Sifa Sita(6) Unazohitaji Ili Kuwa Mjasiriamali Bora.
Kumekuwa na maswali mengi sana katika mitazamo tofauti juu ya ujasiriamali kwa mfano ujasiriamali ni nini? Na mjasiriamali ni mtu mwenye sifa gani?. Basi mpenzi msomaji wa makala hii ya leo utapata kujua nini maana ya ujasirimali na sifa mjasiriamali ni zipi.
Ujasiriamali nini?
Ujasiriamali ni uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazojitokeza na kugeuza au kutumia changamoto hizo kama fursa. Kwa mfano eneo A kuna shida kubwa ya maji basi mjasiriamali atakabiliana changamoto hiyo kwa kuchimba kisima cha maji na hatimaye atakuwa ametupia changamoto hiyo ya maji na kugeuza kuwa fursa.
Sifa za kuwa mjasiriamali bora
- Uwezo wa Kuona Fursa
Mjasiriamali lazima uwe na jicho la kuona fursa au uwezo wa kuona fursa katika jamii yako inayokuzunguka. Mjasiriamali anatumia changamoto zinazojitokeza katika jamii yake na kutumia changamoto hiyo kama fursa kwake. Kwa mfano sehemu unayokaa watu wanauhitaji wa huduma za kibenki kama vile tigo pesa, m-pesa ,airtel money nk. Basi mjasiriamali anaona hiyo fursa kwake kwa kuanzisha vibanda hivyo vya kutolea huduma za kibenki.
SOMA; Njia Rahisi Ya Kutengeneza Matatizo Makubwa Kwenye Maisha Yako.
- Ubunifu
Kama mjasiriamali yakupasa uwe mbunifu. Baada ya kuona fursa sasa katika eneo Fulani buni kitu tofauti, kuwa wa kipekee kwa mfano kama unatengeneza chapati basi zifanye chapati hizo kuwa tofauti na za wengine. Mshawishi mteja onesha utofauti wako katika ubunifu wa bidhaa au huduma unayotoa.
- Kuwa Mvumilivu
Mjasiriamali siyo mtu wa kukata tama, mjasiriamali ni mtu mvumilivu. Tutambue kuwa hakuna mafanikio ya haraka na mafanikio hayatokei kama vile radi au ajali. Bali mafanikio katika jambo lolote lile yakupasa uwe mvumilivu sana, vilevile katika safari ya mafanikio kuna changamoto nyingi sana. Mafanikio yoyote yale yana changamoto hivyo basi uweke hili akilini mwako.
SOMA; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Ili Uweze Kufikia Malengo Yako.
- Mtu Mwenye Malengo
Mjasiriamali ni mtu mwenye malengo. Lazima uwe na malengo ya muda mrefu na mfupi huwezi kuwa mjasiriamali bora kama huna malengo. Lazima ujiwekee malengo kwa mfano ndani ya mwaka mmoja unahitaji ufike wapi, kama umekosa kuwa na malengo umekosa sifa ya kuwa mjasiriamali bora.
- Ari ya Kufanya Kazi/Kujituma
Mjasiriamali unatakiwa kuwa mtu mwenye ari ya kufanya kazi au kujituma kwelikweli ,mtu wa kujitoa unahitaji masaa ya ziada katika kujitoa kwako . Ondoa uvivu, unabidi uweke juhudi ya kufanya kazi, lazima upende kazi yako usiwe mtu wa kusukumwa bali kuwa mtu wa kujituma.
SOMA; Upya Wa Biashara Mpya Na Unavyoweza Kuutumia Vizuri…
- Mtu Anayependa Kujifunza
Kama wewe ni mjasiriamali halafu huwezi kujifunza basi unapitwa na mengi sana. Mjasiriamali unatakiwa kujifunza kila siku kitu kipya, soma vitabu mbalimbali ,jifunze kwa watu waliofanikiwa kila siku kwani kujifunza hakuna mwisho na elimu haina mwisho, hudhuria semina mbalimbali upate maarifa mapya.
Hivyo basi,mjasiriamali anatakiwa awe mtu wa kuongeza thamani na mtu mwenye jicho la kuona fursa katika jamii inayomzunguka.
Makala hii imendikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com
5/18/2015 07:30:00 AM | Labels: UJASIRIAMALI | 0 Comments
Siri Za Kuwa Mjasiriamali Bora Na Kufikia Mafanikio Makubwa.
Wajasiriamali wengi wamekuwa wakijishughulisha shughuli za uzalishaji kama kutoa huduma au kuuza bidhaa na lengo likiwa kupata mafanikio. Katika kufikia mafanikio makubwa wachache wameweza na wengi wao kutofikia au kukua kwa taratibu. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa katika ujasiriamali kuna vitu ambavyo unatakiwa kuvifahamu na kuthubutu kuvifanya ili kupata mafanikio makubwa. Mambo ambayo yana tija kubwa ni mambo madogo madogo ila yana mchango mkubwa sana katika kufikia mafanikio makubwa.
Hizi ndio siri za mjasiriamali bora ambazo zitapelekea kufikia mafanikio makubwa
Kupenda kitu ambacho unakifanya
Kama unatoa huduma au kuuza bidhaa ni muhimu kuipenda na kuithamini huduma ambayo unaitoa ili uweze kuifanya kwa ubora na kukidhi mahitaji ya wateja wako. Ukipenda kitu ambacho unafanya ni rahisi kukifanya bila kuchoka hata kama unakutana na changamoto kwa kiasi gani. Ukipenda huduma unayoitoa utawapenda wateja wako na kuweza kutoa huduma bora.
SOMA; Wajasiriamali Wenye Mafanikio Hufanya Mambo Haya Matano Kila Siku.
Kuwa mvumilivu na kutokata tamaa
Hakuna jambo ambalo unaweza kulifanya kwa urahisi katika dunia ya leo ambayo imejaa changamoto nyingi na kukatishwa tamaa. Ukiwa mjasiriamali unatakiwa kuwa mvumilivu hasa pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo yako. Ukiwa katika ujasiriamali kuna kipindi unakutana changamoto nyingi ambazo usipokuwa makini unaweza kata tamaa ila changamoto hizi zinapima uwezo wako wa ustahimilivu na kupambana na changamoto. Ukiwa umefanikiwa kutatua changamoto hiyo ndivyo ambavyo utapiga hatua na kufikia mafanikio makubwa.
Kuwa na nidhamu ya pesa
Kama unahitaji kuwa mjasiriamali ambaye anakua kila siku nidhamu ya pesa ni muhimu sana katika msingi wa kukuza biashara yako. Matumizi yako yasizidi au yasiathiri ukuaji wa biashara yako. Ili uweze kukuza biashara yako ukawa na matumizi ya kiasi ambayo yatakuwa rafiki wa ukuaji wa biashara yako. Ili uweze kujua kama biashara yako inakua ni vizuri ukawa na kumbukumbu ya biashara yako kuhusu matumizi na mapato.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Kuanza kufanya biashara hata kwa mtaji mdogo
Watu wengi hasa wenye elimu hupenda kuanza kufanya biashara kwa mtaji mkubwa na kuona tatizo kubwa ambalo linafanya washindwe kujiajiri na kwa kutokuwa na mtaji wa kutosha. Kuna faida kubwa ya kuanza kuifanya biashara kwa mtaji mdogo huku ukiendelea kukua kwa taratibu faida hizo ni a) Unapata uwezo kusimamia biashara kwa madaraja yaani kuanzia chini b) Unapata uwezo wa kuzisimamia pesa c) Unapata uwezo mkubwa wa kupambana na changamoto
Kufanya kazi kwa Bidii na Ubunifu
Hakuna kitu ambacho unaweza fikia mafanikio makubwa kama hautofanya kazi kwa bidii. Unaweza kuwa na mtaji mkubwa kama hufanyi kazi kwa bidii na kwa ubunifu ni kazi bure. Mafanikio makubwa yanahitaji kujitoa na kufanya kazi kuliko ambavyo ulikuwa unafanya kazi mwanzo na ikiwezekana fanya kazi zaidi ya masaa ambayo ulikuwa unafanya mwanzo.
Huduma au bidhaa yako ilenge kuisaidia jamii
Ukitoa huduma ambayo itasaidia kutatua matatizo ya jamii husika ni rahisi kwako kuweza kuliteka soko na kuuza bidhaa yako au huduma katika kiwango cha juu. Kama huduma yako itatua tatizo katika jamii ni rahisi kupata wateja wengi na wewe mjasiriamali kuweza kufikia mafanikio makubwa. Biashara nyingi ambazo zimelenga kutatua matatizo ya jamii zinafanya vizuri katika soko na kuwa na ushindani mdogo kuliko bishara za kuiga toka kwa wengine.
SOMA; Huyu Ni Mjasiriamali Mwenye Hamasa Kubwa sana. Unaweza kujifunza kila kitu kutoka kwake.
Jifunze kila siku
Mjasiriamali unatakiwa kujifunza kuhusu biashara mpya au kujifunza zaidi kuhusu biashara ambayo unaifanya ili uweze kuwa bora zaidi na kuifanya kwa ubora. Katika kujifunza jifunze kwa vitu ambavyo vinalenga kuiboresha biashara yako ili uweze kupata mbinu mpya na kuwa bora zaidi. Kujifunza huku kutakufanya kufanya vitu kwa ubora na kuwa tofauti katika kutoa huduma na kuifanya biashara yako kuwa bora na kuvutia wateja wengi zaidi.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422. http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/15/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO, UJASIRIAMALI | 0 Comments
Siri Kubwa Unayotakiwa Kujua Kwenye Mahusiano Ya Kibiashara.
Mahusiano unayojenga na watu kibiashara yanaweza kuwa ya aina mbili;
1. Uhusiano ambao kila mmoja anafaidika(win - win)
2. Uhusiano ambao mmoja ananufaika zaidi ya mwingine(win - lose)
Kwa bahati mbaya sana kwenye mazingira yetu mahusiano yaliyotawala ni ya aina ya pili.
Watu wengi watakaotaka kujenga mahusiano ya kibiashara na wewe watataka kiunufaika zaidi yako.
Kuwa mjanja, angalia mbali.
Ukiona uhusiano wa aina hii kimbia, hautakufikisha mbali.
2/21/2015 04:34:00 PM | Labels: MBINU ZA BIASHARA, UJASIRIAMALI | 0 Comments
Siri Moja Kubwa Ya Kufanikiwa Kwenye Ujasiriamali.
Unapokuwa mjasiriamali elimu yako ndio imeanza. Kwa kweli ili uweze kuwa juu kwenye ujasiriamali ni lazima uendelee kutafuta maarifa yatakayokufanya wewe na biashara yako kuwa bora zaidi.
Mjasiriamali anayeacha kujifunza ni mjasiriamali anayeacha kufaidika.
Wajasiriamali wanajifunza kupitia kusoma vitabu, kujifunza kuhusu watu waliofanikiwa, kusoma majarida yanayohusiana na wanachofanya, kuhudhuria semina na makongamano na njia nyingine nyingi.
Je wewe unatumia njia ipi kujifunza?
2/20/2015 05:15:00 PM | Labels: UJASIRIAMALI | 0 Comments
Siri Moja Kubwa Ya Kufanikiwa Kwenye Ujasiriamali.
Unapokuwa mjasiriamali elimu yako ndio imeanza. Kwa kweli ili uweze kuwa juu kwenye ujasiriamali ni lazima uendelee kutafuta maarifa yatakayokufanya wewe na biashara yako kuwa bora zaidi.
Mjasiriamali anayeacha kujifunza ni mjasiriamali anayeacha kufaidika.
Wajasiriamali wanajifunza kupitia kusoma vitabu, kujifunza kuhusu watu waliofanikiwa, kusoma majarida yanayohusiana na wanachofanya, kuhudhuria semina na makongamano na njia nyingine nyingi.
Je wewe unatumia njia ipi kujifunza?
2/20/2015 03:24:00 PM | Labels: UJASIRIAMALI | 0 Comments