Msingi na ustadi wa kuwekeza kwenye Soko la Hisa
JE ukiwa kama mwananchi wa kawaida usingependelea kuwa mmiliki wa kampuni bila ya kuwa na ulazima wa kufika kazini na kufanya kazi za kila siku?
Hebu tafakari kwa kina, upo nyumbani kwako umepumzika au ukifanya shughuli zako nyingine na ukiiangalia kampuni yako inakua kwa ufanisi na tija na baada ya muda unachukua hundi yako ya gawio huku mtaji wako ukiendelea kukua kila kukicha.
Jambo hili linaweza kuonekana kama ni njozi au ndoto, lakini ukweli ni kwamba lina ukweli usiopingika na jawabu lake ni kuwa na hisa hususani katika kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Kwa hiyo ili kutimiza ndoto yako ya kukidhi mahitaji yako ya fedha na kuanza safari yako ya kumiliki kampuni kupitia Soko la Hisa unatakiwa kuwa na uelewa mzuri wa jinsi gani hisa zinavyouzwa na kununuliwa katika soko la hisa.
Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita, wananchi wengi wa kawaida nchini Tanzania wamekuwa na shauku ya kununua hisa kwenye kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam na kulifanya soko hilo kukua kwa haraka. Hivi sasa hisa zinaonekana ya kwamba ndiyo chombo kinachoweza kuwapatia wananchi ukuaji wa uchumi binafsi kutokana na kumiliki kampuni zilizo katika sekta muhimu katika uchumi wa nchi yetu.
Pamoja na kuwa hisa zimeanza kupata umaarufu mkubwa, lakini watu wengi bado hawajaweza kuwa na uelewa mkubwa kuhusiana na hisa na jinsi ya kuweza kununua na kuuza hisa hizo.
Nadhani mara nyingi mmeweza kusikia baadhi ya watu wakisema maneno yafuatayo:
"Umesikia, mjomba wake Marwa ametengeneza pesa nyingi sana katika hisa za NMB; na kwa sasa atapata bahashishi nyingine..." au vile utasikia "Chukua tahadhari kubwa kwenye hisa zako, kwa sababu unaweza ukapoteza hisa zako ndani ya siku chache!"
Maneno yote haya ni upotoshaji mkubwa kwa sababu yanasababishwa na mawazo potofu ya kupata utajiri wa haraka haraka. Mara nyingi baadhi ya watu wanafikiri ya kwamba ununuaji wa hisa ni njia ya mkato ya kupata utajiri na hakuna hatari ya kupata hasara.
Msukosuko wa masuala ya fedha duniani uliotokea hivi karibuni umeweza kuthibitisha ya kwamba soko la hisa pia linaweza kuyumba.
Ukweli ni kwamba hisa zinaweza kuleta utajiri mkubwa lakini si kwamba hakuna hatari ya kupata hasara. Jambo la msingi la kujilinda ili kutokupata hasara na ni vyema kabla hujanunua hisa, ni vyema ukajua unawekeza pesa zako kwenye hisa za kampuni ipi. Na ndiyo maana kutokana na suala hilo, Soko la Hisa la Dar es Salaam limeanzisha programu inayomsaidia mwanahisa kuweza kufanya maamuzi yake binafsi kujua anafanya uwekezaji katika kampuni ipi bila ya kuwa na shinikizo.
Je, hisa ni kitu gani? Hisa ni nini?
Elimu ya msingi ambayo unatakiwa kuwa nayo kabla ya kufanya uwekezaji katika soko la hisa nikujua hisa ni kitu gani, aina tofauti za hisa na soko la hisa lenyewe linafanyaje kazi.
Kwa hiyo ni vyema tukaanza kwa kujua hisa ni kitu gani.
Kwa kutumia lugha nyepesi ukinunua hisa unathibitisha umilikaji wa kampuni. Hisa zinathibitisha kumiliki mali za kampuni na mapato yake. Jinsi unavyonunua na kuwekeza hisa katika kampuni ndivyo jinsi umiliki wako katika kampuni hiyo unavyoongezeka thamani.
Kwa hiyo, hakuna utofauti wowote kati ya hisa na mtaji; vyote ni sawa na vinawakilisha umiliki wa kampuni.
Aidha, kwa kununua hisa, fedha ambayo ingekuwa imekaa tu bila kufanyiwa kazi au ipo katika akaunti ya akiba na kupata riba ndogo, inaingia katika mzunguko wa fedha ambao unakuwa na tija katika uchumi.
Kuwa mmiliki wa kampuni na faida zake
Kumiliki hisa za kampuni inamaanisha ya kwamba wewe unakuwa miongoni mwa wanahisa wengi ambao wana haki ya kumiliki kila kitu ambacho kampuni inamiliki.
Kisheria inamaanisha ya kwamba wewe ni mmoja wao wanaomiliki rasilimali, samani, vifaa, nembo ya biashara na mikataba yote ya kampuni. Kama mmiliki wa kampuni una haki ya kupata sehemu yako ya mapato ya kampuni na una haki ya kupiga kura kama ilivyoanishwa kwenye hati ya umiliki wa hisa zako.
Hisa kwa kawaida huwakilishwa na hati ya hisa ambayo ndiyo inayothibitisha umiliki wako wa kampuni. Wakati unaponunua hisa unakuwa tayari mwekezaji na hivyo unakuwa mmiliki wa mali za kampuni, faida na hasara za kampuni hiyo.
Pamoja na hayo, kuwa mwanahisa katika moja ya kampuni zilizosajiliwa katika Soko la Hisa hakukufanyi wewe mwanahisa kufanya shughuli za kila siku za kampuni. Haki uliyo nayo ni kupiga kura ya kuwachagua wakurugenzi wa bodi katika mkutano mkuu wa mwaka na si vinginevyo.
Kwa mfano, ukiwa mwanahisa wa Benki ya CRDB, haimaanishi ya kwamba unayo haki ya kumpigia simu mkurugenzi mtendaji na kumwelekeza jinsi ya kuendesha benki hiyo. Pia kwa mwendo huo huo kama mwanahisa wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hauna ruksa ya kuingia kiwandani na kwenda kudai upewe kreti la bia bure!
Kinachotakiwa ni menejimenti ya kampuni kufanya kazi kwa bidii na kuiongezea thamani kampuni kwa faida ya wanahisa waliowekeza fedha zao. Kama menejimenti ikishindwa kufanya hivyo wanahisa wanauwezo wa kupiga kura na kuiondoa. Kwa muundo huu wa kununua hisa hutakiwi kufanya kazi ili upate fedha, menejimenti inatakiwa kukufanyia kazi.
Suala hili la mwisho ni la msingi na ni lazima nilifafanue, ni kwamba umuhimu wa kununua hisa ndani ya kampuni unakupatia haki ya kumiliki mali na faida inayopatikana ndani ya kampuni hiyo bila hivyo hisa zisingekuwa na maana yoyote na hati yake isingekuwa na thamani yoyote.
Jambo jingine la msingi ni ya kwamba kama mwanahisa, kama mtu binafsi huwajibiki kisheria kutokana na kampuni kushindwa kulipa madeni yake. Katika biashara zingine kama za ubia (partnerships) zinasajiliwa kwa kanuni ambazo kama zinafilisika wadai kisheria wanaweza kuwafuata wamiliki wa ubia na kuuza mali zao kama nyumba, gari, vifaa, samani na kadhalika ili kurudisha fedha zao.
Kwa hiyo kisheria, kumiliki hisa ndani ya kampuni kunamaanisha ya kwamba kitu pekee ambacho mwanahisa anaweza kupoteza kama kampuni ikifilisika ni kupoteza thamani ya hisa zako ulizowekeza ndani ya kampuni na si vinginevyo. Huwezi ukapoteza mali zako binafsi.
Moremi Marwa ni Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)
Email: moremi@dse.co.tz
11/02/2014 05:33:00 PM
|
Labels:
SOKO LA HISA(DSE)
|
This entry was posted on 11/02/2014 05:33:00 PM
and is filed under
SOKO LA HISA(DSE)
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
0 comments:
Post a Comment