Fikra TANO Zinazoua Mafanikio Na Jinsi Ya Kuziepuka.

Mpaka sasa unajua kwamba tofauti kubwa ya watu waliofanikiwa na wasiofanikiwa inaanzia kwenye fikra zao. Kama bado hujajua ndio nakuwambia leo na nitakuambia mawazo ya aina tano ambayo yanaua kabisa mafanikio yako.

Tunajua kwamba kuwa na mawazo chanya ni kitu muhimu sana ili kufikia mafanikio. Hivyo kuepuka mawazo hasi ni hatua ya kwanza ya kufikia mafanikio. Ila mawazo ya aina tano tutakayokwenda kujifunz ahapa leo yanaweza yasionekane kama ni hasi na ndio maana watu wengi wanashindwa kuyatambua mapema.

SOMA; Hii Ni Kazi Yenye Malipo Makubwa Sana Ambayo Unaweza Kujifunza Kuifanya

Kwa kujua mawazo haya na jinsi ya kuyaepuka itakuwa msaada sana kwako kufikia mafanikio.

1. Mimi sio mtaalamu.

Mara nyingi sana umekuwa ukitumia sababu hii kwamba unashindwa kufanya zaidi kwenye kazi yako au biashara yako kwa sababu huna utaalamu mkubwa. Sawa huenda ni kweli huna utaalamu mkubwa ila je unachukua hatua gani?

Kumbuka hakuna mtu aliyezaliwa na utaalamu wowote, vitu vyote tunajifunza hapa duniani. Hivyo kama kuna utaalamu ambao unajua utakusaidia sana kwenye kazi au biashara zako anza kujifunza. Kwa bahati nzuri tunaishi kwenye dunia ambayo kujifunza sio lazima uende darasani, popote ulipo unaweza kujifunz ana kutendea kazi yale uliyojifunza na baada ya muda ukawa mtaalamu.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.

2. Hicho kimeshafanyika.

Kuna wakati ambapo unapata wazo zuri la kufanya kitu ambacho kitakufaidisha sana kwenye kazi au biashara. Ila unapofuatilia kwa makini unagundua kwamba kuna watu wengine tayari wanafanya. Kwa kuwa na mawazo ya aina hii unajiondoa mwenyewe kwenye safari ya mafanikio.

Hata kama kitu kimefanyika na watu wengi kiasi gani, kama ndio kitakachokusaidia kifanye. Ila wewe kifanye kwa utofauti na upekee ili uweze kunufaika zaidi. Kama kuna biashara unayotaka kufanya na ukakuta wengine wanaifanya unatakiwa kufurahi kwa sababu tayari una uhakika kwamba soko lipo, hivyo kazi yako ni kujua jinsi gani utavutia na kuwabakiza wateja kwenye biashara yako.

3. Sina ‘connection’

Ni kweli kabisa na pia nilishaandika kwamba haijalishi unajua nini bali unamjua nani, mafanikio yako yatategemea sana na watu unaojuana nao na walioko kwenye mtandao wako. Hivyo ni rahisi sana kuamini kwamba kwa kuwa hujuani na watu waliofanikiwa basi huwezi kufanikiwa.

Swali ni kwamba unataka watu waliofanikiwa waje wakutafute wewe? Wakutafute kwa sababu gani? Wewe ndio unatakiw akuanzisha kitu hiki. Angalia ni watu gani ambao unahitaji kuwa nao kwenye mtandao wako, kisha angalia ni kitu gani unaweza kuwasaidia. Omba nafasi ya kuwasaidia kitu hiko na utakuwa umeanzisha connection muhimu sana kwako. Ndio watu wenye mafanikio ni vigumu sana kuwapata ila kama kweli unataka kuwapata utafanikiwa kuwapata.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

4. Sina hela.

Angalau hii ni sababu ambayo karibu kila mtu anaitumia wakati mmoja au mwingine. Kwa nini huanzi biashara, sina mtaji. Kwa nini biashara yako haikui, sina fedha. Kwa nini hujafikia mafanikio, sina fedha. Sawa huna fedha, swali ni je unataka nani aje akuletee fedha hapo ulipo? Hakuna, kama unasubiri unapoteza muda wako bure. Anzia hapo ulipo, anza na ulichonacho. Kama unataka kuanza biashara anza na kiasi kidogo unachoweza kuanzia, endelea kukua na pale unapokuwa makini utaanza kuona fursa nyingi za kukuza biashara yako. Lakini kama utasema huna fedha, huna mtaji na ukaendelea kulala, nakutakia usingizi mwema.

SOMA; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015.

5. Nimejaribu sana lakini nashindwa.

Umesema nijifunze ili niwe mtaalamu, nimeshajifunza sana lakini siwezi.

JIBU; Bado hujajifunza vya kutosha, au haupo makini kwenye kujifunza kwako. Anza tena na jua ni nini hasa unachotaka. Usikate tamaa mpaka utakapofikia.

Umesema hata kama kitu kimefanywa naweza kukifanya na nikafanikiwa, nimeshajaribu hivyo lakini napata hasara tu.

JIBU; Unafanya kama kila mtu anavyofanya, weka ubunifu, jitofautishe, usiwe wa kawaida.

Unasema kama nahitaji connection nianze mimi kutafuta yule ninayetaka connection yake, nimejaribu sana, nimeenda ofisini kwa mtu niliyetaka kupata connection yake masecretary wamenizuia, wameniambia niandike barua na nieleze shida zangu nitapewa wa kunisaidia ila sio yule ninayemtaka.

JIBU; Ongeza juhudi, badili mbinu za kuweza kumpata mtu huyo, anza kufikiria ni jinsi gani unaweza kumsaidia, mwandikie kila unachofikiri kitamfanya atake kujua ni nani amempa mawazo hayo mazuri. Wakati huo huo kuwa bora kwenye kile unachokifanya, watu watakuongelea na moja kwa moja utapata nafasi ya kuonana na waliofanikiwa zaidi.

Unasema nianze kidogo hata kama mtaji sina, hata hicho kidogo sina, nilijaribu kuanz akidogo nimepata hasara na sasa sina hata pa kuanzia.

JIBU; Kama huna hata kidogo cha kuanzia kuna uwezekano mkubwa hujui unachotaka kufanya. Kama ulianza kidogo na umeshindwa, anza tena, ndio safari ya mafanikio ilivyo.

Hizo ndio fikra tano za kuondokana nazo ili uweze kufikia mafanikio. Kumbuka pamoja na yote haya maamuzi yanabaki kwenye mikono yako. Ukiamua kuyatumia haya kwenye maisha yako, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa. Ukiamua kuachana nayo utaendelea hivyo ulivyo.

Nakutakia kila la kheri.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

 

0 comments: