Hivi Ndivyo Utakoweza Kuishi Na Mtu Wa Aina Yoyote Ile Kwa Furaha Na Amani

Mara nyingi tumekuwa tukiwalaumu watu wanaotuzunguka kuwa wao ndio chanzo cha sisi kutoishi kwa furaha na amani na kwamba watu hawa ni chanzo cha sisi kutofikia mafanikio yetu. Wakati mwingine unaona watu waliopo katika mtaa, ofisi au nyumba unayoishi ni wabaya mno hata unatamani kwenda kuishi mahali pengine ukiwa na imani kuwa watu utakaowakuta huko watakua wa tofauti na kufanya maisha yawe rahisi.

Lakini ukweli ni kwamba kubadili mazingira au eneo ulipo sio suluhisho. Suluhisho ni kubadili namna unavyochukulia mambo. Kubadilika wewe kwanza kwakua hauwezi kumbadili mtu mwingine kama yeye hajaamua kubadilika. Sisi wenyewe ndiyo wenye jukumu la kuleta furaha na kuleta uwezekano wa ama kufikia au kutofikia mafanikio tuliyojiwekea.

SOMA; Ukiwa Na Kitu Hiki Ni Mwanzo Mzuri Wa Kufanikiwa Katika Uwekezaji.

Tunaweza kuamua kuishi kwa amani au kuishi kwa majuto na kuwalaumu wengine kwa kutofanikiwa kwetu. Kwa kulalamika hatuwezi kuleta tofauti yoyote ile zaidi ya kuendelea kuumia na kuwaona wengine wabaya.

Sasa ufanye nini ili kuhakikisha mambo yanakwenda kama ulivyopangilia na kuzuia mtu yeyote asikutoe nje ya mstari? Mambo haya hapa chini yatakusaidia sana kukufikisha mahali pazuri na utaishi vizuri na mtu yeyote Yule.

1. KUWA MSIKIVU.

clip_image001

Jitahidi kuwa msikilizaji badala ya kuwa mwongeaji. Ukiongea sana unaweza ongea vitu ambavyo si vizuri na kuwafanya watu wengine kujihisi vibaya na ukasababisha ugomvi au chuki. Kumbuka kuwa ukiongea kitu mtu anakiweka kichwani na haiwezekani kukifuta kichwani mwake tena. Hivyo kama utaongea jambo baya kwakua ulikua huwa unaongea tu hauna namna ya kubadili kauli yako. Hivyo ni vizuri kujifunza kuwa msikivu.

SOMA; KITABU; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.

2. KUBALI KUKOSOLEWA.

Usijisikie vibaya ukikosolewa unapokuwa umekosea. Jitahidi kutobishana sana unapoambiwa umekosea. Kukosea ni sehemu ya kujifunza. Ukiambiwa umekosea kaa chini na uangalie kwa umakini ni kwa nini ulikosea ili wakati mwingine usirudie kosa ilo hilo. Kila mmoja anakosea katika maeneo fulani nyakati fulani, iwe katika mahusiano, ofisini, shuleni, kwenye jamii nk. Hivyo ukikosolewa usione kama umeonewa. Jua kuwa kukosea ni sehemu ya maisha na ni nafasi nzuri yakuweza kujifunza na kujipanga kufanya vizuri zaidi.

3. USIPENDE KUBISHANA

clip_image002

Jitahidi kuepuka kubishana kusiko na sababu hata kama unajua kuwa upo sahihi. Kubishana sana huleta ugomvi na chuki. Kama upo sahihi hata ukikaa kimya haiubadili ukweli unaoufahamu kuwa uongo. Usiwe mwenye kubishana bishana utaishi kwa amani.

4. TAMBUA KUWA KILA MTU ANAMAWAZO YAKE.

clip_image003

SOMA; KITABU; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.

Tambua kuwa kila mmoja ana namna anavyotafsiri mambo. Kila mmoja ameumbwa tofauti na anamawazo yake. Heshimu mawazo ya wengine kwa kuwa tofauti ndio unaofanya ulimwengu usonge mbele. Kama wote tungekuwa na namna moja tunavyotafsiri vitu ulimwengu ungekua hauvutii hata kidogo. Ukitambua na kuheshimu uko tofauti wa mwingine huwezi kuumia kichwa. Utaishi kwa amani na furaha.

Tuonane wiki ijayo kwenye sehemu ya mwisho ya makala hii. Asante sana.

Kama unaswali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

Makala imepitiwa kwa lugha fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makalaza Kiswahili na Mjasiriamali barua pepe: rumishaelnjau@gmail.comsimu 0713 683422.

0 comments: