Ukiwa Na Kitu Hiki Ni Mwanzo Mzuri Wa Kufanikiwa Katika Uwekezaji.

Kila mtu anatamani mafanikio. Hakuna chini ya jua mtu yeyote asiyependa kufanikiwa. Mafanikio si jambo la mara moja au jambo la kufanya leo na kuona matokeo kesho. Inahitaji kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuweza kufikia katika lengo lako. Lengo lako ni kufanikiwa na kufanya kazi kwa pekee hakuwezi kukufanya ufanikiwe bila kuwa na uhitaji kutoka moyoni mwako (commitment). Mpaka kufikia hapa najua unatamani kujua ni kitu gani hicho cha muhimu unachopaswa kukijua ili uwemwekezaji bora na mfanyabiashara bora mwenye mafanikio. Jibu la kiu yako ni taarifa (information).Utashangaa kidogo lakini ndio ukweli huo. Watu wengi waliofanikiwa wamefanikiwa kwa sababu ya kupata taarifa.

SOMA; USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kuondokana Na Changamoto Za Kuendesha Biashara Na Kuweza Kufikia Mafanikio Makubwa

Taarifa yaweza kuwa habari, fursa, nafasi ya kazi na hata elimu. Watu wamekuwa wakitafuta taarifa kwa udi na uvumba, wengi wamekuwa wakilipia kupata taarifa. Njia hizo zinazolipiwa kupata taarifa ni kama televisheni na magazeti. Taarifa imekuwa na soko kubwa katika karne hii. La kusikitisha ni kwamba watu wamekuwa wakifuatilia taarifa ambazo haziwasaidii katika kujikwamua katika maisha yao. Kufuatilia taarifa zisizokusaidia ni sawa na kujichimbia kaburi lako mwenyewe. Kwa hiyo basi ndipo sasa umuhimu wa kupata taarifa sahihi kwa wakati muafaka unapokuwa na umuhimu. Niseme tu kwamba kupitia taarifa sahihi unazopata unaweza kuamua kufanya uwekezaji unaouona unafaa zaidi. Taarifa kama hali ya hewa yaweza kukusaidia sana katika shughuli za kilimo na hata usafirishaji, utaweza kujua aina za mazao ya kulima na aina ya usafiri utakaoutumia kufikia wateja. Mfano mwingie ni uhitaji wa bidhaa mahali Fulani, ukipata taarifa hizo na wewe ni mzalishaji au msambazaji au mtu uliyeona fursa hiyo baada ya kupata taarifa sahihi unaweza kuchangamkia fursa hiyo na hivyo kuweza kufanikiwa. Taarifa sahihi inaweza kukuonyesha mapungufu yaliopo katika biashara Fulani au mahali Fulani na hivyo kuweza kuwekeza. Hivyo basi napenda kusisitiza taarifa sahihi kwani taarifa zisizo sahihi zaweza kukupelekea katika kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Ili uweze kufanikiwa anza kutafuta taarifa sahihi kwa mafanikio yako. Acha kabisa kufuatilia taarifa ambazo zimekuwa zikikupotezea muda wako mfano taarifa za udaku na zinazofanana na hizo.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyojitengenezea Dharura.

Sehemu za kupata taarifa sahihi

Dunia ya sasa ni kama kijiji. Mawasiliano yamekuwa rahisi kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya mwanadamu. Kuamua kupata ama kutopata taarifa ni juu yako mwenyewe kwani kuna njia nyingi sana za kuzipata.

INTERNET

Nianze na njia ambayo ni maarufu sana ya INTERNET. Naamini wewe unayesoma Makala hii umeweza kuipata kupitia internet. Tumia internet vizuri kupata taarifa sahihi. Katika internet kuna taarifa nyingi sana za uongo na za kweli. Tumia akili yako na maarifa kuweza kuchambua taarifa sahihi.

VYOMBO VYA HABARI

Vyombo vya habari kama redio, televisheni na magazeti na hatabloguzinaweza kutangaza taarifa ambayo kwako ni fursa tosha. Tafuta taarifa sahihi hasa za kibiashara zinazotangazwa na vyombo hivi. Wakati mwingine majanga yanayotekea sehemu Fulani yaweza kuwa fursa yako ya kuweza kufanya biashara au kuwekeza. Mathalani sehemu yenye upungufu wa maji, unaweza kuwekeza kwa kuuza maji au kuchimba visima na kuwauzia wananchi.

WATU/MARAFIKI

Taarifa zimekuwa zikitoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Taarifa hizi zaweza kuwa sahihi au zisiwe sahihi hivyo kabla hujazitumia jitahidi kuzithibitisha. Ishi na watu vizuri na marafiki pia kwani bila watu na hasa marafiki ni vigumu kufanikiwa. Sahau kuhusu jeshi la mtu mmoja. Hakuna jeshi la namna hiyo duniani kote. Tumia taarifa unazopata kwa usahihi na naamini siku moja utakuwa umefanikiwa.

SOMA; Saikolojia Ya Kuuza, Uza Bei Ghali Kabla Ya Rahisi.

Kabla sijahitimisha nipende kurudia kuwa huhitaji taarifa peke yake bali unahitaji kupata taarifa sahihi. Kumbuka ‘Informationispower’ (taarifa ni nguvu) na mwenye taarifa sahihi ndiye aliyebeba mafanikio mikononi mwake.

Tukutane katika Makala nyingine muda mwingine.

Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes ambae ni mjasirimali na mhamasishaji.

Unaweza kuwasiliana na naye kwa: simu: 0712 843030/0753 843030

e-mail:nmyohanes@gmail.com

Pia unaweza kutembelea blogu yake: www.lifeadventurestz.blogspot.comkujifunza zaidi.

0 comments: