Fursa katika Kilimo cha Bustani
Habari msomaji wa makala za kilimo katika jukwaa hili la JIONGEZE UFAHAMU. Wiki hii tutajiongezea ufahamu kuhusu kilimo cha bustani kwa ufupi. Ila kwa wiki zinazokuja tutaingia kwa kina na tutaenda hadi kuchambua kilimo cha baadhi ya mazao, kuanzia uzalishaji hadi soko lake.
Karibu kwenye somo:
Kilimo cha bustani ni sekta ndogo iliyopo ndani ya sekta ya kilimo na ndio inayokua kwa kasi zaidi kuliko sekta ndogo yeyote ya kilimo. Tunaposema kilimo cha bustani tunamaanisha kilimo cha mbogamboga, matunda, maua pamoja na viungo (spices). Kilimo cha bustani ni kilimo ambacho kinalimwa na wakulima wadogo kwa asilimia kubwa, japokuwa upo uwekezaji mkubwa na uwekezaji wa kati ambao unakua kwa kasi pia. Ukweli ni kwamba mazao ya bustani ndio mazao yanayotumika sana kuliko mazao mengine. Huwezi kukwepa kutumia mazao ya bustani, haiwezi kupita siku hujatumia tunda, au mbogambogakama nyanya, kitunguu, mboga za majani, au viungo kama tangawizi, mdalasini, hiliki, karafuu, nazi n.k Pamoja na hayo lakini bado kilimo hichi hatujaweza kufikia kile kiwango cha uwezo wetu. Kutokana na rasilimali ardhi na hali ya hewa nzuri Tanzania inao uwezo wa kuzalisha mazao ya bustani mara 10 zaidi ya jirani zetu Kenya lakini pamoja na hayo yote wenzetu wanazalisha na kuuza nje ya nchi mara 10 zaidi yetu. Hii ni kwasababu kwanza wamegundua fursa iliyopo, wakaamua kutumia teknolojia na mbinu za ki leo katika kilimo, pia wanaongeza thamani ya mazao yenyewe kama kuweka katika madaraja na kuweka kwenye vifungashio. Kitu kingine kikubwa ni kwamba wenzetu wako vizuri sana katika masoko, wachangamfu sana katika kujitangaza na wanajua mbinu mbalimbali za kuteka soko kitu ambacho sisi hatuna. Sisi tunasubiri mteja aje atufuate wakati wenzetu wanalifuata soko.
SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo - 2
Kilimo cha Bustani Duniani
Katika dunia kilimo cha bustani kinakua kwa wastani wa 13% kwa mwaka, kikitegemea masoko ya ndani ya nchi, masoko ya kikanda pamoja na masoko ya kimataifa.Masoko makubwa ya mazao ya bustani ni Marekani, Urusi, India, nchi za Falme za Kiarabu pamoja na nchi za Ulaya. Changamoto ya kwenye soko la kimataifa ni kwamba wanazingatia sana ubora, na zipo taasisi kwa ajili ya kuthibitisha ubora tokea ilipozalishwa mpaka zao linapomfikia mlaji. Taasisi hizo ni kama Global GAP, BRC n.k. Changamoto hii imekua ikiwaathiri zaidi wakulima wadogo maana wanashindwa kukidhi viwango, lakini pia wakulima wadogo hawana uzalishaji endelevu. Mfano kama soko la Urusi unatakiwa kupeleka tani 200 za matunda au mboga kila wiki, wakulima wadogo inawawia changamoto maana yeye anafikiria azalishe akivuna ndioaanze tena kuandaa shamba kupanda tena. Wakati anaandaa shamba kwa ajili msimu unaofuata hana cha kuuza. Kwahiyo panahitajika mifumo ya uzalishaji ambayo inaweza kulihudumia soko katika hali endelevu. Pamoja na kwamba ni changamoto lakini kwa wengine imekua fursa, zipo kampuni zilianzishwa kupitia fursa hii, wao wanachokifanya wanatafuta hayo masoko kama ya Ulaya, Afrika kusini na kwingineko, na wanakua na vigezo vinavyohitajika kwenye soko. Halafu wanaingia mikataba na wakulima wadogo, wakulima wanazalisha kampuni inanunua na kwenda kuongeza thamani, kwa kuweka kwenye madaraja, kuweka kwenye vifungashio na wanauza kwenye hayo masoko.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Kilimo cha Bustani Tanzania
Hapa Tanzania kwa miaka mitano iliyopita kilimo cha bustani kimekua kikiongezeka kwa asilimia 6 hadi 10 kwa mwaka. Maeneo ya nyanda za juu kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Manyara) ndiyo yanayoongoza kwa uzalishaji wa mazao mengi ya bustani. Yapo pia maeneo mengineyanayofaa kwa kilimo hichi kama ukanda wa pwani, nyanda za juu kusini (Mbeya na Katavi), Nyanda za ziwa (Mwanza, Geita, Mara, Kagera n.k) pamoja na nyanda za kati (Dodoma - maarufu kwa kilimo cha Zabibu). Ukichunguza kila kanda in uwanja wa ndege hivyo kuwepo kwa fursa ya kuuza nje ya nchi. Kuna viwanja vya ndege kama Songwe - Mbeya, KIA –Kilimanjaro, Uwanja wa ndege Mwanza, Uwanja wa ndege JK Nyerere .
Katika nchi yetu tuna eneo takribani hekta Milioni 44 (44,000,000)ambalo bado halijatumiwa ipasavyo, kati ya hizo hekta milioni 29 (29,000,000) zinafaa kwa umwagiliaji lakini eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta laki mbili tisini elfu tu (290,000) eneo ambalo ni dogo sana ikilinganishwa na uhalisia wa eneo ambalo linafaa kwa umwagiliaji. Hii ni sawa na asilimia moja tu (1%). Hii ina maana asilimia 99 bado halijafanyiwa kazi.
SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.
Mazao mengi ya bustani unaweza kutumia eneo dogo na ukapata faida zaidi ya mara tatu kama ungezalishia mazao ya nafaka katika eneo lenye ukubwa sawa.
Kuona hilo, wahisani wengi wa miradi ya kilimo kwa wakulima wadogo wamejikita zaidi katika kuhamasisha kilimo cha bustani maana ndio kinachoweza kumkomboa mkulima kwa haraka zaidi.
Hii inatupa ishara kwamba kwa mtu anayetaka kuwekeza kwenye kilimo anashauriwa awekeze kwenye kilimo cha bustani.
Hapa chini nimeweka kiunganishi (link)ya tovuti (website) ya moja ya makampuni yanafanya kilimo cha bustani.Kampuni hii inaitwa StakeAgrobaseInt. Ltd (SAIL) na inamilikiwa na Mtanzania mwenzetu. Mwanzilishi wa kampuni hii alikua daktari wa hospitali ya mkoa, yeye aliona fursa akaichangamkia sasa hivi yuko mbali sana.
Stake AgrobaseInt. Ltd (SAIL)http://www.sailfv.com/aboutus.php
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email)daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
Makala Imehaririwa kwa Kiswahili sanifu na Rumishael Peter wasiliana nae kuhariri kitabu au Makala email:rumishaelnjau@gmail.com simu: +255-713-683422http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/09/2015 07:30:00 AM | Labels: KILIMO | 0 Comments
Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo - 2
Habari za leo msomaji wa makala za kilimo kwenye Jiongeze Ufahamu, ni matumaini yangu unaendelea mbele na juhudi za kuyafikia mafanikio. Nipende kuwashukuru wote ambao mmekua mkijifunza kupitia jukwaa hili, nimepokea barua pepe (email) kadhaa za ndani ya Tanzania na hata nje ya nchi za watu kukiri kujifunza kutokana na makala za kilimo. Wale ambao mmeniandikia barua pepe kwa ajili ya kupata ushauri, wapo ambao tayari nimeshawajibu ila wapo wengine wiki hii mwishoni nitakua nimewajibu wote waliobakia.Tujikumbushe tu kidogo,wiki iliyopita tulianza kujifunza mambo matano ya muhimu kuyafahamukabla ya kuwekeza kwenye kilimo, na tuliweza kujifunza mambo mawiliambayo ni soko na hali ya hewa inayoruhusu kustawi kwa kilimo ulichokusudia. Leo tutaweza kuyamalizia mambo yaliyobakia. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki iliyopita isome hapa; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo.
Karibu kwenye somo
3. Upatikanajiwa rasili watu (Wafanya kazi)
Ukweli ni kwamba hata ukiwa na kiasi kikubwa cha fedha hutaweza kuwekeza kwenye kilimo kama huna rasilimali watu. Wafanyakazi ni rasilimali muhimu sana kama zilivyo fedha, vifaa, mitambo au mashine za utendaji kazi, ndio maana kulijua hilo kampuni nyingi zimeweka utaratibu wa kutunza rasilimali hii muhimu ya watu. Utakuta kwenye makapuni kuna afisa au meneja rasilimali watu. Ukweli ni kwamba vitendea kazi ulivyo navyo vitaendeshwa na watu. Wafanyakazi ni wa muhimu sana kwenye kilimo kuanzia uwekezaji mdogo hadi mkubwa. Wafanyakazi tunaweza kuwaweka kwenye makundi 2, la kwanza ni la wafanyakazi wa kawaida wale ambao hawana ujuzi wa kitaalamu au vibarua, na kundi lingine ni la wafanyakazi wenye utaalamu au ujuzi fulani hasa wa kilimo.Kama unaanza kuwekeza kwenye kilimo kwa uwekezaji wa chini hutahitaji sana wataalamu kwa kuwaajiri, ila utahitaji kutafuta ushauri wa kitaalamu ambao sio gharama kubwa. Lakini pia utahitaji vibarua ambao watakua wakifanya shughuli za shambani, hapo itategemea na ukubwa wa shamba lako. Ila kama unataka kufanya uwekezaji mkubwa lazima utahitaji hao wataalamu wa kilimo, na sio hao tu utahitaji fani nyingine kama washauri wa fedha, wahasibu, utawala, wataalamu wa sherian.k Kumbuka hapo kwa wafanya kazi, sio alimradi wafanya kazi, unahitaji wafanya kazi wenye kufanya kazi kwa bidii, wenye kujituma sio mpaka wasimamiwe ndio wafanye kazi, wenye hamasa ya kazi, wabunifu na wanaoweza kufuata maelekezo vizuri hata kama sio mtaalamu lakini ana uwezo wa kufuata maelekezo ya kitaalamu. Pia bila kusahau mwajiri lazima ujali wafanya kazi wako maana ni rasilimali inayokuzalishia kipato, lazima ujue wafanyakazi ni zaidi ya hizo mashine au mitambo na fedha.
Katika nchi zinazoendelea rasilimali watu ni rahisi kuipata, gharama yake ni rahisi ukilinganisha na nchi zilizoendelea tayari. Katika nchi zilizoendelea gharama ya kumlipa kibarua au mfanya kazi wa kawaida inakaribia kulingana na gharama ya kulipa mtaalamu mwenye ujuzi katika nchi za kwetu, na ndio maana nchi tajiri zinapendelea kuja kuwekeza huku kwenye nchi zinazoendelea.
SOMA; BIASHARA LEO; Ondoka, Hakuna Aliyekuita Hapa.
4. Upatikanaji wa maji wa uhakika
Wakulima wengi baraniAfrika kilimo chao kinategemea mvua, hivyo mvua isiponyesha uzalishaji unakua matatani. Mabadiliko ya tabia nchi yanapelekea mvua zisiwe za uhakika laikini pia majira ya mvua yanabadilika, mfano kama mvua za masika tulikua tumezoea zinaanza mwezi wa pili lakini kwa sasa zinaanza mwezi wa tatu au wanne. Upatikanaji wa maji kila kukicha unakua ni changamoto. Ikumbukwe kwamba ukame huongoza kusababishanjaa au upungufu wa chakula dunia kote. Katika uwekezaji wa kilimo kitu ambacho unatakiwa uwe na uhakika nacho ni maji ya uhakika, uwe na chanzo cha maji cha uhakika. Ili ufanye kilimo cha kibiashara lazima uwe na uwezo wa kuzalisha mwaka mzima, kama huna maji ya uhakika hutaweza kufanya hivyo. Hapa namaanisha kilimo cha umwagiliaji, zipo njia mbali mbali za umwagiliaji kama njia ya mifereji, umwagiliaji wa matone, umwagiliaji wa maji mfano wa mvua. Lakini katika njia zote njia ya umwagiliaji wa matone ndio nzuri maana inatumia maji machache na pia maji yanakwenda pale mmea ulipoota hivyo hakuna upotevu wa maji. Njia hii ya umwagiliaji wa matone unaweza kufanyika katika mashamba ya wazi au katika nyumba ya kupandia mazao maarufu kama Nyumba ya kijani(greenhouse). Unaweza kuwa na vyanzo tofauti vya maji mfano kutoka mtoni, kuchimba kisima cha chini, kuvuna maji ya mvua n.k. Pia ni vizuri kutengeneza miundombinu ya kutunza maji kama Bwawa ambalo litahifadhi maji. Israel ni moja ya nchi zinazofanya vizuri sana kwenye kilimo cha umwagiliaji,ijapokuwa eneo lake kubwa ni ukame wameweza kuvumbua teknolojia nzuri sana kwenye umwagiliaji. Israel mvua ikinyesha siku tatu tu, wana uwezo wa kupanda na kuvuna mazao yakutumia na kuuza nje ya nchi. Hii ni kwasababu wanayo miundo mbinu mizuri katika kuvuna maji ya mvua na kuyatunza kwa ajili ya kutumia kumwagilia kwa njia ya matone. Kwa Tanzania zipo kampuni kadhaa ambazo zimekua zikifanya biashara ya kuuza vifaa vya umwagiliaji wa matone, moja ya kampuni hiyo ni Balton Tanzania ambayo ni kampuni ya Waisraeli. Kwa Tanzania wapo Arusha na pia wanayo ofisi Dar. Pia wanatoa huduma ya kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji.Kwahiyo kwa kumalizia pointi yetu hii ni kwamba, upatikanaji wa maji ni muhimu sana katika uwekezaji wa kilimo maana kama vile maji ni uhai kwa mwanadamu, vivyo hivyo maji ni uhai kwa mimea.
SOMA; UKURASA WA 91; Utashi, kitu muhimu kwako kufikia mafanikio.
5. Miundombinu pamoja na kufifika kwa eneo la uwekezaji
Hapa tunaangalia miundombinu kama barabara, umeme, mawasiliano ya simu n.k Lazima eneo unalowekeza kilimo chako liwe linafikika, hakikisha barabara iko vizuri na inapitika wakati wote, maana utahitaji kusafirisha kwenda shambani vitendea kazi, pembejeo n.k. Pia wakati wa kuvuna utahitaji kusafirisha kupeleka sokoni. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba eneo likiwa ni gumu kufikika hii itaongeza gharama za uzalishaji na hivyo kupelekea kupunguza faida yako. Hivyo pamoja na kuzingatia vigezo vinne vilivyopita ni lazima kuchagua eneo ambalo linafikika, mawasiliano ya simu yako sawa, pia nishati ya umemena mengineyo.
SOMA; Hiki Ndio Unachohitaji Ili Kugeuza Ndoto Yako Kuwa Uhalisia.
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email) daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
Imehaririwakwa Kiswahili sanifunaRumishael Peter
email:rumishaelnjau@gmail.comsimu:+255-713-683422
http://rumishaelnjau.wix.com/editor
4/02/2015 07:30:00 AM | Labels: KILIMO | 1 Comments
Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo.
Wiki iliyopita tuliweza kuona jinsi ambavyo fikra potofu watu walizo nazo kuhusu kilimo zilivyodidimiza kilimo chetu. Pia tuliweza kupata picha ambavyo nchi tajiri zilivyowekeza kwenye kilimo kupitia teknolojia za kisasa zaidi. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki iliyopita isome hapa; Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.
Leo hii napenda tuanze kujifunze mambo matano ambayo kila mtu aliye na ndoto ya kuwekeza kwenye kilimo ni lazima ayafahamu vizuri. Kutotilia maanani moja ya mambo haya kunaweza kupelekea ukakichukia kilimo. Leo tutaanza na mambo mawili.
1. Soko
Hili ndilo jambo la muhimu kwenye kila uwekezaji au kwa maana nyingine biashara yeyote lazima itegemee soko. Na hapa ndipo wengi wanakosea sana wakulima wadogo na hata vijana wanaoingia kwenye kilimo maana wengi wanazalisha kwa kufuata mkumbo kwa vile wengi wanazalisha wakati huo au amesikia labda kilimo cha zao Fulani kinalipa. Kabla ya kuwekeza kwenye kilimo lazima uanze kwa kulitambua soko lako. Lazima uzalishaji wako uwe unaendeshwa na soko. Unatakiwa kua na taarifa za kutosha kuhusu soko, kujua soko linasemaje, ni wakati gani watu wengi wanakua wamezalisha, wakati gani bidhaa hii inakua kwa wingi sokoni, ni wakati gani inakua hadimu na ni kwanini? Usizalishe kwa vile ni msimu wa kuzalisha kwamba unaona mko wengi. Watu wengi wanaofaidika kwenye kilimo ni wale ambao hawafuati mkumbo kwenye kuzalisha wao wanajua kucheza na wakati, wakati bidhaa ile ni hadimu au wakati ambao sio msimu wa kuzalisha, ndio wakati wa wao kuzalisha na hivyo kupelekea kupata faida nzuri zaidi. Hata kampuni kubwa zinazowekeza kwenye kilimo kwanza wanakua na soko la uhakika, aidha baada ya kufanya utafiti wa kutosha au kwa kuingia mikataba na wateja wao. Vyovyote vile lakini wanachokua na uhakika nacho ni kua wanajua ni wapi watauza baada ya kuzalisha. Mfano kwa kampuni zinazozalisha maua Arusha na maeneo mengine soko lao kubwa liko uholanzi (Amsterdam Auction) na ndio maana asilimia kubwa ya wamiliki wa kampuni hizo ni waholanzi maana wanalijua vizuri soko la maua. Ila kwetu hali ni tofauti badala ya kuanzia sokoni sisi tunaenda moja kwa moja shambani kuzalisha baada ya mazao kukomaa na kua tayari kuvuna ndio tunalikumbuka soko, yaaniumeshazalisha ndio unaenda kutafuta soko, bila kujua pengine ulichonacho hakihitajiki na soko.
SOMA; KITABU; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.
Wengine wanaweza kusema hatuwezi kuwekeza kwenye kilimo maana soko hakuna, hasa wakulima wadogo wengi wanafahamu soko ni pale kwenye mkusanyiko wa watu wengi kama kwenye minada, magulio au kwenye masoko kama Kilombero, Arusha, Mabibo Dar es salaam n.k.Unachotakiwa kujua ni kwamba kuna aina kadhaa za masoko mfano masoko ya ndani yasiyo rasmi, masoko ya kitaasisi kama mahoteli, mashule na mahospitali. Pia kuna masoko ya kiviwanda; mfano viwanda vya kuongeza thamani kama vya AZAM au REDGOLD Arusha n.k Bila kusahau masoko ya kimataifa kama Ulaya, Asia na hata nchi za jirani kama Sudan ambako kumekua na vita na watu wamekua hawana muda wa kuzalisha. Hata hivyo kuna vitu vingi sana vya kujifunza kwenye upande wa soko naona kwa leo tuishie hapa kwa upande wa soko, tukipata muda huko mbeleni tutajadili kwa kina.
SOMA; Hii Ni Kazi Yenye Malipo Makubwa Sana Ambayo Unaweza Kujifunza Kuifanya
2. Hali ya hewa inayoruhusu kilimo husika
Kila kilimo cha zao fulani kina hali ya hewa au mazingira yanayo kiruhusu kilimo hicho kustawi vizuri. Kwenye eneo hili tunaangalia maswala ya jotoridi, unyevunyevu kwenye hewa, mvua na sifa za udongo unaosaidia ukuaji wa zao husika. Kuna mazao yanapendelea hali ya joto na kuna mengine yanastawi kwenye hali ya baridi. Mfano kama mananasi yanapendelea ukanda wa joto na ndio maana yana stawi sana ukanda wa pwani huko. Katika sifa za udongo kuna sifa za kikemikali au kifizikia. Mfano wa sifa hizo ni kama pH ambacho ni kipimo cha kiwango cha asidi na alkali ya udongo. Hii ina maana pH ya udongo wako ikiwa ndogo chini ya 5 udongo wako una kiwango cha asidi na ikiwa kubwa zaidi ya 8 maana yake udongo wako una kiwango fulani cha alkali.Katika aina ya udongo inakubidi ufahamu ni udongo mfinyanzi, tifutifu au kichanga. Usije ukapanda mpunga kwenye udongo wa kichanga wakati mpunga unapendelea udongo unaotuamisha maji. Au unapanda vitunguu kwenye udongo unashikamana sana (mfinyanzi) wakati kitunguu kinahitaji udongo wenye kuachia (tifutifu) ili kiweze kujijenga vizuri.Lakini ngoja nisiingie kwa kina sana hapa kwenye udongo maana kuna mambo mengi sana na ndio maana watu wanasomea shahada za chuo kikuu kwenye masuala ya udongo na hata wengine wanakua maprofesa wa udongo.
Lengo la kukupitisha hapa kidogo ni ili ufahamu kwamba baada ya kupata soko la uhakika na kujua ni zao gani kinachofuata ni kujua maeneo gani zao hilo linastawi, ni udongo wa aina gani unaofaa. Unashauriwa kabla ya kupanda uchukue sampuli ya udongo ukapime maabara kujua sifa za udongo wa shamba lako. Zipo taasisi za serikali na binafsi zinazotoa huduma ya upimaji udongo. Taasisi hizo ni kama taasisi za utafiti wa kilimo kama SARI (Arusha) ARI Ukiliguru ( Mwanza), ZARI Kizimbani (Zanzibar), ARI Maruku Kagera, ARI Kibaha n.k Pia zipo taasisi za elimu kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro. Ukishapima udongo unapewa ushauri wa zao gani linaweza kustawi vizuri kwenye shamba lako lakini pia unapata ushauri wa aina gani ya mbolea unatakiwa kutumia. Gharama ya upimaji inategemea na wingi wa vitu unavyotaka kupima kwenye huo udongo.
Kwa kifupi maeneo mengi ya nchi yetu ni mazuri sana kwa kilimo na ndio maana tunaona nchi nyingi zinakuja kuwekeza kwenye kilimo nchini kwetu. Hata hapa kwenye jumuiya ya Afrika mashariki wenzetu wanaimezea mate sana ardhi yetu yenye rutuba. Nchi ya Tanzania inauwezo mara kumi ya Kenya au kwa maneno mengine ina hali ya hewa nzuri katika kuzalisha mbogamboga mara kumi zaidi ya Kenya, maeneo mengi ya Kenya ni makame sana.Lakinicha kushangaza wenzetu wanazalisha mazao hayo na kuuza nje ya nchi mara kumi zaidi ya Tanzania. Je ni kwanini? Basi naomba tukutane tena wiki ijayo hapa hapa
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe (email)daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.
3/26/2015 07:30:00 AM | Labels: KILIMO | 0 Comments
Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.
Sekta ya kilimo ndio sekta inayoajri watu wengi kwa hapa Tanznia inakaridiriwa zaidi ya aslimia 80 ya watanznaia wanategemea sekta hii aidha moja kwa moja au wananufaika kwa namna moja au nyingine. Kwa ujumla hakuna nchi yeyote duniani amabyo iliendelea bila kuwekeza kwenye kilimo, basi kama ipo zitakua ni chache sana. Hata hizo nchi zenye viwanda vikubwa malighafi zake zinatokana na kilimo. Hii inaonyesha kwamba bila kilimo uchumi wa nchi utakua mashakani. Tofauti ya nchi tajiri na nchi masikini(kama zinavyoitwa nchi zinazoendelea) ni kwamba kwa nchi tajiri kilimo ni uwekezaji unatiliwa umuhimu mkubwa sana. Ndio maana huko matajiri ndio wanaolima lakini kwetu kilimo kimechukuliwa ni cha watu masikini. Na ndio maana ukiwa unalima unaonekana kuwa wewe ni mtu wa kaliba ya chini au uliyeshindwa maisha. Mfano unawezakuta watu mjini wakitoa kauli zinazoonyesha kilimo ni kama chaguo la mwisho. Mara kadhaa utasikia watu wakisema kama mjini pamekushinda rudi kijijini ukalime. Hapa wakimaanisha kilimo ni kama shughuli za ya kishamba na ndio chaguo la mwisho ukishashindwa kila kitu.
SOMA; Matumizi Mawili Ya Mbegu Za Mahindi.
Kwa bahati mbaya sio mjini tu ndiko wanakodharau kilimo hata kijijini kwenyewe wapo watu wengi wanaona kilimo ni kama adhabu fulani. Nakumbuka nikiwa kijijini kwetu baada kumaliza kidato cha sita na kupata nafasi ya kwenda kusoma kilimo Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Morogoro baadhi ya ndugu waliumia sana kusikia kwamba naenda kusomea kilimo tena chuo kikuu. Ndugu mmoja alidiriki kuniambia mwanangu naona umepoteza dira yaani unaenda kusomea kilimo chuo kikuu, sasa kweli huko kuna hela? si bora ungeenda hata upolisi ambapo unaanza kupata hela mapema na ajira ni uhakika. Yaani huoni wenzako wanasomea uhasibu kozi nyingne zenye hela. Lakini niliamini ipo siku moja watageuza mtazamo walio nao na mimi ndio nitakua chachu ya mageuzi hayo ya fikra.
SOMA; Huu Ni Uwekezaji Wa Uhakika Ambao Hautakuangusha.
Hoja ninayoijenga hapa ni kwamba sisi wenyewe ndio tumekua chanzo cha kufanya vibaya kwa kilimo chetu kwa sababu ya fikra potofu tulizonazo juu ya kilimo. Tunasahau kwamba kilimo ni biashara kama zilivyo biashara nyingine. Hivi tunajifunza nini tunapoona makampuni makubwa yanawekeza kwenye kilimo? Mfano mji wa Arusha kuna Makampuni zaidi ya 20 ya wawekezaji wa nje ambao wamewekeza kwenye kilimo cha maua, mboga mboga, matunda na hata nafaka. Hivyo hivyo kwenye mikoa mingne kuna uwekezaji kutoka nje. Wakati sisi tunachukulia kilimo kama jambo la hovyo hovyo wenzetu wanaingiza teknolojia kwenye kilimo. Mfano nimewahi kufanya kwenye kampuni moja inayozalisha mbegu chotara ambayo ipo Arusha ambapo nilikua Meneja Msaidiz kwenye kitengo cha Operesheni na Uzalishaji ambapo wana mwagilia kwa kutumia mfumo wa kompyuta (Computerized Irrigation system). Huhitaji kuwepo ili mashamba yamwagiliwe hata ukiwa haupo una seti mitambo automatiki kazi inaendelea. Pia mimea inawekewa feni za kisasa ili kudhibiti hali ya hewa( joto na unyevunyevu kwenye hewa au humidity) ili kuhakikisha mbegu inakua na ubora wa hali ya juu.
SOMA; Fikra TANO Zinazoua Mafanikio Na Jinsi Ya Kuziepuka.
Lakini swali la kujiuliza je walianzia wapi hadi wakafika hapo? Jibu ni kwamba walianzia mbali sana, kampuni yenyewe ina zaidi ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, na ilianzishwa kama kama kampuni ya familia huko nchini Uholanzi mnamo mwaka 1938, mwanzilishi alianza kwa kuuza mbegu za mbogamboga kwa wakulima wenzie, baadaye akaanza kidogokidogo kuzalisha mbegu leo hii ndio kampuni inayoongoza duniani kwa kuzalisha mbegu chotara za mbogamboga. Kwa sasa imesambaa zaidi ya nchi 20 duniani ikiwemo Tanzania na ni kampuni ya mabilioni ya hela. Hivi sasa kampuni inaongozwa na mjukuu yaani aliyeianzisha aliiongoza akamwachia motto wake naye akaiongoza leo hii mjukuu ndiye CEO na bado inakua kwa kasi sana. Japo mwanzilishi alianzia katika hali duni na ya chini sana lakini alikua na maono makubwa na alikua kiipenda kazi yake.
SOMA; Hatua TANO Za Kuongeza Uzalishaji Wako Ili Kufikia Mafanikio.
Tunachojifunza hapa ni kwamba hatuhitaji mabilioni ya hela kufika walikofika wenzetu, hayo yote kwa sasa hayatatusaidia. Ndio maana kila mwaka tunatenga mabilioni ya hela lakini kilimo chetu bado hikipigi hatua. Tunasahau kwamba hatuwezi kubadilisha nje wakati ndani bado hatujabadilika. Vijana wengi tunataka pesa za haraka haraka tukiambiwa tuwekeze kwa malengo ya kuanza kupata faida miaka 3 au 5 mbele hakuna nayetaka kusikia hiyo habari. Tunakosa uvumilivu. Angalia hata matajiri wengi wa Tanzania kilimo ndicho kiliwatoa. Baadhi ya watu ambao nimekua nikiwafuatilia ni Bilionea Eric Shigongo. Leo hii tunamwona Shigongo hapo alikofika amefanya sana kilimo, amelima sana mananasi huko pwani na ni biashara iliyokua inamlipa sana. Sasa hivi anawekeza kwenye madini na biashara nyingine kubwa lakini mweynyewe anakiri kilimo ndicho kilimtoa.
Hitimisho: Niseme tu napenda kutambua juhudi za watu ambao wameanza kuamka na kuchukulia kilimo kama uwekezaji unaolipa. Wapo watu amabo wameadhamiria kufanya kitu katika kilimo. Natamani kuona watanzania wengi tukifuata nyayo zao. Lazima tubadili fikra zetu lazima tuwe na mitazamo chanya kuhusu kilimo. Asanteni sana tukutane wiki ijayo katika makala nyingne ya kilimo.
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana nae kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au email daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com
3/19/2015 07:30:00 AM | Labels: KILIMO | 0 Comments