Kuna Watu Hawa Ambao Hawawezi Kukuelewa, Wajue Na Waepuke Ili Uweze Kufikia Mafanikio.

Ni kawaida kuona watu wakikushangaa kwa kuwa unafanya hicho unachokifanya maana wanakuwa hawakuelewi. Hawaoni kwa nini unafanya hicho kitu, wanakosa sababu ya msingi ya kuwafanya wakuelewe kwa wewe kushikilia hicho kitu. Wakati mwingine hata wewe unaweza kuwa unawashangaa kwa nini hawakuelewi, hivyo unakuta wote wawili hamuelewani kwa kuwa hamuoni kitu kilekile sawasawa.
Unaweza kukutana na mtu anakuuliza kwa nini unafanya hiyo kazi wakati wanaoweza kufanya au wanaoonekana kuifanya ni wa aina fulani tu au wana sifa fulani na wewe hauna sifa hizo? Hivyo wanashindwa kukuelewa kabisa na hata ukijitahidi kuwaeleza hauwezi kueleweka kwao, maana wamechagua kuona hivyo, japo wapo baadhi wanaweza kukuelewa kwa kadri unavyozidi endelea. Kuna mtu mwingine anajua na amekariri kuwa shughuli fulani hufaa kufanywa na watu wa aina fulani tu kwa kuwa ndivyo alivyoambiwa na kuaminishwa hivyo. Na yeye akakubali kuamini hayo, hadhani kama anaweza kukutana na mtu anayeweza kumfanya aone alichoaminishwa siyo kweli, pia na yeye hayuko tayari kupokea taarifa iliyo kinyume na hiyo, hataki kubadili namna anavyotazama jambo hilo, kaamua hivyo ni ngumu kumbadili mtazamo huo maana yeye ndiye mwenye uamuzi wa kuamua kubadili anavyotazama mambo.
SOMA;  Tatizo La Kuweka Kinyongo...
Kuna mwingine anaweza akaamua kukuangalia kwa jinsi alivyokuona jana au anaweza akaamua kushikilia jana yako na hata akionana na wewe leo anakataa kukuona wewe wa leo, yeye kamshikilia yule yule. Akili yake na ufahamu wake vimebaki kwenye jana yako na historia yako, hivyo hata akiona unafanya kitu kingine tofauti na kile alikuona ukifanya anaona kuwa hauwezi, hawi tayari hata kukupa nafasi ya kufanya hicho kitu bali yeye anatoa uamuzi na hukumu kwa kuangalia jana yako. Kuna mwingine labda anajua mambo yako mabaya tu hivyo leo akiona unafanya mazuri na akaona watu wakikubali kile unafanya bado yeye atahakikisha anawaambia watu vile ulivyokua jana ili waweze badili wanavyokuona leo, na akikutana na watu ambao hawajielewi ni rahisi kuwabadili lakini akikutana na mtu mwenye kuelewa kuwa jana yako haiwezi kuwa leo, atampuuza tu na kuendelea kukuona anavyokuona leo. Na mara nyingi watu wengi wamekuwa wakivutwa chini na watu walioamua kuwaona kama walivyokuwa jana, walioshindwa kukubali na mtu wanayemuona leo, na wanajitahidi hata kuwashawishi watu wengi waamini wakuhukumu leo kwa ile jana yako. Kwa dunia yetu wengi ni wepesi wa kuamini vile ulivyokuwa jana kuliko ulivyo leo, mtu anaweza kukubali aliyoambia kuhusu jana yako leo, kuliko wewe anayekuona leo, anaamua na kuchagua kukuona hivyo, inachukua muda watu hawa kuja kukuelewa.
Kitu cha msingi katika maisha haya ni vyema kuishi vile ulivyo leo, usiishi ili kuwafanya watu fulani wakukubali au kukuelewa, ishi wewe ulivyo leo hata kama wapo wengi wanaokuona kivingine au walioshikilia jana yako, usiwaangalie hao, bali wewe endelea kuishi maisha yako, kufanya yale unayafanya kwa usahihi ili mradi haumkosei muumba wako na wala hauvunji sheria za nchi, maana ni ngumu kubadili watu wanavyokuona na kukutafsiri lakini ikiwa unaishi uhalisia wako, hauigizi , watakuelewa tu hata kama ni baada ya muda mrefu.
Imeandika na Beatrice Mwaijengo
Mobile number: +255755350772

0 comments: