Tabia Hizi Zitakusaidia Sana Kufikia Malengo Yako Kwa Haraka - 2

Habari ndugu msomaji wa mtandao huu wa JIONGEZE UFAHAMU. Nina imani ulikua na wiki nzuri. Karibu tena kwenye sehemu hii ya pili ya makala inayokukumbusha juu ya tabia zitakazokusaidia kufikia malengo yako kwa haraka. Wiki iliyopita tuliangalia baadhi ya tabia hizo na wiki hii tutamalizia tabia zilizobaki.

Kama hukusoma makala ya wiki iliyopita unaweza kuisoma hapa; Tabia Hizi Zitakusaidia Sana Kufikia Malengo Yako Kwa Haraka.

5. Heshimu kila mtu.

Usimdharau mtu yeyote unayekutana naye, iwe unamfahamu au haumfahamu. Inawezekana mtu huyo ni njia ya wewe kutimiza malengo yako. Katika utamaduni wa kiafrika heshima ni tabia njema, muheshimu mtu yeyote hata mwenye kipato kidogo kiasi gani. Kila mtu anamchango fulani katika maisha yako ambao kwa namna moja au nyingine mchango huo unakusaidia wewe kukamilisha ndoto zako, kama wewe pia ulivyo na mchango katika kutimiza ndoto za wengine. Iwe ni mfanya usafi, mvulana au msichana wa kazi, mbeba mizigo n.k

SOMA; BIASHARA LEO; Lengo La Biashara Sio Kupata Faida, Bali Ni Hili Hapa.

6. Jenga mahusiano mazuri na watu wote.

Kuna kitu kipya cha kujifunza kwa kila mtu unayekutana naye, iwe unamfahamu au haumfahamu. Watu ni rasilimali muhimu sana katika kufikia malengo yetu. Mtu unayekutana naye anaweza kuwa mteja, mshauri wako katika jambo fulani, unaweza kumtumia mtu kama msaada wa nguvu kazi au mtu anaweza kukupa msaada wa kifedha. Ona kila mtu anavyoweza kukusaidia kufikia malengo yako huku ukitoa msaada kwa wengine ili nao pia wafikie malengo yao.

7. Tafuta rafiki mwenye malengo yanayofanana na yako.

Waswahili wanasema “ndege wenye mbawa zinazofanana huruka pamoja

Ni rahisi kufikia malengo kama utakaa na watu wenye ndoto na muelekeo kama ulionao. Ni rahisi kusaidiana na kutiana nguvu ili kukamilisha malengo yenu kama wote mnaelekea njia moja. Pia kuwa na marafiki waliofanikiwa katika jambo ambalo nawe pia unatamani kufanisha, hao watakusaidia sana kukupa mbinu za kufikia mafanikio katika lengo lako.

SOMA; NENO LA LEO; Hiki Ndio Chanzo Cha Wivu.

8. Jitahidi kuishi maisha yako na sio kuiga maisha ya wengine.

Waswahili wanasema “miluzi mingi humpoteza mbwa”.

Kila binadamu amepangiwa maisha yake na Mungu na maisha yake hayo hayafanani na maisha ya mtu mwingine yeyote. Usikubali kuishi kama fulani anavyotaka uishi, kumbuka kuwa hakuna anayefanana na wewe zaidi ya wewe mwenyewe. Kutaka kuwa kama fulani, au kuishi namna fulani ili umfurahishe mtu mwingine kutakufanya uumie na wakati mwingine kutofikia viwango ambavyo Mungu amepanga wewe ufikie. Kutamani kwa uzuri maisha ya mwingine ni jambo zuri lakini sio kujaribu kuiga kila kitu chake. Wewe ni wa pekee vile ulivyo. Kubali na fanya mambo yatakayokusaidia kutimiza malengo yako na si malengo ya watu wanaokuzunguka.

SOMA; Utashi, kitu muhimu kwako kufikia mafanikio.

9. Jitahidi kuwa na furaha kila wakati, jivishe tabasamu usoni pako.

clip_image002

Mambo mengi tunayoyafanya vizuri huwa yanafanyika wakati tukiwa na furaha na utulivu wa akili. Hatufanyi vitu vizuri tunapokuwa na chuki,kinyongo na huzuni. Jitahidi kuwa na furaha kila wakati. Epukana na msongo wa mawazo. Ukiwa na akili iliyotulia nirahisi kuona fursa zitakazokusaidia kufikia malengo yako.

Nakutakia maisha yenye furaha.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110/ 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

0 comments: