Vitu VITATU Vinavyoathiri Kipato Chako Na Jinsi Ya Kukiongeza.

Katika mfumo wa uchumi tunaoishi sasa hivi duniani, ni dhahiri kwamba kipato chako kinaathiriwa na vitu vingi sana.

Kipato chako kinaweza kuathiriwa na hali ya uchumi inavyokwenda. Kwa mfano mfumuko wa bei unapokuwa mkubwa, kipato chako kinaweza kisitoshe matumizi yako. Lakini hii ni nguvu ya nje ambayo huwezi kuiathiri.

Kipato chako pia kinaathiriwa na mambo ambayo yanatokana na wewe binafsi na mambo haya unawezakuyabadili ili kubadili kipato chako.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

Leo tutajadili vitu vitatu muhimu vinavyoathiri kipato chako na jinsi unavyoweza kuvitumia kubadili kipato chako.

Ni ukweli usiopingika kwamba kila mtu anapenda kipato chake kiongezeke, ila sasa unaanzia wapi kukiongeza? Jua vitu hivi vitatu na vifanyie kazi.

1. Unafanya nini.

Kitu cha kwanz akabisa kinachoathiri kipato chako ni unafanya kitu gani? Yaani ni shughuli gani unayofanya ili kujitengenezea kipato? Unafanya biashara? Umeajiriwa? Kama unafanya biashara je ni biashara gani? Na kama umeajiriwa je una utaalamu gani? Tunajua kabisa vipato vinatofautiana na kutokana na kile unachofanya. Kipato cha mwalimu hakiwezi kuwa sawa na cha daktari. Kipato cha boda boda hakiwezi kuwa sawa na cha dala dala.

Kuongeza kipato chako kwenye njia hii ni kuhakikisha unafanya kitu ambacho kina uwezekano mkubwa wa kutengeneza kipato kikubwa.

SOMA; HADITHI_FUNZO; Aliyenusurika Kufa Kutokana Na Tabia Yake Nzuri.

2. Unafanya kwa ubora gani?

Tumeona vipato vinatofautiana kutokana na vitu tofauti. Vile vile ndani ya fani moja au biashara moja, bado vipato havilingani. Watu wawili wanaweza wote kuwa walimu wenye kiwango sawa cha elimu lakini vipato vikawa tofauti. Watu wawili wanaweza kuwa wanaedesha boda boda na wanapaki eneo moja lakini vipato vikawa tofauti. Kwa yule ambaye anafanya kwa ubora wa hali ya juu kipato chake lazima kitakuwa kikubwa.

Hakikisha kile ambacho unakifanya unakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.

3. Ugumu wa kukubadili.

Kipato chako pia kinaathiriwa na ugumu wa kukubadili wewe kwenye hiko unachofanya. Pata picha wewe unafanya kazi ambayo ni wewe tu unaweza kuifanya, hii ina maana kwamba kama usipokuwepo kazi yako haiwezi kufanywa na mtu mwingine hivyo thamani ya kipato chako inakuwa kubwa. Hali kadhalika kama unafanya biashara kwa kiwango ambacho mteja wako hawezi kukipata sehemu nyingine, lazima utakuwa na kipato kikubwa.

Anza sasa kujitengenezea mazingira ya wewe kuw avigumu kubadilishwa. Na sio ufanye hivyo kwa kuwafanyia wengine majungu, ila kwa kujiboresha zaidi na hivyo kufanya kazi au biashara yako kwa ubora wa hali ya juu.

Chukua hatua leo ili kuboresha kipato chako, acha kulalamika, maamuzi ni yako.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.

0 comments: