Karibu Kwenye Semina Ya Mafanikio Kwenye Biashara Mwaka 2015.
Huu ni wakati ambao karibu kila mtu anahitaji kuingia kwenye biashara. Haijalishi mtu ameajiriwa au hana ajira, haijalishi kiwango cha elimu mtu alichonacho na wala haijalishi umri wa mtu, kwa sasa kila mtu anahitaji kuwa kwenye biashara.
Ajira zimekuwa za shida kupatikana na hata wale wanaozipata bado haziwawezeshi kuyamudu maisha. Changamoto ni nyingi sana. Njia ya uhakika ya kuweza kupambana na changamoto hizi ni kuingia kwenye biashara,
Mazingira ya kuingia kwenye biashara nayo yamebadilika pia. Tofauti na zamani ambapo ilihitaji mtu kuwa na uwezo mkubwa sana wa kifedha ndio aweze kuingia kwenye biashara, sasa hivi unaweza kuingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo sana.
Pamoja na umuhimu huu wa kuingia kwenye biashara na urahisi wa kufanya biashara, bado kuna changamoto kubwa sana wkenye biashara. Biashara nane kati ya kumi zinazoanzishwa zinakuwa zimeshakufa ndani ya miezi 18. Na hata zile ambazo zinapona kipindi hiki, nyingi hazifikii mafanikio makubwa.
Watu wengi wanaweka juhudi kubwa sana kwenye biashara ila bado hawaoni mafanikio waliyotarajia. Hili linawaangusha wengi sana na wengi kukata tamaa.
Matatizo haya mengi yanatokana na kukosekana kwa elimu sahihi ya biashara, kukosa mtazamo sahihi wa kufanikiwa kwenye biashara, kutokujua mbinu za mafanikio kwenye biashara na kufanya biashara kwa mazoea.
Ili kuwasaidia wafanyabiashara na wale ambao wanapanga kuingia wkenye biashara kuweza kuondokana na changamoto hizi, AMKA CONSULTANTS imeandaa SEMINA YA MAFANIKIO KWENYE BIASHARA 2015. Semina hii itakupatia wewe elimu sahihi, mbinu muhimu na mtazamo sahihi utakaokuwezesha kufanikiwa kwenye biashara yako.
Hii sio semina ya kukosa kwa sababu imejaa mambo mengi ambayo hujawahi kuyapata sehemu nyingine yoyote.
Semina hii imeandaliwa kuweza kukidhi mahitaji ya kufanikiwa kwenye biashara kwa mazingira yetu ya kitanzania. Semina hii itakuwezesha wewe kutoka hapo ulipo sasa na kupiga hatua kubwa sana kibiashara.
Semina hii itaendeshwa kwa njia ya mtandao na itaendeshwa kwa kipindi chote cha mwezi wa tano.
Washiriki wa semina hii watatumiwa email ya mafunzo kila siku asubuhi, kupata nafasi ya kuisoma na kuweza kuuliza swali popote ambapo hajaelewa. Email hizi zitakuwa na mafunzo yaliyofanyiwa utafiti w akina pamoja na mifano ambayo itamwezesha mshiriki kpata mawazo tofauti anayowez akuyatumia kwenye biashara yake na akafanikiwa sana.
Semina hii itafundisha mambo yafuatayo;
SEMINA YA MAFANIKIO KATIKA BIASHARA.
Anza, kuza na fanikiwa kupitia biashara.
Yatakayofundishwa;
1. Utangulizi
1.1. Huu ni wakati mzuri wa wewe kuwa kwenye biashara.
1.2. Unawezakufanikiwa kwenye biashara.
1.3. Utakachokipata kwenye kozi hii.
2. Wazo la biashara
2.1. Biashara sahihi kwako kufanya
2.2. Jinsi ya kupata wazo bora la biashara
2.3. Jinsi ya kuboresha wazo lako la biashara
2.4. Baadhi ya mawazo ya biashara.
3. Mchanganuo wa biashara.
3.1. Umuhimu wa mchanganuo
3.2. Vitu muhimu vya kuweka kwenye mchanganuo wako
3.3. Udhaifu na uimara wako
3.4. Utafiti wa biashara yako
3.5. Ushindani.
3.6. Kuajiri wasaidizi bora kwenye biashara yako.
4. Mtaji na vyanzo vyake.
4.1. Aina za mtaji unaohitaji kwenye biashara
4.2. Mtaji wa fedha na vyanzo vyake
4.3. Njia bora za wewe kupata mtaji wa biashara.
5. Urasimishaji wa biashara
5.1. Umuhimu wa kusajili biashara yako.
5.2. Aina za usajili na faida zake
5.3. Hatua za kusajili biashara yako
5.4. Umuhimu na jinsi ya kulinda biashara yako.
6. Thamani ya biashara yako
6.1. Maandalizi ya bidhaa au huduma
6.2. Upatikanaji na upakiaji wa bidhaa au huduma
6.3. Upangaji wa bei.
7. Masoko na uuzaji.
7.1. Chagua soko la biashara yako
7.2. Mpango bora wa kutangaza biashara yako.
7.3. Njia rahisi za kutangaza biashara yako.
7.4. Mbinu za kuongeza mauzo kwenye biashara yako.
8. Mzunguko wa fedha.
8.1. Mauzo na faida.
8.2. Gharama muhimu za biashara
8.3. Gharama za kuepuka kwneye biashara
8.4. Kujilipa wewe mwenyewe.
8.5. Hesabu za fedha na umuhimu wa mhasibu.
9. Huduma kwa wateja.
9.1. Lengo la biashara ni kutengeneza wateja.
9.2. Jinsi ya kutoa huduma bora kwa mteja.
9.3. Mfanye mteja atangaze biashara yako.
9.4. Mteja ni mfalme na mwisho wa ufalme wake.
10. Changamoto za biashara.
10.1. Changamoto zinazoua biashara nyingi
10.2. Umuhimu wa mabadiliko
10.3. Mbinu za kufufua biashara inayokufa.
11. Mafanikio ya biashara yako
11.1. Jifunze kila siku
11.2. Matumizi mazuri ya muda
11.3. Kujihamasisha mwenyewe
11.4. Mafunzo kwa wafanyakazi wako
11.5. Usimamizi mzuri wa biashara yako.
11.6. Kununua uhuru wako kutoka kwenye biashara yako.
Gharama za kushiriki semina hii ni tsh elfu 30(30,000/=), ili kupata nafasi ya kushiriki semina hii tuma fedha za kushiriki kwa Mpesa 0755953887 au tigo pesa/airtel money 0717396253 kisha tuma majina yako na email kwenye moja ya namba hizo na utaandikishwa kwenye semina hii. Uandikishaji unaanza leo tarehe 20/04/2015 na utasitishwa tarehe 01/05/2015. Wahi kujiandikisha mapema kwani nafasi ni chache na zitakapojaa utakosa nafasi hii adimu ya kupata maarifa ya kukuwezesha kufanikiwa kwenye biashara yako.
Kumbuka semina inafanyika kwa njia ya mtandao hivyo popote ulipo Tanzania na hata nje ya Tanzania unaweza kushiriki semina hii.
Semina itaanza rasmi tarehe 04/05/2015 na itaendeshwa kwa mwezi mzima.
Karibu kwenye semina hii ambayo itakupatia kila unachohitaji ili kufanikiwa kwenye biashara yako.
Kumbuka maarifa ni nguvu, pata maarifa sahihi kupitia semina hii ili uweze kuwa na nguvu za kutosha na zitakazokuletea mafanikio makubwa.
Karibu sana na hakikisha hukosi semina hii kwa sababu yoyote ile.
TUPO PAMOJA.
4/20/2015 05:00:00 PM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO | 0 Comments
Kijana Punguza Mambo Haya Ili Uweze Kupata Mtaji Wa Kuanza Biashara -1
Vijana wengi wamekuwa wakilalamika ni wapi wanaweza kupata mtaji na kuweza kufanya biashara ili kuboresha maisha yao. Lakini vijana hao ndio watu wa kwanza wanaongoza kwa matumizi mbalimbali yasiyo na tija na kufanya starehe sana bila kujua kuwa hizo starehe wanazofanya wangezipunguza au kuacha kabisa na kuweka hiyo hela ili waweze kupata mtaji wa kufanya biashara wanazopenda .
Punguza Mambo Haya ili uweze kupata mtaji
1. Kamari (Kubeti)
Watu wazima hata vijana wengi siku hizi wanapoteza sana rasilimali muda katika kucheza kamari. Huwezi kuwa na uhuru wa kifedha (tajiri) kwa kucheza kamari, watu waliofanikiwa duniani na wenye uhuru wa kifedha hawajafanikiwa kwa kucheza kamari kama wewe unavyodhania na kuendelea kubeti kila siku na kuliwa kila siku katika mchezo huo.
SOMA; Hii Biashara Inaliangamiza Taifa, Tujiepushe Nayo.
Watu wengine wanaweza kubeti kwa siku zaidi hata ya elfu 20 kwa siku akitegemea atashinda hela nyingi na mambo humwendea mrama bila mafanikio yoyote. Kesho pia anajaribu tena kubeti akiwa na imani kuwa ipo siku ataweza kushinda. Mchezo huu wa kubeti anayefaidika ni Yule anayemiliki hiyo kampuni na siyo wewe bali wewe ndio una mtajirisha bila wewe kujua.
Je unaweza kujiuliza tokea uanze kubeti mpaka leo umepoteza shilingi ngapi?
Je kama ungeweza kuwekeza hela zako hizo kila siku bado tu hujapata mtaji? Mpaka hapo hujaweza kujiajiri?
Ni vema sana na ni bora sana ukaitumia fedha hiyo unayopoteza kila siku katika kamari na kuiwekeza fedha hiyo katika soko la hisa na kuendelea kupata faida bila kupoteza hela yako kama ulivyokuwa unapoteza katika kamari au kama unavyoendelea kupoteza fedha yako katika kamari.
Huu ni ushauri wa bure ambao unaweza ukautumia na kujikomboa kuliko kuendelea kucheza kamari.
SOMA; Hawa Ndio Wateja Rahisi Kuwapata Kwenye Biashara Yako.
2. Ulevi
Kitu chochote ukizidisha ni sumu, ulevi wa kupindukia ni sumu pia, siwezi kukuzuia kunywa ila kunywa kiasi punguza pombe au vilevi unavyotumia kila siku na kutumia hela hiyo unayopunguza kupitia pombe hizo unazonunua kila siku na kuweka akiba yako ili uweze kupata mtaji wako wa kufanya biashara halali unayoipenda na kuweza kupata kipato chako .
Vijana wengi wamekuwa ni watu wa starehe kupita kiasi ambayo baadaye inakuletea madhara makubwa utakuja kushtuka pale ambapo huwezi tena kufanya kazi. Ni vema ukautumia muda huu kufanya mabadiliko, amka kijana, amka Mtanzania ili uweze kuhalalisha ndoto yako.
Kama una uwezo wa kunywa bia tano au zaidi kwa siku kwa bei ya sasa ya bia moja na ukijinyima kwa mwezi bado hujapata mtaji?
Usisubiri mpaka upate mtaji mkubwa sana anza na mtaji mdogo na Ujasiriamali mdogo mdogo ambao utakupeleka juu kufikia mafanikio makubwa. Tunaweza kupata mfano kwa bilionea kutoka Afrika Alihaji Aliko Dangote ukisoma wasifu wake yaani wasifu wake alianza kupenda ujasiriamali tokea yuko darasa la tatu na alikuwa anauza pipi au peremende je leo yuko wapi?
SOMA; Ni Lipi Dhumuni Lako Kwenye Maisha? Langu Ni Hili Hapa.
Angalia mapinduzi anayofanya Mtwara kujenga bandari na kujenga kiwanda cha saruji ni jinsi gani mtu huyu ataweza kuwakomboa watanzania wa mahali husika ambapo anajenga vitu hivyo na kuleta mabadiliko chanya mengi. Hivyo usidharau kidogo anza nacho leo kipende na ujifunze utafanikiwa.
Mpenzi msomaji wa makala hii asante kwa muda wako na endelea kufuatilia tena mwendelezo wa makala hii wiki ijayo siku kama ya leo (Jumatatu).
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au barua pepe deokessy.dk@gmail.com au tembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye anatafsiri/kuhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali barua pepe: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422. tovuti http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/20/2015 07:30:00 AM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Kuna watu ambao wangetamani kuwa wajasiriamali. Wanapoona mafanikio ya wajasiriamali wakubwa wanatamani sana kama wangekuwa wao.
Hijalishi unatamani kiasi gani kuwa mjasiriamali, tamaa yako tu haitakuwezesha kufikia mafanikio katika ujasiriamali. Ni lazima uwe na misingi ambayo utaisimamia ndio uweze kuona mafanikio makubw akupitia ujasiriamali.
Kwanza ni lazima uondoke kwenye kutamani na uingie kufanya na ukishaingia kufanya uwe tayari kukabiliana na lolote litakalojitokeza mbele yako.
SOMA; Maswali Matatu Muhimu Ya Kujiuliza Kwenye Wazo Lako La Biashara.
Leo hapa UTAJIONGEZA na vitu vitano muhimu vya kufanya unapokuwa tayari kuingia kwenye ujasiriamali.
1. Usianze tena kujishuku.
Ukishaamua kwamba wewe umechagua njia ya ujasiriamali, sahau kuhusu kujishuku na kuanza kuwa na wasi wasi kama kweli utaweza. Kikubwa ni nia yako ya kufikia mafanikio kupitia ujasiriamali. Matatizo, changamoto na vikwazo kila mtu anavipitia. Hivyo acha kuwa na wasi wasi kama utaweza na jitoe kwa asilimia 100 kufanya kile ambacho umeamua kufanya.
Kwenye ujasiriamali hakuna kujaribu, kuna kufanya. Fanya sasa na ondoa wasi wasi na hofu.
SOMA; SIRI YA 20 YA MAFANIKIO; Iendee Dhahabu...
2. Kuwa na mshauri.
Kuna ushauri wa bure ambao unapatikana kila mahali kwenye maisha yetu ya kitanzania. Ushauri kama, biashara fulani inalipa kweli yani, ukianza kuifanya tu, utapata mafanikio makubwa. Ukimuangalia anayekupa ushauri huo nae amesikia kwamba biashara hiyo inalipa.
Sasa hawa sio washauri ambao nakuambia uwe nao. Nakuambia uwe na mshauri ambaye anaelewa ni nini hasa anachokuambia. Mtu ambaye amekuwa kwenye safari ya ujasiriamali na anaujua ugumu wa safari hiyo. Mtu ambaye hatakuwa mnafiki kwako kukuambia mambo ili tu kukupa moyo na kukufurahisha, bali atakuambia ukweli, na ukweli huu utakufanya uweze kutumia mazingira yako vizuri kufikia mafanikio.
SOMA; UKURASA WA 43; Ushauri Wa Bure Una Gharama Kubwa.
3. Jitengenezee utaratibu wako wa kila siku, ambao utauheshimu.
Tofauti ya ujasiriamali na kazi zingine ni kwamba kwenye ujasiriamali wewe unajiongoza mwenyewe. Hakuna atakayekugombeza au kukutishia kukufukuza kazi kama utakuwa mzembe. Na hii ni hatari kubwa sana kwa sababu kama huwezi kujiongoza mwenyewe utashindwa kwenye ujasiriamali.
Njia rahisi ya kuweza kuanza kujiongoza mwenyewe ni kuwa na utaratibu wako wa kila siku ambao utaufuata na kuuheshimu. Ipangilie siku yako kabla hujaianza na weka vipaumbele kwenye malengo na mipango yako kwenye maisha na kupitia ujasiriamali unaofanya.
4. Acha kukaa na watu ambao wanakurusisha nyuma.
Tumeshajadili hili mara nyingi sana kwamba wewe ni wastani wa watu watano ambao wanakuzunguka. Hivyo kama umezungukwa na watu watano ambao hawana malengo yoyote kwenye maisha yako, ni vigumu sana wewe kuweka malengo na kuyasimamia. Hivyo wewe unapoamua kuingia kwenye ujasiriamali usikubali kukaa tena na watu ambao mawazo yao yanakurudisha wewe nyuma. Wewe unajua kwamba kwenye ujasiriamali, hasa wakati wa mwanzo unaweza kujikuta unafanya kazi mpaka masaa 16 au 20 kwa siku, lakini rafiki zako wanataka kila siku jioni mkutane mkipata moja moto na moja baridi, hii hutaiweza wewe kama mjasiriamali, niamini.
SOMA; UKURASA WA 11; Watu Hawa Wanakurudisha Nyuma.
5. Kuza mtandao wako.
Tumesema sana hili pia, haijalishi unajua nini bali unamjua nani. Unapoamua kuingia kwenye ujasiriamali hakikisha kila mtu anayehusika na aina ya ujasiriamali unaofanya anajua kuhusu wewe na kile unachofanya. Angalia watu muhimu ambao unahitaji ushirikiano wao, watafute, angalia ni jinsi gani unaweza kuwasaidia ili nao wakusaidie, kukua zaidi.
Kama unafikiri kwenye ujasiriamali utashinda kwa jeshi la mtu mmoja umepotea njia, ongea na watu wengi uwezavyo, wajue unachofanya na wao watakuunganisha na watu wengi zaidi.
Haya ndio mambo matano muhimu sana ya wewe kufanya pale unapoamua kwamba ujasiriamali ndio maisha yako. Na miaka sio mingi kila mtu atahitaji kuwa mjasiriamali, hivyo ni vyema kama utaanz akujiandaa mapema.
Kwa ushauri wowote kuhusu biashara na ujasiriamali tafadhali tuma email kwenda ushauri@kisimachamaarifa.co.tz
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio kupitia ujasiriamali.
TUPO PAMOJA.
2/19/2015 12:00:00 PM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA BIASHARA | 0 Comments
Maswali Matatu Muhimu Ya Kujiuliza Kwenye Wazo Lako La Biashara.
Hakuna changamoto kubwa kama kupata wazo zuri la biashara na ambalo litakuwezesha kupata mafanikio na mafanikio makubwa.
Japo nimeshaandika mara nyingi sana jinsi ya kutengeneza wazo zuri la biashara, bado maswali mengo ninayopata kutoka kwa wasomaji ni wazo gani la biashara ni zuri na lenye faida.
Leo tutajifunza maswali matatu muhimu ya kujiuliza kwenye wazo lolote la biashara ili kujua kama litakuletea faida.
SOMA; Vitu VITATU Vinavyoathiri Kipato Chako Na Jinsi Ya Kukiongeza.
Muhimu ni kujua kwamba kila wazo la biashara ni zuri na linaweza kuleta faida. Changamoto ni jinsi gani unaweza kulitekeleza wazo hilo ili liweze kukuletea faida hiyo. Kupitia maswali haya matatu utaweza kuliweka wazo lako vizuri na hatimaye kuweza kutengeneza biashara kubw akupitia wazo hilo.
1. Je nawezaje kulipwa kwa wazo hili?
Jiulize swali hili muhimu sana kwamba unawezaje kulipwa kwa wazo ulilonalo. Unawezaje kulipwa kwa kile unachopenda kufanya?
Tuseme labda unapenda kuchora, je unawezaje kulipwa kwa kuchora? Hapa unaweza kupata majibu kama kuchora kazi za kisanaa, kuchora ramani za majengo, kuanzisha jarida la vibonzo na mengine mengi.
2. Je nitalipwa kiasi gani kutokana na wazo hili?
Kupata uhakika wa kulipwa kutokana na wazo bado hakutoshi wewe kujihakikishia biashara. Swali jingine muhimu la kujiuliza ni nitalipwa kiasi gani kwa wazo hili? Ni lazima ujue kiwango ambacho unaweza kulipwa kutokana na wazo lako. Na pia uone kiwango hiko unacholipwa kitakuwezesha kuendelea na biashara hiyo.
Kwenye mfano wetu wa kuchora hapo juu, huendakuchora vibonzo kunalipa, ila kuchora ramani za majengo kunaweza kulipa zaidi.
SOMA; Sheria NANE Za Kufanikiwa Kwenye Biashara Kutoka Kwa Warren Buffett.
3. Je kuna njia ambayo naweza kulipwa zaidi ya mara moja?
Wazo zuri la biashara ni lile ambalo unaweza kulipwa zaidi ya mara moja. Kama una biashara ambayo mtu akishanunua ndio imetoka na hawezi kurudi kwako tena ni vigumu sana kutengeneza biashara endelevu.
Ila kama utakuwa na njia ya kuweza kulipwa zaidi ya mara moja, au mteja kuja tena na tena utaweza kujenga biashara nzuri na yenye mafanikio makubwa.
Jiulize na kujijibu maswali hayo matatu na utaweza kulijenga wazo lako la biashara na likakuletea mafanikio makubwa sana.
TUPO PAMOJA.
2/18/2015 01:00:00 PM | Labels: BIASHARA | 0 Comments
Vitu VITATU Vinavyoathiri Kipato Chako Na Jinsi Ya Kukiongeza.
Katika mfumo wa uchumi tunaoishi sasa hivi duniani, ni dhahiri kwamba kipato chako kinaathiriwa na vitu vingi sana.
Kipato chako kinaweza kuathiriwa na hali ya uchumi inavyokwenda. Kwa mfano mfumuko wa bei unapokuwa mkubwa, kipato chako kinaweza kisitoshe matumizi yako. Lakini hii ni nguvu ya nje ambayo huwezi kuiathiri.
Kipato chako pia kinaathiriwa na mambo ambayo yanatokana na wewe binafsi na mambo haya unawezakuyabadili ili kubadili kipato chako.
Leo tutajadili vitu vitatu muhimu vinavyoathiri kipato chako na jinsi unavyoweza kuvitumia kubadili kipato chako.
Ni ukweli usiopingika kwamba kila mtu anapenda kipato chake kiongezeke, ila sasa unaanzia wapi kukiongeza? Jua vitu hivi vitatu na vifanyie kazi.
1. Unafanya nini.
Kitu cha kwanz akabisa kinachoathiri kipato chako ni unafanya kitu gani? Yaani ni shughuli gani unayofanya ili kujitengenezea kipato? Unafanya biashara? Umeajiriwa? Kama unafanya biashara je ni biashara gani? Na kama umeajiriwa je una utaalamu gani? Tunajua kabisa vipato vinatofautiana na kutokana na kile unachofanya. Kipato cha mwalimu hakiwezi kuwa sawa na cha daktari. Kipato cha boda boda hakiwezi kuwa sawa na cha dala dala.
Kuongeza kipato chako kwenye njia hii ni kuhakikisha unafanya kitu ambacho kina uwezekano mkubwa wa kutengeneza kipato kikubwa.
SOMA; HADITHI_FUNZO; Aliyenusurika Kufa Kutokana Na Tabia Yake Nzuri.
2. Unafanya kwa ubora gani?
Tumeona vipato vinatofautiana kutokana na vitu tofauti. Vile vile ndani ya fani moja au biashara moja, bado vipato havilingani. Watu wawili wanaweza wote kuwa walimu wenye kiwango sawa cha elimu lakini vipato vikawa tofauti. Watu wawili wanaweza kuwa wanaedesha boda boda na wanapaki eneo moja lakini vipato vikawa tofauti. Kwa yule ambaye anafanya kwa ubora wa hali ya juu kipato chake lazima kitakuwa kikubwa.
Hakikisha kile ambacho unakifanya unakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.
3. Ugumu wa kukubadili.
Kipato chako pia kinaathiriwa na ugumu wa kukubadili wewe kwenye hiko unachofanya. Pata picha wewe unafanya kazi ambayo ni wewe tu unaweza kuifanya, hii ina maana kwamba kama usipokuwepo kazi yako haiwezi kufanywa na mtu mwingine hivyo thamani ya kipato chako inakuwa kubwa. Hali kadhalika kama unafanya biashara kwa kiwango ambacho mteja wako hawezi kukipata sehemu nyingine, lazima utakuwa na kipato kikubwa.
Anza sasa kujitengenezea mazingira ya wewe kuw avigumu kubadilishwa. Na sio ufanye hivyo kwa kuwafanyia wengine majungu, ila kwa kujiboresha zaidi na hivyo kufanya kazi au biashara yako kwa ubora wa hali ya juu.
Chukua hatua leo ili kuboresha kipato chako, acha kulalamika, maamuzi ni yako.
SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.
1/23/2015 02:00:00 PM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO | 0 Comments
Sheria NANE Za Kufanikiwa Kwenye Biashara Kutoka Kwa Warren Buffett.
Warren Buffett ni mmoja wa watu matajiri sana duniani. Utajiri wake huu ameupata kupitia biashara na uwekezaji. Alianza biashara akiwa na miaka 11 na sasa ana miaka 83. Kwa miaka zaidi ya 60 ambapo amekuwa kwenye biashara una uzoefu wa kutosha kutufundisha sisi ni vitu gani vya kuzingatia kwenye biashara.
Hizi hapa ni sheria 8 za kufanikiwa kwenye biashara kutoka kwa Warren Buffett.
1. Tulia wakati wa matatizo/changamoto.
Katika biashara kuna wakati ambao utakutana na changamoto na matatizo mbalimbali. Huu ni wakati ambao Warren anatushauri tutulie badala ya kuvurugwa na hatimaye kuharibu kila kitu.
SOMA; Maswali Matatu Kwa Anayetaka Kuwa Mjasiriamali Kujiuliza Kutoka Kwa Richard Branson.
2. Zungukwa na watu wazuri.
Kama unafanya biashara kwa kushirikiana na mtu au watu wengine, hakikisha watu hawa wana maadili mazuri na wanandoto kubwa ya mafanikio kama uliyonayo wewe.
3. Ng’ang’ania kile unachokitaka.
Warren anashauri kwamba usiache lengo lako kuu kwa sababu kuna vitu vizuri umeviona pembeni, kufanya hivi kutakuletea kushindwa.
4. Weka gharama chini.
Hakikisha gharama za kuendesha biashara yako zinakuwa chini sana ili uweze kuuza kwa bei ambayo wateja wako wanaweza kuimudu na wewe kupata faida.
SOMA; Hakuna Anayejua Anachofanya, Na Huo Ndio Uzuri Wa Maisha.
5. Toa zawadi kwa wafanyakazi wako.
Warren anashauri kwamba pale wafanyakazi wanapofanya vizuri uwape zawadi hata kama ni ndogo kiasi gani. Hii inawafanya waone unajali.
6. Epuka matatizo.
Warren aliwahi kumwandikia mshirika wake kwenye biashara hivi “nachotaka kujua ni wapi nitaenda kufa hivyo nisiende hapo kamwe”. Kama unataka kufanikiwa kwenye biashara unahitaji kuepuka matatizo maana matatizo mengi yanasababishwa na wewe mwenyewe.
7. Fanya kuwa ndogo.
Buffett anasema kwamba biashara inapokuwa kubwa sana inakuwa vigumu kubadilika na urasimu unakuwa mkubwa kiasi cha kuwachosha wafanyakazi na hata wateja. Anashauri kurahisisha uongozi wa biashara hivyo hata ikikua sana bado ionekane ni ndogo na rahisi kuongoza na kuwasiliana.
8. Linda heshima yako.
Buffett anasisitiza kwamba heshima yako ni kitu muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara. Anashauri kuwa mwaminifu na kutofanya kitu chochote ambacho usingependa kiripotiwe kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti. Anasisitiza hili kwa kauli hizi mbili;
Poteza hela za biashara na nitakuelewa, poteza sifa ya biashara na nitakuwa mbaya sana kwako.
Inakuchukua miaka 20 kujenga heshima na dakika tano kuiharibu. Ukifikiria hili utafanya mambo kwa tofauti.
Tumia sheria hizi nane kwenye maisha yako ya kila siku na ya biashara na zitakusaidia sana kufikia mafanikio.
SOMA; Hii Ni Kazi Yenye Malipo Makubwa Sana Ambayo Unaweza Kujifunza Kuifanya
1/21/2015 11:54:00 AM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO | 3 Comments
Usianze Biashara Kama Hujui Kitu Hiki Kimoja.
Kama mwaka huu 2015 umepanga kuanza biashara usifanye kosa moja ambalo huwa linafanywa na wafanyabiashara wengi wanapoanza.
Usianze biashara kama hujui miaka mitano ijayo biashara yako itakuwa imefika wapi.
Ni muhimu sana kuwa na picha kubwa ya biashara yako ili unapoanza usisahau ulipotaka kufika.
Kama utaanza biashara ukiwa hujui miaka mitano utakuwa wapi hutafika popote. Maana biashara itakapoanza kukuchanganya utajikuta ukihangaika na matatizo yanayokusonga na kusahau kukuza biashara yako.
Pata picha ya kule unakokwenda kabla hata ya kuanza safari.
1/16/2015 06:29:00 PM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA BIASHARA | 0 Comments
Mbinu Kumi(10) Za Kuepuka Kuchoka Sana 2015.
Bado tupo kwenye mwanzo wa mwaka, na mwanzo wa mwaka kila mtu anakuwa na nguvu kubwa sana ya kufanya majukumu yake. Huu ni muda ambao kila mtu anakazana kujaribu kutimiza malengo yake.
Kadiri siku zinavyozidi kwenda watu wengi huanza kuchoka na mpaka kuja kufika mwezi wa kumi au kumi na moja asilimia kubwa ya watu wanakuwa wamechoka sana kiasi cha kushindwa kuwa na uzalishaji mzuri.
Hali hii ina madhara sana katika ufanisi wetu wa kazi na hata biashara. Na kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa, unahitaji kuwa kwenye ufanisi mkubwa kwa angalau mwaka mzima au wiki 50 kati ya wiki 52 za mwaka.
Leo hapa UTAJIONGEZA na mbinu 10 za kuepuka kuchoka sana mwaka huu 2015.
1. Upe mwili wako kazi. Kama kazi zako ni za ofisini au za kukaa, kufanya hivyo kila siku kutaufanya mwili wako uwe hovyo sana. Hivyo ni vyema kuupa mwili wako kazi, fanya mazoezi, cheza, tembea, kimbia, na hii ni kila siku.
2.Pata muda wa kutosha wa kulala. Kulingana na kazi zako unaweza ukasema huwezi kupata muda wa kutosha wa kulala, ila kulala kutaufanya mwili wako kuwa na nguvu na hata akili yako kuwa na ubunifu. Anza kulala nusu saa kabla ya muda wako wa kawaida wa kulala. Pia pata muda kidogo wa kulala mchana kama inawezekana kwako.
3. Pata dakika tano za kufanya tajuhudi/taamuli.
Hizi ni dakika chache ambapo unakaa kimya na kuondoa mawazo yote kwenye kichwa chako. Njia rahisi ya kufanya hili ni kukaa sehemu iliyotulia na kufunga macho yako kisha kuanza kuhesabu pumzi zako. Itakusaidia sana kusafisha akili yako.
4. Weka orodha ya vitu unavyoshukuru kuwa navyo. Haijalishi una matatizo kiasi gani kuna vitu unafurahi kuwa navyo, huenda ni familia inayokupenda, huenda ni biashara nzuri. Weka orodha hii na ipitie kila siku.
5. Kuwa na muda maalumu usiku ambapo unazima vifaa vyako vyote, yaani kompyuta, simu, tv na chochote kile. Fanya muda wako wa kupumzika kuwa wa kupumzika kweli.
6. Kuwa na picha inayokupa furaha na kukuhamasisha. Inaweza kuwa picha ya mtoto wako au kitu chochote. Itumie picha hii pale unapoona uvivu wa kufanya jambo.
7. Jisamehe. Kuna makosa mengi umeyafanya kwenye maisha yako, acha kuendelea kujitesa, jisamehe na songa mbele.
8. Kuwa mkarimu, wasaidie wengine, utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.
9. Tumia kipaji ulichonacho. Hata kama kazi au biashara unayofanya sio inayohusisha kipaji chako, tenga muda ambao utafanya kipaji chako. Kwa kufanya hivi utakuwa na nguvu na hamasa kubwa utaporudi kwenye kazi yako.
10. Fanya jambo moja kwa wakati. Kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kutachangia wewe kuchoka haraka sana. Fanya jambo moja likiisha ndio uanze jambo jingine.
Hizi ni mbinu rahisi unazoweza kuanza kuzitumia leo ili kuhakikisha mwaka mzima unakuwa na ufanisi mkubwa sana.
Nakutakia kila la kheri.
1/16/2015 10:23:00 AM | Labels: BIASHARA, MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Kuhusu Uwekezaji Tanzania
Kupitia mtandao huu utajifunza fursa mbalimbali za uwekezaji na pia kupata taarifa zinazohusu uwekezaji.
AINA ZA UWEKEZAJI TANZANIA.
Kwa bahati nzuri sana kuna aina nyingi sana za uwekezaji Tanzania. Kuna kila rasilimali na fursa mbalimbali za uwekezaji. Ugunduzi wa mafutra na gesi unaoendelea kufanyika Tanzania unaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi sana.Kuna aina mbalimbali za uwekezaji zinazoweza kufanyika Tanzania.
1. Uwekezaji wa mali.
Tanzania kuna arhi kubwa sana ambapo mtu anaweza kununua na kuendeleza kwa kujenga majengo ya kibishara na hata makazi.Pia ardhi hii inaruhusu kilimo na hivyo mtu unaweza kuwekeza kwenye kilimo cha biashara.
2. Bishara.
Kwa kuwa uchumi wa tanzania unakua kwa kasi sana mtu yeyote anayweza kuwekeza kwenye biashara anaweza kuapata faida kubwa. Biashara za bidhaa na huduma zinakua kwa kasi sana kutokana na ongezeko la watu na muingiliano wa kimataifa.3. Uwekezaji katika maliasili na gesi.
Tanzania ina gesi nyingi sana ambayo bado haijachimbwa. Hii inatoa fursa kubwa sana ya uwekezaji.4. Uwekezaji wa hisa na vipande.
Hii ni fursa nzuri ya uwekezaji kwa watu ambao wana miotaji kidogo. Soko la hisa la dar es salaa limeorodhesha makampuni mbalimbali ambayo mtu anaweza kununua hisa.Pia dhamana ya uwekezaji UTT, inatoa fursa kwa watu kununua vipande na vipande hivyo kuongezeka thamani na hivyo kunufaika zaidi.
Kuna fursa nyingi sana za uwekezaji ambazo utajifunza kupitia mtandao huu.
11/02/2014 04:58:00 PM | Labels: BIASHARA, DHAMANA YA UWEKEZAJI(UTT), FEDHA, HABARI ZA UWEKEZAJI, SOKO LA HISA(DSE), UCHUMI, UWEKEZAJI WA MALI(PROPERT) | 0 Comments
