Showing posts with label UCHAMBUZI WA VITABU. Show all posts
Showing posts with label UCHAMBUZI WA VITABU. Show all posts

Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinachoitwa FLIGHT PLAN The Real Secret Of Success.

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu. Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa FLIGHT PLAN The real secret of success. Kitabu kimeandikwa na mwandishi mashuhuri wa vitabu Brian Tracy. Kitabu kinaitwa Flight Plan au kwa Kiswahili Mpango wa ndege au mpango wa kusafiri kwa ndege. Mwandishi anayafananisha maisha na safari, safari ambayo unaweza kutumia usafiri wowote unaotaka, aidha, gari, pikipiki, kwa miguu au ndege. Mwandishi ameandika kitabu hiki ili kumwezesha msafiri achague njia ya kusafiri kwa ndege ili kufika mapema kwenye kusudio lake. Anaelezea kwamba safari ya ndege ndiyo yenye uhakika wa kufika haraka kuliko njia nyingine. Lakini pia anatoa hatua muhimu za kufanya ili uweze kusafiri kwa ndege. Moja wapo ni kujua unakwenda wapi halafu ndiyo uanze kuchagua aina ya ndege uitakayo. Kitabu hiki ni kizuri na cha kipekee pia.
Karibu tujifunze zaidi.
1. Fanya kazi muda wote wa kazi.
Kuanza kazi na kuimaliza ni changamoto kwa watu wengi. Unakuta unafanya kazi fulani, mara umeacha, umeshika kitu kingine, mara umepokea simu, mara umeanza kuchati, halafu ndio unairudia tena ile kazi. Unagusagusa tena hapo, mara unachepuka kwenye mambo mengine, au unaanza kupiga soga za mambo yasiyo ya maana, au una anza kupiga stori mara za michezo mara stori za siasa, halafu siku inaisha. Kama kweli unataka mpango wako uwe kama wa safari ya ndege ni lazima ufanye kazi uimalize ndio ufanye vitu vingine, weka nguvu zako zote kwenye shughuli hiyo. Mfano ndege ikishapaa, hua haina vituo huko angani, ikianza safari ni mpaka imefika kwenye lengo, na rubani wa ndege anakua makini muda wote kufanya marekebisho pale yanapohitajika. Na ndio maana kama ndege umeambiwa itatumia dk 45 toka Uwanja wa KIA kwenda Dar, itatumia dakika hizohizo. Lakini hebu panda daladala uone, au Coaster, unaweza kuchelewa zaidi ya hata saa moja kwa safari za karibu, safari za mbali unaweza kuchelewa hata masaa 3 zaidi ya yale yaliyokua yamepangwa. Jifunze kufanya mpango wako uwe mpango wa ndege ambayo haisimami mpaka imefika kwenye lengo. Work all the time you work.
2. Chagua mustakabali wako (choose your destination). Siri ya hakika ya mafanikio, ni kwamba maisha ni kama safari ndefu ya ndege, lazima kwanza uanze kuchagua unakotaka kufika, halafu uchague ndege na kukata tiketi halafu ndipo uondoke kuelekea kwenye lengo lako. Hauanzi na kuchagua ndege wakati hujui unakwenda wapi. Aina ya ndege utakayopanda itategemea na unakotaka kwenda. Hivyohivyo mpango unategemea lengo. Unapokua na uhakika wewe ni nani, ni nini unataka, na wapi unataka kwenda utakua na mafanikio mara 10 ya mtu wa kawaida ambaye anaamini maisha ndiyo yanaamua yeye apate nini.
3. Fikiri kwa mrengo wa kutoa suluhisho na si kuendeleza tatizo. Watu hodari ni watu wenye kutoa suluhisho zaidi. Wanafikiria suluhisho ni nini, na nini kifanyike, na sio kufikiri tatizo na nani wa kulaumu. Watu hodari Ni watu wenye mtazamo wa mbele zaidi, wakifikiria zaidi ni hatua gani zichukuliwe haraka ili kudhibiti uharibifu au madhara yanayoweza kusababishwa na tatizo lililotokea. Kua hodari leo kwa kuanza kua na mtazamo wa suluhisho kuliko kutafuta nani mchawi anayepaswa kubeba lawama au kuadhibiwa.
4. Chukua hatua ya Kwanza.
Tofauti ya msingi kati ya ukuu (greatness) na ukawaida (mediocrity) ni katika kuchukua hatua ya kwanza. Watu wakuu (great people) wao wanaweka malengo makubwa, wanapangilia hatua zinazotakiwa kufikia kwenye lengo halafu wanachukua hatua ya kwanza. Wanaanza na hatua ya kwanza. Upande mwingine kwa watu wa kawaida, wanakua na matumaini, ndoto, matarajio, na shauku kadhaa, pengine kama vile watu wakuu/waliofanikiwa wanavyokua. Ila sasa Hofu ya kushindwa na kupoteza/hasara inawazidi nguvu wakati wanapotakiwa kufanya maamuzi ili kuchukua hatua ya kwanza, mwishowe wanarudi nyuma.
5. Kama ukifanya vile ambavyo waliofanikiwa wanafanya, ukafanya tena na tena mpaka ikawa tabia yako basi hakuna kitakachoweza kukuzuia wewe kupata matokeo wanayoyapata.
6. Kupata zaidi, lazima uwe zaidi (To have more, you must first be more). Kwa maneno mengine ukitaka kutengeneza maisha tofauti ni lazima uwe mtu wa tofauti kwanza. Lazima ujifunze na kukua na kupata uzoefu muhimu ambao utakupa hekima na ufahamu wa kuishi maisha ya viwango vya juu. Hakuna njia ya mkato
7. Kila mtu anaanzia chini. Kila unayemuona ambaye yuko juu katika tasnia (field) yako kuna wakati walianzia chini kabisa au hata hawakuwepo kabisa kwenye hiyo tasnia. Lakini Leo hii wamefika hapo juu na wanaingiza kipato kikubwa ambacho ni mara kadhaa ya kipato cha mtu wa kawaida. Habari njema ni kwamba vyote ambavyo wengine wamefanya wakafanikiwa hata wewe unaweza kufanya kama tu utaamua kujifunza ni jinsi gani vinafanyika. Hakuna aliye bora kukuzidi na hakuna aliye nadhifu kuliko wewe, walichokuzidi nacho ni kwamba wao walianza mapema kufanya hivyo vilivyowafanya kufikia hapo. Pengine ungeanza na wao ungekua mbali zaidi. There are no limits except those that you impose on yourself with your own thinking.
8. Katika nyanja yeyote uliyochagua itakuchukua miaka 7 kufikia nafasi ya juu. Watu wengi hawapendi kuusikia huu ukweli, lakini huo ndio ukweli, kwamba eneo lolote, liwe biashara, kazi au ufundi, itakuchukua miaka saba ili uweze kufuzu na kubobea katika viwango vya juu kabisa. Itakuchukua miaka saba biashara yako kufikia mafanikio ya juu. Wengi tukisikia hivi tunakata tamaa na kuacha kujiboresha, tukisahau kwamba hata tukiacha muda ndio unakwenda, hata usipofanya chochote hiyo miaka 7 itapita tu, sasa si bora ukafanya kitu ili baadaye ufaidi matunda ya kuutumia muda vizuri. Maana hata usipoutumia muda utakwenda tu.
9. Moja ya tamaa zenye nguvu kwa binadamu ni kutaka kupata kitu bure, au kwa gharama ndogo sana. Hili ni janga kubwa sana, ndio maana watu wengi wanafikiria njia za kufanikiwa haraka haraka na kwa njia rahisi. Na ndio maana unaona wimbi la vijana kwenye michezo kama kamari na mingineyo mwishowe wanaishia mikono mitupu huku hali zao za mwisho zikiwa mbaya kuliko awali. Ukitaka kumshawishi mtu siku za leo mmpe matumaini ya kufanikiwa haraka haraka bila kuvuja jasho. Hata dini nyingi zenye wafuasi wengi siku za leo ni zile zinazowashawishi watu kua watapata mafanikio ya haraka. Hakuna cha bure. No free lunch
SOMA; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.
10. Jiandae kulipa gharama.
Hakuna kirahisi wakati wa kuanza jambo. Kila ufanikishaji mkubwa ni matokeo ya mamia na maelfu ya juhudi ndogo ndogo ambazo hakuna mtu anayeziona au kuzitambua. Kila tajiri unayemuona ni matokeo ya juhudi, ufanyaji kazi kwa bidii na uzoefu wa muda mrefu. Wakati mwingine hata likizo au mapumziko kwao ilikua ni ngumu, kwa maneno mengine walikubali kulipa gharama. Tatizo kubwa linalokumba watu wengi ni kutokutaka kutia bidii ya vitu ambavyo watu wengine hawavioni. Watu wanataka kila wanachofanya waonekane na wapongezwe. Waliofanikiwa ni wale wanaojitoa sadaka (sacrifice) kwenye mambo ambayo ni nadra sana kukuta wakipongezwa maana mambo hayo wengi hawayaelewi.
11. Maboresho yote ya utu wa nje yanaanzia ndani. Ukitaka kua bora nje lazima uanze kujiboresha ndani, maana ulimwengu wako wa nje ni matokeo ya ulimwengu wako wa ndani. Anza kuboresha jinsi unavyowaza, badili imani ulizonazo ambazo si sahihi, badilisha mtazamo wako, badili jinsi unavyofanya maamuzi n.k. Ukiweza kubadilisha ulimwengu wako wa ndani ulimwengu wa nje na huo utabadilika ili kuakisi mabadiliko yaliyotokea ndani.
12. Ubora wa maisha yako ya baadaye utaamuliwa na uchaguzi na maamuzi unayofanya leo, hususani uchaguzi na maamuzi unayofanya katika yale maeneo ambayo ni ya muhimu katika kufanikisha malengo yako na kufikia hatima ya maisha yako. Uchaguzi wa aina ya kazi au aina ya kampuni ya kufanyia kazi, au aina ya biashara utakayoanza, vinaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yako. Hivyo unapaswa kutumia muda wa kutosha kufikiri na kuridhika kabisa na uchaguzi unaotaka kufanya kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
13. Msingi wa utajiri ni thamani. Kama lengo lako ni kufanikiwa kifedha, kuna njia moja pekee ya kuweza kupata mafanikio hayo ya kudumu, na njia hiyo ni kuongeza thamani. Mafanikio ya muda mrefu ya utajiri wa kudumu yanatokana nakuongeza thamani katika maisha ya watu. Mafanikio hayo yanatokana na kuwahudumia watu kwa kuwapatia bidhaa na huduma ambazo wanazihitaji na wako tayari kuzilipia ili kuzipata.
14. Unapokua na lengo la kufanikiwa kifedha anza kwa kutengeneza orodha ya njia ambazo utaweza kuzitumia ili kupata matokeo. Jinsi unavyokua na machaguo mengi ndivyo utakavyoweza kufanya maamuzi mazuri zaidi. Kwa Mfano:
· Unaweza kufikia lengo kwa kuanzisha biashara mpya
· Unaweza kununua biashara ambayo ipo inaendelea
· Unaweza kua bora sana kwa kile unachokifanya na kua unalipwa ghali zaidi, na kwa uangalifu ukawa unawekeza na kuweka akiba pesa zako kwa kipindi cha muda mrefu
· Unaweza ukawa unawekeza kwenye mali zisizohamishika (real estate) kama nyumba na ardhi/viwanja, inaweza kua ni kwa kununua nyumba na kuzifanyia ukarabati na maboresho halafu unaziuza kwa bei ya juu zaidi n.k
15. Matumaini sio Mkakati (Hope Is Not a Strategy). Fanya uchunguzi kabla ya kuwekeza muda wako, fedha au hisia zako kwenye kazi, biashara au mahusiano. Usiishie tu kua na matumaini kwamba kila kitu kipo sawa au kitakua sawa. Pata ushauri kwa wale ambao tayari wameshaipita ile njia unayotaka kuipitia na wamefanikiwa. Jifunze kutoka kwa wataalamu, tafuta wale ambao wameshafikia pale unapotaka kwenda uliza wamefikaje hapo. Jifunze na weka mkakati wa kujiboresha zaidi.
16. Uwezo wako wa kufikiri ndio mali yenye thamani zaidi. Thamani ipo katika Uwezo wako wa kufikiri kua wewe ni nani na unataka nini hasa. Zaidi ya asilimia 80 ya mafanikio yako yatakua ni matokeo ya uwezo wako wa kufikiri vizuri na kwa usahihi. Uwezo wako wa kuweka malengo yanayoeleweka, yanayopimika ambayo una shauku kubwa kuyafikia, yenye kuendana na uwezo na vipaji ulivyo navyo, itakua ni hatua kubwa ya kwanza ya wewe kufikia kwenye mustakabli na mafanikio ya maisha marefu. Tunachotakiwa kujifunza ni kutengeneza huo uwezo wa kufikiri, kuweka malengo na kuweza kuyasimamia
17. Fanyika/kuwa mshauri wako mwenyewe (Become Your Own Consultant)
Hebu jaribu kufikiri wewe ni mshauri na umeitwa kuja kumshauri wewe mwenyewe (to advise yourself) kwenye jambo fulani ambalo ni la muhimu wewe kulifanya ili uweze kufikia mustakabali wako. Ukiwa kama mshauri wako mwenyewe, jilazimishe kuwa tulivu, kuwa mpole na uwe na mtazamo chanya katika kupokea ushauri unaojipatia. Jenga tabia hii ya kujishauri mara kwa mara, kabla hujafanya maamuzi yenye athari aidha chanya au hasi kwenye maisha yako kaa chini jipatie ushauri. Hebu piga picha kwamba wewe ndio unamshauri mtu mwingine kwenye hilo jambo, ungetoa ushauri gani, fanya hivyo kwa uhalisia na bila upendeleao wowote. Halafu jitahidi sasa kuupokea ushauri huo hata kama ni mchungu tekeleza. Don’t fall in love with your ideas, especially your initial ideas. Always be open to the possibility that there is a better way to achieve the same goal.
18. Omba/Uliza kile unachotaka. Katika biashara, maisha yako binafsi au kazini, kumbuka vigezo na sheria/taratibu viliwekwa na mtu fulani na vinaweza kubadilishwa na mtu fulani. Hii inaweza kua mshahara, mazingira ya ajira, vigezo vya mkataba wa kazi, gharama za bidhaa au huduma, gharama za kukodisha sehemu ya biashara, vigezo na masharti ya mikopo n.k hivi vyote viliwekwa na watu. Kama haufurahii kitu hapo usiwe mgumu kuuliza/kuomba. Kitu cha tofauti na kilichopangwa. Usiogope jibu la hapana. Kumbuka kabla ya kuomba/kuuliza kitu jibu hua ni hapana. Na kama hata baada ya kuomba jibu limekua hapana, basi ulichopoteza hapo ni hizo sekunde chache tu ulizo tumia kuomba. Ila kama jibu litakua ndiyo, hii inaweza kubadili maisha yako. The Bible says, “You have not because you ask not.” Never be afraid to ask.
SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.
19. Mali yako isiyoshikika (Your Intangible Assets). Uwezo wako wa kutengeneza kipato (earning ability) ndiyo mali yako hadimu isiyoshikika. Ni vigumu kuikadiria au kuipima. Watu wawili wanaweza kua na akili sawa na wakawa wamepata matokeo sawa wakati wakiwa shuleni, tena inawezekana wamesoma chuo kimoja, na kozi moja, na kuanza kazi pamoja. Miaka kumi baadaye unakuta mmoja wapo amepandishwa cheo mara kadha na anapata kipato mara 5 au 10 zaidi ya mwenzake. Kwanini hii inatokea? Kwa ufupi ni kwamba hawa watu wanatofautiana katika uwezo wao wa kutengeneza kipato (earning ability. Uwezo huo unaweza kuwa unaongezeka thamani au unashuka thamani. Unapoweka juhudi za kudumu katika kujifunza, kuendelea kuongeza maarifa na ujuzi ili kuongeza thamani popote pale unapokua, uwezo wako wa kuingiza kipato unaongeza thamani yake. Kwa maneno mengine ni kwamba lazima kipato chako lazima kiongezeke.
20. Tengeneza mpango mbadala (Plan B). Endapo mpango wako wa kwanza utashindwa kufanya kazi, kusonga kwako mbele kwa haraka kutategemea mpango mbadala au Plan B. Kamwe usidhanie (assume) kila kitu kitaenda sawia kama kilivyo kwenye mpango wa kwanza. Kama upo bado shuleni, kama Plan A ni kuajiriwa, basi weka na Plan B, ili ukifika mtaani, ajira ikishindikana uwe una chakufanya yaani hiyo Plan B. Changamoto ni kwamba hata hiyo Paln A wengi hawana, ndiyo maana Plan B nayo inakua ngumu. Unakutana na mtu kamaliza chuo mwaka umeisha hana ajira, ukimuuliza unafanya nini sasa, anasema anasubiria bado serikali haijatoa nafasi za ajira, au mwingine anaporomosha malalamiko lukuki kwa serikali ilivyoshindwa kutoa ajira kwake na wenzake. Ukiona mtu wa namna hiyo ujue kakosa Plan B. Always develop a “Plan B” in case your first plan doesn’t work out. Never assume that everything will turn out the way you expect
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinaitwa SELF-IMPROVEMENT 101.

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu. Leo tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinaitwa SELF-IMPROVEMENT 101. Kitabu kimeandikwa na mwandishi aliyebobea kwenye maswala ya uongozi, mwandishi anayeheshimika katika eneo lake la kutengeneza viongozi, sio mwingine mwandishi huyo ni John Maxwell.
Kitabu hiki kinahusu jinsi ya kujiboresha wewe binafsi, ukitaka biashara yako ikue lazima ukue wewe kwanza maana Biashara haiwezi kukua kukuzidi wewe mmiliki. Lakini pia mwandishi anasema kwamba unapojiboresha na vinavyokuzunguka ghafla vinakua bora. Na wengi hawatambui hili, wanahangaika kujaribu kuboresha wengine au biashara zao mwishowe wanashindwa. Sasa njia rahisi ya kufikia mafanikio ni kujiboresha wewe, na njia nzuri ni kuchagua kua mwanafunzi wa kudumu.
Usikome kujifunza, soma vitabu, majarida, hudhuria semina na tafuta mtu (mentor) aliyefanikiwa katika eneo unalotaka kujiboresha jifunze kwake. Heshimu mentor wako na pia fanyia kazi anachokuelekeza, usionyeshe kwamba una uwezo wakati unahitaji kujifunza. Mwishoni anasema gharama ya kutojiboresha ni kubwa sana kuliko ya kujiboresha. Lipa gharama sasa hivi, maana gharama ya baadaye ni kubwa sana.
Kwa ufupi kitabu hiki ni kizuri sana. Hupaswi kukosa mambo ya wiki hii.
Karibu tujifunze mambo mengine.
1. Ukuaji lazima uwe wa kukusudia, kama unataka kukua lazima ukusudie. Tunaweza kutamani maisha yetu yawe bora lakini tukaishia kutamani, tukifikiri ukuaji unatokea tu kama ajali. Kuna tofauti ya kutamani (wish) na kukusudia (intention). Kukusudia kunaambatana na utendaji. Growth must be intentional— nobody improves by accident.
2. Kila mtu anafikiria kuibadilisha dunia, na hakuna anayefikri kujibadilishe yeye mwenyewe kwanza. Watu wengi wanapambana na mabadiliko (fight against change) hasa kama yanawagusa kibinafsi. Unapaswa kutambua kwamba mabadiliko hayaepukiki, lakini pia kwa upande mwingine mabadiliko ni uchaguzi. Unaweza kuchagua kukua au kupambana na ukuaji. But know this: people unwilling to grow will never reach their potential.
3. Tofauti ya Waliofanikiwa na wasiofanikiwa haipo katika uwezo wao na watu wengi hawatambui hilo. Watu hawa Wanatofautiana kwenye shauku (desire) ya kufikia uwezo wao. Maana shauku hii ndiyo inayowasukuma kujifunza ili kukua kufikia uwezo wao. And nothing is more effective when it comes to reaching potential than commitment to personal growth.
4. Watu wengi hua tunasherehekea pindi tunapopata diploma au digrii (shahada) zetu na tunajisemea “Asante Mungu imepita hiyo” Ngoja sasa nipate kazi, maana nimemaliza kusoma/kujifunza. Lakini Fikra za mtindo huu hazitakupeleka mbali zaidi ya kuishia kua mtu wa wastani tu. Unapomaliza shule yako sio mwisho wa kujifunza, ndio kwanza kunakua kumekucha. Maana ukienda mtaani unagundua kumbe kuna vitu vingi sana ambavyo hukuweza kujifunza pindi ulipokua shuleni. If you want to be successful, you have to keep growing. The happiest people I know are growing every day.
5. Chagua maisha ya ukuaji (Choose a life of growth). Njia pekee ya kuboresha maisha yako ni kujiboresha wewe mwenyewe. Kama unataka kukuza shirika au kampuni lazima ukue kama kiongozi. Kama unataka kua na watoto bora lazima uwe baba bora kwanza. Kama unataka kupata mke/mume bora lazima wewe binafsi uwe bora kwanza. Hakuna njia ya uhakika ya kuwafanya watu wanaokuzunguka kua bora. Watu wengi wanasumbuka kweli kuboresha watu wanao wazunguka lakini wanashindwa. Kitu pekee ambacho kweli unao uwezo wa kukiboresha ni wewe mwenyewe. Na maajabu ni kwamba ukifanya kitu hicho (kujiboresha) kila kitu kinachokuzunguka ghafla kinakua bora. So the bottom line is that if you want to take the success journey, you must live a life of growth. And the only way you will grow is if you choose to grow.
6. Anza kukua leo. Sio kile utakachofanya, bali ni kile unachofanya sasa hivi ndio kinachojalisha. Usisubiri kuanza Kukua kesho, anza leo. Watu wengi ambao hawajafanikiwa wana ugonjwa unaoitwa “siku moja” nitafanya hiki au kile, wakati wangeweza kuanza mara moja kufanya vitu vyenye kuleta thamani kwenye maisha yao, lakini hawafanyi na kuishia kusema ipo siku nitafanya. The best way to ensure success is to start growing today. No matter where you may be starting from, don’t be discouraged; everyone who got where he is started where he was.
7. Ukuaji hautokei moja kwa moja (Growth is not automatic). Unaweza kua mdogo mara moja tu, lakini unaweza kua mchanga (Immature) kwa muda usiojulikana, hii ina maana ukuaji hauji automatic. Sio kwa vile umri unakwenda basi ufikiri ndio unakua, sio hivyo. Unaweza kua na miaka 50 lakini bado ukawa mchanga. Ukuaji unahitaji kuweka juhudi za dhati. The sooner you start, the closer to reaching your potential you’ll be.
8. Ukuaji wako wa leo ndio utakaofanya kesho yako iwe bora. Kila unachofanya leo kinajijenga kwenye kile ulichofanya jana, na vyote (vya jana na leo) ndivyo vitakavyoamua kesho yako itakua vipi. Growth today is an investment for tomorrow.
9. Ukuaji wako ni wajibu wako. Ulipokua mdogo wazazi wako walikua na wajibu kwako, hata elimu na ukuaji wako ilikua ni wajibu wao. Lakini sasa umeshakua mtu mzima, wewe ndio unabeba wajibu mzima wa maisha yako. Usipofanya ukuaji wako kua wajibu wako, basi ujue kamwe haitatokea.
10. Kamwe usiridhike au kubweteka na mafanikio uliyoyapata. Adui mkubwa wa mafanikio yako ya kesho ni mafanikio yako ya leo. Maana unapojiona umefanikiwa leo na kubweteka, unakua unahujumu mwenyewe mafanikio yako ya kesho. Kule kufikiri kwamba “umefika” unapofanikisha lengo kuna madhara sawa na kuamini kwamba unajua yote. Hii inaondoa hamasa au shauku ya kujifunza zaidi. Huu ni ugonjwa na watu wengi wanaumwa na huu ugonjwa. Lakini watu waliofanikiwa hawapumziki na kusema sasa nimefika, wanatambua kwamba kushinda kama ulivyo kushindwa ni jambo la muda kidogo (temporary), kwa hiyo wanafahamu fika wanapaswa kuendelea kukua zaidi na zaidi ili kuendelea kua na mafanikio. Don’t settle into a comfort zone, and don’t let success go to your head. Enjoy your success briefly, and then move on to greater growth.
11. Unapaswa kuwa mwanafunzi wa kudumu. Kama tulivyoona kwamba adui mkubwa wa mafanikio yako ya kesho ni mafanikio yako ya leo, ili kuweza kuvuka hiki kikwazo lazima uwe mwanafunzi wa kudumu. Ukiwa mwanafunzi wa kudumu hutabweteka na mafanikio uliyoyapata, utagundua kwamba vipo vingi sana vya kujifunza, na hapo ulipo bado sana hujaweza kufikia uwezo wako ulionao. Watu wengi walio fanikiwa wanasonga mbele kwenye mafanikio kwenye muda uleule ambao wengine wanaupoteza. Kumbuka unapopoteza muda, kuna mwingine muda huo anautumia kujiboresha na kusonga mbele, na kamwe hamtaweza kua sawa, lazima awe mbali tu.
12. Tengeneza mpango wa Kukua/kujiboresha (develop a plan for growth). Ufunguo wa kua na maisha ya kujifunza na kujiboresha bila kukoma umejificha kwenye mpango maalumu wa kujifunza. Weka mpango wa kila siku, andika mpango wako mahali, kwenye mpango wako andika vitu ambavyo unataka kujifunza, andika pia na njia utakazotumia kujifunza. Inaweza kua ni kwa kusoma, kuhudhuria semina, kufanya maongezi na wale waliofanikiwa kwenye eneo unalotaka kujifunza n.k Ukimaliza kazi iliyobaki ni kuwa na nidhamu ya kutendea kazi mpango huo. Usiruhusu udhuru. No excuse
13. Kama ulichokifanya jana bado kinaonekana ni kitu kikubwa basi ujue leo umefanya kidogo tu au haujafanya kabisa. Mara nyingi utasikia watu wakisifia uwezo wao au mafanikio yao ya siku za nyuma. Utasikia “ yaani mimi nilikua kichwa balaa, nilikua naongoza darasani” au “yaani enzi zangu ungenikuta kwenye ubora wangu nilikua ni shiiida” Sasa ngoja ni kwambie kitu Ukiona unajisifia kuhusu jana ujue leo hujafanya kitu.
14. Kwa kujiboresha wewe dunia nayo inakua bora. Usiogope unapokua kwa taratibu, cha kuogopa ni kusimama tu sehemu moja, au kudumaa. Sahau makosa uliyofanya lakini usisahau yale uliyojifunza kutoka kwenye hayo makosa. Jinsi gani unaweza kua bora kesho? Ni kwa kua bora leo. Anza kujiboresha leo
15. Wakati mzuri wa kupanda mti ulikua ni miaka ishirini iliyopita, ila wakati mwingine mzuri na sahihi wa kupanda mti ni leo. Yamkini unatamani ungeanza mapema , au pengine unatamani ungepataga mwalimu mzuri au mshauri mzuri miaka kadhaa iliyopita. Hakuna hata moja hapo lenye kuleta maana. Kuangalia nyuma na kuanza kulalamika hakutakusaidia wewe kusonga mbele. Muda ulionao sasa ndio una uwezo wa kuutumia kubadilisha maisha yako.
16. Adui mkubwa wa kujifunza ni kufahamu/kujua. Lengo la kujifunza ni kutenda na sio kufahamu/kujua, kwani ukishajua na kukaa nacho tu kina faida gani? Wengi wanaingia kwenye mtego wa KUJUA, pengine una digrii yako au masters yako, unafarijika kwamba unajua vitu vingi hivyo unaona huna cha kujifunza tena. Unaishia kusema kwa maneno mimi ni graduate au mimi nina master.. so what? Tunachotaka kuona ni utendaji na sio maneno yako. Unapojifunza zaidi ndipo unagundua kumbe hujui vingi na utaendelea kuwa na hamasa ya kujifunza. Huwa napenda kujifunza kutoka kwa tajiri Warren Buffet, japo ana umri zaidi ya miaka 84, na ni tajiri wa 3 wa ulimwengu, lakini haachi kujifunza kwa kubweteka kwa mafanikio aliyonayo, sasa wewe ni nani wakati hata kwenye kitongoji chako tu kwenye orodha ya watu matajiri haupo.
17. Kama unachokifanya hakina mchango kwako au kwa wengine basi hebu kaa chini uhoji uthamani wa hicho unachokifanya, na uhalali wa wewe kuendelea kukifanya kama hakina thamani kwako wala kwa wengine.
18. Wafanye marafiki zako kua waalimu wako, tengeneza marafiki ambao wanaokupa changamoto na kuongeza thamani kwako, na wewe pia ujitahidi kuongeza thamani kwao.
19. Kama wewe una kipaji sana, unaweza kua na wakati mgumu kufundishika. Kwanini? Kwa sababu watu wenye vipaji mara kadhaa hudhani kwamba wanajua kila kitu. Na hivyo kufanya vipaji vyao kushindwa kuongezeka/kutanuka zaidi. Kufundishika haina maana sana kuhusu uwezo au uwezo wa akili kama ilivyo kuhusu mtazamo. Kufundishika ni ile shauku au nia ya kusikiliza, kujifunza, na kutendea kazi. Ni kule kua na njaa ya kugundua na kukua. Teachability is the willingness to learn, unlearn, and relearn.
20. Kipaji peke yake hakitoshi kukufanikisha. Unaweza kuwa na kipaji na wala kisikusaidie. Tumeona watu wengi wenye vipaji ambao wameishia kuzika vipaji vyao kwa sababu moja kubwa ambayo ni Kutokufundishika. Wengi wamekua wakidhani ukiwa na kipaji basi mafanikio umepata. Kua na kipaji ni kitu kimoja tena cha kawaida sana, maana kwa taarifa tu ni kwamba kila mtu ana kipaji chake. Kua na kipaji ni kitu kimoja na kuweza kukifikisha kipaji chako hatua ya juu ni kitu kingine. Ujuzi ambao ni wa muhimu sana ambao unapaswa kua nao ni kujifunza jinsi ya KUJIFUNZA (learning how to learn), ukifaulu hapo lazima kipaji chako kitakupeleka hatua za juu.
Asanteni sana tukutane wiki ijayo. Kama utapenda kupata kitabu hiki Nitakupatia bure kabisa, niandikie email kupitia dd.mwakalinga@gmail.com
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana nae kwa simu 0763 071007 au email daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com Tembelea blog yake www.kilimobiasharablog.blogspot.com na ujifunze mengi kuhusu kilimo.

Mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu 85 INSPIRING WAYS TO MARKET YOUR SMALL BUSINESS. (Njia 85 za kutangaza biashara yako)

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu.  Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa 85 INSPIRING WAYS TO MARKET YOUR SMALL BUSINESS.  Kitabu kimeandikwa na mwandishi  anayejulikana  kama Jackie Jarvis. Kitabu hiki kinaangazia njia 85 ambazo unaweza kuitangaza biashara yako ndogo ikawa moja ya biashara kubwa ulimwenguni. Kama una biashara ndogo basi jitahidi ukisome maana yapo mambo mengi sana ya kujifunza.

Karibu tujifunze

1.     Kuna Njia tatu kuu za kukuza biashara ambazo ni (a) kupata wateja wapya  (b) Kuongeza kiwango cha matumizi cha wateja (Kuuza zaidi). Mfano kama mteja hua anafanya manunuzi ya 20,000 basi jitahidi kuongeza thamani hadi aweze kuongeza na kufikia manunuzi ya 40,000 au zaidi. (c) Kuongeza marudio (frequency) ya kufanya biashara na wewe. Mfano kama wateja wako wanafanya biashara na wewe mara 2 kwa mwezi, unatakiwa kuongeza juhudi kufanya wateja waongeze marudio pengine kufika mara 4 au 5 kwa mwezi.

2.     Itazame biashara yako kwa jicho la mteja. Kama unataka kuwashawishi wateja wako ili wafanye biashara na wewe ni lazima uweze kuwaelewa na kua na mahusiano mazuri na wateja. Unapoitazama biashara yako kwa jicho la mteja utaweza kuiona kwa mtazamo tofauti. Hebu jaribu kuvaa kiatu cha mteja wako, itazame biashara yako ukiwa umevaa miwani ya mteja, unaona nini? je unaona kitu tofauti? Unapaswa uone tofauti. Wamiliki wengi wa biashara wanashindwa kua na mtazamo huu, maana wanaishia kuitazama biashara kwa jicho la mmiliki wa biashara. Ukifanya hivi utashindwa kutambua mahitaji ya mteja, lakini ukitazama kwa jicho la mteja, utajua ni nini hasa mteja anahitaji.


3.     Uwezo wako na ujuzi ulionao ni wa kipekee kwako, na vinaweza kua sehemu kubwa ya kukutofautisha wewe na wengine na pia ndivyo vinavyojenga thamani ya ushauri utakao wapa wateja wako. Uwezo na ujuzi ulionao ni sehemu ya historia yako, historia iliyojenga biashara uliyonayo leo. Unaweza kuwa umetumia miaka kadhaa kujenga ujuzi ulionao, unaweza kua umetumia miaka mingi kupata uzoefu ulionao. Lakini si rahisi kwa wateja kutambua hayo, kama wanafahamu ni sawa ila swali ni je wataona thamani zaidi katika kile unachowapa? Je uzoefu wako na ujuzi wako vina mchango katika thamani wanayotaka kuipata?

4.     Jiamini mwenyewe kabla hujaaminiwa. Imani binafsi ni kule kujiamini katika ujuzi na uzoefu ulionao. Ni ile sauti ya ndani inayosema NAWEZA KUFANYA HILI. Kujiamini haina maana kwamba umekamilika, au kwamba hauna mapungufu au madhaifu la hasha. Kujiamini mwenyewe ni kule kukubaliana na madhaifu uliyonayo, lakini kwa upande mwingine ukitazama uwezo ulionao na kuweza kuutumia kufanya vizuri kufunika madhaifu yako.


5.     Unapoongeza bei ya huduma au bidhaa yako, kwanza angalia ni thamani gani utakayoiongeza kwenye huduma yako ili kuhalalisha ongezeko la bei. Ukitaka kudumisha wateja wako pindi uongezapo bei ya huduma au bidhaa yako ni lazima kuongezeka huko kwa bei kuambatane na ongezeko la thamani kwa mteja. Think value before price.

6.     Kua mbunifu mara zote. Ubunifu katika biashara ni kule kua na uwezo wa kuja na njia za kufanya vitu kwa utofauti. Ni kule kufikiri nje ya mipaka ya kawaida, au kufikiri nje ya sheria zilizopo. Pia kua mbunifu ni kule kufikri nje ya boksi ambapo wengi wamo humo ndani.

7.     Watambue washindani wako wa kibiashara. Usikae kama upo kwenye kisiwa peke yako. Hakikisha unawatambua washindani wako wa kibiashara, tambua uwezo wao kibiashara, pia tambua udhaifu wao ambao wewe utaweza kuutumia kujinadi zaidi, kwa kuboresha lile eneo ambalo mshindani wako ameshindwa.


8.     Chagua njia bora zaidi za kunadi biashara yako. Njia bora ni zile ambazo zinakuwezesha kulenga watu sahihi kwa ujumbe sahihi na kuweza kupata mapato makubwa kutoka kwenye uwekezaji ulioufanya. Tumia chombo sahihi kuinadi biashara yako. Kwanza tambua ni wateja gani unaowalenga ndio ujue ni chombo kipi kitawafikia kirahisi. Mfano unawalenga watu wa vijijini halafu unatangaza kwenye mtandao (online marketing), hii itakua sio sahihi maana wahusika hawana uwezo wa kupata hizo taarifa kupia mitandao.


9.     Jenga utaratibu wa kuwasiliana na wateja wako ulionao. Kuwadumisha wateja wako ili waendelee kufanya biashara na wewe inategemea sana na jinsi unavyowasiliana na kuhusiana nao. Kuwasiliana nao mara kwa mara kutafanya waone unawajali hata pale wanapokua hawajaja kununua kitu kwako. Unaweza kutumia njia mbalimbali kuwasiliana na wateja wako, kama vile barua pepe, ukaribisho wa kwenye tukio lolote, unaweza kuwatumia zawadi za kadi kama kadi za Christmas, maulid, pasaka n.k

10.           Jenga mahusiano ya kuaminiana/uaminifu na wateja wako. Mahusiano ya uaminifu ndio yanayojenga uti wa mgongo wa biashara iliyofanikiwa.  Katika ulimwengu wa leo ambapo kuna machaguo mengi sana, watu wanawasaidia wale wanaowaamini zaidi. Ukikosa kuaminiwa ndio mwanzo wa kudidimia kwa biashara yako. Chunga sana imani ambayo wateja wako wanayo kwako. Maana imani hii inajengwa kwa muda mrefu, lakini inaweza kutoka ndani ya dakika chache. Trust can take a long time to build and an instant to break.

11.           Vitu vinavyojenga imani/uaminifu kwenye mahusiano ya kibiashara ni kama kuonyesha heshima kwa watu, kuuliza maswali na kusikiliza watu kwa makini, kua mkweli hata kama kufanya hivyo kutasababisha usiuze bidhaa zako, kutoa kile ulichoahidi, pia kama umeshindwa kutoa kama ulivyoahidi hakikisha wahusika wanapata taarifa mapema n.k

12.           Pitia upya mahitaji ya wateja wako. Unatakiwa kufahamu kwamba sababu iliyofanya mtu akawa mteja wako kwa mara ya kwanza, sio sababu hiyohiyo itakayoendelea kumfanya aendelee kua mteja wako katika kipindi kijacho.  Wateja wako waliopo wana mahitaji yanayobadilikabadilika, hivyo wanahitaji uelewa na mawasiliano endelevu. Ulivyokua ukimuelewa mteja fulani mwaka jana ni tofauti na mwaka huu, kwa hiyo usitegemee kumhudumia kama mwaka jana. Lazima uwe na utaratibu wa kupitia mahitaji yao mara kwa mara, usiseme “ huyu najua tu anachotaka, mahitaji yake nayajua” wateja hawapendi wahudumiwe kimazoea, wanatamani kila siku waonekane wapya, wahudumiwe kwa mbinu mpya. Maana mahitaji yao ndiyo yanayoashiria mahitaji ya soko kwa wakati huo.

13.           Elimisha wateja. Elimu kwa wateja kunawapa wateja fursa ya kujifunza zaidi kuhusu bidhaa au huduma unayotoa. Vile wateja wanaelewa thamani wanayopata kwako ndivyo itakavyokua rahisi kwao kununua. Kuelimisha wateja ni moja ya njia nzuri sana za kupata wateja wapya.  Elimu kwa wateja inaweza kua hatua ya mwanzo katika mchakato wa kufanikisha mauzo. Maana wanunuzi wengi wanatenga muda kutafuta taarifa kabla ya kuwa tayari kuchagua ni kwa nani wanunue.

14.           Sehemu ya faida rudisha kwa jamii. Hii itakufanya kua karibu zaidi na wateja wako, maana watu wengi wanapenda kua karibu na watu wanaosaidia wengine. Pia kusaidia jamii kwa utoaji ni nguzo muhimu sana ya kiroho ya biashara yako. Hakuna aliyetoa akafilisika, tunaona kina Bill Gates kila kukicha wanatoa mabilioni ya pesa kusaidia masikini na wasiojiweza, lakini ndio kwanza utajiri wao unaongezeka.

15.           Hamasisha timu yako. Wafanyakazi wanapokua wamehamasika wanafanya kazi vizuri zaidi na hivyo kupelekea kupata zaidi. Kwa mmiliki wa biashara ni muhimu kua kiongozi zaidi kuliko kua meneja.  Jifunze jinsi ya kuongoza watu, jinsi ya kuwahamasisha wafanyakazi wako wawe na nguvu kila mara ili kuongeza ufanisi kwenye kazi.


16.           Pima mapato yanayotokana na utangazaji wa biashara yako. Ukiona hakuna tofauti ya mapato baada ya kutangaza biashara yako, basi sitisha halafu jipange upya kutafuta njia sahihi ya utangazaji wa biashara hiyo. Maana utangazaji wa biashara unatumia fedha, sasa kama hakuna mapato ya ziada yanayopatikana baada ya kutangaza ni dhahiri kwamba unapata hasara, hivyo ni muhimu sana kupima matokeo ya utangazaji hasa kwenye mapato.

17.           Tengeneza dhamana (guarantee). Dhamana ni ofa unayoitoa kwa mteja, ili kupunguza au kuondoa ile hatari (risk) ya kimtazamo ambayo imekua ikimfanya asite kununua. Dhamana inasaidia kuondoa hofu kwa mteja ya kufanya manunuzi. Dhamana zinaweza kua za aina tofauti. Mfano unaweza kuweka dhamana ya matokeo ya bidhaa unayouza. Mfano kama unauza dawa ya kupunguza uzito, unaweza kumhakikishia mteja kwamba akitumia ndani ya wiki moja na asipoona matokeo yeyote atarudishiwa fedha yake. Hii itampa ujasiri wa kununua maana atajihisi hapotezi fedha na yuko upande salama maana amepewa uhakika. Lakini pia dhamana ni rahisi kutumika kama njia ya kunadi biashara yako. Maana huyo mteja ni rahisi kumwambia mwenzake kuhusu dhamana inayotolewa kwako.

18.           Yafanyie kazi malalamiko ya wateja. Malalamiko ni kule kujieleza kwa wateja kwa kutoridhika na huduma waliyopata. Kumbuka wateja wana machaguo mawili  wanapokua hawajaridhika na huduma au bidhaa yako, moja ni aidha waongee (walalamike) au waondoke kabisa waende kwingine. Kama wataondoka ujue hutapata fursa ya kutoa suluhisho la tatizo na wala hutajua ni nini tatizo maana hawajasema wameondoka kimyakimya. Watu wengi hawapendi kulalamika kwako moja kwa moja hata kama hawajaridhika na huduma yako, sababu ya kutokusema inaweza kuwa pengine hawataki kukusumbua, au hawajui waanze vipi, hivyo wanachofanya ni kuwaambia watu wengine, ambapo taarifa hii inaweza kuwafikia hadi watu 20. Hivyo ukipata malalamiko ya wateja unachotakiwa ni kuyachukulia kwa mtazamo chanya na kufanya marekebisho husika haraka kadri inavyowezekana.

19.           Rahisisha jinsi wateja watakavyo nunua kutoka kwako. Kwa sasa watu wengi wako bize, na biashara zinazoweza kufanikiwa ni zile tu ambazo mchakato wa kununua ni mfupi. Ukiwa na urasimu mwingi hutapata wateja labda uwe ni wewe pekee unayetoa huduma hiyo, na hata hivyo hutafika mbali. Kwa jinsi utakavyorahisisha mfumo wa manunuzi, utaendelea kudumisha wateja na pia utavutia wengine wapya.


20.           Wafanye wateja wako wawe wenye furaha wakati wote. Kama wateja watakua wanakufurahia wewe pamoja na biashara yako, ni kwamba wataendelea kubakia waaminifu na wataendelea kununua kutoka kwako. Sio hivyo tu bali watawashauri na wengine waje kununua kwako, hivyo wateja watazidi kuongezeka. Hata pale utakapoongeza bei ya huduma sio rahisi kuondoka maana tayari wanafurahia thamani wanayoipata kutoka kwako.

Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu EAT THAT FROG.

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu.  Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa EAT THA FROG. Kitabu kimeandikwa na mwandishi mashuhuri wa vitabu Brian Tracy. Mwandishi wa kitabu anaongelea kuhusu” KULA HUYO CHURA”, kwa kawaida hakuna mtu anayependa kula chura, lakini ukijizoesha kula chura, baada ya muda utazoea na utamla chura kirahisi zaidi. Mwandishi anafananisha Chura na shughuli, kazi au jukumu ambalo linaonekana ni gumu kufanya na ambalo ni rahisi kuahirisha. Mara nyingi majukumu tunayoahirisha ndiyo yenye kuleta matokeo makubwa katika maisha.

Karibu tujifunze mambo mengine

1.     Katika ulimwengu wa leo unalipwa kutokana na matokeo unayoyapata au kuyasababisha. Ukitaka kuongezwa mshahara basi kwanza ongeza matokeo kazini mwako.

2.     Mafanikio yanasababishwa na tabia. Tabia ndio zinavuta mafanikio. Tabia yakuweka vipaumbele,  kuepuka kuahirisha mambo na kushughulika na jambo lenye umuhimu ni ujuzi wa kiakili na kimwili. Tabia hii unaweza kujifunza kwa kufanyia mazoezi, kurudia rudia mpaka pale inapokua tabia ya kudumu. Ikishakua tabia ya kudumu inakua ni rahisi

3.     Asilimia 3 ya watu wazima ndio wenye malengo yaliyoandikwa. Na watu hawa wanafanikisha mambo mara 10 zaidi ya wale ambao hawajaandika malengo yao. Kamata kalamu na karatasi andika malengo yako.

4.     Hakuna njia ya mkato, kufanyia mazoezi ndio njia pekee inayoweza kumudu kutengeneza tabia na kuongeza ujuzi. Unaweza usione mabadiliko katika hatua za mwanzo, lakini ukiweza kudumisha mazoezi, lazima tu mabadiliko yatatokea.

5.     Kanuni yenye nguvu ya kuweka malengo na kuyafanikisha. Kanuni hiyo ina hatua saba. Hatua ya Kwanza: Amua ni nini hasa unataka. Watu wengi hawajui hasa ni nini wanataka, tafuta mahali palipotulia kaa kwa utulivu, jaribu kutafakari na kupambanua nini hasa unachotaka. Kama umeajiriwa pia njia ya kuweza kutimiza malengo ya kampuni, kaa chini na bosi wako, muulize hasa ni nini anachotegemea kutoka kwako.

6.     Hatua ya Pili: Andika mahali. Haitoshi kuamua ni nini unataka, nenda mbali zaidi andika mahali. Usipoandika malengo yako yanakua hayana nguvu, unapoandika chini unatengeneza kitu ambacho unaweza kukishika na kukiona.

7.     Hatua ya 3: Wekea malengo yako muda (deadline). Lengo linapokosa muda linakosa uharaka, na hatimaye kuendelea kuliahirisha, maana unaona bado hujachelewa kulifanya. Ila ukiliwekea muda, itakufanya ulitekeleze maana utaona muda unayoyoma.

8.     Hatua ya 4: Weka orodha yenye kila kitu ambacho unafikiri  utahitaji ili kufanikisha malengo yako. Orodha iwe pia na vitu utakavyotakiwa kufanya ili kufikia kule ulikopanga.

9.     Hatua ya 5: Orodha ya vitu utakavyohitaji kuvifanya, ipangilie kwenye mpango kazi. Unapopanga jua ni kipi kinapaswa kutangulia, kitakachofuata hadi kufikia kwenye malengo. Lazima mpango wako uwe kwenye mtiririko mzuri wa vipaumbele.

10.           Hatua ya 6: Anza utekelezaji mara moja. Mpango wa kawaida ambao unafanyiwa kazi ni mzuri zaidi, kuliko ule mpango ambao ni wa viwango vya juu lakini umebakia kwenye makaratasi.
Hatua ya 7:  Amua kufanya kitu kila siku. Hakikisha haipiti siku bila kufanya chochote chenye mchango kwenye malengo yako.

11.           Panga siku yako mapema. Ni vizuri kujenga tabia ya kuipangilia siku yako siku moja kabla.  Jitahidi usikubali kulala bila kuweka mpango wa siku inayofuata. Kila dakika unayotumia kupanga, unaokoa dakika 10 za utekelezaji. Itakuchukua dakika 10 hadi 12 kupanga siku yako inayofuata, lakini utaokoa hadi masaa 2 ya utekelezaji katika shughuli za siku inayofuata.

12.           Mara zote hakikisha unafanya shughuli ambazo zipo kwenye orodha ya mpango kazi wa siku. Usitekeleze shughuli iliyopo nje ya ulizopanga ikiwa ulizopanga hazijaisha, na kama ikikulazimu kufanya hivyo basi kwanza ijumuishe shughuli hiyo kwenye orodha kabla haujaifanya.

13.           Adui mkubwa ambaye tunapaswa kumshinda tunapokua kwenye njia ya mafanikio sio kukosa uwezo au kukosa fursa, bali ni hofu ya kushindwa na kukataliwa. Njia pekee ya kumshinda adui huyu hofu ni kufanya kile kitu unachokiogopa

14.           Kamwe usiache kujifunza. Maboresho binafsi na maboresho ya kitaaluma ni moja ya njia nzuri za kuukomboa muda. Maana unapokua bora wewe hata ufanyaji wa kazi unakua ni rahisi na kwa muda mfupi zaidi. Continuous learning is the minimum requirement for success in any field.

15.           Teknolojia inaweza kua rafiki yako mzuri au adui yako mbaya. Ukuaji wa teknolojia umesababisha watu wengi kupoteza muda mwingi, mitandao ya kijamii kwa sasa ndiyo inayoongoza kusababisha watu kuahirisha  mambo ya muhimu. Mbaya zaidi ni kwamba mitandao hii inalevya (addiction) yaani hata kama hupendi unajikuta tu ushaingia, facebook, whatsapp twiter, instagram, sijui na wapi kule. Lazima uweke mikakati kabambe ya kukabiliana na ulevi wa kwenye teknolojia hasa mitandao hii ya kijamii, maana wakati wewe unapoteza muda wako huko, wamiliki wa mitandao hiyo ndio wanaingiza pesa. Unapokua unafanya kazi hakikisha unaweka simu mbali na wewe mpaka umemaliza kazi, unaweza ukatenga muda maalumu wa kuangalia simu.

16.           Ukitaka kumla tembo, ukimkabili kwa kutaka kumla mzima mzima, utaona haiwezekani, laini ukimkata vipande vipande, na kuanza kimoja hadi kingine, utakuta tembo kaisha bila kujua. Hivyohivyo unapokua na jukumu kubwa, usilikabili kwa ujumla, ligawanye vipengele vipengele, halafu anza na kipengele kimoja baada ya kingine. Baada ya muda utakua umemaliza jukumu hilo.

17.           Watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya shughuli (activity) na Ufanikishaji (Accomplishment). Wanaongea tu, wanafanya vikao visivyoisha, na kutengeneza mipango mizuri sana, lakini cha kushangaza mwishowe ukifanyika uchambuzi au tathimini unakuta hakuna aliyefanya kazi hiyo na kupata matokeo yaliyotakikana.  Tatizo tunajiweka ‘bize’ na shughuli ila mwishowe ufanikishaji unakua mdogo. Amua leo kujikita katika ufanikishaji kuliko shughuli, maana shughuli kila mtu anaweza kufanya, ila kupata matokeo yaliyokusudiwa au hata zaidi yake ni wachache sana wanaoweza. Ila ukiamua unaweza.

18.           Tumia kanuni ya ABCDE. Unapopanga majukumu yako ya siku, unapoyaandika kwenye karatasi mbele ya shughuli husika weka alama A, au B au C, D au E. Majukumu yanayoangukia kwenye A ni yale ya muhimu sana, kuyafanya yataleta manufaa mazuri, na usipofanya yataleta madhara makubwa. Kama una shughuli za muhimu zaidi 1, unaweza kuandika A1, A2, A3 …..Usifanye jukumu la B kabla ya majukumu yote yaliyopo kwenye A hayajaisha.  Majukumu yanayoangukia kwenye B ni yale majukumu unayopaswa kuyafanya, ila ukiyafanya au usipoyafanya hayana madhara kivile. Majukumu yanayoangukia kwenye kundi C ni yale mabao haya umuhimu wowote, mfano kumpigia rafiki yako simu wakati wa kazi. Kundi D ni yale majukumu ambayo unaweza kumpatia mtu mwingine akafanya kwa niaba yako (Delegate). Kundi E ni la yale majukumu ambayo hupaswi wala kufanya, unaweza kuyaondoa yasifanyike kabisa (Eliminate)

19.           Sehemu ya kufanyia kazi iwe safi. Kama unafanyia kazi mezani hakikisha panakua safi kwanza. Sehemu unayofanyia kazi kama sio safi ni rahisi kuahirisha kufanya shughuli.  Sehemu safi akili inakua na utulivu na inafanya kazi kwa ufanisi zaidi.

20.           Tambua muda gani katika siku akili yako inakua katika uwezo wake wa juu, na kisha panga muda huo kufanya shughuli ya muhimu . Anza na shughuli ile ngumu zaidi, maana muda huo akili yako ndio inafanya kazi vizuri zaidi. Watu wengi wanakua na nguvu ya akili wakati wa asubuhi, baadhi ni mchana na wachache akili zao zinakua na nguvu zaidi jioni



Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com