Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu; GO IT ALONE

Habari rafiki, ni matumaini yangu unaendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu. Leo tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa GO IT ALONE, Do what you do best let other do the rest. Kitabu kimeandikwa na Bruce Judson

1. Mawazo mazuri ya biashara yapo kila mahali. Unachotakiwa tu ni kufumbua macho. Ukiwa na jicho la fursa nakuhakikishia utaziona nyingi mpaka unawezashindwa kujua uanze na ipi. Tatizo ni kwamba tumekua watu wakulalamika mno, ikilalamika unafanya akili yako kushindwa kugundua fursa. Matatizo au changamoto zinazowakabili watu ndio fursa kwako, jikite kwenye kutafutasuluhisho la changamoto hizo, lazima watu watanunua suluhisho za changamoto zinazowakabili. Goodideasareeverywhere.

2. Katika biashara usijikite kutengeneza faida mwanzoni, bali jikite katika kutengeneza thamani ya biashara yako zaidi. Na pia Katika hatua za mwanzo usiitegemee biashara yako kama chanzo cha kipato. Faida inayopatikana itumike kwenye kuongeza thamani ya biashara na kuitanua zaidi.

3. Mjasiriamali unapaswa kua na mtazamo wa kufanya majaribio mara zote (experimentalattitude). Fanya majaribio tena na tena, fanya tena na tena mpaka umepata njia mpya. Hakuna jibu la kweli kwa wakati wote. Unaweza kugundua ukweli wa leo..lakini kesho ukawa haufanyi kazi au ukawa ni uongo. Bill gate wakati anaanza kutengeneza kompyuta miaka ila ya 70, watu walimwambia dunia nzima itahitaji kompyuta 5 tu, maana yake kutakua ni hakuna soko la hizo kompyuta anazotengeneza, pengine huo ndio ukweli wa kipindi kile. Lakini je ukweli wa leo ukoje, dunia inahitaji kompyuta kuliko ilivyofikiriwa mwanzoni. Kompyuta zimerahisisha mambo mengi sana. Laiti Bill Gate angesikiliza ushauri wao., leo tungekua nyuma sana. Alichofanya Bill Gate ni kuendelea kujaribu na kujaribu ili kupata ukweli mpya ambao ulikuja kubatilisha ukweli wa zamani.

4. Jiweke katika nafasi ya kutatua tatizo na si kulaumu. Sio kila wakati wewe ni mtu wa kunung’unika tu, hiyo hata Mungu hapendi. Kumbuka hata Mungu alitaka kulifutilia mbali taifa la Israel wakati walikua wakilalama. Ukilalamika ni ishara ya kukosa imani. Tumeumbwa na uwezo mkubwa sana, wa kutatua matatizo, sasa tunamuudhi hata aliyetuumba maana uwezo huo ameshatupa, ila tunakaa tu na kulalamika wengine waje watutoe tulipo au tunarudi kila saa kwake na kumuuliza tufanyeje wakati kila kitu tunacho. Dunia ina watu watatuzi wa matatizo wachache sana na ndio waliofanikiwa. Jitahidi uwe mtatuzi wa tatizo na si mkosoaji na mlalamikaji. Kumbuka wajasiriamaliwengi wanapata mawazo ya kibiashara wakati wanapojaribu kutatua matatizo yanayowakabili katika maisha.

SOMA; USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kuondokana Na Changamoto Za Kuendesha Biashara Na Kuweza Kufikia Mafanikio Makubwa

5. Unapofanya mabadiliko ya biashara yako usiende mbali saana na wateja wako, usifanye mabadiliko makubwa sana ambayo yatafanya mteja kuingia gharama, au usumbufu. Mabadiliko yaendehatua kwa hatua. Hebu fikiri teknolojia ya simu, ingetoka kwenye kutumia simu za mezani na kwenda moja kwa moja kwenye Smartphones. Maana kwanza wakati huo hata simu za mkononi zilikua haizifahamiki na waliokua nazo walikua wachache sana. Hata kuongeza bei, ukifanya hivyo ghafla na kukawa na tofauti kubwa ni kwamba utapoteza wateja. Mabadiliko yeyote yatakayomgharimu mteja kwa ghafla hata kama yana nia njema, utapoteza wateja wako. Fikiria mabadiliko makubwa sana, ni sawa kabisa, lakini katika utekelezaji nenda hatua kwa hatua, ili wateja nao waweze kwenda na wewe vizuri.

6. Usiishie kufanya biashara na wateja unaowafahamu pekee. Ukiona unafanya biashara mwaka 1 na wateja wako ni wale unaowafahamu pekee basi ujue upo hatarini sana. Biashara inayokua ni ile inayoweza kuleta wateja wapya mara kwa mara, na wale waliopo wanarudiarudia kufanya biashara na wewe. Ongeza wigo wa wateja.

7. Huwezi kufanya kila kitu wewe. Kama biashara yako inakutegemea wewe kila kitu, hapo huna biashara. Ujasiriamali wa ukweli, ni kuweza kutumia uwezo wa watu wengine (leverage). Ukijishughulisha na kila kitu kwenye biashara yako ukadhani kwamba unaokoa fedha za kuwaajiri watu, ujue ndiounaelekea kubaya sana. Maana kila kitu kikikutegemea wewe, utakosa muda wa kufikiri, kuibua mawazo mapya. Maana ubunifu na mawazo mazuri yanaihitaji uwe na muda mzuri wa kufikiri, sasa kama kila siku huna muda, utaishia kua wakawaida tu. Cha kufanya tafuta watu wenye uwezo kukuzidi wewe wape zile nafasi zinazohitaji utaalamu, na wewe tafuta kitu kimoja ambacho unadhani unaweza kukifanya vizuri kuliko wengine, hapo weka nguvu zako zote, achia wengine wafanye. Napenda kutoa rai kwa wale hasa wenye mpango wa kuanzisha biashara, kua na fikra za kutafuta watu wa kuchukua nafasi zao wakati ili kupata muda wa kufanya mambo mengine kabisa nje ya kampuni. Mfano kama wewe ni MD, au CEO, fikiria nani atakuja kuchukua nafasi hiyo pale biashara itakapokua na uwezo wa kujiendesha, anza kumwandaa mapema. Hii itakupa kua na muda mzuri wa kufikiri mambo mengine mazuri ya kuendeleza biashara.

8. Hakuna kitu cha bahati. Hapa ndio nilipataga shida sana katika kuamini kwamba eti bahati inatengenezwa. Lakini hatimaye nilielewa falsafa yenyewe. Na sasa ni muumini wa kwamba bahati hutengenezwa. Kwa ufupi ni kwamba bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa. Unapokutana na fursa unakua umejiandaa vya kutosha. Hii ina maana bahati zipo nyingi sana sema tunashindwa kuzipata maana hatuna maandalizi, tunaishia kusema.. “Haikuwa bahati yangu”. Ukikaa tu halafu usubiri bahati utaishia kusema mimi sina bahati. Sasa ngoja nikupe siri moja ya bahati, Ili upate bahati nyingi ongeza maandalizi, ongeza kujifunza vitu vipya usiishie kwenye vile unavyojua tu. Kumbuka fura hutoa upendeleo kwa wale waliojiandaa

9. Katika biashara kuna uchaguzi, aidha uwe mbunifu au ufunge biashara ukafanye kitu kingine. Maana tunaishi katika dunia yenye ushindani mkubwa wa kibiashara. Na Kinachotenganisha biashara moja kuonekana iko juu na nyingine iko mahututi (ICU) ni ubunifu. Unakuta ni biashara 2 au 3 hata 10 zinauzwa bidhaa au huduma sawa. Ila katika hizo kuna moja au mbili ndio zina wateja wengi, cha kufahamu ni kwamba kinachowafanya wawe vile ni ubunifu katika kutoa bidhaa au huduma bora. Na ubunifu huu unafanyika mara kwa mara.

10. Kufanikiwa kwenye biashara ni kutengeneza bidhaa au huduma ambayo wateja watarudi tena na tena. Mfano huduma ya kupiga simu. Mteja ili aweze kuwasiliana itabidi anunue vocha, kila akitaka kuwasiliana atahitaji kununua vocha. Hebu fikiri kama mitandao ya mawasiliano, ingekua inatoa huduma ya kununua vocha mara moja tu basi, ukishanunua ndio unawasiliana milele. Ukweli ni kwamba wangeshafunga ofisi zao kitambo. Kitu kidogo lakini chenye kujirudia rudia kina faida kuliko kikubwa ambacho ni cha mara moja tu. Na hapa ndipo unaweza kushangaa kwanini anayeuza unga, pipi, biskuti anapesa kuliko anayeuza samani za ndani (furnitures). Hapo ndio utaona kwanini Bwana CarlosSlimHelu tajiri namba 2 wa dunia anajihusisha na teknolojia ya mawasiliano ana pesa kuliko anayetengeneza magari ya BMW. Ndio maana hata kwenye biashara za mtandao zinazofanikiwa ni zile zenye bidhaa ambazo hutatumia maramoja tu, bali utahitaji tena na tena.

SOMA; Huyu Ndiye Mtu Ambaye Umasikini Huwezi Kumbugudhi.

11. Wapo wajasiriamali wengi wanaanzisha biashara zao kwenye muda wao wa ziada kabla ya kuacha kazi. Ukijaribu kuangalia wengi wa wajasiriamali kabla ya kua wajasiriamali walikua waajiriwa, waliweza kutumia muda wao wa ziada kuanzisha biashara zao. Hii inawasaidia kutokupata shida sana pale mwanzoni kama ana watu wanamtegemea. Wote tunajua kwamba biashara katika hatua ya mwanzo haitengenezi faida hata kama inatengeneza faida hiyo inatakiwa kutumika kwa ajili ya kuongeza biashara. Kama unafanya kazi ukaacha na hujaanza biashara yako ina maana utaitegemea sana hiyo biashara, wakati mwingine utalazimisha kupata faida pale mwanzoni ili uweze kujikimu, sasa hapo ndipo utajikuta unaharibu biashara. Maana mwanzoni mwa biashara watu hawajikiti kutengeneza faida, bali kutengeneza thamani ya biashara yao kwa wateja. Sasa haimaanishi kwamba hawapo wanaofanikiwa wanaoanzisha biashara kwa kuacha kazi kabla, wapo. Pia usipokua na hekima pointi hii inaweza kukufunga wewe mwajiriwa, ukawa unajifariji, kwamba utaanza kesho, utaanza kesho, kesho yenyewe unajishtukia miaka 15 ndani ya ajira. Ngoja ni kwambie kitu hichi ni ushauri wangu binafsi; ukiona mwajiri amekuongeza mshahara hapo sasa ndipo unatakiwa kuongeza spidi ya kuanza mikakati ya kuondoka, maana hapo ni amekufunga kamba mguu wa pili ili uzidi kutumika vizuri katika hali ya kujiona unapendwa zaidi. Ukiona kwenye ajira uko comfortable.. watchoutplease…

12. Imani sio lile wazo unalimiliki, bali ni wazo linakumiliki wewe. Na ndio maana inakua ngumu sana kuwatoa watu kwenye imani fulani, maana sio wao wanamiliki zile imani bali wanamilikiwa na zile imani. Mtu anatetea sana imani fulani, kwa vile yeye ni milki ya hiyo imani lazima amtumikie bosi wake vizuri. Kama una imani kwenye mambo ambayo sio sahihi ni hatari kubwa sana.

13. Hua tunajiaminisha kwamba mjasiriamali lazima awe na wazo zuri sana la kibiashara, mwishowe tunajikuta tunaona mawazo ya biashara yameisha. Wazo halihitaji kua zuri kivilee, hata lile unalolizarau laweza kua ni ukombozi wako.

14. Janga kubwa katika maisha sio kwamba hatuna nguvu za kutosha, ni kwamba tunashindwa kutumia nguvu tulizonazo. Sio kwamba huna mtaji wa kutosha, la hasha, ni kwamba umeshindwa kutumia mtaji uliona nao. Maana kwanza una imani kwamba mtaji ni fedha tu. Hujui kwamba mtaji namba moja ni muda ulionao, unaoutumia vibaya kwa kulalamikia serikali, halafu huwezi tatua chochote unabaki palepale, unasahau hata ujuzi ulionao ni mtaji mkubwa pia. Chochote unachokifahamu ambacho kinaweza kuwasaidiawengine ni mtaji tosha.

15. Wajasiriamali wengi wanashindwa kwasababu wana mielekeo mingi (toomanydirections) kwa wakati mmoja na mwishowe hawawezi kutekeleza vizuri chochote. Badala ya kulenga katika kufanya vizuri kuhudumia masoko yao makubwa, wanawagawanya watu/wateja wao na muda wao, kwa kujaribu kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyokaribisha Ushindani Kwenye Biashara Yako.

16. Siku za leo gharama na muda wa kuanzisha biashara na kuwa bosi wako mwenyewe zimepungua sana. Mtu anaweza kuanzisha biashara ikasimama ndani ya muda mfupi kuliko ilivyokua huko zamani. Leo hii kuna vitu vingi sana vya kutusaidia kufikisha huduma zetu kwenda kwa wateja kwa haraka. Moja wapo ni mawasiliano. Unaweza kutangaza biashara yako kwa bei nafuu zaidi na ikawafikia watu wengi ulimwenguni kuliko ilivyokuwa awali.

17. Intaneti ni nyenzo kubwa sana, yaani kubwa sana katika biashara. Leo hii dunia ingekua wapi kama intaneti isingekuwepo. Hata usingeweza kusoma haya mambo bila kuwepo intaneti. Hata hziwhataspp, facebook, twitter zote zinategemea intaneti. Leo hii unaweza kufanya biashara ukiwa nyumbani kwako, yaani nyumbani ndio ikawa ofisi yako na ukafanya biashara na dunia, hii ni kwasababu ya intaneti. Unaweza agiza gari toka pande yeyote ya dunia na ikakufikia hapo ulipo. Sasa tambua kwamba hii ni fursa kubwa sana. Sasa hii inatupa funzo kwamba intaneti ni utajiri tunaocheza nao pasipokujua, yaani unacheza na dhahabu halafu unalia umasikini. Mmiliki wa facebook ni tajiri kuliko hata mmiliki yeyote wa Mgodi wa Dhahabu au madini yeyote.

18. Chanzo kikuu kwa watu wengi kuhangaika sana kitaaluma au kimaisha binafsi, ni kukosa lengo (lackoffocus) hujui kwa kujikita ni wapi, unasubiria maisha yakuchagulie. Kuna nguvu kubwa sana kama utakua na focus

19. Pamoja namipango mizuri unayoweza kua nayo kama hamna vitendio, huna tofauti na Yule asiye na mipango kabisa. Watu hawatishwi na mipango, kila mtu anaweza sema mipango yake, lakini je vitendo vinavyoendana na hiyo mipango. Je hayo uliyapanga umeshaanza kuyatenda? Matendo ndio uhai wachemchemu ya kufanikiwa kwako. Hakuna Biashara inayokua imekamilika ikiwa kwenye makaratasi tu. Ondoka kwenye makaratasi anza utendaji. Kua mtu wa vitendo zaidi

20. Hofu ni adui mkubwa sana. Hofu imezika mawazo mengi sana. Hofu ndiyo sababu kubwa ya umaskini wa watu wengi. Watu wengi wameshindwa kuanzisha biashara kwa sababu kubwa ya kuhofia kushindwa na kuchekwa na watu. Ni bora ukashindwa na kuchekwa sasa hivi ukiwa kijana na nguvu zako, kuliko kuja kulazimika kujaribu ukiwa uzeeni, hata ukishindwa huna nguvu tena ya kujaribu. Hujaona mtu anastaafu ndio anaanza biashara, ya hardware ya vifaa vya pikipiki, au anaanza kufuga kuku wa mayai, hujawahi kujaribu, halafu unakuja kuweka pesayako ya mafao uliyokusanya miaka yote ya kutumikia watu. Sasa ukishindwa utaweza kurudi tena ukatumike ulikukusanya tena mafao kwa ajili ya mtaji?. Usikubali hofu ukufanye uje kupata fedheha uzeeni. Jaribu sasa. Wakati uliokubalika ni sasa

Asanteni

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepedaudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Makala imeangaliwa ufasaha wa lugha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.Tovuti http://rumishaelnjau.wix.com/editor

0 comments: