Siri Hii Itakusaidia Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo Wa Kukosa Muda Katika Ulimwengu Huu Wa Utandawazi - 3

Leo ni siku ya mwisho ya kujiunga na SEMINA YA MAFANIKIO KUPITIA BIASHARA. Kwa maelezo zaidi bonyeza HAPA.

Habari ndugu msomaji karibu tena katika sehemu hii ya mwisho ya makala ya jinsi ya kuondokana na msongo wa mawazo wa kukosa muda katika ulimwengu huu wa utandawazi. Tumeangalia baadhi ya siri hizi wiki mbili zilizopita na kama haukusoma waweza soma hapa; Siri Hii Itakusaidia Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo Wa Kukosa Muda Katika Ulimwengu Huu Wa Utandawazi - 2

Siri nyingine ni:

4. PANGA KAZI KUTOKANA NA UMUHIMU NA UHARAKA WAKE.

Kila mara tunakuwa na kazi nyingi sana za kufanya lakini haraka na umuhimu wa kazi hizi hutofautiana. Kuna baadhi ya kazi hata usipofanya haraka hazileti athari yoyote katika kukamilisha malengo yako uliyojiwekea. Ni vizuri sana kufahamu kazi ipi unatakiwa uanze kuifanya ipi ifuate na umalizie na kazi gani. Kwa kufanya hivi unaipa akili uwezo wa kutulia na kufanya kazi kwa ufanisi. Usipofahamu kazi ipi ianze unaweza kujikuta ukifanya kazi ambazo hazina umuhimu sana na kuacha kazi ambazo zinatakiwa kufanyika kwa haraka.

5. HAKIKISHA UNAMALIZA KAZI UNAYOIANZA.

Ukianza kazi basi hakikisha unaimaliza kabisa ili uweze kuendelea na kazi nyingine. Hii inakupa hamasa ya kufanya kazi inayofuata na kuwa na uhakika kuwa utaimaliza pia. Usianze kazi na kuiacha njiani kwasababu yoyote ile isiyo ya msingi sana. Kufanya kazi nusu huleta uvivu wa kuanza kazi nyingine. Kila ukifikiri kuwa kuna kazi haukuimaliza na itakufanya uchanganyikiwe na kushindwa kuendelea na kazi nyingine.

SOMA; Kitu Hiki Kimoja Ni Muhimu Kuliko Kiwango Cha Fedha Unachotaka.

6. FANYA KAZI HUSIKA.

Jitahidi kuzuia akili yako kukusukuma kufanya shughuli ndogo ndogo na kukwepa kufanya shughuli unayohitaji kuifanya. Mfano umefungua kompyuta unataka kuandika ripoti akili yako inakushawishi uanze kupanga vizuri( folders ) faili zako badala ya kuandika ripoti. Au badala ya kusoma akili inakusukuma ukaloweke nguo kwanza ili ukimaliza kusoma ukafue. Lakini baada ya kuloweka unajikuta umeanza kufua na kuona bora umalize kufua kwanza ndipo ukasome. Ukimaliza kufua ile motisha ya kusoma huna tena na akili inakushawishi kuwa kazi zote zilikuwa muhimu. Baadaye unaona bado unakazi nyingi muhimu zinazokusubiri. Hakikisha unafanya kazi uliyopanga na si vinginevyo.

7. EPUKANA NA MARAFIKI WANAOKUPOTEZEA MUDA.

Marafiki wanamchango mkubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Ni vizuri kuwa na marafiki lakini ni lazima pia kutimiza malengo yako kama vile ulivyokusudia. Ni vizuri kuwaeleza rafiki zako juu ya ratiba yako ili usipoteze marafiki na kama kweli ni marafiki wazuri basi watakuelewa na kukuacha ufanye kazi muhimu. Kama marafiki hawa hawatakuelewa usiharibu ratiba zako ili kuwafurahisha. Kwa kuwa kama unashughuli nyingi hata ukiwa nao kila mara utakumbuka shughuli hizo badala ya kukaa nao kwa furaha. Kuwa makini sana na uepukane na marafiki wanaokupotezea muda.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kuondokana Na Hofu.

8. JIPONGEZE UNAPOMALIZA SHUGHULI ZAKO.

Kila mmoja hufurahia anapopongezwa. Ni muhimu pia kujipongeza wewe mwenyewe kila mara unapomaliza shughuli ulizojipangia. Orodhesha shughuli zako na jiandikie ni zawadi gani utajipa baada ya kumaliza shughuli hizo. Ukifanya hivyo unakuwa na hamasa ya kumaliza shughuli hizo ili ujipe zawadi yako. Zawadi yaweza kuwa kitu chochote mfano kula chakula Fulani, kusikiliza muziki, kulala kwa muda, kuangalia video Fulani au kuoga maji ya moto mazuri n.k.

Ni imani yangu kuwa siri hizi zitakusaidia kwa namna moja au nyingine kupunguza msongo wa mawazo unaotokana na kubanwa na kazi nyingi na kuona kuwa muda hautoshi. Nakutakia utekelezaji mwema na ni imani yangu kuwa shughuli zako zitaenda vizuri tangu sasa

Kama unaswali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

0 comments: