Kwanini ni Muhimu kuwekeza kwa Muda Mrefu.
Unapofanya uwekezaji au jambo lolote unashauriwa kuwa na malengo ambayo utakuwa unayafuata katika utekelezaji wako. Na ukifanya uwekezaji hasa katika hisa ni vyema ukawa na malengo ya kukaa na Hisa zako kwa muda Fulani. Uwekezaji katika Hisa unamanufaa ikiwa utawekeza kwa muda mrefu na utapata manufaa makubwa.
Kwanini uwekeze kwa muda mrefu?
Ukiwekeza kwa muda mrefu uwekezaji wako utakua kwa kiwango kizuri, uwekezaji wa kuanzia mwaka 1 au 2 au zaidi ni rahisi kwa mwekezaji kuona ukuaji wa uwekezaji wake katika ongezeko la thamani. Mara nyingi ongezeko la bei ni rahisi kulitambua katika uwekezaji wako ikiwa utawekeza kwa muda mrefu. Vile vile katika kipindi hicho ni rahisi kwa mwekezaji kupata gawio la mwaka au miezi sita.
SOMA; Kinachokufanya Ukwame, Na Uwe Na Maisha Magumu.
Ukiwekeza kwa muda mrefu unaondoa hatari ya kupata hasara, kama utafanya uwekezaji wa muda mrefu katika Hisa ni rahisi kuondoa hatari ya kupata hasara kutokana na kupanda na kushuka kwa bei za hisa. Bei za hisa hupanda na kushuka, kwa hiyo ikiwa utawekeza kwa muda mfupi ni rahisi kupata hasara kama utauza kipindi ambacho bei zimeshuka ndani muda mfupi.
Ukiwekeza kwa muda mrefu una nafasi nzuri ya kupata gawio, kama utawekeza kwa miezi miwili ni vigumu kupata gawio kwa kuwa kampuni nyingi hutoa gawio kila baada miezi sita au mwaka. Kwa mwekezaji ambaye atawekeza kwa muda mrefu ana nafasi nzuri ya kupata gawio na kunufaika na uwekezaji wake.
Muda ambao mwekezaji anashauriwa kuwekeza na kukaa na uwekezaji wake
Unashauriwa kuwekeza kwa muda wa mwaka 1 au zaidi na uwekeze katika kampuni zaidi ya moja. Ukiwekeza kwa mwaka mmoja au zaidi na kwa kampuni tofauti unazuia hatari ya kupoteza pesa yako na uwekezaji kukua kwa kiwango kizuri.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano: emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania,blogspot.com
5/13/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Fanya Uwekezaji Huu Ambao Ni Rahisi Kwako Na Una Faida Kubwa.
Watu wengi wamekuwa wakitamani kufanya biashara au shughuli yoyote ambayo itakuza kipato chao, lakini wengi wao hukatishwa tamaa jinsi gani ataweza kusimamia biashara hiyo. Changamoto ya usimamizi wa biashara ni kubwa sana kwa watu wengi hasa wale ambao ni wafanyakazi katika serikali na kampuni binafsi. Na wengi ambao wamejaribu kufanya biashara wameshindwa kutokana na usimamizi mbovu wa biashara zao. Wengi wanatamani kukuza vipato kwa njia nyingine. Nini kifanyike?
Uwekezaji katika hisa ni suluhisho kwa wale wote ambao wanakutana na changamoto ya muda wa usimamizi wa biashara zao. Uwekezaji katika hisa ni rahisi, unahitaji muda mdogo wa usimamizi, unakua na kuongeza kipato kwa mwekezaji.
SOMA; Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.
Uwekezaji huu unafanyikaje?
Mtu yoyote Yule anaweza kuwa mwanahisa akiwa popote pale Tanzania. Unaweza kununua hisa katika soko la Hisa la Dar es salaam kupitia mawakala wake ( Brockers) au kupitia Benki ya CRDB ukiwa mkoa wowote ule hapa Tanzania. Wasiliana wakala utapata utaratibu wowote jinsi ya kununua hisa. Unachotakiwa kuwa nacho ni pesa yako kwa ajili ya kununua hisa, akaunti yako ya benki na mawasiliano ya Mawakala wa soko la Hisa au Benki ya CRDB.
Kwanini uwekezaji huu ni rahisi?
Ni uwekezaji ambao unaweza kuufanya ukiwa katika mkoa wowote ule hapa Tanzania kwa gharama ndogo na wewe kuwa mmiliki wa hisa na kutengeneza faida. Ukihitaji kununua au kuuza hisa zako unachotakiwa kuwasiliana na mawakala wa soko la hisa ukiwa mkoani au sehemu yoyote ile kwa njia ya mtandao ( simu, barua pepe na benki). Utapata utaratibu wote kuhusu kuuza na kununua hisa.
Uwekezaji huu unahitaji muda mdogo wa usimamizi
Ukiwekeza katika hisa Mfano CRDB, TBL au SWIS hutahusika katika shughuli za kila siku za Kampuni. Wewe kama mwanahisa unahitajika kufuatilia utendaji wa Kampuni katika taarifa za fedha ambazo hutolewa kila baada ya miezi mitatu, sita na mwaka. Kama mwekezaji utasubiri katika kushiriki katika mkutano mkuu wa mwaka kwa ajili ya kutoa kushiriki katika vikao vya maamuzi ya wanahisa. Baada ya hapo unasubiri hisa zako kuongezeka thamani na kupata gawio.
SOMA; Huoni Kwa Sababu Hutaki Kuona.
Ni uwekezaji ambao unakua na mwekezaji anapata kipato
Ukiwa mwekezaji katika hisa, huku ukiwa unaendelea na kazi yako kama mwajiriwa au mfanyabiashara hisa zako zinaongezeka thamani na wewe mwekezaji utapata gawio kila baada ya miezi sita au mwaka. Utafaidika kwa haya ikiwa utaamua leo kwa kununua hisa za Kampuni ambazo zimesajiliwa katika soko la Hisa.
Faida ya Kuwa mmiliki wa Hisa
- Gawio
Ukiwa miliki wa hisa utapata gawio ikiwa Kampuni itapata faida katika kipindi hicho cha mwaka na wanahisa wakaridhia utoaji wa gawio. Gawio hutolewa mara mbili au moja kwa mwaka kutokana sera ya kampuni na maamuzi ya wanahisa.
- Ongezeko la thamani
Wanahisa pia huweza kupata faida itokanayo na ongezeko la thamani iwapo bei ya hisa itaongezeka kwenye soko la hisa. Ikiwa ulinunua hisa moja kwa Tsh 800 na baada ya mwaka hisa hizo sokoni zikauzwa kwa Tsh 1,400 basi unakuwa umepata ongezeko la thamani ya shilingi 6,00 kwa kila hisa. Hii ni faida tofauti na gawio, ikiwa utawekeza katika kampuni nzuri utapata gawio na ongezeko la thamani ndani ya mwaka mmoja. Vile vile ikiwa bei itashuka na kufikia Tsh 600 utapata hasara ya Tsh 200. Ila ukiwekeza katika kampuni nzuri ni vigumu kupata hasara na unakuwa na uhakika wa bei kuongezeka kwa 20% au 40% au zaidi kwa mwaka.
- Dhamana
Hisa kwa mwekezaji anaweza kuzitumia kama dhamana anapohitaji kupata mkopo.
- Huokoa muda wa usimamizi
Ni uwekezaji ambao humpatia mwekezaji uhuru wa kufanya shughuli nyingine na kwa wale ambao hawana muda wa usimamizi katika biashara huu ni uwekezaji mzuri kwao.
- Ni mali inayohamishika kwa urahisi
Ni mali ambayo inahamishika ki urahisi na kwa haraka pale mwekezaji anapohitaji pesa yake kwa ajili ya shughuli nyingine.
- Akiba
Njia ya kujiwekea akiba kwa ajili ya baadaye.
- Ushiriki wa jamii katika Uchumi
Inasaidia kuongeza ushiriki wa jamii katika shughuli za kifedha na kukuza uchumi.
Kama unahitaji kushiriki katika Uwekezaji katika hisa kwa kununua hisa soma makala hii Hivi ndivyo unavyoweza kununua hisa katika soko la Hisa
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano: emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
5/06/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Hivi Ndio Vitu Vinavyopelekea Ongezeko La Thamani Ya Hisa Kwa Mwekezaji.
Moja ya faida kwa mwekezaji kuwekeza katika Hisa ni pamoja na ongezeko la thamani ya hisa zake. Hisa ikiongezeka thamani kwa mwekezaji na uwekezaji wake unakua. Na ili uweze kufanya uwekezaji wenye manufaa ni vizuri ukawekeza kwenye Kampuni ambayo thamani ya Hisa inakua kwa kiwango cha chini kabisa 20% kwa mwaka. Ili thamani ya hisa iongezeke kuna vitu ambavyo huwa vinachochea kwa ukuaji wa thamani ya hisa hizo katika soko.
Vitu hivi hupelekea ongezeko la thamani ya Hisa kwa mwekezaji
Nguvu ya soko
Bei za hisa kuongezeka hutegemea ushindani kati ya wauzaji na wanunuzi wa hisa katika soko. Wanunuzi wakiwa wengi katika soko na wauzaji ni wachache hupelekea kupanda kwa bei kwa kuwa watashindana kwa bei. Ili hisa za kampuni hiyo ziwe na wanunuzi wengi hutegemea na ufanisi wa kampuni hiyo, hasa katika taarifa za fedha na utoaji wa gawio.
SOMA; Mambo 6 Yakukusaidia Kujua Shughuli Iliyokuleta Duniani.
Hali ya kiuchumi
Hali ya kiuchumi ya nchi hupelekea mwananchi kupata kipato ambacho hupelekea uwekezaji kuwa mkubwa. Mwenendo wa uchumi hupelekea ufanisi wa baadhi ya kampuni na kuchochea kuongezeka kwa bei zake katika soko kwa kuwa kampuni hiyo huwavutia wawekezaji kutokana na kufanya vizuri. Hali ya uchumi ikiwa sio nzuri hupelekea ufanisi katika soko kuwa mdogo na bei kushuka kwa baadhi ya kampuni.
Gawio
Gawio kwa mwekezaji ni kipato na faida mojawapo ya uwekezaji wake. Gawio hutolewa kutoka na faida ya Kampuni ambayo imepata na maamuzi wa wanahisa katika kikao na hutolewa mara moja au mara mbili. Kampuni ambazo hutoa gawio ambalo linaongezeka katika kiwango kizuri na kikubwa huchochea ukuaji wa bei zake. Wawekezaji wengi huvutiwa kuwekeza katika kampuni hizo na ushindani kuwa mkubwa na bei kuongezeka.
Ufanisi wa kampuni
Utendaji wa kampuni husika katika kutoa huduma au bidhaa huwavutia wateja na kampuni kufanya vizuri. Vile vile ufanisi wa kampuni katika taarifa zake za fedha kama ukuaji wa mauzo, faida, gawio na uwezo wa kampuni katika kupunguza gharama na madeni. Kampuni ikifanya vizurihupelekea bei zake kupanda kwa kuwa wawekezaji wengi huvutiwa kuwekeza katika Kampuni hiyo.
Thamani inayotegemewa/Mipango ya kampuni
Mipango mizuri na yenye tija kwa kampuni kwa kipindi kijacho huwavutia wawekezaji wengi kununua hisa za kampuni kwa kuwa wanajua katika kipindi kijacho kampuni hiyo itafanya vizuri. Mfano pale kampuni inapotangaza kufungua matawi katika sehemu nyingine au inapotangaza kuongeza bidhaa mpya sokoni. Vitu hupelekea wawekezaji wengi kuvutiwa kununua hisa za kampuni hiyo na ushindani kuwa mkubwa na bei kuongezeka.
“Wekeza Inalipa”
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano: emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
4/29/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Siri Ya Kutambua Kampuni Nzuri Ya Kuwekeza Ili Upate Faida.
Unapohitaji kufanya uwekezaji katika hisa inatakiwa kutambua kampuni sahihi za kuwekeza mtaji wako ili uweze kukua. Katika kuchagua kampuni sahihi ya kuwekeza unahitajika kuzingatia vitu muhimu ambavyo vitasaidia kujua kampuni hii inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri. Ili uweze kutambua kampuni inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri unatakiwa kuzingatia vitu vifuatavyo ambavyo ni muhimu kuvifahamu.
Ukuaji wa Mauzo (Revenue)
Kampuni ambayo mauzo yake yanaongezeka kila mwaka, hii inaonyesha kwa kiasi gani kampuni hiyo inafanya bidii katika masoko na bidhaa zake zinafanya vizuri katika soko. Ukuaji huu unaashirilia hata uongozi upo makini katika kutekeleza mipango yao kwa umakini. Vile vile ukuaji wa mauzo unaonyesha kwa kiasi gani kampuni hiyo bidhaa yake ilivyo na umuhimu katika matumizi ya watu katika eneo husika.
SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.
Kufahamu ukuaji wa faida ya kampuni
Kampuni ambayo inaukuaji mzuri wa faida kuanzia 20% au 25% kwa mwaka ni nzuri kwa kuwekeza kwa kuwa gawio litakua na kuwavutia wawekezaji wengi zaidi. Vile vile kampuni itapata pesa ya kuwekeza katika fursa nyingine ambazo zitaongeza faida kwa kipindi kijacho. Ukuaji wa faida unaonyesha kwa kiasi gani kampuni ambavyo ipo makini katika kudhibiti matumizi yasiyo ya msingi katika uendeshaji wa kampuni na kupelekea ongezeko la faida.
Ukuaji mzuri wa Gawio
Kampuni ambayo inaukuaji mzuri wa gawio ni ishara kuwa hata ukuaji wa faida ni mzuri. Gawio likiongezeka mwekezaji anapata kipato vile vile huwavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika kampuni hiyo na bei kuongezeka kutokana na ushindani kuwa mkubwa katika soko. Gawio ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wengi kuwekeza katika kampuni yoyote na gawio likikua na ushindani huwa mkubwa katika soko la hisa na kupelekea bei zake kupanda.
SOMA; Tabia Saba Za Watu Wasiokuwa Na Mafanikio.
Ukuaji mdogo wa madeni
Kampuni ambayo ukuaji wake wa madeni ni mdogo au madeni ya kampuni yanapungua huashiria kuwa kampuni hiyo ina mipango madhubuti katika kukuza mauzo na kupunguza madeni ili kupunguza hatari ya kufirisika. Kampuni ambayo madeni yake yanaongezeka kwa kila mwaka na kwa kiwango cha juu hii inaashiria kampuni haifanyi vizuri na kuna hatari ya kushindwa kulipa madeni.
Ukuaji wa bei za hisa za kampuni
Sehemu mojawapo kwa mwekezaji kupata faida kupitia uwekezaji wake kwa kupitia ongezeko la bei za hisa. Bei ya hisa ikiongezeka kwa kiwango kizuri na mwekezaji hupata faida ambayo hutokana na ongezeko la thamani. Kampuni ambayo ina ongezeko la bei kwa 20% au zaidi kwa mwaka ni kampuni nzuri kwa kuwekeza kwa kuwa mwekezaji atapata ongezeko la thamani ya hisa zake katika kiwango kinachorizisha. Katika soko la hisa kuna kampuni ambazo zina ukuaji bei za hisa wa zaidi ya 40% kwa mwaka ambazo ni nzuri kuwekeza kwa mwekezaji.
SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Umuhimu Na Jinsi Ya Kujijengea Tabia Ya Shukrani.
Kufahamu mipango ya Kampuni kwa miaka ijayo
Kampuni ili iweze kufanya vizuri katika soko ni kuwa na mipango mizuri kwa miaka ijayo ili iweze kuendana na mabadiliko yanayotokea. Mwekezaji ataweza kufahamu mipango ya kampuni kwa kuangalia taarifa za mwaka za kampuni (Annual Report) ambapo kampuni huonyesha mipango yao katika kipindi kijacho kama wanahitaji kuongeza bidhaa mpya au kuongeza matawi katika sehemu nyingine au nchi nyingine.
Hivi ni vitu vya msingi kwa mwekezaji kuviangalia unapohitaji kuwekeza katika hisa ili uweze kupata manufaa na kuwekeza kwa faida na kukuza mtaji wako. Tukutane katika makala nyingine ambazo zinakujenegea uwezo zaidi katika kuwekeza katika hisa.
SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.
Ili uweze kupata taarifa za kiswahili zitakozokuwezesha kutamua ukuaji wa mauzo, faida ya kampuni, ukuaji wa bei na mipango ya kampuni tuwasiliane kwa mawasiliano hapo chini.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
4/08/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Jinsi ya kuzuia hatari ya kupata hasara kupitia uwekezaji katika hisa
Uwekezaji katika hisa ni kama biashara nyingine unaweza kupata hasara au faida, ila uwekezaji huu ni wa upekee ni jinsi ambavyo unafanyika. Ili uweze kukuza thamani ya pesa yako kupitia uwekezaji katika hisa na kuondoa hatari ya kupoteza pesa yako kuna vitu vya kuzingatia.
Jinsi ya kuzuia hatari ya kupata hasara kupitia uwekezaji katika hisa
1) Wekeza katika kampuni ambayo inafanya vizuri
Ili kuondoa hatari ya kupoteza pesa yako kupitia uwekezaji katika hisa ni kuwekeza katika kampuni ambazo zinafanya vizuri. Kuwekeza kwa kampuni ambazo zinafanya vizuri ni rahisi kukuza mtaji wako na kupata gawio lako. Katika somo lililopita tumeona jinsi ya kuchagua kampuni ambayo inafanya vizuri, kwa hiyo ni vizuri kwa mwekezaji kuwekeza katika kampuni ambayo inafanya vizuri.
SOMA; Kila Sehemu Utakayokwenda Utawakuta Watu Hawa.
2) Wekeza kwa muda mrefu
Unapoamua kuwekeza katika hisa ni vizuri ukawa na malengo ya kuwekeza kwa muda mrefu. Uwekezaji wa muda mrefu una manufaa makubwa kwa mwekezaji na unapunguza hatari ya kupata hasara. Huwezi ukawekeza kwa mwezi mmoja na ukasema wewe ni mwekezaji bali wewe ni mtu ambaye anabahatisha au mtu ambaye ana Bet. Kuonyesha jinsi gani kuwekeza kwa muda mrefu kuna manufaa kuna moja wa msomaji katika blogu yangu ya www.wekezamtanzania.blogspot.com alikiri kuwa alinunua hisa za kampuni ya SWIS mwaka 2013 kwa bei ya shilingi 2000 na mpaka sasa hisa za kampuni ya SWIS zinauzwa kwa shilingi 6,500. Bei ya hisa imeongezeka mara tatu ya bei ya mwanzo, kuwa na malengo ya kuwekeza kwa muda mrefu kuna manufaa makubwa kwa mwekezaji.
SOMA; BIASHARA LEO; Fukuza Wateja Hawa, Ni Mzigo Kwako.
3) Wekeza kampuni zaidi ya moja
Njia nzuri ya kulinda na kukuza uwekezaji wako ni kuwekeza kwenye kampuni zaidi ya moja katika soko la hisa. Ukiwekeza kwenye kampuni tatu au zaidi ikiwa kampuni moja haitofanya vizuri utafidiwa na ukuaji mzuri wa kampuni nyingine katika soko la Hisa. Hii ni njia mojawapo ambayo ina manufaa makubwa kwa mwekezaji. Ikiwa unataka kuwekeza unaweza ukatenga kiasi cha mwezi wa kwanza unanunua hisa katika kampuni ya SWIS, mwezi mwingine unanunua za CRDB na mwezi unaofuata unanunua za TBL. Au unaweza ukagawa kiasa sawa kwa kampuni ambazo umechagua kuwekeza mfano. SWIS 25%, CRDB 25%, TBL 25% na NMB 25% ni asilimia ishirini na tano ya akiba yako ya kuwekeza.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com/0714445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
SOMA; Haya Ndio Matumizi Mazuri Ya Mshahara Wako Ambayo Yatakuletea Furaha Na Mafanikio.
4/01/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Maswali ambayo huulizwa mara nyingi kuhusu uwekezaji katika hisa.
Watu wengi wanatamani kufanya uwekezaji katika hisa na kufahamu jinsi ambavyo uwekezaji huu unavyofanyika ila kuna vitu vingi hawavifahamu katika uwekezaji. Maswali haya yatakufungua mwanga jinsi ya kutambua uwekezaji katika hisa, jinsi ambavyo unafanyika na jinsi ambavyo mwekezaji atapata manufaa katika uwekezaji huu.
1. Nini ushiriki wa soko la hisa (DSE) katika kupanda na kushuka kwa thamani ya Hisa?
Soko la Hisa (DSE) haihusiki kabisa katika kuchangia kupanda na kushuka kwa thamani ya hisa. Vitu ambavyo vinasababisha kushuka na kupanda kwa za hisa ni nguvu ya soko (yaani wanunuzi na wauzaji). Wanunuzi wakiwa wengi katika hisa ya kampuni Fulani hupelekea kupanda kwa bei kwa sababu watashindana kwa bei ili kila mtu aweze kununua hisa hizo.
2. Wapi unaweza kupata bei za hisa?
Ili uweze kupata taarifa za bei ya hisa za kila siku tembelea tovuti yao ambayo ni www.dse.co.tz. Katika tovuti yao utaweza kufahamu bei za kampuni ambazo zimeongezeka na kampuni ambazo bei zake zimeshuka.
SOMA; Changamoto Inayokusumbua Kwenye Biashara.
- Naweza kununua hisa kuanzia ngapi?
Kiwango cha chini cha kununua hisa katika soko ni hisa 100 ila mwekezaji unaweza kununua hisa chini ya mia moja kwa lugha kingereza huitwa odd lots board. Kwa hiyo mwekezaji yoyote anaweza kununua hisa chini ya mia moja katika soko la hisa yaani unaweza nunu hisa 5, 10, 20 au zaidi.
4. Hisa zinauzwa wapi?
Hisa zinauzwa sehemu mbili i) katika soko la wali, hapa ni pale kampuni ambapo inauza hisa zake kwa mara ya kwanza kabla ya kusajiliwa katika soko la hisa. ii) Hisa zinauzwa kwa madalali wa soko la Hisa au unaweza nunua katika tawi la benki ya CRDB lolote lile. Anwani za madalali wa soko la Hisa zinapatikana katika tovuti ya DSE au soma makala hivi ndivyo unavyoweza kununua hisa.
5. Nalipia hisa mara moja tu au ni kila mwezi kwenye Kampuni husika?
Ukinunua hisa pesa unatoa mara moja tu, ikiwa utahitaji kununua hisa zingine utalipia kwa hisa ambazo unaongeza. Baada ya kununua hisa zako hakuna gharama nyingine zaidi ya kusubiri hisa zako kuongezeka thamani na kupata gawio. Ikiwa utahitaji kununua hisa nyingine utalipia kwa bei ambayo ipo sokoni.
SOMA; KITABU; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.
- Kwa sisi tulioko mikoani tunawezaje kununua hisa?
Mmoja wa madalali wa soko la Hisa ameingia ubia na benki ya CRDB kwa hiyo popote lililopo tawi la benki ya CRDB unaweza ukanunua hisa. Vile vile kuna kampuni nyingine za madalali ambalo watafanya utaratibu wa kununua hisa.
- Je unaweza kupata taarifa za utendaji na ufanisi wa kampuni unapokuwa mwanahisa?
Kampuni yoyote ambayo imesajiliwa katika soko la hisa ni lazima iweke taarifa zake muhimu kuhusu utendaji wake na taarifa za fedha za kila mwaka, miezi mitatu na miezi sita. Kama mwekezaji taarifa hizi zitakusaidia kujua kampuni ambayo inafanya vizuri na ambayo haijafanya vizuri ili uweze kuchagua kampuni bora ya kuwekeza.
- Hisa zinapatikana muda wote au ni kwa muda Fulani tu?
Kuna aina mbili ya masoko ya hisa, soko la awali ambapo hisa huuzwa kwa mara ya kwanza na kwa kipindi maalumu tu na kuna soko la upili ambapo soko la hisa halina kipindi maalum unaweza kununua na kuuza muda wowote iwe tu ni siku ya kazi (Jumatatu hadi Ijumaa). Katika soko la upili ndipo soko la Hisa linapofanya kazi zake kila siku ya kazi ambapo mwekezaji atanunua na kuuza hisa zake.
SOMA; Haya Ndio Matumizi Mazuri Ya Mshahara Wako Ambayo Yatakuletea Furaha Na Mafanikio.
- Je gawio hutolewa mara ngapi na kampuni kwa wawekezaji?
Gawio hutolewa kulingana na sera ya kampuni husika. Kuna kampuni ambazo hutoa gawio mara mbili kwa mwaka na kuna kampuni ambazo hutoa gawio mara moja kwa mwaka. Ukiwa mmiliki wa hisa unayo haki ya kupata gawio ikiwa kampuni itatoa gawio hilo kulingana idadi ya hisa ambazo unamiliki.
- Je nikifariki hisa zako atamiliki/atarithi nani?
Soko la hisa limeandaa utaratibu ambao kila mwekezaji ambaye ananunua hisa katika fomu ambazo unapewa utajaza mrithi wako. Mrithi wa hisa unaweza kumchagua mtu yoyote Yule ambaye wewe ungependa awe mrithi wako.
Endelea kutembelea mtandao huu kuendelea kupata makala nzuri kuhusu uwekezaji katika Hisa na mfulululizo wa maswali na majibu kuhusu bidhaa ya Hisa.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com simu 0714445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.
3/25/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Jinsi ya kuchagua Kampuni ya kuwekeza katika Soko la Hisa
Unapohitaji kuingia kwenye uwekezaji katika Hisa swali la kwanza utajiuliza je ni kampuni gani inafaa kuwekeza. Swali hili ni zuri kwa mwekezaji kwa sababu anahitaji kuweka pesa yake katika sehemu salama na ambayo itafanya biashara yake izidi kukua. Kuchagua kampuni inayofanya vizuri katika soko la ni jambo gumu kwa watu wengi hasa ambao hawana ujuzi kuhusu uwekezaji katika Hisa. Leo tutaangalia mbinu ambazo zitamsaidia mtu ambaye hana ujuzi kuhusu uwekezaji ili aweze kuchagua kampuni ya kuwekeza katika soko la Hisa.
SOMA; Hivi ndivyo unavyoweza kununua Hisa katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE)
Kwa kuanza kuwekeza sasa ndipo unapoanza kujifunza kuhusu uwekezaji katika Hisa. Na ukiendelea kusoma makala kama hizi utaendelea kukuza uelewa katika uwekezaji katika Hisa na kuweza kuwekeza bila wasiwasi.
Kampuni ambazo ni nzuri kwa ajili ya kuwekeza kwa mtu ambaye ana ujuzi mdogo
1. Wekeza katika Kampuni ambayo unaipenda/unaifahamu
Katika kampuni ambazo zimesajiliwa katika soko la Hisa kuna kampuni ambayo utakuwa unaipenda. Anza kuwekeza toka katika Kampuni hiyo kwa sababu unaipenda hata kama haitafanya vizuri utakuwa mvumilivu na kusubiri kwa kipindi kijacho.
2. Wekeza katika kampuni kubwa
Katika soko la Hisa kuna Kampuni kubwa na ndogo, kwa mwekezaji ambaye anafuatilia taarifa katika soko la Hisa ni rahisi kufahamu kampuni kubwa na kampuni ndogo ambazo zimesajiliwa katika soko la Hisa, Ukiwekeza katika kampuni kubwa una hatari ndogo kuweza kupoteza mtaji wako.
SOMA; Weka Pamoja Vitu Hivi Vitatu Na Tayari Wewe Ni Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.
3. Wekeza kwa Kampuni ambayo inauza hisa zake kwa mara ya kwanza (IPO)
Njia nzuri kwa mwekezaji ambaye anao ujuzi mdogo kuweza kuwekeza katika soko la Hisa. Ni vizuri kuanza kuwekeza katika Kampuni ambazo zinauza Hisa zake kwa mara ya kwanza katika soko. Mara nyingi bei zake huwa chini ya thamani halisi hivyo ni rahisi bei kuongezeka zikisajiliwa katika soko. Nunua hisa kwa kampuni ambazo zinakaribia kusajiliwa katika soko la Hisa. Ili kufahamu kampuni ambazo zinauza hisa zake kwa mara ya kwanza tembelea www.dse.co.tz au nitakuwa natoa taarifa kupitia blog hii ya Jiongeze ufahamu au www.wekezamtanzania.blogspot.com .
SOMA; Maswali Matatu Kwa Anayetaka Kuwa Mjasiriamali Kujiuliza Kutoka Kwa Richard Branson.
Jinsi kuchagua kampuni inayofanya vizuri
Ufanisi wa Kampuni husika
Hapa tunaangalia ufanisi wa kampuni yenyewe kutokana na taarifa zake za fedha. Kwa mwekezaji anayeanza ataangali vitu vifuatavyo katika taarifa za fedha za kampuni
· Revenue/Sales/Interest income (Ukuaji wa mauzo)
· Net Income (Faida baada ya kutoa gharama zote pamoja na kodi)
· Earnings per share (kwa kiasi gani kila hisa imepata toka kwenye faida ya kampuni)
· Share Price (Bei za hisa kwa kipindi fulani)
· Dividend (Ukuaji wa gawio)
Kwa vitu ambavyo nimevionyesha hapo juu utaangalia katika taarifa za fedha za kampuni kupitia website ya DSE na kama unapata shida unaweza kunitafuta kwa mawasiliano nitakayoweka hapo chini.
Ili uweze kufanya kwa urahisi utaandaa table kama iliyopo hapo chini ili kuweza kujua ni kampuni ipi imefanya vizuri. Ili uweze kufanya uamuzi sahihi unatakiwa kulinganisha kampuni ambazo zinafanya biashara inayofanana.
|
|
| 2012 | 2013 |
|
|
| MAKAMPUNI | Details |
|
| Ongezeko % | Nafasi |
| NMB | Interest income | 287,923 | 355,686 | 23.5 | 3 |
|
| Net Income | 97,401 | 133,906 | 37.5 | 2 |
|
| Earnings per share (EPS) | 195 | 267.81 | 37.3 | 1 |
|
| Share Price | 1,120 | 2,620 | 133.9 | 1 |
|
| |||||
| DCB | Interest income | 18,600 | 24,665 | 32.6 | 2 |
|
| Net Income | 1,908 | 3,711 | 94.5 | 1 |
|
| Earnings per share (EPS) | 50 | 55 | 10 | 3 |
|
| Share Price | 620 | 490 | -20.9 | 3 |
Mabadiliko ya bei kwa kampuni zilizo katika soko la Hisa
Ni vizuri ukawa na taarifa ya mabadiliko ya bei za Hisa kwa Kampuni ambazo zipo katika soko la Hisa kwa miaka miwili nyuma. Ili uweze kufahamu ongezeko la bei za Hisa katika soko. Taarifa hizi zitakuasidia kujua kama kampuni bei zake zinaongeze, zinapungua au zinashuka kwa miaka miwili. Taarifa hizi utazipata kupitia website ya DSE.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com/0714445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
3/18/2015 07:30:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Hivi ndivyo unavyoweza kununua Hisa katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE)
Watu wengi wanatamani kununua hisa kupitia soko la Hisa la Dar es salaam ila bado hawafahamu ni jinsi gani wanaweza kununua hisa wakiwa mahali popote pale Tanzania. Soko la Hisa limetengeneza njia rahisi ambayo kila mtu anaweza kununua hisa akiwa sehemu yoyote ile Tanzania.
Unapohitaji kununua Hisa katika soko la Hisa unatakiwa kuwa na email, akaunti ya bank na kuwa na mawasiliano brocker yoyote Yule ambaye amesajiliwa katika soko la Hisa.
SOMA; Soko la Hisa la Dar: Fursa ya kipekee kwa wajasiriamali wazalendo Tanzania
Hivi ndivyo unavyoweza kununua Hisa
Baada ya kufanya maamuzi ya kampuni gani ya kununua katika soko la Hisa. Unaweza kutamfuta brocker ambaye amesajiliwa na soko la Hisa kwa ajili ya kununua hisa zako.
1. Wasiliana Brocker kwa ajili ya kununua hisa
Wasiliana na brocker yoyote ambaye amesajiliwa katika soko la hisa. Baada ya kuwasiliana na brocker ataomba email yako kwa ajili ya kukutumia fomu za kujaza. Utaprint fomu hizo ambazo zitakuwa mbili; moja kwa ajili ya taarifa zako binafsi na nyingine kwa ajili ya ununuzi wa hisa.
Hii ni orodha ya Brockers waliosajiliwa na soko la Hisa
· CORE securities Ltd; Mawasiliano Tel: +255 22 212 3103 au info@coresecurities.co.tz
· Orbit Securities Co. Ltd; Mawasiliano Tel: +255 22 211 1758 au orbit@orbit.co.tz
· Rasilimali Ltd; Mawasiliano Tel: +255 22 211 1711 au rasilimali@africaonline.co.tz
· Tanzania Securities Ltd; Tel: +255 22 211 2807 au info@tanzaniasecurities.co.tz
· Vertex International Securities Ltd; Tel: +255 22 211 6382 au vertex@vertex.co.tz
· Solomon Stockbrokers Co. Ltd; Tel: +255 22 211 2874 au solomon@simbanet.net
· E.A. Capital Ltd P.O. Box 20650, Dar es Salaam au Tel +255 779740818/ +255 784461759
EC@EACAPITAL-TZ.COM
· ZAN Securities Ltd P.O. Box 5366, Dar es Salaam au Tel +255 22 2126415
info@zansec.com
2. Jaza fomu ulizopewa
Baada ya kuprint fomu ulizotumiwa utajaza kutokana na mahitaji ya fomu husika. Baada ya kumaliza kujaza fomu zako, utazi scan zote na kuzituma kama attachment kwenye email ya brocker na kusubiri majibu kutoka kwake.
SOMA; Msingi na ustadi wa kuwekeza kwenye Soko la Hisa
3. Utatumiwa kiasi cha kutuma na akaunti ya benki kwa ajili ya kuingiza pesa
Baada ya kutuma fomu zako kwa brocker atazipitia na kujua ni kiasi gani ulipie ili uweze kununua hisa hizo. Baada ya kupata akaunti ya benki ya utaingiza kiasi cha pesa ambacho umeambiwa kwenye akaunti ya kampuni ya brocker. Baada ya kulipia benki pesa za ununuzi wa hisa uta scan risiti ya benki.
4. Tuma risiti ya benki ambayo umescan kwenye email ya brocker
Baada ya kuscan risiti ya benki utatuma kwa brocker ili kuthibitisha kuwa umefanya malipo hayo kwenye akaunti yao na wewe ni muhusika. Baada ya kutuma atakujibu kuwa amepata na usubiri hisa zako kununuliwa.
SOMA; Hatua Muhimu Kuzifahamu Unapohitaji Kuwekeza Katika Hisa.
5. Subiri kununuliwa kwa hisa zako
Baada ya kupitia hatua zote, subiri kwa ajili ya kununuliwa kwa hisa zako. Kutoka na kupanda na kushuka kwa bei unaweza kumwambia kuwa brocker anunue hisa zako kulingana na bei ya soko hii ni kwa sababu wakati unajaza fomu ulipanga bei ya kununulia.
Kumbuka: Vitu vyote nilivyoelewa unaweza kufanya ndani ya siku moja ikiwa utawasiliana na brocker mapema na kufanya kwa uharaka. Vile vile unaweza tumia gmail akaunti kwa urahisi wa utumaji wa taarifa zako.
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com/0714445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
3/11/2015 09:00:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Hatua Muhimu Kuzifahamu Unapohitaji Kuwekeza Katika Hisa.
Uwekezaji katika Hisa limekuwa jambo geni kwa watu wengi. Kwa kuwa mmiliki wa Hisa unapata fursa ya kuweza kuongeza kipato chako huku ukiendelea shughuli zako nyingine ambazo zinakuingizia kipato. Uwekezaji katika nchi yetu bado ni mchanga, kwa hiyo kuna fursa kubwa ya kuweza kutengeneza kipato. Kama unataka kuwa mwekezaji katika Hisa ni muhimu kufahamu hatua hizi.
SOMA; Soko la Hisa la Dar: Fursa ya kipekee kwa wajasiriamali wazalendo Tanzania
Hatua Muhimu kuzifahamu unapohitaji kuwekeza katika Hisa
1. Fanya maamuzi kuwekeza
Kufanya maamuzi ni jambo zuri na inafanya akili yako kuwa tayari kwa ajilia ya kuingia kwenye uwekezaji huu.
2. Kufahamu ni sehemu gani ambayo unaweza kununua au kuuza Hisa
Ili uweze kuwa mmiliki wa Hisa ni lazima uweze kufahamu sehemu ambayo unaweza kununua Hisa zako. Kuna sehemu mbili ambazo unaweza kununua Hisa i) Kampuni inapouza Hisa zake kwa mara ya kwanza kabala kusajili katika soko la Hisa (IPO), ni vizuri ukanunua Hisa kwa kampuni ambayo inakaribia kusajiliwa katika Soko la Hisa; i) Unaweza kununua kupitia Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) kwa kupitia mawakala wake.
SOMA; Msingi na ustadi wa kuwekeza kwenye Soko la Hisa
3. Kufahamu ni kampuni gani unahitaji kuwekeza
Katika soko la Hisa la Dar es salaam kuna kampuni ishirini na moja (21) ambazo zimesajiliwa na soko hilo. Unapohitaji kuwa mmiliki wa Hisa unatakiwa kuchagua Kampuni ambayo inakufaa kwa ajili ya uwekezaji wako. Katika kuchagua Kampuni unatakiwa kuwa na taarifa sahihi kuhusu kampuni hiyo na ufanisi wa kampuni hiyo katika soko la Hisa ili uweze kufanya uwekezaji wenye manufaa.
4. Muda mzuri kwa mwekezaji kununua Hisa
Kama mwekezaji ni vizuri ukafahamu muda mzuri kwako kununua Hisa wenye manufaa. Muda mzuri kwa mwekezaji kununua Hisa zake i) Kampuni inapouza hisa kwa mara ya kwanza kwa sababu mara nyingi kampuni bei zake huwa chini ya thamani halisi ili kuvutia wawekezaji ii) Kipindi cha januari hadi Machi kwa sababu watu wengi huuza hisa zao kwa shida mbali mbali na mara nyingi kipindi hiki Uchumi haufanya vizuri sana iii) Bei za Hisa zinaposhuka ila lazima utambue sababu ya kushuka kwa bei zake kama ni ya muda mfupi.
SOMA; Sheria NANE Za Kufanikiwa Kwenye Biashara Kutoka Kwa Warren Buffett.
5. Muda mzuri kwa mwekezaji kuuza Hisa
Vile vile unapoingia kwenye uwekezaji katika Hisa ukafahamu muda mzuri wa kuuza hisa zako. Muda mzuri wa kuuza hisa zako ni pale kampuni inapokuwa haifanyi vizuri, bei zake zinaposhuka na zinaonyesha zitaendelea kushuka. Unapofanya maamuzi ya kuuza hisa zako ni vizuri ukawa na taarifa sahihi za Kampuni husika. Ni vizuri kwa mwekezaji akawa na malengo ya uwekezaji kwa kipindi cha muda mrefu.
6. Hatua ya mwisho unaweza kununua Hisa na kuwa mmiliki wa kampuni
Baada ya kupitia hatua zote hapo juu unaweza kufanya maamuzi ya kununua hisa katika soko la Hisa. Unaweza kununua hisa katika soko la Hisa kwa kupitia mawakala wa soko la hisa (Brockers) ambao wamesajiliwa na soko la Hisa au kununua hisa zinapouzwa na Kampuni kwa mara ya kwanza. Vitu vya msingi kuwa navyo unapohitaji kununua hisa i) uwe na email ambayo itakusaidia kutuma baadhi ya taarifa na akaunti ya benki.
SOMA; Vitu VITATU Vinavyoathiri Kipato Chako Na Jinsi Ya Kukiongeza.
Hawa ni baadhi ya mawakala wa soko la Hisa (Brockers) ambao wamesajiliwa
CORE securities Ltd; Mawasiliano Tel: +255 22 212 3103 au info@coresecurities.co.tz
Orbit Securities Co. Ltd; Mawasiliano Tel: +255 22 211 1758 au orbit@orbit.co.tz
Rasilimali Ltd; Mawasiliano Tel: +255 22 211 1711 au rasilimali@africaonline.co.tz
Tanzania Securities Ltd; Tel: +255 22 211 2807 au info@tanzaniasecurities.co.tz
Mwandishi: Emmanuel Mahundi
Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com/0714445510
Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com
3/04/2015 07:00:00 AM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Maazimio Matano Muhimu Ya Fedha Kwa Kila Kijana Kuweka Mwaka Huu 2015.
Bado tupo kwenye msimu wa mwaka mpya na huu ni wakati muhimu wa kuweka maazimio na malengo mbalimbali ili kuboresha maisha yetu zaidi.
Huenda tayari umeshaweka malengo na mipango yako ya mwaka 2015, leo tutakumbushana mambo machache ambayo ni ya muhimu sana kuyajumuisha kwenye malengo yako ya mwaka huu 2015.
Kama bado hujaweka malengo mpaka leo bado hujachelewa, unaweza kukaa chini leo na kuandika malengo yako kwenye karatasi na kuanza kuyafanyia kazi.
Kama huna mpango wa kuweka malengo kabisa kwa mwaka huu pole…
Yafuatayo ni maazimio muhimu kuweka kwenye malengo yako ya kifedha kwa mwaka huu 2015;
1. Weka akiba zaidi ya ulivyoweka mwaka jana.
Kama mwaka jana ilikuwa unaweka akiba, mwaka huu ongeza kiwango cha akiba unachoweka. Kama huna utaratibu wakujiwekea akiba kabisa anza na kuweka pembeni asilimia 10 ya kile unachopata. Ukipata elfu kumi, weka elfu moja pembeni. Ukipata laki moja weka elfu kumi pembeni. Baada ya muda mfupi utaona mabadiliko makubwa ya kifedha kwenye maisha yako.
2. Punguza madeni yako.
Madeni ni mzigo, madeni ni utumwa, mtu anayekudai anaweza kunyanyasa utu wako muda wowote. Mwaka huu weka azimio la kupunguza madeni yako na kama ikiwezekana lipa yote kabisa. Kaa chini na wale wanaokudai na wape pendekezo la njia rahisi kwako kuwalipa kisha anza kuwalipa. Utanunua uhuru wako ulioupoteza.
3. Tengeneza, badilisha bajeti yako.
Ni muhimu sana kuishi kwa bajeti, kama mpaka sasa huna bajeti tafadhali sana tengeneza bajeti yako leo. Amua ni kiasi gani utakachoishi nacho kwa siku, wiki na hatimaye mwezi. Na jitahidi sanakuishi kwa kiasi hiko, usinunue vitu kwa tamaa tu, nunu kile ulichopanga kwenye bajeti. Kama umepanga mwezi huu hununui nguo, usishawishike kununua nguo hata ukikutana nayo nzuri kiasi gani, nguo nzuri huwa haziishi. Siku ambayo bajeti yako inaruhusu utapata nzuri kuliko uliyokutana nayo.
4. Jifunze kuhusu uwekezaji.
Bila shaka uwekezaji ni somo gumu sana kwa vijana. Wengi hawapendi kusikia kitu hiki na huona ni kitu kinachohitaji elimu kubwa. Ukweli ni kwamba uwekezaji ni rahisi na ni njia rahisi kwako kukuza kipato chako. Kuna aina nyingi za uwekezaji, kuna uwekezaji wa kununua mali, uwekezaji wa fedha na kadhalika. Unaweza kuanza kujifunza hapa hapa kwa kubonyeza maandishi haya
Soma; Hivi ndivyo unavyoweza kutajirika kwa kuanza na shilingi elfu moja.
5. Jijengee nidhamu ya fedha.
Kama hutakuwa na nidhamu ya fedha, yote tuliyojadili hapo juu hayataweza kukusaidia. Mara zote tumia pungufu ya unachokipata, yaani matumizi yako yasizidi mapato yako. Na pia kwenye kuweka akiba weka akiba na inayobaki ndio ufanye matumizi. Ukifanya matumizi ili inayobaki ndio uweke akiba hutabakiwa na kitu.
Wewe kama kijana ni muhimu sana kwako kujijengea misingi imara ya kifedha na kiuchumi. Weka maazimio hayo matano muhimu mwaka huu 2015 na anza kuyafanyia kazi.
1/12/2015 11:20:00 AM | Labels: FEDHA, SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Soko la Hisa la Dar: Fursa ya kipekee kwa wajasiriamali wazalendo Tanzania
Soko letu limekuwa likiwanufaisha zaidi wageni na wananchi wa nchi jirani ambao hulitumia kikamilifu kujinufaisha na wazalendo wengi kutoelewa nini kinachoendelea. Kwa wale waliokwisha jitosa, huwezi amaini jinsi wanavonufaika na kuwekeza zaidi na zaidi.
Leo kidogo tutupe jicho kwenye hii sekta ya hisa… Si sekta ngeni sana ila kwa hapa nchini wananchi wengi hawajaigundua na kushiriki kikamilifu kama nchi jirani na Tanzania. Wenzetu Kenya wamejitahidi kwenye ushiriki wa soko lao la Hisa la Nairobi (Nairobi Stock Exchange). Na kwa Afrika Mashariki, hili Soko la Hisa la Nairobi ndilo soko kubwa kuliko yote.
Pamoja na changamoto zake, hili soko lina faida kubwa kwa wale walioligundua na wanaoendelea kulitumia. Kuna mjasiriamali mmoja, yeye alinunua hisa za Twiga mwishoni mwa miaka ya 90 au mwanzoni mwa miaka ya 2000 zikiwa zinauzwa kati ya 200-300 kwa kipande. Leo hii kipande hicho hicho cha Twiga Cement kinauzwa kati ya 2500-2006 kiasi cha miaka 13 tu mbele.
Mdau huyu wa soko hilo anakiri kama angejua ukuaji ni wa kiasi hiki basi angenunua zaidi ya hizo alizonunuaga. Na ameendelea kuongeza vipande vyake kila awezapo. Anadai yeye hupenda kuwekeza kwenye hisa sababu hakuna usumbufu wa uendeshaji . Ukishanunua hisa unakaa na kungoja zipande ama zishuke ili na wewe uuze za kwako. Anakiri kuwa soko hili limemnufaisha sana na anawashauri wengine wajiunge nalo wapate kunufaika pia.
Wengi wetu wenye mitaji midogo midogo tunaweza kunufaika kwa kujiunga na hili soko la hisa la Dar es Salaam na kununua vipande kwa pesa tuliyonayo. Vipande vingi vimeonesha kupanda thamani yake ikiwemo hisa za makampuni ya bia (TBL na SBL), Saruji (Twiga na Simba ) na Bank kama NMB. Kama mwekezaji mzalendo, ukijitosa ukanunua hisa zako za 2,000,000 leo, baada ya miaka 4 unaweza kuziuza hata kwa faida kubwa tu bila kuteseka na usumbufu wa uendeshaji kama zilivyo biashara nyingine.
Upande wa pili soko hili la hisa pia lina magumu yake kama kupotea kwa mtaji wako kutokana na kushuka kwa thamani ya vipande. Hili kwa mfano, limewaathiri wawekezaji walionunua hisa za CRDB na TOL ambazo zimekuwa zikikumbwa na kushuka kwa thamani mara kwa mara. Muhimu ni kuwa makini tu kwa kuchagua vyema ni hisa zipi ununue na kampuni ipi uwekeze.
Soko letu limekuwa likiwanufaisha zaidi wageni na wananchi wa nchi jirani ambao hulitumia kikamilifu kujinufaisha na wazalendo wengi kutoelewa nini kinachoendelea. Kwa wale waliokwisha jitosa, huwezi amaini jinsi wanavonufaika na kuwekeza zaidi na zaidi.
Huu ni wito wangu kwenu wazalendo wenzangu, mkajiunge na soko la hisa la Dar es Salaam na kufaidi matunda yake!
Chanzo cha makala haya ni FIKRA PEVU.
11/02/2014 05:57:00 PM | Labels: HABARI ZA UWEKEZAJI, SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Msingi na ustadi wa kuwekeza kwenye Soko la Hisa
JE ukiwa kama mwananchi wa kawaida usingependelea kuwa mmiliki wa kampuni bila ya kuwa na ulazima wa kufika kazini na kufanya kazi za kila siku?
Hebu tafakari kwa kina, upo nyumbani kwako umepumzika au ukifanya shughuli zako nyingine na ukiiangalia kampuni yako inakua kwa ufanisi na tija na baada ya muda unachukua hundi yako ya gawio huku mtaji wako ukiendelea kukua kila kukicha.
Jambo hili linaweza kuonekana kama ni njozi au ndoto, lakini ukweli ni kwamba lina ukweli usiopingika na jawabu lake ni kuwa na hisa hususani katika kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Kwa hiyo ili kutimiza ndoto yako ya kukidhi mahitaji yako ya fedha na kuanza safari yako ya kumiliki kampuni kupitia Soko la Hisa unatakiwa kuwa na uelewa mzuri wa jinsi gani hisa zinavyouzwa na kununuliwa katika soko la hisa.
Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita, wananchi wengi wa kawaida nchini Tanzania wamekuwa na shauku ya kununua hisa kwenye kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam na kulifanya soko hilo kukua kwa haraka. Hivi sasa hisa zinaonekana ya kwamba ndiyo chombo kinachoweza kuwapatia wananchi ukuaji wa uchumi binafsi kutokana na kumiliki kampuni zilizo katika sekta muhimu katika uchumi wa nchi yetu.
Pamoja na kuwa hisa zimeanza kupata umaarufu mkubwa, lakini watu wengi bado hawajaweza kuwa na uelewa mkubwa kuhusiana na hisa na jinsi ya kuweza kununua na kuuza hisa hizo.
Nadhani mara nyingi mmeweza kusikia baadhi ya watu wakisema maneno yafuatayo:
"Umesikia, mjomba wake Marwa ametengeneza pesa nyingi sana katika hisa za NMB; na kwa sasa atapata bahashishi nyingine..." au vile utasikia "Chukua tahadhari kubwa kwenye hisa zako, kwa sababu unaweza ukapoteza hisa zako ndani ya siku chache!"
Maneno yote haya ni upotoshaji mkubwa kwa sababu yanasababishwa na mawazo potofu ya kupata utajiri wa haraka haraka. Mara nyingi baadhi ya watu wanafikiri ya kwamba ununuaji wa hisa ni njia ya mkato ya kupata utajiri na hakuna hatari ya kupata hasara.
Msukosuko wa masuala ya fedha duniani uliotokea hivi karibuni umeweza kuthibitisha ya kwamba soko la hisa pia linaweza kuyumba.
Ukweli ni kwamba hisa zinaweza kuleta utajiri mkubwa lakini si kwamba hakuna hatari ya kupata hasara. Jambo la msingi la kujilinda ili kutokupata hasara na ni vyema kabla hujanunua hisa, ni vyema ukajua unawekeza pesa zako kwenye hisa za kampuni ipi. Na ndiyo maana kutokana na suala hilo, Soko la Hisa la Dar es Salaam limeanzisha programu inayomsaidia mwanahisa kuweza kufanya maamuzi yake binafsi kujua anafanya uwekezaji katika kampuni ipi bila ya kuwa na shinikizo.
Je, hisa ni kitu gani? Hisa ni nini?
Elimu ya msingi ambayo unatakiwa kuwa nayo kabla ya kufanya uwekezaji katika soko la hisa nikujua hisa ni kitu gani, aina tofauti za hisa na soko la hisa lenyewe linafanyaje kazi.
Kwa hiyo ni vyema tukaanza kwa kujua hisa ni kitu gani.
Kwa kutumia lugha nyepesi ukinunua hisa unathibitisha umilikaji wa kampuni. Hisa zinathibitisha kumiliki mali za kampuni na mapato yake. Jinsi unavyonunua na kuwekeza hisa katika kampuni ndivyo jinsi umiliki wako katika kampuni hiyo unavyoongezeka thamani.
Kwa hiyo, hakuna utofauti wowote kati ya hisa na mtaji; vyote ni sawa na vinawakilisha umiliki wa kampuni.
Aidha, kwa kununua hisa, fedha ambayo ingekuwa imekaa tu bila kufanyiwa kazi au ipo katika akaunti ya akiba na kupata riba ndogo, inaingia katika mzunguko wa fedha ambao unakuwa na tija katika uchumi.
Kuwa mmiliki wa kampuni na faida zake
Kumiliki hisa za kampuni inamaanisha ya kwamba wewe unakuwa miongoni mwa wanahisa wengi ambao wana haki ya kumiliki kila kitu ambacho kampuni inamiliki.
Kisheria inamaanisha ya kwamba wewe ni mmoja wao wanaomiliki rasilimali, samani, vifaa, nembo ya biashara na mikataba yote ya kampuni. Kama mmiliki wa kampuni una haki ya kupata sehemu yako ya mapato ya kampuni na una haki ya kupiga kura kama ilivyoanishwa kwenye hati ya umiliki wa hisa zako.
Hisa kwa kawaida huwakilishwa na hati ya hisa ambayo ndiyo inayothibitisha umiliki wako wa kampuni. Wakati unaponunua hisa unakuwa tayari mwekezaji na hivyo unakuwa mmiliki wa mali za kampuni, faida na hasara za kampuni hiyo.
Pamoja na hayo, kuwa mwanahisa katika moja ya kampuni zilizosajiliwa katika Soko la Hisa hakukufanyi wewe mwanahisa kufanya shughuli za kila siku za kampuni. Haki uliyo nayo ni kupiga kura ya kuwachagua wakurugenzi wa bodi katika mkutano mkuu wa mwaka na si vinginevyo.
Kwa mfano, ukiwa mwanahisa wa Benki ya CRDB, haimaanishi ya kwamba unayo haki ya kumpigia simu mkurugenzi mtendaji na kumwelekeza jinsi ya kuendesha benki hiyo. Pia kwa mwendo huo huo kama mwanahisa wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hauna ruksa ya kuingia kiwandani na kwenda kudai upewe kreti la bia bure!
Kinachotakiwa ni menejimenti ya kampuni kufanya kazi kwa bidii na kuiongezea thamani kampuni kwa faida ya wanahisa waliowekeza fedha zao. Kama menejimenti ikishindwa kufanya hivyo wanahisa wanauwezo wa kupiga kura na kuiondoa. Kwa muundo huu wa kununua hisa hutakiwi kufanya kazi ili upate fedha, menejimenti inatakiwa kukufanyia kazi.
Suala hili la mwisho ni la msingi na ni lazima nilifafanue, ni kwamba umuhimu wa kununua hisa ndani ya kampuni unakupatia haki ya kumiliki mali na faida inayopatikana ndani ya kampuni hiyo bila hivyo hisa zisingekuwa na maana yoyote na hati yake isingekuwa na thamani yoyote.
Jambo jingine la msingi ni ya kwamba kama mwanahisa, kama mtu binafsi huwajibiki kisheria kutokana na kampuni kushindwa kulipa madeni yake. Katika biashara zingine kama za ubia (partnerships) zinasajiliwa kwa kanuni ambazo kama zinafilisika wadai kisheria wanaweza kuwafuata wamiliki wa ubia na kuuza mali zao kama nyumba, gari, vifaa, samani na kadhalika ili kurudisha fedha zao.
Kwa hiyo kisheria, kumiliki hisa ndani ya kampuni kunamaanisha ya kwamba kitu pekee ambacho mwanahisa anaweza kupoteza kama kampuni ikifilisika ni kupoteza thamani ya hisa zako ulizowekeza ndani ya kampuni na si vinginevyo. Huwezi ukapoteza mali zako binafsi.
Moremi Marwa ni Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)
Email: moremi@dse.co.tz
11/02/2014 05:33:00 PM | Labels: SOKO LA HISA(DSE) | 0 Comments
Kuhusu Uwekezaji Tanzania
Kupitia mtandao huu utajifunza fursa mbalimbali za uwekezaji na pia kupata taarifa zinazohusu uwekezaji.
AINA ZA UWEKEZAJI TANZANIA.
Kwa bahati nzuri sana kuna aina nyingi sana za uwekezaji Tanzania. Kuna kila rasilimali na fursa mbalimbali za uwekezaji. Ugunduzi wa mafutra na gesi unaoendelea kufanyika Tanzania unaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi sana.Kuna aina mbalimbali za uwekezaji zinazoweza kufanyika Tanzania.
1. Uwekezaji wa mali.
Tanzania kuna arhi kubwa sana ambapo mtu anaweza kununua na kuendeleza kwa kujenga majengo ya kibishara na hata makazi.Pia ardhi hii inaruhusu kilimo na hivyo mtu unaweza kuwekeza kwenye kilimo cha biashara.
2. Bishara.
Kwa kuwa uchumi wa tanzania unakua kwa kasi sana mtu yeyote anayweza kuwekeza kwenye biashara anaweza kuapata faida kubwa. Biashara za bidhaa na huduma zinakua kwa kasi sana kutokana na ongezeko la watu na muingiliano wa kimataifa.3. Uwekezaji katika maliasili na gesi.
Tanzania ina gesi nyingi sana ambayo bado haijachimbwa. Hii inatoa fursa kubwa sana ya uwekezaji.4. Uwekezaji wa hisa na vipande.
Hii ni fursa nzuri ya uwekezaji kwa watu ambao wana miotaji kidogo. Soko la hisa la dar es salaa limeorodhesha makampuni mbalimbali ambayo mtu anaweza kununua hisa.Pia dhamana ya uwekezaji UTT, inatoa fursa kwa watu kununua vipande na vipande hivyo kuongezeka thamani na hivyo kunufaika zaidi.
Kuna fursa nyingi sana za uwekezaji ambazo utajifunza kupitia mtandao huu.
11/02/2014 04:58:00 PM | Labels: BIASHARA, DHAMANA YA UWEKEZAJI(UTT), FEDHA, HABARI ZA UWEKEZAJI, SOKO LA HISA(DSE), UCHUMI, UWEKEZAJI WA MALI(PROPERT) | 0 Comments
