Hivi Ndio Vitu Vinavyopelekea Ongezeko La Thamani Ya Hisa Kwa Mwekezaji.

Moja ya faida kwa mwekezaji kuwekeza katika Hisa ni pamoja na ongezeko la thamani ya hisa zake. Hisa ikiongezeka thamani kwa mwekezaji na uwekezaji wake unakua. Na ili uweze kufanya uwekezaji wenye manufaa ni vizuri ukawekeza kwenye Kampuni ambayo thamani ya Hisa inakua kwa kiwango cha chini kabisa 20% kwa mwaka. Ili thamani ya hisa iongezeke kuna vitu ambavyo huwa vinachochea kwa ukuaji wa thamani ya hisa hizo katika soko.

Vitu hivi hupelekea ongezeko la thamani ya Hisa kwa mwekezaji

Nguvu ya soko

Bei za hisa kuongezeka hutegemea ushindani kati ya wauzaji na wanunuzi wa hisa katika soko. Wanunuzi wakiwa wengi katika soko na wauzaji ni wachache hupelekea kupanda kwa bei kwa kuwa watashindana kwa bei. Ili hisa za kampuni hiyo ziwe na wanunuzi wengi hutegemea na ufanisi wa kampuni hiyo, hasa katika taarifa za fedha na utoaji wa gawio.

SOMA; Mambo 6 Yakukusaidia Kujua Shughuli Iliyokuleta Duniani.

Hali ya kiuchumi

Hali ya kiuchumi ya nchi hupelekea mwananchi kupata kipato ambacho hupelekea uwekezaji kuwa mkubwa. Mwenendo wa uchumi hupelekea ufanisi wa baadhi ya kampuni na kuchochea kuongezeka kwa bei zake katika soko kwa kuwa kampuni hiyo huwavutia wawekezaji kutokana na kufanya vizuri. Hali ya uchumi ikiwa sio nzuri hupelekea ufanisi katika soko kuwa mdogo na bei kushuka kwa baadhi ya kampuni.

Gawio

Gawio kwa mwekezaji ni kipato na faida mojawapo ya uwekezaji wake. Gawio hutolewa kutoka na faida ya Kampuni ambayo imepata na maamuzi wa wanahisa katika kikao na hutolewa mara moja au mara mbili. Kampuni ambazo hutoa gawio ambalo linaongezeka katika kiwango kizuri na kikubwa huchochea ukuaji wa bei zake. Wawekezaji wengi huvutiwa kuwekeza katika kampuni hizo na ushindani kuwa mkubwa na bei kuongezeka.

SOMA; USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kuondokana Na Changamoto Za Kuendesha Biashara Na Kuweza Kufikia Mafanikio Makubwa.

Ufanisi wa kampuni

Utendaji wa kampuni husika katika kutoa huduma au bidhaa huwavutia wateja na kampuni kufanya vizuri. Vile vile ufanisi wa kampuni katika taarifa zake za fedha kama ukuaji wa mauzo, faida, gawio na uwezo wa kampuni katika kupunguza gharama na madeni. Kampuni ikifanya vizurihupelekea bei zake kupanda kwa kuwa wawekezaji wengi huvutiwa kuwekeza katika Kampuni hiyo.

Thamani inayotegemewa/Mipango ya kampuni

Mipango mizuri na yenye tija kwa kampuni kwa kipindi kijacho huwavutia wawekezaji wengi kununua hisa za kampuni kwa kuwa wanajua katika kipindi kijacho kampuni hiyo itafanya vizuri. Mfano pale kampuni inapotangaza kufungua matawi katika sehemu nyingine au inapotangaza kuongeza bidhaa mpya sokoni. Vitu hupelekea wawekezaji wengi kuvutiwa kununua hisa za kampuni hiyo na ushindani kuwa mkubwa na bei kuongezeka.

“Wekeza Inalipa”

Mwandishi: Emmanuel Mahundi

Mawasiliano: emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510

0 comments: