Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Ili Uwe Tajiri.
Kabla ya kitu chochote hakijaweza kuwa katika hali yake ya uhalisia huanza katika wazo. Nyumba haiwezi kujengwa kabla ya kuanza kuwa na mchoro unaongoza ujenzi wa hiyo nyumba. Katika maana nyingine rahisi unaweza kusema tunafikiri kwanza halafu tunafuata utekelezaji au kuweka katika matendo kile tunachokifikiri.
Jaribio rahisi ambalo linaweza kukufanya ujue kama mtu ataishia kuwa tajiri au tayari ni tajiri ni kwa kutazama yale mambo anayoyafanya kwa kuwa yale anayoyafanya yanaweza kutabiri matokeo yanayotarajiwa. Mambo anayoyafanya mtu huyafanya kutokana na mwongozo anaopata kutoka katika kiwanda chake cha kuzalisha mawazo.
Jaribio lenyewe ni kutazama mawazo ambayo anayatengeneza kupitia jinsi anavyoilisha akili yake. Chunguza ni mambo gani au vitabu vya aina gani au majarida ya aina gani au makala za aina gani huyo mtu anasoma. Katika hivyo vitabu au majarida mwangalie vipengele gani ambavyo anavyovisoma na pia uangalie vipengele gani katika majarida au vitabu hivyo hivyo huwa havipi mkazo kuvisoma. Katika vile vipengele anavyovisoma chunguza anavisoma katika mpangilio gani au mfuatano upi?
Jaribio hili unaweza kulifanya hata kwako binafsi kama kweli una kiu ya kubadili hali yako ya sasa kuwa tajiri au kama tayari ni tajiri basi kuufanya utajiri wako ukue zaidi. Watu ambao ni matajiri walio kaa chini kutafakari na kuamua kwa kusudia kuwa wanataka kuwa matajiri tofauti na wale ambao labda wameshinda bahati nasibu au wamerithishwa mali huchagua vitabu au majarida ambayo yanaongeza thamani katika utajiri wao, huchagua vipengele katika majarida au vitabu ambavyo kweli vinaongeza thamani katika maisha yao, havipi mkazo vipengele vile ambavyo haviongezi thamani na katika haya majarida au vitabu utagundua huwa wanasoma vipengele vinavyohusiana na fedha au biashara kwanza kabla ya kusoma vipengele vingine.
SOMA; Tabia Saba Za Watu Wasiokuwa Na Mafanikio.
Ukitaka kuwa daktari ni muhimu sana usomee udaktari, au ukitaka kuwa msanifu majengo ni muhimu sana usome kuhusu masuala ya usanifu majengo ili uwe na uwezo wa kufanya kazi yako kwa ufanisi na usiwe mbabaishaji katika eneo husika ulilolichagua. Matajiri wote ambao wamechagua kwa makusudi kuwa matajiri wamejifunza kwa njia mbalimbali kuhusu utajiri. Mmoja wa wana mafanikio maarufu duniani Jim Rohn hupenda kusema ukihitaji furaha nenda ujifunze furaha, ukihitaji uhuru wa kifedha nenda ujifunze kuhusu uhuru wa kifedha, ukihitaji afya bora nenda ujifunze kuhusu afya bora, orodha hii inaweza kuendelea zaidi lakini Jim alihitimisha kwa kusema kila kitu unachokihitaji ni kujifunza, ndiyo maana nikasema kama unataka utajiri jifunze utajiri. Kujifunza huku sio kwa kukaa darasani kwa sababu mifumo yetu ya elimu haina mitaala inayowaelekeza watu namna ya kuwa matajiri bali ina mitaala ambayo inawaandaa watu kuwa waajiriwa. Matajiri wengi waliamua kujiendeleza binafsi kwa kusoma makala, vitabu na majarida ambayo yanawapatia maarifa ambayo hayajawekwa katika mitaala ya mifumo wa elimu tulio nao.
Mafunzo makubwa ambayo wamejifunza ni namna ambavyo matajiri wengine kabla yao jinsi wanavyowaza kwa kudhibiti malighafi inayotumika katika kiwanda cha mawazo kupitia ulishaji wa akili zao kwa yale wanayoyasoma, wamejifunza namna matajiri waliotangulia wanavyofanya kazi, wanavyokula, wanavyoishi , wanavyoweka akiba, wanavyowekeza katika vitega uchumi mbalimbali. Wamejifunza kwa kujaribu kuongea na watu matajiri ili kuwapa mbinu za kufanikiwa kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuwaelekeza mambo ambayo wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuepuka kutetereka. Wamejifunza kwa kuuliza maswali sahihi, maswali sahihi ni yale maswali ambayo ukiuliza yanaenda kugusa na kubadili maeneo maisha yako moja kwa moja. Wamesoma mahojiano mbalimbali ambayo hawa matajiri waliotangulia wameyafanya, wamesoma kuhusu wasifu wa hawa matajiri waliotangulia. Hayo ndio masomo ambayo wanajifunza katika chuo cha utajiri.
SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Tabia Ya Kuahirisha Mambo.
Kama kweli umeamua kwa makusudi kabisa unahitaji kuwa tajiri ni lazima ujiendeleze kwa kuwa na uelewa pamoja na maarifa ya kujitosheleza kuhusu utajiri.
Mwandishi: Goodluck Moshi
Mawasiliano: Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi
Pia unaweza kutembelea blogu yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.
4/30/2015 07:30:00 AM
|
Labels:
FEDHA,
MBINU ZA MAFANIKIO
|
This entry was posted on 4/30/2015 07:30:00 AM
and is filed under
FEDHA
,
MBINU ZA MAFANIKIO
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
0 comments:
Post a Comment