Hivi Ndivyo Utakoweza Kuishi Na Mtu Wa Aina Yoyote Ile Kwa Furaha Na Amani - 2
Karibu tena kwenye mwendelezo wa makala hii . Kama haukusoma makala iliyopita unaweza kusoma kwa kubonyeza maandishi haya; Hivi Ndivyo Utakoweza Kuishi Na Mtu Wa Aina Yoyote Ile Kwa Furaha Na Amani
1. Sio kila wakati utakua sahihi.
Tambua kuwa sio kila wakati utakua sahihi. Kuna nyakati unaweza kukosea na usitambue kuwa umekosea. Sikiliza maoni ya wengine na ushauri wao pia. Maisha ni kujifunza, tunajifunza kila kukicha kutokana na matukio na kutoka kwa watu mbalimbali wanaotuzunguka. Ili kubadilika na kukua ni vizuri kukubali kwamba sio lazima kila wakati tuwe sahihi. Kuna wakati mwingine tunakosea na wanaotuzunguka wanaweza kutushauri na tunatakiwa kufanya maboresho katika maeneo husika.
2. Waza juu ya mambo mazuri kuhusu wengine.
Fikiri juu ya mambo mazuri kuhusu wengine. Wawazie mema watu wengine, usiwaze mabaya juu yao. Ukiwaza kuwatendea vizuri wengine basi utawatendea hivyo. Ukiwaza vibaya ni lazima utawatendea vibaya.
Hata kama wale wanaokuzunguka wanakutendea vile usivyopenda, usiwawazie mabaya. Endelea kuwatendea na kuwawazia mazuri. Kama kila mmoja angefanya hivi basi sisi sote tungeishi kwa amani. Anza wewe kufanya hivi na ulete mabadiliko mahali ulipo.
SOMA; BIASHARA LEO; Usianze Biashara Upya Kila Siku…
3. Usiingilie kati mwingine aongeapo.
Jitahidi kuwa msikivu wakati mtu mwingine aongeapo na wewe. Subiri mwenzio aongee mpaka mwisho ndipo umjibu. Kuingilia kati mtu mwingine aongeapo ni dalili ya kudharau kile anachoongea na kuona kuwa yale unayotaka kuongea wewe ndiyo ya maana zaidi. Lakini hii pia ni dalili kuwa haumsikilizi ila kuna vitu unawaza kichwani mwako kwa wakati huo huo.
Kama mtu anakuambia kitu ukamwingilia kwa kumalizia sentensi yake na yeye hakutaka kuimalizia kama hivyo ulivyoimalizia, unamnyima mnyima mtu huyo nguvu ya kuendelea kuongea na wewe tena. Hivyo unaweza kukuta watu wengi hawapendi kukaa na kuongea na wewe kwakuwa kila mara wewe hupenda kuwa muongeaji mkuu.
4. Jifunze kuwa na huruma, kusamehe na kuomba msamaha.
Katika maisha ya kila siku mambo mbalimbali hutokea ikiwemo kuudhiwa na watu wengine. Ni vizuri kuwa na huruma , kuwahurumia wanaotukosea na kuwasamehe pia. Kwakuwa kama mtu akikukosea na ukakasirika anayebaki na maumivu ni wewe na si mkosaji. Hivyo kwa usalama wako mwenyewe ni bora kuamua kusamehe na kuendelea na maisha yako ya furaha.
Lakini pia ni vizuri kuomba msamaha pale tunapokosea. Kuomba msamaha haimaanishi kuwa umejidhalilisha kwa mtu uliyemuomba msamaha ila ni ishara kuwa hukupenda kufanya jambo ulilolifanya na ungependa yule uliyemfanyia aliachie na muendelee na maisha ya amani na furaha kama hapo awali.
SOMA; Mambo 20 niliyojifunza Kwenye Kitabu LITTLE BETS.
5. Usiwe mtu wa lawama.
Usiwalaumu wengine kwa kila baya linalotokea. Kwa kuwa na lawama utajikuta ukigombana na kila mtu anayekuzunguka. Chukua jukumu kwa vitu ambavyo havikwenda sawa na uangalie ni nini haukukamilisha au haukukifanya kilichosababisha kwa namna moja au nyingine mambo kwenda tofauti na ulivyotarajia. Ukiwalaumu wengine huwezi kubadilika , huwezi kukua na huwezi kufanya marekebisho pale ulipokosea.
6. Kumbuka kuwa chanzo cha furaha yako ni wewe mwenyewe.
Usisahau kuwa wewe mwenyewe ndiye mwenye jukumu la kujipa furaha na sio mtu mwingine yeyote au kitu chohote kile. Ukishakua na furaha basi ni rahisi hata watu wanaokuzunguka kuendelea kuidumisha furaha yako na hata wakifanya kinyume na hivyo basi endelea kuwa na mtazamo chanya ndani yako na utaweza kuitunza furaha uliyonayo.
SOMA; Njia Rahisi Ya Wewe Kuondokana Na Tabia Usiyoipenda.
7. Usipende kuongelea habari za wengine.
Jitahidi usikae kati ya watu na kuanza kumjadili mtu mwingine na kumzungumzia mambo mabaya. Fanya shughuli zako ukimaliza soma, sikiliza kanda nzuri zinazojenga. Ongea na watu kuhusu mambo ya maendeleo na vitu vitakavyokufanya ukue. Kujiepusha na kuongelea mambo ya watu kutakuweka mbali na chuki na ugomvi na watu wengine.
Kumbuka kua ulimwengu huu unachangamoto nyingi. Zipo kila sehemu, hakuna mahali utakapokwenda kuishi ambapo kutakuwa hakuna changamoto. Hivyo ni vizuri kuwa makini na kujifunza kuishi na watu vizuri ili uweze kukamilisha majukumu yako ya kila siku na kufikia malengo ya maisha uliyojiwekea. Maisha ni mtihani ni vizuri kutafuta ujuzi kila siku wa namna ya kufaulu mtihani huu.
Nakutakia utekelezaji mwema wa haya uliyojifunza.
Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110
5/15/2015 07:30:00 AM
|
Labels:
MBINU ZA MAISHA
|
This entry was posted on 5/15/2015 07:30:00 AM
and is filed under
MBINU ZA MAISHA
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
0 comments:
Post a Comment