Showing posts with label MBINU ZA MAFANIKIO. Show all posts
Showing posts with label MBINU ZA MAFANIKIO. Show all posts

Sehemu 7 Ambazo Unatumia Kupoteza Rasilimali Muda Wako

Muda au wakati ni rasilimali ambayo ikipotea hairudi tofauti na rasilimali fedha ambayo ukipoteza utaitafuta lakini ukipoteza muda huwezi kuupata hata kwa fedha. Mtunzi wa kitabu cha The Secret Code of Success ambaye ni Noah St. John anasema muda ni rasilimali ambayo huwezi kununua hata mabilioni ya Bill Gates hayawezi kununua hata dakika moja ya jana.
Hivyo basi, kumbe muda ni rasilimali muhimu ambayo hatuwezi kununua. Utajiri ambao tumepewa duniani bure kwa watu wote matajiri na masikini ni rasilimali muda. Wote tuna wakati sawa wa masaa 24 kwa siku. Kwa hiyo kila mtu duniani ni Tajiri wa muda au wakati. je unautumiaje utajiri wa rasilimali muda wako hapa duniani?
Zifuatazo ni Baadhi ya Sehemu Ambazo Unatumia Kupoteza Rasilimali Muda
1. Kuangalia Tv
Watu wengi wamekuwa wakipoteza muda sana kuangalia tv, mtu anapoteza masaa matatu mpaka matano kuangalia tv akifuatilia tamthilia kwenye tv. Kuangalia vipindi ambavyo havina tija kwako vipindi ambavyo havina matokeo chanya kwako, kiongozi wa kanisa Katoliki duniani papa francis, ana miaka 25 sasa hajawahi kuangalia tv yaani luninga mara ya mwisho kuangalia tv ilikuwa ni tarehe 15 mwezi saba mwaka 1990. Je tunajifunza nini kutoka kwa kiongozi huyu? Kama yeye ni kiongozi mkubwa wa kanisa hilo duniani mbona hajapungukiwa wala hajapitwa kwa nini wewe usiweze?
2. Kufuatilia Udaku
Unapoteza muda kumfuatilia msanii Fulani leo amefanya nini badala ya kutumia muda huo kuboresha maisha yako. Watu wengi ni wazuri kufuatilia magazeti ya udaku, habari za udaku, mitandao au blog za udaku kuliko kufuatilia blog nzuri zinazotoa elimu ya jinsi kuboresha maisha yako moja wapo ni hii unayosoma makala hii nzuri. Utumie muda wako kufuatilia vitu vya maana ambayo vinabadili fikra yako acha kuwa mtumwa wa kila siku wa kufuatilia habari za udaku.
SOMA; MUDA–Kitu Chenye Thamani Kubwa Ila Kisichothaminika Na Wengi.
3. Kufuatilia Mitandao ya Kijamii kwa Faida Hasi
Kuwa katika mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, na kadhalika siyo mbaya, je uko katika mitandao hiyo ya kijamii kwa malengo gani? Unatumiaje muda wako katika mitandao hiyo ya kijamii kila dakika uko online kwenye mtandao zaidi ya mmoja unapata muda wapi wa kufanya kazi yako kwa ufanisi? Tenga muda wako vizuri kataa kabisa kuwa mtumwa wa kisaikolojia ukikaa kidogo bila kuingia unahisi unapitwa na habari wenzako wanaingiza siku wewe unafuatilia habari.
4. Kukaa Vijiweni
Wimbi la watu kukaa vijiweni na kupoteza muda linaongezeka kila siku ukipita kona hii utakuta watu wamekaa makundi vijiweni wakijadili serikali pengine sijui chama Fulani wamefanya hivi ni mambo mengi yanayojadiliwa kwenye magenge ya watu. Watu hawana kazi za kufanya wanapoteza muda bure na wala hajutii kwa muda anaoupoteza. Tumia muda huo kujifunza namna gani unaweza kubadili maisha yako. Acha kauli hizi za kusema ngoja niende kwa Fulani au kijiweni nikapoteze muda kidogo.
5. Kubishana
Hii ni sehemu moja wapo ambayo watu pia wanapoteza rasilmali yao nzuri ya muda katika kubishana. Watu wanabishania vyama vya siasa, timu za mipira kuna wengine wanabishana katika mpira mpaka wanapigana hii ni kwa sababu kila mmoja anataka asikilizwe kile anachosema yeye katika timu yake ndio sahihi. Unapoteza muda kushabikia vitu wakati huna hata hisa moja katika vitu hivyo unavyobishania ambavyo havikusaidii kuboresha maisha yako kabisa zaidi ya kukusababishia hasara ya kuendelea kuwa mtumwa wao.
SOMA; Lakini Nitapitwa.... (Sababu Ya Kijinga Inayokufanya Upoteze Muda)
6. Umbea na Majungu
Unapoteza muda kuongea maneno ya uchonganishi juu ya mtu Fulani unapiga umbea na majungu. Unaongea maneno ambayo yanaleta majeraha katika maisha ya watu, unapandikiza chuki kwa watu kwa kupiga majungu unapoteza muda wako bure kupiga umbea na majungu bila malipo yoyote ni hatari sana tumia muda wako kujenga na kuongea thamani yako katika jamii ya yako na acha kuwa mtu wa umbea na majungu kila siku.
7. Kuhudhuria Vikao au Mikutano Ambayo Haikupi Faida
Kuna vikao vingi sana katika jamii zetu, mikutano mingi ya kila siku ambayo haina matokeo chanya kwetu bali ni kupoteza wakati wako. Leo nakuomba sema HAPANA kwa vikao au mikutano ambayo haikupi faida yoyote ambavyo vinakula muda wako bure ambao muda huo ungeweza kutumia vizuri kuboresha maisha yako au hata kuongeza thamani katika jamii yako.
Hivyo basi, acha kutumia muda wako kudhurura ovyo yaani kutembea bila sababu ya msingi, tumia muda wako vema, muda ni mali katika karne hii usikubali mtu akupotezee muda kwa kitu ambacho hakina manufaa kwako fanya kile ambacho unatamani kufanya kwa muda huu katika Nyanja zote usisubiri ruhusa ukiendelea kusubiri ruhusa ndio unazidi kupoteza muda na umri pia unakwenda omba samahani kuokoa muda, Muda siyo rafiki na maisha ni mafupi .
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

Una Nini Cha Tofauti Mpaka Watu Wakufuate Na Kukusikiliza? Jua Hapa.

Katika dunia ya sasa ni kawaida sana kukutana na mtu akimthamini na kumjali mtu kwa kuwa ipo faida anaipata au ananufaika kwa njia moja au nyingine. Mfano huenda ni katika eneo lako la kazi, pengine bosi wako kwa kuwa tu wewe ni mfanyakazi mzuri basi ataonekana kukubali na kukuheshimu sana tu kumbe anafanya hayo kwa kuwa tu ipo faida anaipata kwa uwepo wake mahali pale pa kazi, pengine usipokuwepo naye nafasi yake itakuwa hatarini maana ni mapengo mengi unayaziba na kumfanya aonekane kuwa bora sana mahali pake pa kazi, unampa thamani mahali pale, hivyo naye anaonekana kukuthamini tu kwa kuwa ana anachopata kwako. Ile thamani uliyo nayo inamlazimisha kukujali na hata kukutumia zaidi.
Au kwa wanafunzi unapokuwa shuleni unakuta kuna mwenzio ana uwezo zaidi kwenye somo fulani hivyo unakuta mtu yule anategemewa na wengi na anaweza kuonekana kupendwa na wengi kwa kuwa anawasaidia wengi kuweza kufanya vizuri kwenye masomo anayowasaidia kuwafundisha ili waweze kuelewa zaidi, ukiangalia kwa kawaida unaweza ona kama yule mtu anapendwa na wengi, lakini ukiangalia zaidi utagundua pale hapendwi mtu bali kipo kitu cha thamani ambacho kinapendwa kwa mtu yule, kipo kitu watu wanakifuata kwa mtu yule ambacho pengine kwa wakati ule hakuna mahali pengine tena wataweza kupata kitu hicho, hivyo naweza sema wanakuwa hawana namna mbadala ya kupata huduma ile, wanalizimika kumkubali mtu yule hata kama hawampendi, wanalazimika kumsikiliza na wanakubali kufundishwa naye maana hakuna mwingine anaweza kufanya lile.
SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako Yote.
Pengine unaweza kukutana na mtu ukamshangaa na usimwelewe kwa kuwa anaambatana na mtu fulani, pengine wewe ukiangalia kwa macho yako ya kawaida unakuwa huioni thamani ya huyo mtu, huoni cha maana alichonacho cha kumfanya mtu mwingine asitake kuwa mbali naye, unajitahidi sana kukiona hicho lakini huoni, lakini wewe ukiwa katika hali hiyo kuna mwingine ameona thamani kwa huyo mtu, na anajua namna ya kuipata, hivyo anahakikisha anamtumia huyo mtu kuweza kupata kile mtu anacho, anamtumia yule mtu kuweza kufika pale anaelekea, usiishie kushangaa ni kwa nini mtu fulani anamkubali sana yule, usiwe mwepesi kumpuuza au kuona amepotoka wakati huelewi hasa ni kwa nini anafanya vile. Kama ukiwa mwelewa na mjanja mwenye nia ya kujifunza na kueleweshwa utatumia hekima na busara ili kuweza kuona kile mwenzio anaona kwa huyo mtu, utauliza na ukielekezwa uwe tayari kuheshimu hata mawazo ya wengine, uweze kuona thamani hata kwa wengine, hata kama wewe unadhani unajua kila kitu lakini tambua wapo wengine pia wanaoweza kuwa na uelewa kuliko wewe.
Wakati mwingine unaweza kukutana na mtu na ukamshangaa kwa nini anaambatana na mtu fulani maana wewe kwa viwango vyako na vipimo vyako unaona yule mtu si sahihi au hana sifa za kuweza kuwa na mtu yule na pengine unaweza kujaribu hata kumshawishi asiwe na mtu yule, pengine hata kwa kumweleza ni jinsi gani unaona hafai kwa kuelezea yale mabaya yake au madhaifu yake lakini cha ajabu unashangaa pamoja na hayo bado mtu yule anaendelea na msimamo wake wa kuambatana na mtu yule. Tambua yule ni mtu mwenye uelewa wa kutosha naamini ni yeye anaelewa ni kwa nini anaambatana na mtu yule, anajua ni kwa nini anashirikiana na mtu yule kwenye shughuli zake, yeye ndiye anajua ameona nini kwa mtu yule, pengine wewe huoni thamani kwa mtu yule, lakini yeye ameiona hiyo na hiyo ina nguvu kuliko sauti yako ya kumwaminisha kinyume, sauti yako anaona kama kelele tu, unatakiwa ujiulize unavyomwambia hayo wewe unaonekanaje kwa mtu huyo? Kwanini aamini unayosema? Una nini cha kukufanya aamini unachosema? Je una sababu za msingi za kuona yule mwingine hafai? Huyo ambaye hafai unamwelewaje? Unamfahamu sawasawa?
SOMA; Ushauri Kwa Waajiriwa Wapya Wote Wa Mwaka Wa Fedha 2014/2015
Tambua kuwa mtu yule yule unayemuona hafai , ipo sehemu anafaa sana kwa kuwa wale watu wameona kinachofaa au wameona thamani kwa mtu yule, huenda wamechagua kuiona thamani au mazingira yamewalazimisha kuona hivyo , maana hata kama hawamkubali au kumpenda lakini ndiye anayeweza jambo fulani ambalo wanalihitaji ili kuweza kufikia malengo yao katika maisha yao, hivyo wanalazimika kuwa na mtu yule, kumtumia mtu yule kama ngazi ya kufika kule. Kila mtu anaweza kumuona mtu yule yule kwa tofauti, inategemea kama una mtazamo gani juu ya wengine, kuwa na mtazamo chanya, tarajia kuona thamani hata kwa wengine, na ukiiona kama inakufaa itumie, usione aibu kusaidiwa hata na mtu unayeona hafai au hana hadhi ya kukusaidia au kukuelekeza jambo fulani, kumbuka Muumba wetu anaweza kumpa hata yule unayeona hafai thamani na ukalazimika kwenda kuhitaji huduma yake hata kama umemdharau sana, hata kama ulishaona hawezi kukuhudumia.
Katika maisha unavyoishi hebu jiulize una nini? Kwanini watu wakae chini wakusikilize? Unacho cha kuwasikilizisha? Kwanini niache wote nije kwako? Nitapata nini cha maana au cha tofauti?
Imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772

Ushauri Kwa Waajiriwa Wapya Wote Wa Mwaka Wa Fedha 2014/2015

Habari mpenzi msomaji , na karibu tena katika usomaji wa makala kupitia tovuti hii kama ukitumia vema makala hizi za kila siku zinazotolewa na blog hii hakika utaboresha maisha yako kwa namna moja au nyingine.
Awali ya yote nitumie fursa hii kuwapongeza wote walioajiriwa mwaka wa fedha 2014/2015 katika sekta mbalimbali. Mara nyingi watu huwa wanajisahau sana pale tu wanapopata ajira. Leo napenda kukushauri mambo ya msingi ya kufanya ili uendelee kuboresha maisha yako.
Vitu ambazo unatakiwa kuvifanyia kazi ni;
1. Kuweka Akiba
Huwezi kufikia uhuru wa kifedha kama wewe ni mtu ambaye hujui kuweka akiba, mtu ambaye ukipata mshahara unatumia wote na kusubiri mwingine mwezi ujao. Hii ni tabia mbaya sana ambayo itakuletea athari kubwa sana mbeleni akiba haiozi hivyo basi ya kupasa kuweka akiba weka asilimia 10 ya mshahara wako katika akaunti maalumu ambayo itakusaidia ukiwa na dharura.
Umuhimu wa akiba utaujua pale tu utakapopata tatizo au dharura katika maisha kwani matatizo yapo kila siku na hakuna binadamu ambaye hana tatizo kila mtu ana matatizo yake hivyo basi anza sasa kuweka akiba ili ufikie mafanikio hapo mbeleni unapokuwa huna ajira.
SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.
2. Usitegemee Chanzo Kimoja Cha Mapato
Kuendelea kutegemea chanzo kimoja cha mapato yaani ajira ni hatari sana .hivyo basi nakushauri mbinu mbadala ya kuwa na vyanzo vingine vya mapato tofauti na ajira ambayo unayo kwa sasa buni miradi mbalimbali ambayo itakusaidia na kukupelekea kuwa na uhuru wa kifedha. Anza maandalizi sasa ya kuandaa kuwa na vyanzo vingine vya mapato tofauti na ajira.
3. Ishi Chini ya Kipato Chako
Hili limekuwa ni tatizo kwa watu wengi kuishi juu ya vipato vyao ,watu wamekuwa wanaishi maisha ya kuiga sana bila kuangalia kipato chake ni kidogo maisha ya kushindana ni mabaya sana. Kwa mfano unakuta mtu kipato chake ni laki mbili lakini mtu huyo anaishi maisha juu ya laki mbili hapo ndipo tatizo linapoanzia.
Kuishi juu ya kipato chako kitakupelekea kwenye madeni na kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo kabisa kwa sababu tu unaishi maisha ambayo siyo yako ishi maisha yako mwenye na wala hupaswi kuiga.
4. Kuwa na Nidhamu ya Pesa
Hata uwe na hela kiasi gani kama huna nidhamu na pesa ni tatizo sana, acha tabia ya kununua vitu kwa hisia kwa sababu tu Fulani kanunua na wewe unapata shauku ya kuwa nacho usitumie pesa ovyo tumia tu kwa mahitaji muhimu sana, punguza au acha kabisa starehe ambazo zinamaliza pesa zako kila siku acha kuwa mtumwa wa kisaikolojia wa uvutaji wa sigara, ulevi nakadhalika.
5. Endelea Kujifunza Kila Siku
Kumaliza shahada au stashahada siyo wa kusoma au mwisho wa kujifunza. Unahitajika kujifunza kila siku ,unahitajika kukua kila siku kesho uwe zaidi ya leo ulivyo sasa, ongeza maarifa chanya kila siku katika maisha yako. Chakula cha ubongo wako ni maarifa na akili yako ni kiwanda cha maarifa soma, soma, soma vitabu kadiri uwezavyo vitabadili maisha yako ,jifunze kwa waliofanikiwa utafika mbali kuliko kuendelea kuridhika na kujiona kuwa umeshamaliza chuo huna haja tena ya kujifunza.
SOMA; Kozi 1100 Unazoweza Kujifunza Bure Kupitia Mtandao.
Kwa hiyo , ili uweze kufika safari yako ya kimafanikio ya kupasa uwe na malengo na mipango juu ya maisha yako kuishi bila malengo ni sawa na kusafiri safari ambayo hujui unapokwenda ni wapi. Jali sana afya yako kwani katika safari ya mafanikio kitu cha kwanza cha kuzingatia ni afya. Kumbuka kujilipa pia 10% ya kipato chako pay yourself first hivyo basi zingatia kujilipa kwanza wewe kwani wewe ndio unafanya kazi na unawalipa watu wengi lakini unajisahau kujilipa na hela unayojilipa ifanyie uwekezaji ili ikusaidie.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

Hatua Saba (07) Muhimu Za Kukamilisha Malengo Yako Makubwa.

Watu wengi hufikiri kuwa na lengo lilio fasaha pamoja na kuwa na mtazamo chanya kuhusiana na ukamilishaji wa lengo ndio msingi mkuu wanaohitaji ili kuweza kuwa na furaha pamoja na kufanikiwa. Lakini kumbe hata kabla hujaanza safari yako ya kukamilisha lengo lako ni muhimu kuwa na mipango hatua kwa hatua inayokuhakikishia uwezekano mkubwa wa kukamilisha lengo lako.
Hapa ninakuletea hatua saba zitakazokuwezesha kukamilisha lengo lolote ambalo unajiwekea
1. Amua ni nini hasa unakihitaji katika kila eneo la maisha yako. Unahitaji kufafanua lengo lako katika lugha rahisi kiasi kwamba mtoto mdogo aweze kuelewa. Mfano unaweza kusema lengo lako ni kuwa na fedha nyingi, lakini uwingi wa fedha unazotaka haujaweka ni fedha nyingi kiasi gani. Sasa kutokuwa fasaha katika lengo kunakupelekea kutokuwa na hamasa na kufanya maamuzi ya kukamilisha lengo.
2. Andika lengo lako na lifanye liwe linaweza kupimika. Lengo ambalo halijaandikwa linakuwa ni lengo ambalo halijahuishwa au halijapewa nguvu ya kuwa hai. Ukilifanya lipimike maanake unakuwa umetengeneza tageti unayotaka kuifikia.
SOMA; Jinsi Ya Kutengeneza Kipato Cha Ziada Ukiwa Unaendelea Kufanya Unachofanya Sasa.
3. Weka ukomo wa kukamilisha. Unahitaji kuwa fasaha ni lini unahitaji kukamilisha lengo husika. Sehemu ya ubongo inayoitwa “subconscious” inapenda kuwa na ukomo na hii inakusaidia kuwa na nguvu na kukupa hamasa ya kuelekea kufanikisha lengo husika
4. Ainisha vikwazo ambavyo unahitaji kuvivuka ili kukamilisha lengo. Fahamu kitu gani kinaweza kwenda tofauti. Fahamu ni kitu gani kipo kati yako na lengo. Fahamu kwa nini bado haupo katika lengo lako.
5. Tambua maarifa na ujuzi wa ziada ambao utahitaji ili kuweza kufikia lengo lako. Ili kuweza kufanikiwa kukamilisha malengo ambayo hujawahi kuyakamilisha hapo kabla unahitaji kujifunza na kuwafanya vitu vya tofauti ambavyo hujawahi kufanya kabla.
6. Watambue watu ambao utawahitaji wakusaidie au waungane nawe ili uweze kufikia malengo yako. Kufikia malengo makubwa unahitaji kuwa natimu ya watu wengi wa kukusaidia. Kwa hiyo unahitaji kuwa na ufasaha ni watu wa aina gani hasa unaowahitaji ili uweze kuwa na timu ambayo itakupa msaada unaouhitaji.
7. Tengeneza orodha ya maelezo kwa kila kipengele ambavyo nimeanisha hapo juu na uweke mpangilio katika mfuatano yaani kipi kinaanza na kipi kinafuata na pia ni muhimu kuwa na kipaumbele. Ni muhimu kujua kipi unahitaji kwanza, kipi ni muhimu.
Baada ya kukamilisha hatua hizo saba ni muhimu kufanya kila siku japo kwa udogo sehemu ya kufikia lengo lako.
Mwandishi: Goodluck Moshi
Mawasiliano:
Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi
Pia unaweza kutembelea blog yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.

Maisha Ni Safari Na Jinsi Unavyoweza Kufika Salama Safari Hii.

Habari ndugu msomaji wa makala za JIONGEZE UFAHAMU. Ni matumaini yangu u mzima. ni mwisho wa wiki sasa, kumbuka kufanya tathmini ya mambo uliyoyafanya wiki nzima, pitia malengo yako ya wiki hii kama yote yametimia na ongeza juhudi kukamilisha mipango yako ili uweze kufikia malengo ya mwaka uliyojiwekea. Napenda nikukumbushe kuwa kila siku unayoianza ni siku ya kipekee, haitaweza kurudia tena maishani mwako, ni zawadi nzuri sana ambayo Mungu amekupa. Tumia kila siku vizuri, uwe na furaha na uguse maisha wengine pia.
Maisha ni safari. Sio mara ya kwanza kuusikia usemi huu. Naomba leo nikupe mtazamo mwingine kuhusu usemi huu.
 
Siku za hivi karibuni nilikua nasafiri safari ndefu kiasi. Safari yangu ilikuwa ni ya kutoka Kigoma kuelekea Dodoma lakini nilipanda magari yanayoenda mpaka Dar-es-salaam. Nilivyoingia kwenye gari tu saa kumi na mbili asubuhi baada ya dakika chache nilipitiwa na usingizi. Baada ya muda nilishtuka na nikaona asilimia kubwa ya abiria wakiwa wamesinzia. Baada ya mwendo mrefu sana kama masaa saba nilihisi kuchoka tena nikasinzia.
Nilipoamka kama kawaida kuna baadhi ya abiria walikua wamesinzia, wengine walikua wanasimama na kukaa ili kupunguza uchovu waliokuwa nao. Makondakta wa gari walifanya hivyo pia. Kuna wakati walikua wakirudi kwenye viti vya mwisho wa basi wanalala kidogo halafu baada ya muda wanaenda tena mbele kuongea na dereva.
SOMA; Najua Umeshasikia Hili Mara Nyingi, Sio Vibaya Ukasikia Tena Na Leo.
Safari hii ilikuwa ndefu na ilimchosha kila mmoja aliyekua ndani ya basi. Hata bila kuuliza unagundua kuwa kila mtu amechoka. Abiria wengi walikua wamekunja sura zao wakijigeuza upande huu na upande ule, hayo yote yaliashiria uchovu waliokuwa nao.
Lakini cha ajabu, wakati wote huo dereva alikua halali wala hapumziki. Nilifikiria kwa muda jinsi ambavyo dereva alivumilia. Dereva katika akili yake alikua akifikiria furaha ya kutufikisha salama kule tulikokua tunaelekea. Sisi tulipokua tunalala bado yeye hakuwaza kuhusu usingizi na kuona kama sisi tunafaidi. Kama ingekuwa hivyo angetuamsha wote ili anapokuwa akiendesha gari na sisi tusilale kama yeye ambavyo halali. Lakini basi achana na sisi abiria, hata makondakta wa gari hilo nao walikua wakipumzika. Lakini dereva hakujali kwakua alikua akifahamu lengo lake lilikua ni kuendesha gari na kutufikisha kule tunakokwenda salama. Akikutana na vikwazo ajue jinsi ya kuvikwepa bila kushauriwa na mtu yeyote pembeni, lengo kuu ni kutufikisha salama kule tuendako.
Yaani kwa kifupi dereva yeye aliangalia lengo ambalo ni kusafirisha abiria na kuwafikisha salama kule wanakoenda .
Tunajifunza nini?
Ni vizuri kuwa dereva wa gari linaloitwa maisha yako. Ukiona unasinzia, unataka upumzike, unaangalia kama wengine wamepumzika, unawalazimisha wengine wakusaidie kuendesha gari lako ambalo ni maisha yako, unategemea maoni ya wengine ili ulifikishe gari lako salama ujue kuwa upo kwenye hatari ya kusababisha ajali ya maisha yako. Kama ambavyo kuna kanuni na sheria za barabarani ndivyo ambavyo kuna kanuni mbalimbali katika maisha ya kila siku.
Dereva alikua akiongea na kondakta na mara nyingine abiria , lakini pia trafiki aliokuwa akionana nao njiani. Lakini nia yake, lengo lake lilikua ni kufika alikokua amepanga kwenda ambako alikuwa anakufahamu. Hakuna aliyeweza kumtoa nje ya kusudio lake. Pale alipokutana na vikwazo alivuka vikwazo hivyo yeye mwenyewe bila kutegemea msaada wa mtu yeyote Yule. Gari lilipoharibika, fundi alilirekebisha lakini bado yeye alibaki kuwa dereva.
SOMA; Uadilifu, Kioungo Muhimu Cha Kufikia Mafanikio.
Ni vyema kuwa imara na wenye malengo yasiyoyumbishwa kama dereva huyu. Katika safari hii ya maisha utahitaji mawazo, msaada kutoka kwa wengine, utakutana na vikwazo na mambo mengine mengi njiani. Lakini haya yote yasikutoe nje ya malengo yako uliyonayo. Hakikisha wewe ndiye unayeshikilia usukani wa maisha yako kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari yako ili uweze kufurahia pale unapokuwa umefikia malengo yako na sio malengo ya wengine.
Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110
Whatsaap: 0652 025244
Face book: ESTHER ESTHER
estherngulwa87@gmail.com

Aina TANO(5) za Uwekezaji Zinazoweza Kubadili Maisha Yako



Ili kuweza kuwa na utajiri endelevu katika maisha yako na unaojitosheleza ni muhimu ukawa mwekezaji. Uwekezaji upo wa aina nyingi. Hapa ninakuletea aina za uwekezaji unazoweza kuzifanya ili kukuwezesha wewe na wale watu wako wa karibu kuishi maisha ya utajiri wa kujitosheleza:
1.     Uwekezaji binafsi
Watu ambao wanatengeza utajiri wanafanya uwekezaji binafsi . hawa wanakuwa wasomaji kwa kujifunza. Daima huweka jitihada ya kujiboresha wao wenyewe siku hadi siku na kuongeza mipaka ya maeneo ambayo wanona wakijaribu watafanikiwa. Wanaongeza maarifa na uwezo wa kushawishi siku hadi siku. Na kiwango cha jitihada wanachoweka katika kujiboresha huwa kipo katika hali ya kukua siku hadi siku.
2.     Kuwekeza kwa wengine
Mwanamafanikio maarufu duniani Zig Ziglar alisema ukitaka kupata kitu chochote katika maisha ni vizuri uwasaidie wengine wapate vile wanavyovihitaji katika maisha yao. Watu wenye utajiri utagundua wamewekeza kuwasaidia wengine wafikie malengo yao na hivyo kusababisha na wao kufanikiwa kwa kuwafanikisha wenzao

3.     Wekeza katika taasisi
Katika taasisi unayofanya wekeza katika kuijenga taasisi hiyo ili iweze kuwa bora na taasisi inapoweza kuwa bora inawezesha kuongeza upataji wa mapato. Kuongezeka kwa mapato kwa taasisi kwa ujumla kunasaidia pia wale waliosababisha kuongezeka kwa mapato kuneemeka na hiyo faida. Kwa hivyo hili likifanyika katika kipindi chako cha kutumikia taasisi yako maanake utaongeza kujenga utajiri siku hadi siku.
4.     Wekeza katika mali zinazoongezeka thamani
Ubadilishaji wa fedha kwenda katika mali ambazo zinaongezeka thamani na zinafanya kazi badala yako siku hadi siku huongeza utajiri kwako. Mfano wa hili ni nyumba ambayo imejengwa kwa lengo la kupangasha au kukodisha. Sasa ile fedha uliyowekeza katika hiyo nyumba utaipata kwa kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka bila yaw ewe kufanya kazi.
5.     Wekeza katika mawazo
Vitu vingi tunavyoviona leo havikuanza moja kwa moja bila kupitia hatua Fulani, vingi vilianza kama wazo na kuendelezwa. Mawazo amabyo ni mazuri yakichanganywa na uchukuaji hatua wa kuyaweka katika matendo huleta matokeo mazuri ambayo yanaleta utajiri


Mwandishi: Goodluck Moshi
Mawasiliano:
Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi
Pia unaweza kutembelea blog yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.

Kama Hutengenezi Hiki Mahali Ulipo Hustahili Kulipwa Chochote.



Ndugu msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU salamu. Karibu katika makala yangu ya leo. Napenda kutumia wasaa huu kuzungumza na wewe japo kwa ufupi kuhusu maisha. Katika maisha tumekuwa tukifanya mambo mengi sana, mengine yana faida lakini mengine mengi ni ya hasara sana kwetu hasa ukizingatia kwamba muda tulio nao hapa duniani ni mfupi sana na umehesabiwa na aliyetuumba, hivyo katika kila unachofanya ni vyema sana ukautumia muda wako vizuri kwani hutaweza kamwe kupata nyongeza ya japo saa moja kwa siku ili yafike 25.
Ndugu msomaji nikiandika hapa najua unasoma kwa sababu kuna kitu cha muhimu ambacho najua utakwenda kukipata. Unajua unapofanya kitu chochote katika dunia hii kuna malipo ambayo kwa kiasi kikubwa unayategemea ambayo yanaweza kuwa katika vitu au isiwe katika vitu (material and non-material things). Kwa wengi mategemeo haya yamekuwa yakiwasukuma kufanya kazi na kupata hicho wanachokitarajia. Kama ni mfanyakazi unategemea upate mshahara na marupurupu na kama ni mfanyabiashara unategemea kupata faida. Lakini hata kama wewe ni mwanafunzi nawe unahitaji kufaulu katika hatima ya masomo yako. Najua na naelewa vyema kuwa hakuna mtu atakayekupa hayo yote kama hakuna ulichokifanya.
Ndugu msomaji huwezi kulipwa kwa sababu wewe unafanya kazi saa nyingi kwa siku, huwezi kulipwa kwa sababu wewe una elimu kubwa wala huwezi kulipwa kwa sababu wewe ni mtanashati au mrembo sana. Utalipwa tu kama umefanya jambo lenye thamani. Kama hutatengeneza thamani yoyote kazini, shuleni, biasharani au popote pale ambapo wewe unapaswa kuwapo basi hustahili kulipwa chochote na wakati mwingine unastahili adhabu. Thamani utakayoitengeneza katika kile unachokifanya itatoa mchango katika nyanja za maisha ambazo wewe umezisimamia. Mchango wako katika sehemu ndio pia ambao utakupa furaha na kukuongezea uwezo wa kujiamini. Huwezi kujiamini kama hujatekeleza yale ambayo unapaswa wewe kuyafanya.
Ili uweze kutengeneza thamani katika kile ambacho unakifanya ni lazima kwanza uutumie vyema muda wako katika kufanya yale yenye thamani kubwa kwako kwanza kabla ya yale yenye thamani ndogo na pia kufanya jambo moja kwa wakati mmoja na sio kushika mambo elfu kwa wakati mmoja. Ukweli ni kwamba utafanya yote lakini hakuna hata moja ambalo utalifanya kwa ubora wake na hivyo kuondoa thamani yake. Kuwa yule mtu ambaye akikosekana sehemu kwa muda mfupi umuhimu wake unaweza kuonekana na thamani yake yaweze pia kuonekana. Kama ulipo hauna thamani ni muda wa wewe kujiongezea thamani au uondoke kwani hakuna utofauti wa wewe kuwepo ama kutokuwepo. Ninaposema fanya jambo moja kwa wakati mmoja (focus) namaanisha kuwa fanya kile unachokikusudia kukifanya tu na si vinginevyo. Mathalani upo kazini lakini unachokifanya ni kupiga soga, kutembelea mitandao ya kijamii na kutega tega kazi kiasi kwamba kufikia muda wa kuondoka unakuwa umetumia chini ya asilimia sabini katika kazi na kuwa na mzigo wa kuufanya unaporudi nyumbani. Kwa wale washabiki wa mpira wanajua thamani ya mchezaji haitokani na chenga anazopiga au kasi yake uwanjani bali idadi na uwezo wake wa kufunga magoli. Kumbuka katika mpira wa miguu chenye thamani ni magoli ambayo ndiyo huleta ushindi.
Labda nikupe mfano mdogo, wewe ni meneja masoko wa kampuni fulani na unaona mwenendo wa kampuni sio mzuri katika mauzo unaweza kubuni mbinu mpya na kuongeza mauzo. Katika hili umetengeneza thamani na wewe umeongeza thamani yako pia. Kwa maana hiyo unaweza kumfuata bosi wako na kumwambia akuongeze mshahara naye bila shaka atakubali kulingana na faida unazoleta.
Ni wakati wa wewe kukaa chini sasa na kutafakari kuhusu thamani yako sehemu uliyopo. Ongeza thamani yako na wewe pia utafaidika. Usikae kulalamika kuwa mshahara hauongezewi wakati bosi wako haoni unachokifanya. Usitegemee kufanya jambo lile lile kwa namna ile ile na utegemee kuongeza thamani bali badili namna unavyoenenda nawe utaona mafanikio.
Mwisho nirudie kwa kusema kuwa thamani yako mahali ulipo haitokani na kiasi gani muda unaokaa kazini, kiwango cha elimu ulicho nacho, uzuri, au uwezo wako bali kitu kimoja tu ambacho ni thamani unayotengeneza.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes
Unaweza kuwasiliana na nae kwa: simu: 0712 843030/0753 843030
                                                                     e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake:  www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.