Siri Ya Mfereji Wa Upendo Kuelekea Kwenye Bahari Ya Mafanikio
Kama ukipenda ukampenda mtu waswahili wanasema hata jalala lao utaliona zuri. Yaani hakuna ubaya utakaouona kwa mtu kama ukimpenda. Lakini hata akikuudhi kiasi gani utamsamehe kwakua unampenda sana.
Ukipenda wale wanaokuchukia, usipolipiza kisasi, usipowaonyesha ubaya wowote, kama wanakuchukia basi wanaweza kubadilika. Kama wasipobadilika basi wataondoka mahali ulipo. Upendo una nguvu sana.
Mahali palipo na upendo kuna maendeleo sana. Kama wanandoa, wanafamilia, wanaukoo au wanakijiji fulani wanapendana basi mambo yao mengi huenda vizuri. Kwakua kila mmoja yupo katika eneo lake kuhakikisha kuwa mwenzake anaishi kwa furaha. Ni rahisi kufanikiwa kama una upendo na hauna kinyongo na watu wengine.
Unawezaje kuwapenda hata wale wanaokuudhi?
“Kuna usemi wa Kiswahili unaosema “akuchomaye mchome” au “mpende akupendaye asiyekupenda achana naye” kuna baadhi ya watu hutafsiri vibaya usemi huu. Yaani mtu akimfanyia kitendo kibaya na yeye analipiza. Sio busara na sio jambo jema kumfanyia mtu ubaya hata kama yeye amekufanyia hivyo. Kwa kufanya hivyo utaongeza chuki na uadui.
Katika vitabu vya dini tunashauriwa kuwapenda wasiotupenda ili tupate thawabu. Kwakua kuwapenda wanaotupenda pekee kutawafanya wale wanaotuchukia wasibadilike kwakua sisi pia tunawachukia na hakutakuwa na mabadiliko hivyo hatupati thawabu kwa kuwachukia wanaotuchukia.
Lakini ukimpenda anayekuchukia basi ataona aibu tu. Sio kwa siku moja lakini baada ya muda mtu huyu anaweza kubadilika.
Naomba nikufundishe mbinu moja itakayopunguza kasi ya chuki na kuleta upendo ndani yako. Ukiamka tu, sema moyoni ninawapenda watu wote. Endelea kujikumbusha neno hili siku nzima. Kila unayeonana nae jiambie kuwa unampenda. Hata akiongea neno baya wewe jiambie moyoni kwa nguvu zote kuwa unampenda. Akikufanyia kitu kibaya, muhurumie huwezi kufahamu ana msongo wa mawazo kiasi gani. Badala ya kujenga chuki juu yake ambayo inaweza kukuletea madhara ya kiafya jiambie kuwa unampenda. Itakusaidia kupunguza vurugu na utaona moyoni mwako una amani.
Mara nyingi watu wenye chuki hupenda kupinga na kukebehi maneno au juhudi za mtu mwenye mawazo ya mafanikio. Watu hawa hufanya hivi mbele za watu ili kupata mashabiki na kukufanya wewe ujisikie vibaya. Hutamani ubishane nao na kugombana au baadae upate muda wa kutafakari yale unayotaka kufanya kuwa hayawezekani. Usiwape nafasi watu wa aina hii kukupotezea malengo yako. Usifanye mambo yako ili kuwaonyesha kama unaweza pia. Fanya kwaajili yako na kwaajili ya furaha ya moyo wako na ya wale ambao wako upande wako kuhakikisha unafikia pale unapotamani ufike. Kama hukufanikiwa kufikia pale ulipokusudia jipange vizuri na uendelee na mapambano. Lakini usimchukie mtu yeyote kwani ukiwa na chuki mafanikio kwako ni ndoto. Upendo na roho safi ni mfereji muhimu kuendea kwenye bahari ya mafanikio.
Makala hii imeandikwa na Esther Nguluwa.
7/17/2015 07:43:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Ulizaliwa Uishi Wewe, Usiishi Kwa Ajili Ya Wengine.
Hata mimi uandishi wangu wa makala hauwezi kufanana na wa mwingine, ninayo namna yangu ya kuandika ambayo Mungu aliiweka na naenenda kwa hiyo. Nikijaribu kuwa kama mwingine au kuiga nitashindwa tu, inabidi niwe mimi. Ni wajibu wa kila mtu kwa imani yake kuweza kugundua kile ameumbiwa kufanya.
Kuna mwingine amezaliwa kufundisha wengine tu, popote alipo ualimu wake utaonekana tu, yaani atafurahia kufundisha tu hata kama hamna kipato anapata lakini yeye kuna amani anaipata ndani mwake, kuna kile kitu unaweza kufanya bila kutanguliza malipo, kile ambacho usipofanya unasikia kama una deni, unaona haujatimiza wajibu wako sawasawa. Ukishagundua kusudi la wewe kuwepo ni wajibu wako wewe mwenyewe kulisimamia na kuliishi hilo, ukimshirikisha Muumba wako katika kila hatua.
Pengine baada ya kugundua kusudi lako ni lipi, unaweza kukutana na vikwazo vingi katika kuliishi hilo kusudi. Ndugu yangu tambua kwamba ni wewe na Mungu wako mnaelewa hilo kusudi hivyo usitegemee kila mtu akuelewe kirahisi, usishangae kuona uliotegemea wakuelewe wasipokuelewa. Na hiyo isiwe sababu ya wewe kuona labda umepotea au hauko sawasawa, hata mimi kuweza kuandika hata makala yenye maneno hata mia mbili tu haikuwa rahisi mwanzoni. Kuna wakati nilipompa mtu ambaye nadhani ni wa karibu aipitie na kunipa maoni nilipata maoni ya kukatisha tamaa sana, lakini uzuri ni kwamba wapo waliolewa na kunitia moyo. Lakini si vyema kumpuuza anayekupinga pia maana walikuwa na sababu zao za msingi pia, mwingine anakuambia hujawahi kusomea uandishi au wewe na ufundi wako na uandishi wa makala kama hizi vinahusianaje? Waliona hivyo , hawakubahatika kuona kile kimewekwa ndani mwangu Lakini mimi ndio nilijua kwa nini naandika, maana naamini siandiki ili kupoteza muda wangu bali kuna mtu akisoma anapata uwezo wa kusogea hatua moja mbele, kuna badiliko linatokea ndani mwake, kuna maisha ya mtu yanaguswa na kumfanya awe mtu bora zaidi, na ndiyo furaha yangu hiyo.
Hivyo haijalishi unakutana na nini, naomba kama kweli una uhakika ndicho kitu umeitiwa endelea kufanya, ng’ang’ana tu wapo watakaokuelewa baadae, kuna watu mtoto akizaliwa wanashindwa kuelewa kama anafanana na nani lakini kadri anavyoendelea kukua wanamtambua vizuri na kuzidi kumfurahia hata kama mwanzoni hawakumkubali.
Kuna mtu anajua kabisa anachokifanya sicho kitu anatakiwa kufanya lakini anafanya tu kwa kuwa kuna watu wanamtaka afanye hilo. Wakati mwingine hata mzazi anaweza kukutaka uwe mtu fulani kwa sababu zake binafsi na pengine nzuri tu. Mwingine anaweza kukutaka ufanye kitu fulani kwa manufaa yake. Ishi wewe vile ulikusudiwa kuwa, tumia hekima na busara kuwaelewesha wanaotaka uwe tofauti na ulivyo wakati wewe una uhakika hivyo ndivyo unavyopasa kuwa. Wakati mwingine ikibidi ni bora unyamaze na kuwaacha waone kwa vitendo kile unamaanisha maana hauwezi kujieleza kwa kila mtu.
Hivyo ni wajibu wako na uamuzi wako wewe kwa kuwa ndiwe unajua nini unataka, kuamua kwa dhati kusimamia na kufanya kile unafurahia kufanya, kile kinakupa amani moyoni, kile unakifanya bila kuhangaika au kutumia nguvu nyingi zaidi. Kumbuka kuogopa kufanya kitu unachokipenda kwa kuhofia watu watasemaje haikupi wewe furaha wala amani, bali itakufanya wewe kuwa mtumwa wa nafsi yako mwenyewe, hauishi wanavyotaka watu au jamii, unatakiwa kuishi kama Mungu alivyokukusudia uwe, Ukijaribu kutimiza matakwa ya wanadamu unatakiwa ujue kuwa wanabadilika kila leo, leo wanaweza kukukubali na kukupenda kwa kuwa unafanya hilo lakini using’ang’ane leo watu hao hao wakikugeuka.
Hivyo tafuta sana kujijua wewe ni nani? Kwanini upo? Ukilijua kusudi lako basi liishi hilo kusudi lako , ni kwa kufanya hivyo utaweza kupata ile amani ya kweli maishani mwako, na pia kwa kuishi lile kusudi uliloumbiwa hautumii nguvu nyingi sana ili kuwa hapo, ukishajitambua mambo mengine yote yanakuwa yasharahisishwa, ukiwa kwenye mkondo wa maji, maji yakiwepo yatakupitia tu. Wajibu wako ni kutafuta mkondo wa maji ulipo.
Makala hii imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
Namba ya simu : +255 755 350 772
7/15/2015 07:32:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Sehemu 7 Ambazo Unatumia Kupoteza Rasilimali Muda Wako
Hivyo basi, kumbe muda ni rasilimali muhimu ambayo hatuwezi kununua. Utajiri ambao tumepewa duniani bure kwa watu wote matajiri na masikini ni rasilimali muda. Wote tuna wakati sawa wa masaa 24 kwa siku. Kwa hiyo kila mtu duniani ni Tajiri wa muda au wakati. je unautumiaje utajiri wa rasilimali muda wako hapa duniani?
Zifuatazo ni Baadhi ya Sehemu Ambazo Unatumia Kupoteza Rasilimali Muda
1. Kuangalia Tv
Watu wengi wamekuwa wakipoteza muda sana kuangalia tv, mtu anapoteza masaa matatu mpaka matano kuangalia tv akifuatilia tamthilia kwenye tv. Kuangalia vipindi ambavyo havina tija kwako vipindi ambavyo havina matokeo chanya kwako, kiongozi wa kanisa Katoliki duniani papa francis, ana miaka 25 sasa hajawahi kuangalia tv yaani luninga mara ya mwisho kuangalia tv ilikuwa ni tarehe 15 mwezi saba mwaka 1990. Je tunajifunza nini kutoka kwa kiongozi huyu? Kama yeye ni kiongozi mkubwa wa kanisa hilo duniani mbona hajapungukiwa wala hajapitwa kwa nini wewe usiweze?
2. Kufuatilia Udaku
Unapoteza muda kumfuatilia msanii Fulani leo amefanya nini badala ya kutumia muda huo kuboresha maisha yako. Watu wengi ni wazuri kufuatilia magazeti ya udaku, habari za udaku, mitandao au blog za udaku kuliko kufuatilia blog nzuri zinazotoa elimu ya jinsi kuboresha maisha yako moja wapo ni hii unayosoma makala hii nzuri. Utumie muda wako kufuatilia vitu vya maana ambayo vinabadili fikra yako acha kuwa mtumwa wa kila siku wa kufuatilia habari za udaku.
SOMA; MUDA–Kitu Chenye Thamani Kubwa Ila Kisichothaminika Na Wengi.
3. Kufuatilia Mitandao ya Kijamii kwa Faida Hasi
Kuwa katika mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, na kadhalika siyo mbaya, je uko katika mitandao hiyo ya kijamii kwa malengo gani? Unatumiaje muda wako katika mitandao hiyo ya kijamii kila dakika uko online kwenye mtandao zaidi ya mmoja unapata muda wapi wa kufanya kazi yako kwa ufanisi? Tenga muda wako vizuri kataa kabisa kuwa mtumwa wa kisaikolojia ukikaa kidogo bila kuingia unahisi unapitwa na habari wenzako wanaingiza siku wewe unafuatilia habari.
4. Kukaa Vijiweni
Wimbi la watu kukaa vijiweni na kupoteza muda linaongezeka kila siku ukipita kona hii utakuta watu wamekaa makundi vijiweni wakijadili serikali pengine sijui chama Fulani wamefanya hivi ni mambo mengi yanayojadiliwa kwenye magenge ya watu. Watu hawana kazi za kufanya wanapoteza muda bure na wala hajutii kwa muda anaoupoteza. Tumia muda huo kujifunza namna gani unaweza kubadili maisha yako. Acha kauli hizi za kusema ngoja niende kwa Fulani au kijiweni nikapoteze muda kidogo.
5. Kubishana
Hii ni sehemu moja wapo ambayo watu pia wanapoteza rasilmali yao nzuri ya muda katika kubishana. Watu wanabishania vyama vya siasa, timu za mipira kuna wengine wanabishana katika mpira mpaka wanapigana hii ni kwa sababu kila mmoja anataka asikilizwe kile anachosema yeye katika timu yake ndio sahihi. Unapoteza muda kushabikia vitu wakati huna hata hisa moja katika vitu hivyo unavyobishania ambavyo havikusaidii kuboresha maisha yako kabisa zaidi ya kukusababishia hasara ya kuendelea kuwa mtumwa wao.
SOMA; Lakini Nitapitwa.... (Sababu Ya Kijinga Inayokufanya Upoteze Muda)
6. Umbea na Majungu
Unapoteza muda kuongea maneno ya uchonganishi juu ya mtu Fulani unapiga umbea na majungu. Unaongea maneno ambayo yanaleta majeraha katika maisha ya watu, unapandikiza chuki kwa watu kwa kupiga majungu unapoteza muda wako bure kupiga umbea na majungu bila malipo yoyote ni hatari sana tumia muda wako kujenga na kuongea thamani yako katika jamii ya yako na acha kuwa mtu wa umbea na majungu kila siku.
7. Kuhudhuria Vikao au Mikutano Ambayo Haikupi Faida
Kuna vikao vingi sana katika jamii zetu, mikutano mingi ya kila siku ambayo haina matokeo chanya kwetu bali ni kupoteza wakati wako. Leo nakuomba sema HAPANA kwa vikao au mikutano ambayo haikupi faida yoyote ambavyo vinakula muda wako bure ambao muda huo ungeweza kutumia vizuri kuboresha maisha yako au hata kuongeza thamani katika jamii yako.
Hivyo basi, acha kutumia muda wako kudhurura ovyo yaani kutembea bila sababu ya msingi, tumia muda wako vema, muda ni mali katika karne hii usikubali mtu akupotezee muda kwa kitu ambacho hakina manufaa kwako fanya kile ambacho unatamani kufanya kwa muda huu katika Nyanja zote usisubiri ruhusa ukiendelea kusubiri ruhusa ndio unazidi kupoteza muda na umri pia unakwenda omba samahani kuokoa muda, Muda siyo rafiki na maisha ni mafupi .
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com
7/13/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Tabia Ya Mtu Ni Kama Kikohozi, Na Jinsi Ya Kujua Tabia Ya Mtu Kabla Hujamwamini.
Tabia ya mtu nzuri haiwezi kufunikwa na tabia mbaya hata kama utachukua muda kumwelewa lakini matendo yake na zungumza yake itakuonyesha huyu ni mtu wa namna gani, anaweza akajitahidi kuendana na kundi alilolikuta lakini utashangaa ikifika eneo fulani anaonekana sio mwenzao, naona hujanielewa ni hivi kama umepanda gari na askari wa usalama barabarani amevaa tu kiraia halafu dereva/konda akaanza kufanya upuuzi utamwona akinyanyua mdomo yeye mwenyewe kumkemea hata kama mtakemea wote lakini kemea yake itakuwa tofauti.
SOMA; Matatizo Yote Ya Mahusiano Yanaanzia Hapa... Sehemu Ya Pili(2)
Tabia ya mtu mbaya pia huwezi kuifunika kwa tabia nzuri, japo utaweza kufanya mbinu ya kuiweka vizuri mwisho wa yote utabaki kuonekana wewe sio mtu mzuri maana ubaya wa mtu haupo kwenye macho bali ndani ya moyo wa mtu ndipo zinapotoka takataka zote hata akifanya nini ukweli utabaki palepale, ndio maana wengi wanasema aisee fulani nilimwona ni mpole na anajituma lakini siku hizi amekuwa ana tabia mbaya sio amekuwa na tabia mbaya ni kitu kilichokuwa ndani yake na kama hakuwa nacho ujue uharibu umeanza muda mrefu ndani ya moyo wake sasa hayo unayoyaona ni matokeo tu ya matunda ya kile kilichoanza siku nyingi kabla mwingine hajakiona.
Ukiona mtu uliyemwamini amebadilika ghafla jua sio ghafla ni katabia chake sema alivaa tu kasura cha uzuri wa nje ila ndani kwake sura halisi ndio hiyo tabia unayoiona, ni sawa na rafiki yako umempa taarifa kuwa utamtembelea kwake leo au wiki ijao nakwambia hata kama ni mchafu kiasi gani siku hiyo lazima ajitahidi kufanya usafi wa hali ya juu iwe kwa kufanyiwa ama kufanya yeye lazima ahakikishe mgeni wake aone hayo ndio maisha anayoishi.
SOMA; Maisha Ni Mchezo Na Sheria Za Kuushinda.
Unapata picha gani hapa? wengi kumbe maisha wanayoishi hawayapendi ila hawataki kuyaacha wameng'ang'ana kuishi maisha ya kinyonga lakini tatizo lao limebaki palepale. Kwa hiyo tunaona unaweza kujizua kukohoa (kubanja) kutokana na mazingira uliopo ila mwisho wa saa bila wewe kujua utaachia tu kikohozi chako tena kwa kishindo kikubwa kuliko awali.
Sasa basi mtu usiyemjua yaani mmefahamiana naye muda mfupi usipende kumwamini asilimia zote hata mimi usijilazimishe kuniamini hata kama unaniona naandika maneno mengi mazuri hii isikufanye ukaniamini haraka nenda taratibu mpaka uhakikishe moyo wako umeniamini, ndio maana wengi wakitokewa na jambo baya kuhusu mtu aliyemwamini kwa haraka utasikia aisee moyo wangu ulikuwa unakataa kabisa nisimpe kitu fulani ama nisimwambie kitu fulani, hivi hujawahi kuona unamuulizia mtu fulani kwenye makazi yake ama kazini kwake unatajiwa na alivyo, mfano; aisee unamuulizia yule kijana mwizi mwizi sana wa vitu vya watu, unamuulizia yule dada anayetoa sana mimba au unamuulizia yule kaka anayetembea sana na wadada yaani huyo kaka malaya sana jana tu ameingia hapa na mabinti wawili tofauti tofauti wa tatu wamegongana na mwenzake wameleteana fujo kweli... yaani badala ya kuelekezwa unapewa shutuma zake.. hiyo tunasema huwezi kuzuia kikohozi kwa kukibana muda mrefu hata kama mtu atavaa sura ya ubaya kama sio mbaya itajulikana tu.
Mwisho nikuase kwamba usihangaike kumjua mtu wala kumfuatilia sana habari zake... zipo nje nje tu ndio maana ukimgusia tu kwa kumsifia kitu fulani watu wanaguna wanajua unachoongea hujui chochote.
Makala hii imeandikwa na Samson Ernest, waweza wasiliana nami kwa njia ya WhatsApp 0759808081, email; samsonaron0@gmail.com
Nakutakia siku njema yenye mafanikio makubwa kiroho na kimwili.
7/10/2015 08:04:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Una Nini Cha Tofauti Mpaka Watu Wakufuate Na Kukusikiliza? Jua Hapa.
Au kwa wanafunzi unapokuwa shuleni unakuta kuna mwenzio ana uwezo zaidi kwenye somo fulani hivyo unakuta mtu yule anategemewa na wengi na anaweza kuonekana kupendwa na wengi kwa kuwa anawasaidia wengi kuweza kufanya vizuri kwenye masomo anayowasaidia kuwafundisha ili waweze kuelewa zaidi, ukiangalia kwa kawaida unaweza ona kama yule mtu anapendwa na wengi, lakini ukiangalia zaidi utagundua pale hapendwi mtu bali kipo kitu cha thamani ambacho kinapendwa kwa mtu yule, kipo kitu watu wanakifuata kwa mtu yule ambacho pengine kwa wakati ule hakuna mahali pengine tena wataweza kupata kitu hicho, hivyo naweza sema wanakuwa hawana namna mbadala ya kupata huduma ile, wanalizimika kumkubali mtu yule hata kama hawampendi, wanalazimika kumsikiliza na wanakubali kufundishwa naye maana hakuna mwingine anaweza kufanya lile.
SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako Yote.
Pengine unaweza kukutana na mtu ukamshangaa na usimwelewe kwa kuwa anaambatana na mtu fulani, pengine wewe ukiangalia kwa macho yako ya kawaida unakuwa huioni thamani ya huyo mtu, huoni cha maana alichonacho cha kumfanya mtu mwingine asitake kuwa mbali naye, unajitahidi sana kukiona hicho lakini huoni, lakini wewe ukiwa katika hali hiyo kuna mwingine ameona thamani kwa huyo mtu, na anajua namna ya kuipata, hivyo anahakikisha anamtumia huyo mtu kuweza kupata kile mtu anacho, anamtumia yule mtu kuweza kufika pale anaelekea, usiishie kushangaa ni kwa nini mtu fulani anamkubali sana yule, usiwe mwepesi kumpuuza au kuona amepotoka wakati huelewi hasa ni kwa nini anafanya vile. Kama ukiwa mwelewa na mjanja mwenye nia ya kujifunza na kueleweshwa utatumia hekima na busara ili kuweza kuona kile mwenzio anaona kwa huyo mtu, utauliza na ukielekezwa uwe tayari kuheshimu hata mawazo ya wengine, uweze kuona thamani hata kwa wengine, hata kama wewe unadhani unajua kila kitu lakini tambua wapo wengine pia wanaoweza kuwa na uelewa kuliko wewe.
Wakati mwingine unaweza kukutana na mtu na ukamshangaa kwa nini anaambatana na mtu fulani maana wewe kwa viwango vyako na vipimo vyako unaona yule mtu si sahihi au hana sifa za kuweza kuwa na mtu yule na pengine unaweza kujaribu hata kumshawishi asiwe na mtu yule, pengine hata kwa kumweleza ni jinsi gani unaona hafai kwa kuelezea yale mabaya yake au madhaifu yake lakini cha ajabu unashangaa pamoja na hayo bado mtu yule anaendelea na msimamo wake wa kuambatana na mtu yule. Tambua yule ni mtu mwenye uelewa wa kutosha naamini ni yeye anaelewa ni kwa nini anaambatana na mtu yule, anajua ni kwa nini anashirikiana na mtu yule kwenye shughuli zake, yeye ndiye anajua ameona nini kwa mtu yule, pengine wewe huoni thamani kwa mtu yule, lakini yeye ameiona hiyo na hiyo ina nguvu kuliko sauti yako ya kumwaminisha kinyume, sauti yako anaona kama kelele tu, unatakiwa ujiulize unavyomwambia hayo wewe unaonekanaje kwa mtu huyo? Kwanini aamini unayosema? Una nini cha kukufanya aamini unachosema? Je una sababu za msingi za kuona yule mwingine hafai? Huyo ambaye hafai unamwelewaje? Unamfahamu sawasawa?
SOMA; Ushauri Kwa Waajiriwa Wapya Wote Wa Mwaka Wa Fedha 2014/2015
Tambua kuwa mtu yule yule unayemuona hafai , ipo sehemu anafaa sana kwa kuwa wale watu wameona kinachofaa au wameona thamani kwa mtu yule, huenda wamechagua kuiona thamani au mazingira yamewalazimisha kuona hivyo , maana hata kama hawamkubali au kumpenda lakini ndiye anayeweza jambo fulani ambalo wanalihitaji ili kuweza kufikia malengo yao katika maisha yao, hivyo wanalazimika kuwa na mtu yule, kumtumia mtu yule kama ngazi ya kufika kule. Kila mtu anaweza kumuona mtu yule yule kwa tofauti, inategemea kama una mtazamo gani juu ya wengine, kuwa na mtazamo chanya, tarajia kuona thamani hata kwa wengine, na ukiiona kama inakufaa itumie, usione aibu kusaidiwa hata na mtu unayeona hafai au hana hadhi ya kukusaidia au kukuelekeza jambo fulani, kumbuka Muumba wetu anaweza kumpa hata yule unayeona hafai thamani na ukalazimika kwenda kuhitaji huduma yake hata kama umemdharau sana, hata kama ulishaona hawezi kukuhudumia.
Katika maisha unavyoishi hebu jiulize una nini? Kwanini watu wakae chini wakusikilize? Unacho cha kuwasikilizisha? Kwanini niache wote nije kwako? Nitapata nini cha maana au cha tofauti?
Imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772
7/08/2015 08:18:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Hatua Saba (07) Muhimu Za Kukamilisha Malengo Yako Makubwa.
Hapa ninakuletea hatua saba zitakazokuwezesha kukamilisha lengo lolote ambalo unajiwekea
1. Amua ni nini hasa unakihitaji katika kila eneo la maisha yako. Unahitaji kufafanua lengo lako katika lugha rahisi kiasi kwamba mtoto mdogo aweze kuelewa. Mfano unaweza kusema lengo lako ni kuwa na fedha nyingi, lakini uwingi wa fedha unazotaka haujaweka ni fedha nyingi kiasi gani. Sasa kutokuwa fasaha katika lengo kunakupelekea kutokuwa na hamasa na kufanya maamuzi ya kukamilisha lengo.
2. Andika lengo lako na lifanye liwe linaweza kupimika. Lengo ambalo halijaandikwa linakuwa ni lengo ambalo halijahuishwa au halijapewa nguvu ya kuwa hai. Ukilifanya lipimike maanake unakuwa umetengeneza tageti unayotaka kuifikia.
SOMA; Jinsi Ya Kutengeneza Kipato Cha Ziada Ukiwa Unaendelea Kufanya Unachofanya Sasa.
3. Weka ukomo wa kukamilisha. Unahitaji kuwa fasaha ni lini unahitaji kukamilisha lengo husika. Sehemu ya ubongo inayoitwa “subconscious” inapenda kuwa na ukomo na hii inakusaidia kuwa na nguvu na kukupa hamasa ya kuelekea kufanikisha lengo husika
4. Ainisha vikwazo ambavyo unahitaji kuvivuka ili kukamilisha lengo. Fahamu kitu gani kinaweza kwenda tofauti. Fahamu ni kitu gani kipo kati yako na lengo. Fahamu kwa nini bado haupo katika lengo lako.
5. Tambua maarifa na ujuzi wa ziada ambao utahitaji ili kuweza kufikia lengo lako. Ili kuweza kufanikiwa kukamilisha malengo ambayo hujawahi kuyakamilisha hapo kabla unahitaji kujifunza na kuwafanya vitu vya tofauti ambavyo hujawahi kufanya kabla.
6. Watambue watu ambao utawahitaji wakusaidie au waungane nawe ili uweze kufikia malengo yako. Kufikia malengo makubwa unahitaji kuwa natimu ya watu wengi wa kukusaidia. Kwa hiyo unahitaji kuwa na ufasaha ni watu wa aina gani hasa unaowahitaji ili uweze kuwa na timu ambayo itakupa msaada unaouhitaji.
7. Tengeneza orodha ya maelezo kwa kila kipengele ambavyo nimeanisha hapo juu na uweke mpangilio katika mfuatano yaani kipi kinaanza na kipi kinafuata na pia ni muhimu kuwa na kipaumbele. Ni muhimu kujua kipi unahitaji kwanza, kipi ni muhimu.
Baada ya kukamilisha hatua hizo saba ni muhimu kufanya kila siku japo kwa udogo sehemu ya kufikia lengo lako.
Mwandishi: Goodluck Moshi
Mawasiliano:
Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi
Pia unaweza kutembelea blog yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.
7/02/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Kabla Hujakubali Kila Unachoambiwa, Kumbuka Jambo Hili Moja Muhimu Sana.
SOMA; Jinsi Ya Kujua Kama Unachofanya Ni Sahihi Katika Maisha Yako.
Tukiangalia katika wakati tulionao wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna vitu vingi vizuri sana tu lakini vipo na vibaya vilivyokuja na hii teknolojia, Hivyo kwa sababu hizo nilizosema mwingine anaweza kuona kuwa kukua kwa teknolojia kuna madhara sana, hakufai, mfano huu utandawazi wengi wanauona kama jambo baya lisilofaa kabisa, na wengi wanatumia nguvu nyingi sana kujaribu kufanya kila mtu aone kuwa ni kitu kisichofaa kwa jamii, na wanaposema hivi wana sababu za msingi za kuamini wanavyoamini, maana kuna mambo mengi yasiyofaa yanaendelea mitandaoni, watu wanaiga mambo yasiyofaa humo na hata maadili ya jamii yanamomonyoka, lakini kwa kuwa tu wapo wanaoona hivyo haimaanishi kwamba ni kweli utandawazi ni mbaya na hauna faida, zipo faida nyingi tu za utandawazi ikiwa utautumia vizuri unaweza kunufaika sana tu. Wapo watu wengi wamefaidika sana na mitandao hii ya kijamii kwa kukutana na watu wapya ambao wamewafundisha vitu vingi, watu wamenufaika kiroho na hata kijamii kwa namna ambavyo wametumia mitandao hii ya kijamii, maana kupitia hii hauhitaji kuonana na mtu ili muweze kufundishana au hata kujadilia baadhi ya mambo, pia inasaidia hata kutunza muda na hata gharama za kukutana au kumfuata mtu mahali fulani kwa ajili ya majadiliano, naweza kuwa hospitali, barabarani na nikasoma vizuri au hata kuhudhuria mafundisho au hata ibada bila shida kabisa.
SOMA; Kuna Watu Hawa Ambao Hawawezi Kukuelewa, Wajue Na Waepuke Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
Pia katika maisha haya iwe kazini , nyumbani au popote ulipo unaweza kukutana na mtu akakuambia kuwa mtu fulani ni mbaya sana au ana sifa hizi na hizi na pengine akakupa mabaya tu ya huyo mtu, akajitahidi kukuelezea na kukufanya umuone mtu huyo hafai kabisa katika jamii, au hafai kuwa rafiki yako kabisa na pengine si mtu hata wa kufanya naye biashara n.k, Sasa hapo ni wajibu wako wewe kama mtu unayejielewa na kuelewa kuwa sisi binadamu hatupo kama watu wanavyosema tupo, au kwa kuwa fulani ameniona mimi sifai au mimi ni mzuri haimaanishi kwamba kila mtu ataniona hivyo, hivyo hata kama umeambiwa nini kuhusu mtu fulani hebu usiende kwake ukiwa na hiyo picha uliyopewa, bali amua kuona mwenyewe kama kweli yupo kama ulivyoambiwa au yuko tofauti na vile, maana ukienda kwa namna ulivyoambiwa unaweza kujikosesha fursa nyingi sana kwa ujinga wako wa kutotumia akili na maarifa uliyopewa na Muumba wako, mtu mwingine anaweza kukuambia mtu fulani yupo hivi kwa kuwa tu ana chuki na huyo mtu au pengine hata hamjui huyo mtu, au alisikia tu watu wakisema hivyo lakini hajathibitisha mwenyewe
Tambua kuwa hatuwezi wote kuona jambo lilelile sawasawa maana kila mtu ni wa pekee, hivyo ni vyema kuheshimu mtazamo wa kila mtu lakini usiutumie mtazamo wa mwingine kama ndio mamlaka ya mwisho ya wewe kuona. Hivyo hata kama umeambiwa kitu fulani hakifai hakikisha kuwa unatumia akili zako na utashi wako kufanya uchunguzi kuona kama kweli kitu hiki kipo kama unavyoambiwa kipo, ni muhimu kutambua kuwa binadamu tunaona vitu vilevile kwa tofauti, ndio maana kuna mtu ni mzuri kwangu lakini wewe waweza kumuona mbaya au hafai kwa kuwa kila mtu ana vigezo vyake vinavyomfanya aone anavyoona, usiishi kwa kufanya yale uliyoambiwa bali ishi kama vile unavyotakiwa kuishi na Muumba wako, umuone kila mtu kuwa bora, mwenye uwezo wa kufanya jambo la maana maishani, usimkadirie mtu kwa kusikia maneno ya kuambiwa kamwe maishani.
Imeandika na Beatrice Mwaijengo
Mobile number: +255755350772
7/01/2015 07:41:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Maisha Ni Safari Na Jinsi Unavyoweza Kufika Salama Safari Hii.
Maisha ni safari. Sio mara ya kwanza kuusikia usemi huu. Naomba leo nikupe mtazamo mwingine kuhusu usemi huu.
Siku za hivi karibuni nilikua nasafiri safari ndefu kiasi. Safari yangu ilikuwa ni ya kutoka Kigoma kuelekea Dodoma lakini nilipanda magari yanayoenda mpaka Dar-es-salaam. Nilivyoingia kwenye gari tu saa kumi na mbili asubuhi baada ya dakika chache nilipitiwa na usingizi. Baada ya muda nilishtuka na nikaona asilimia kubwa ya abiria wakiwa wamesinzia. Baada ya mwendo mrefu sana kama masaa saba nilihisi kuchoka tena nikasinzia.
Nilipoamka kama kawaida kuna baadhi ya abiria walikua wamesinzia, wengine walikua wanasimama na kukaa ili kupunguza uchovu waliokuwa nao. Makondakta wa gari walifanya hivyo pia. Kuna wakati walikua wakirudi kwenye viti vya mwisho wa basi wanalala kidogo halafu baada ya muda wanaenda tena mbele kuongea na dereva.
SOMA; Najua Umeshasikia Hili Mara Nyingi, Sio Vibaya Ukasikia Tena Na Leo.
Safari hii ilikuwa ndefu na ilimchosha kila mmoja aliyekua ndani ya basi. Hata bila kuuliza unagundua kuwa kila mtu amechoka. Abiria wengi walikua wamekunja sura zao wakijigeuza upande huu na upande ule, hayo yote yaliashiria uchovu waliokuwa nao.
Lakini cha ajabu, wakati wote huo dereva alikua halali wala hapumziki. Nilifikiria kwa muda jinsi ambavyo dereva alivumilia. Dereva katika akili yake alikua akifikiria furaha ya kutufikisha salama kule tulikokua tunaelekea. Sisi tulipokua tunalala bado yeye hakuwaza kuhusu usingizi na kuona kama sisi tunafaidi. Kama ingekuwa hivyo angetuamsha wote ili anapokuwa akiendesha gari na sisi tusilale kama yeye ambavyo halali. Lakini basi achana na sisi abiria, hata makondakta wa gari hilo nao walikua wakipumzika. Lakini dereva hakujali kwakua alikua akifahamu lengo lake lilikua ni kuendesha gari na kutufikisha kule tunakokwenda salama. Akikutana na vikwazo ajue jinsi ya kuvikwepa bila kushauriwa na mtu yeyote pembeni, lengo kuu ni kutufikisha salama kule tuendako.
Yaani kwa kifupi dereva yeye aliangalia lengo ambalo ni kusafirisha abiria na kuwafikisha salama kule wanakoenda .
Tunajifunza nini?
Ni vizuri kuwa dereva wa gari linaloitwa maisha yako. Ukiona unasinzia, unataka upumzike, unaangalia kama wengine wamepumzika, unawalazimisha wengine wakusaidie kuendesha gari lako ambalo ni maisha yako, unategemea maoni ya wengine ili ulifikishe gari lako salama ujue kuwa upo kwenye hatari ya kusababisha ajali ya maisha yako. Kama ambavyo kuna kanuni na sheria za barabarani ndivyo ambavyo kuna kanuni mbalimbali katika maisha ya kila siku.
Dereva alikua akiongea na kondakta na mara nyingine abiria , lakini pia trafiki aliokuwa akionana nao njiani. Lakini nia yake, lengo lake lilikua ni kufika alikokua amepanga kwenda ambako alikuwa anakufahamu. Hakuna aliyeweza kumtoa nje ya kusudio lake. Pale alipokutana na vikwazo alivuka vikwazo hivyo yeye mwenyewe bila kutegemea msaada wa mtu yeyote Yule. Gari lilipoharibika, fundi alilirekebisha lakini bado yeye alibaki kuwa dereva.
SOMA; Uadilifu, Kioungo Muhimu Cha Kufikia Mafanikio.
Ni vyema kuwa imara na wenye malengo yasiyoyumbishwa kama dereva huyu. Katika safari hii ya maisha utahitaji mawazo, msaada kutoka kwa wengine, utakutana na vikwazo na mambo mengine mengi njiani. Lakini haya yote yasikutoe nje ya malengo yako uliyonayo. Hakikisha wewe ndiye unayeshikilia usukani wa maisha yako kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari yako ili uweze kufurahia pale unapokuwa umefikia malengo yako na sio malengo ya wengine.
Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110
Whatsaap: 0652 025244
Face book: ESTHER ESTHER
estherngulwa87@gmail.com
6/26/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAFANIKIO, MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Jinsi Ya Kujua Kama Unachofanya Ni Sahihi Katika Maisha Yako.
Kila mtu anapokuja hapa ulimwenguni anakuwa amebeba maagizo maalum ambayo anatakiwa ayatekeleze kwa ajili ya kufanya ulimwengu kuwa sehemu bora ya kuishi. Njia nzuri ya kuweza kujua kile unachofanya kama ni sahihi ni kwa kuyafahamu maagizo uliyobeba ambayo hakuna mwingine zaidi yake anaweza kuyatekeleza. Na maagizo hayo unaweza kuyafahamu kwa kuanza kujitathimini kwa njia ya maswali kama je umeshatambua maagizo uliyoyabeba? Au je una kipaji, uwezo, shauku gani ambayo ni ya kipekee kwako na hakuna mtu mwingine wa aina yoyote anayo isipokuwa wewe tu? Au ya mwisho ambayo ni nzuri zaidi ni kwa kuangalia kile unachokifanya na kujiuliza je unachokifanya ndicho ulichokusudiwa au sababu ya wewe kuwepo hapa ulimwenguni?
Hapa ninakuletea viashiria ambavyo vitakusaidia kujitathmini kama kwanza upo katika kada au eneo sahihi lakini la muhimu zaidi ni lile unalofanya katika hilo eneo ndilo lile unalopaswa au sababu ya wewe kuwepo hapa ulimwenguni.
1. Unakuwa unapenda kile unachokifanya kwa kuwa kinakuvutia , kinakupa shauku na mvuto wa kipekee kukifanya
2. Unakuwa unataka kuwa bora sana katika kile unachokifanya. Na miongoni mwa asilimia kumi ya watu walio bora katika eneo au kada yako unataka na wewe uwepo
3. Unawapenda wale wote ambao wako katika eneo au kada uliyopo na pia unapenda kufikia mafanikio ambayo wao pia wameyafikia
4. Unapenda kujifunza kuhusiana na hilo eneo au kada yako kwa kusoma mambo yanayohusu kada yako, kuhudhuria semina au mihadhara ambayo inazungumzia mambo yanayohusu eneo au kada yako, kusikiliza program za sauti zilizorekodiwa kuhusiana na kada yako. Na zaidi hata iweje unakuwa huchoki kujifunza katika hilo eneo lako.
5. Kada au eneo sahihi kwako ni lile ambalo kwako ni rahisi kujifunza na pia ni rahisi kuweka katika matendo yale uliyojifunza. Ila kwa wengine inaonekana ni vigumu na kwako inakuwa kawaida sana kufanya.
SOMA; Haijalishi Umeshindwa Mara Ngapi…
6. Kutokana na kufurahia kile unachofanya unakuta muda unakuwa kama umesimama kwako na inaweza ikawa imekukolea sana hadi unasahau kula, kunywa hata kwenda mapumziko7. Mafanikio unayoyapata katika eneo ndiyo inayokupa hamasa ya kipekee na furaha adimu. Na pia unakuwa huwezi kuacha kusubiri au kukaa muda mrefu bila kufanya kitu kikusogeze hatua moja mbele upate mafanikio mengine
8. Unapenda kufikiri kuhusu hilo eneo au kada yako na pia wakati haufanyi kitu unapenda kuzungumza kuhusu eneo au kada yako. Maisha yako yote yanakuwa yamezungukwa na mambo yanayohusu eneo au kada yako
9. Unapenda kuwa na mahusiano na kuwa karibu na watu zaidi ambao wapo katika eneo lako.
10. Na mwisho ni kuwa unapenda kufanya hayo unayofanya kwa maisha yako yote, hutaki kustaafu kuyafanya kwa kuwa unafurahia jinsi unavyoyafanya
Kwa kuweza kutambua eneo au kada yako sahihi ambayo unatakiwa uwe itakusaidia kupata mafanikio na hii itakusaidia kuelekeza moyo wako kufanya vizuri na vizuri zaidi.
Mwandishi: Goodluck Moshi
Mawasiliano:
Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi
Pia unaweza kutembelea blog yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.
6/25/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Kuna Watu Hawa Ambao Hawawezi Kukuelewa, Wajue Na Waepuke Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
Unaweza kukutana na mtu anakuuliza kwa nini unafanya hiyo kazi wakati wanaoweza kufanya au wanaoonekana kuifanya ni wa aina fulani tu au wana sifa fulani na wewe hauna sifa hizo? Hivyo wanashindwa kukuelewa kabisa na hata ukijitahidi kuwaeleza hauwezi kueleweka kwao, maana wamechagua kuona hivyo, japo wapo baadhi wanaweza kukuelewa kwa kadri unavyozidi endelea. Kuna mtu mwingine anajua na amekariri kuwa shughuli fulani hufaa kufanywa na watu wa aina fulani tu kwa kuwa ndivyo alivyoambiwa na kuaminishwa hivyo. Na yeye akakubali kuamini hayo, hadhani kama anaweza kukutana na mtu anayeweza kumfanya aone alichoaminishwa siyo kweli, pia na yeye hayuko tayari kupokea taarifa iliyo kinyume na hiyo, hataki kubadili namna anavyotazama jambo hilo, kaamua hivyo ni ngumu kumbadili mtazamo huo maana yeye ndiye mwenye uamuzi wa kuamua kubadili anavyotazama mambo.
SOMA; Tatizo La Kuweka Kinyongo...
Kuna mwingine anaweza akaamua kukuangalia kwa jinsi alivyokuona jana au anaweza akaamua kushikilia jana yako na hata akionana na wewe leo anakataa kukuona wewe wa leo, yeye kamshikilia yule yule. Akili yake na ufahamu wake vimebaki kwenye jana yako na historia yako, hivyo hata akiona unafanya kitu kingine tofauti na kile alikuona ukifanya anaona kuwa hauwezi, hawi tayari hata kukupa nafasi ya kufanya hicho kitu bali yeye anatoa uamuzi na hukumu kwa kuangalia jana yako. Kuna mwingine labda anajua mambo yako mabaya tu hivyo leo akiona unafanya mazuri na akaona watu wakikubali kile unafanya bado yeye atahakikisha anawaambia watu vile ulivyokua jana ili waweze badili wanavyokuona leo, na akikutana na watu ambao hawajielewi ni rahisi kuwabadili lakini akikutana na mtu mwenye kuelewa kuwa jana yako haiwezi kuwa leo, atampuuza tu na kuendelea kukuona anavyokuona leo. Na mara nyingi watu wengi wamekuwa wakivutwa chini na watu walioamua kuwaona kama walivyokuwa jana, walioshindwa kukubali na mtu wanayemuona leo, na wanajitahidi hata kuwashawishi watu wengi waamini wakuhukumu leo kwa ile jana yako. Kwa dunia yetu wengi ni wepesi wa kuamini vile ulivyokuwa jana kuliko ulivyo leo, mtu anaweza kukubali aliyoambia kuhusu jana yako leo, kuliko wewe anayekuona leo, anaamua na kuchagua kukuona hivyo, inachukua muda watu hawa kuja kukuelewa.
Kitu cha msingi katika maisha haya ni vyema kuishi vile ulivyo leo, usiishi ili kuwafanya watu fulani wakukubali au kukuelewa, ishi wewe ulivyo leo hata kama wapo wengi wanaokuona kivingine au walioshikilia jana yako, usiwaangalie hao, bali wewe endelea kuishi maisha yako, kufanya yale unayafanya kwa usahihi ili mradi haumkosei muumba wako na wala hauvunji sheria za nchi, maana ni ngumu kubadili watu wanavyokuona na kukutafsiri lakini ikiwa unaishi uhalisia wako, hauigizi , watakuelewa tu hata kama ni baada ya muda mrefu.
Imeandika na Beatrice Mwaijengo
Mobile number: +255755350772
6/24/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Usimtafute Mtu Mwaminifu Bali Kuwa Mwaminifu Wewe, Wengine Watajifunza Kwako.
6/17/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Njia Nne Za Kuishi Na Watu Vizuri.
6/16/2015 07:30:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
