Showing posts with label MBINU ZA KAZI. Show all posts
Showing posts with label MBINU ZA KAZI. Show all posts

Hatua TANO Za Kuongeza Uzalishaji Wako Ili Kufikia Mafanikio.

Kuna usemi mmoja maarufu sana unaosema “ukiendelea kufanya unachofanya sasa, utaendelea kupata matokeo unayopata sasa”. Kwa lugha nyingine kama unataka kubadili matokeo yako, ni lazima uanze kwa kubadili kile unachofanya.

Ili uweze kufikia mafanikio zaidi ya uliyonayo sasa, kwa sababu mpaka hapo ulipo tayari una mafanikio, unahitaji kubadili njia unazotumia sasa. Na kitu cha kwanza kabisa kubadili ni uzalishaji wako.

Uzalishaji tunaozungumzia hapa ni ile kazi au thamani unayotoa kwa wengine kwa muda unaofanya kazi. Hivyo kama utazalisha thamani zaidi kwa muda mfupi maana yake una uzalishaji mkubwa. Na hii ni njia nzuri ya kufikia mafanikio kwenye chochote unafanya, iwe ni kazi au biashara.

Kiuchumi, utajiri au thamani ya kampuni, mtu binafsi na hata jamii kwa ujumla unapimwa kwa ongezeko la uzalishaji.

SOMA; Sifa TATU Unazohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Ujasiriamali.

Leo UTAJIONGEZA na hatua tano unazoweza kutumia na ukaongeza uzalishaji wako na hatimaye kufikia mafanikio zaidi.

Hatua ya kwanza na rahisi kabisa ya kuongeza uzalishaji wako ni kuwa bora kwenye majukumu yako. Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuendelea kujifunza zaidi. Kama unafanya biashara, ijue vizuri biashara yako na ongeza juhudi. Kama umeajiriwa, unajua majukumu yako kikazi, yatekeleze vizuri.

Hatua ya pili ni kutafuta mtu ambae anaweza kufanya hiko unachofanya na kwa bei rahisi kisha unampa afanye. Kama ni mfanyabiashara maana yake unatafuta watu wa kukusaidia. Kama ni ajira unafanya kazi na watu wengine ambao wanakusaidia. Ukweli ni kwamba kazi inayofanyika kwa timu inafanyika kwa uzalishaji mkubwa.

SOMA; Tabia Mbaya KUMI(10) Zinazopunguza Ufanisi Wako.

Hatua ya tatu ya kuongeza uzalishaji ni kutumia teknolojia iliyopo. Hapa unatafuta njia ambayo teknolojia inaweza kurahisisha kazi unazofanya. Kwa mfano badala ya kuandika kila barua kwa mkono, inaweza kuandikwa moja na zikatolewa kopi na mashine. Kila kazi inaweza kusaidiwa na teknolojia.

Hatua ya nne ni kuvumbua teknolojia mpya inayoweza kurahisisha kazi zako. Na ukifikia hatua hii unakuwa umetatua tatizo la wengi. Inawezekana kwa kila kazi unayofanya kuvumbua njia rahisi ya kiteknolojia ya kuirahisisha.

Hatua ya tano na ya mwisho ya kuongeza uzalishaji wako ni kujua vitu vinavyoleta uzalishaji mkubwa kwako na kufanya hivyo tu. vingine vyote unaacha kuvifanya kwa sababu vinakupotezea muda. Kwa mfano asilimia 80 ya mafanikio yako inatokana na asilimia 20 ya kazi unazofanya. Je ni kazi zipi hizo zinakuletea faida kubwa? Zijue kazi hizi na zifanye kwa ufanisi mkubwa na utaongeza uzalishaji wako.

SOMA; SIRI YA 4 YA MAFANIKIO; Itumie Sheria Ya Wastani Kukuletea Mafanikio.

Mwisho wa siku kinachoongeza uzalishaji ni pale unapojua kile chenye faida kwako na kukifanya. Hii ndio inayoleta faida kwenye makampuni, biashara na hata kazi. Wale wanaojaribu kufanya kila kitu huishia kuwa na uzalishaji mdogo. Wale wanaochagua vichache na kuvifanya vizuri huwa na uzalishaji mkubwa.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Tabia Mbaya KUMI(10) Zinazopunguza Ufanisi Wako.

Huenda unatamani kufanya zaidi ya unavyofanya sasa lakini kila ukijitahidi huoni mabadiliko. Huenda una ufanisi mdogo kiasi kwamba kila mtu anakuona wewe ni mvivu sana.

Sio kweli kwamba wewe ni mvivu bali kuna tabia ambazo zinakufanya ushindwe kutekeleza majukumu yako kwa wakati.

Leo utajiongeza na tabia kumi mbaya ambazo zinakufanya uwe na uzalishaji mdogo na ukiweza kuziepuka utaongeza uzalishaji wako.

1. Unzanza siku yako bila ya kuipangilia. Usipopangilia siku yako utafanya nini utajikuta unafanya chochote kinachotokea mbele yako.

2. Unaangalia facebook au email kila baada ya dakika kumi. Kama mawasiliano yako yanakufanya uwe na shauku kubwa ya kutaka kujua ni nini kinaendelea kwenye mitandao ya kijamii itakuwa vigumu sana kwako kukamilisha majukumu yako kwa wakati.

3. Unasubiri muda muafaka ndio ufanye ulichopanga kufanya. Kuna wakati unafikiri kama kitu fulani kikitokea basi nitafanya kitu fulani, mwishowe unaishia kutokufanya kabisa.

4. Unajaribu kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Mwishowe unaishaia kushindwa kumaliza hata moja, kama mtu anayekimbiza sungura wawili, hakamati hata mmoja.

5. Unagoma kujifunza vitu vipya. Dunia ya sasa karibu kila kazi imerahisishwa sana. Kuna utaalamu mwingi ambao unaweza kuutumia kurahisisha kazi yako, ila unapogoma kujifunza unabaki nyuma.

6. Unasubiri mpaka dakika ya mwisho ndio ufanye jambo. Unapokuwa na muda wa kufanya jambo mara nyingi huwa unaona ni mwingi, ni mpaka muda unapokaribia kuisha unaona kwamba ulipoteza muda mwingi.

7. Unalaumu vifaa unavyofanyia kazi. Labda unasema kompyuta unayotumia ipo taratibu sana, mashine unayotumia inakurudisha nyuma. Hizi zote ni sababu ambazo hazina msingi.

8. Huna muda maalumu wa kula. Kama huna muda maalumu wa kula au wakati mwingine unaacha kula itakuwa vigumu sana kwako kuweza kuwa na nguvu ya kutekeleza majukumu yako.

9. Unatumia muda mwingi sana kupanga. Inawezekana unapanga, halafu unakaa unafikiria mipango yako, baadae unapanga tena. Kwa kupanga huwezi kutimiza chochote, unatakiwa kufanya kazi.

10. Huapati usingizi wa kutosha. Kama kila siku unachelewa kulala na kuamka umechoka ni vigumu sana kuweza kutekeleza majukumu yako.

Epuka tabia hizo kumi mwaka huu 2015 ili uweze kuongeza ufanisi wako.