Siri Ya Kutambua Kampuni Nzuri Ya Kuwekeza Ili Upate Faida.

Unapohitaji kufanya uwekezaji katika hisa inatakiwa kutambua kampuni sahihi za kuwekeza mtaji wako ili uweze kukua. Katika kuchagua kampuni sahihi ya kuwekeza unahitajika kuzingatia vitu muhimu ambavyo vitasaidia kujua kampuni hii inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri. Ili uweze kutambua kampuni inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri unatakiwa kuzingatia vitu vifuatavyo ambavyo ni muhimu kuvifahamu.

Ukuaji wa Mauzo (Revenue)

Kampuni ambayo mauzo yake yanaongezeka kila mwaka, hii inaonyesha kwa kiasi gani kampuni hiyo inafanya bidii katika masoko na bidhaa zake zinafanya vizuri katika soko. Ukuaji huu unaashirilia hata uongozi upo makini katika kutekeleza mipango yao kwa umakini. Vile vile ukuaji wa mauzo unaonyesha kwa kiasi gani kampuni hiyo bidhaa yake ilivyo na umuhimu katika matumizi ya watu katika eneo husika.

SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.

Kufahamu ukuaji wa faida ya kampuni

Kampuni ambayo inaukuaji mzuri wa faida kuanzia 20% au 25% kwa mwaka ni nzuri kwa kuwekeza kwa kuwa gawio litakua na kuwavutia wawekezaji wengi zaidi. Vile vile kampuni itapata pesa ya kuwekeza katika fursa nyingine ambazo zitaongeza faida kwa kipindi kijacho. Ukuaji wa faida unaonyesha kwa kiasi gani kampuni ambavyo ipo makini katika kudhibiti matumizi yasiyo ya msingi katika uendeshaji wa kampuni na kupelekea ongezeko la faida.

Ukuaji mzuri wa Gawio

Kampuni ambayo inaukuaji mzuri wa gawio ni ishara kuwa hata ukuaji wa faida ni mzuri. Gawio likiongezeka mwekezaji anapata kipato vile vile huwavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika kampuni hiyo na bei kuongezeka kutokana na ushindani kuwa mkubwa katika soko. Gawio ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wengi kuwekeza katika kampuni yoyote na gawio likikua na ushindani huwa mkubwa katika soko la hisa na kupelekea bei zake kupanda.

SOMA; Tabia Saba Za Watu Wasiokuwa Na Mafanikio.

Ukuaji mdogo wa madeni

Kampuni ambayo ukuaji wake wa madeni ni mdogo au madeni ya kampuni yanapungua huashiria kuwa kampuni hiyo ina mipango madhubuti katika kukuza mauzo na kupunguza madeni ili kupunguza hatari ya kufirisika. Kampuni ambayo madeni yake yanaongezeka kwa kila mwaka na kwa kiwango cha juu hii inaashiria kampuni haifanyi vizuri na kuna hatari ya kushindwa kulipa madeni.

Ukuaji wa bei za hisa za kampuni

Sehemu mojawapo kwa mwekezaji kupata faida kupitia uwekezaji wake kwa kupitia ongezeko la bei za hisa. Bei ya hisa ikiongezeka kwa kiwango kizuri na mwekezaji hupata faida ambayo hutokana na ongezeko la thamani. Kampuni ambayo ina ongezeko la bei kwa 20% au zaidi kwa mwaka ni kampuni nzuri kwa kuwekeza kwa kuwa mwekezaji atapata ongezeko la thamani ya hisa zake katika kiwango kinachorizisha. Katika soko la hisa kuna kampuni ambazo zina ukuaji bei za hisa wa zaidi ya 40% kwa mwaka ambazo ni nzuri kuwekeza kwa mwekezaji.

SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Umuhimu Na Jinsi Ya Kujijengea Tabia Ya Shukrani.

Kufahamu mipango ya Kampuni kwa miaka ijayo

Kampuni ili iweze kufanya vizuri katika soko ni kuwa na mipango mizuri kwa miaka ijayo ili iweze kuendana na mabadiliko yanayotokea. Mwekezaji ataweza kufahamu mipango ya kampuni kwa kuangalia taarifa za mwaka za kampuni (Annual Report) ambapo kampuni huonyesha mipango yao katika kipindi kijacho kama wanahitaji kuongeza bidhaa mpya au kuongeza matawi katika sehemu nyingine au nchi nyingine.

Hivi ni vitu vya msingi kwa mwekezaji kuviangalia unapohitaji kuwekeza katika hisa ili uweze kupata manufaa na kuwekeza kwa faida na kukuza mtaji wako. Tukutane katika makala nyingine ambazo zinakujenegea uwezo zaidi katika kuwekeza katika hisa.

SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.

Ili uweze kupata taarifa za kiswahili zitakozokuwezesha kutamua ukuaji wa mauzo, faida ya kampuni, ukuaji wa bei na mipango ya kampuni tuwasiliane kwa mawasiliano hapo chini.

Mwandishi: Emmanuel Mahundi

Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510

Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com

0 comments: