulijua hilo kampuni nyingi zimeweka utaratibu wa kutunza rasilimali hii muhimu ya watu. Utakuta kwenye makapuni kuna afisa au meneja rasilimali watu. Ukweli ni kwamba vitendea kazi ulivyo navyo vitaendeshwa na watu. Wafanyakazi ni wa muhimu sana kwenye kilimo kuanzia uwekezaji mdogo hadi mkubwa. Wafanyakazi tunaweza kuwaweka kwenye makundi 2, la kwanza ni la wafanyakazi wa kawaida wale ambao hawana ujuzi wa kitaalamu au vibarua, na kundi lingine ni la wafanyakazi wenye utaalamu au ujuzi fulani hasa wa kilimo.Kama unaanza kuwekeza kwenye kilimo kwa uwekezaji wa chini hutahitaji sana wataalamu kwa kuwaajiri, ila utahitaji kutafuta ushauri wa kitaalamu ambao sio gharama kubwa. Lakini pia utahitaji vibarua ambao watakua wakifanya shughuli za shambani, hapo itategemea na ukubwa wa shamba lako. Ila kama unataka kufanya uwekezaji mkubwa lazima utahitaji hao wataalamu wa kilimo, na sio hao tu utahitaji fani nyingine kama washauri wa fedha, wahasibu, utawala, wataalamu wa sherian.k Kumbuka hapo kwa wafanya kazi, sio alimradi wafanya kazi, unahitaji wafanya kazi wenye kufanya kazi kwa bidii, wenye kujituma sio mpaka wasimamiwe ndio wafanye kazi, wenye hamasa ya kazi, wabunifu na wanaoweza kufuata maelekezo vizuri hata kama sio mtaalamu lakini ana uwezo wa kufuata maelekezo ya kitaalamu. Pia bila kusahau mwajiri lazima ujali wafanya kazi wako maana ni rasilimali inayokuzalishia kipato, lazima ujue wafanyakazi ni zaidi ya hizo mashine au mitambo na fedha.

Katika nchi zinazoendelea rasilimali watu ni rahisi kuipata, gharama yake ni rahisi ukilinganisha na nchi zilizoendelea tayari. Katika nchi zilizoendelea gharama ya kumlipa kibarua au mfanya kazi wa kawaida inakaribia kulingana na gharama ya kulipa mtaalamu mwenye ujuzi katika nchi za kwetu, na ndio maana nchi tajiri zinapendelea kuja kuwekeza huku kwenye nchi zinazoendelea.

SOMA; BIASHARA LEO; Ondoka, Hakuna Aliyekuita Hapa.

4. Upatikanaji wa maji wa uhakika

Wakulima wengi baraniAfrika kilimo chao kinategemea mvua, hivyo mvua isiponyesha uzalishaji unakua matatani. Mabadiliko ya tabia nchi yanapelekea mvua zisiwe za uhakika laikini pia majira ya mvua yanabadilika, mfano kama mvua za masika tulikua tumezoea zinaanza mwezi wa pili lakini kwa sasa zinaanza mwezi wa tatu au wanne. Upatikanaji wa maji kila kukicha unakua ni changamoto. Ikumbukwe kwamba ukame huongoza kusababishanjaa au upungufu wa chakula dunia kote. Katika uwekezaji wa kilimo kitu ambacho unatakiwa uwe na uhakika nacho ni maji ya uhakika, uwe na chanzo cha maji cha uhakika. Ili ufanye kilimo cha kibiashara lazima uwe na uwezo wa kuzalisha mwaka mzima, kama huna maji ya uhakika hutaweza kufanya hivyo. Hapa namaanisha kilimo cha umwagiliaji, zipo njia mbali mbali za umwagiliaji kama njia ya mifereji, umwagiliaji wa matone, umwagiliaji wa maji mfano wa mvua. Lakini katika njia zote njia ya umwagiliaji wa matone ndio nzuri maana inatumia maji machache na pia maji yanakwenda pale mmea ulipoota hivyo hakuna upotevu wa maji. Njia hii ya umwagiliaji wa matone unaweza kufanyika katika mashamba ya wazi au katika nyumba ya kupandia mazao maarufu kama Nyumba ya kijani(greenhouse). Unaweza kuwa na vyanzo tofauti vya maji mfano kutoka mtoni, kuchimba kisima cha chini, kuvuna maji ya mvua n.k. Pia ni vizuri kutengeneza miundombinu ya kutunza maji kama Bwawa ambalo litahifadhi maji. Israel ni moja ya nchi zinazofanya vizuri sana kwenye kilimo cha umwagiliaji,ijapokuwa eneo lake kubwa ni ukame wameweza kuvumbua teknolojia nzuri sana kwenye umwagiliaji. Israel mvua ikinyesha siku tatu tu, wana uwezo wa kupanda na kuvuna mazao yakutumia na kuuza nje ya nchi. Hii ni kwasababu wanayo miundo mbinu mizuri katika kuvuna maji ya mvua na kuyatunza kwa ajili ya kutumia kumwagilia kwa njia ya matone. Kwa Tanzania zipo kampuni kadhaa ambazo zimekua zikifanya biashara ya kuuza vifaa vya umwagiliaji wa matone, moja ya kampuni hiyo ni Balton Tanzania ambayo ni kampuni ya Waisraeli. Kwa Tanzania wapo Arusha na pia wanayo ofisi Dar. Pia wanatoa huduma ya kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji.Kwahiyo kwa kumalizia pointi yetu hii ni kwamba, upatikanaji wa maji ni muhimu sana katika uwekezaji wa kilimo maana kama vile maji ni uhai kwa mwanadamu, vivyo hivyo maji ni uhai kwa mimea.

SOMA; UKURASA WA 91; Utashi, kitu muhimu kwako kufikia mafanikio.

5. Miundombinu pamoja na kufifika kwa eneo la uwekezaji

Hapa tunaangalia miundombinu kama barabara, umeme, mawasiliano ya simu n.k Lazima eneo unalowekeza kilimo chako liwe linafikika, hakikisha barabara iko vizuri na inapitika wakati wote, maana utahitaji kusafirisha kwenda shambani vitendea kazi, pembejeo n.k. Pia wakati wa kuvuna utahitaji kusafirisha kupeleka sokoni. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba eneo likiwa ni gumu kufikika hii itaongeza gharama za uzalishaji na hivyo kupelekea kupunguza faida yako. Hivyo pamoja na kuzingatia vigezo vinne vilivyopita ni lazima kuchagua eneo ambalo linafikika, mawasiliano ya simu yako sawa, pia nishati ya umemena mengineyo.

SOMA; Hiki Ndio Unachohitaji Ili Kugeuza Ndoto Yako Kuwa Uhalisia.

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email) daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Imehaririwakwa Kiswahili sanifunaRumishael Peter

email:rumishaelnjau@gmail.comsimu:+255-713-683422

http://rumishaelnjau.wix.com/editor

1 comments:

Nasheedtz said...

Ahsante kaka mungu akupe afya njema ili uzidi kutuelimisha