Siri Za Kuwa Mjasiriamali Bora Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

Wajasiriamali wengi wamekuwa wakijishughulisha shughuli za uzalishaji kama kutoa huduma au kuuza bidhaa na lengo likiwa kupata mafanikio. Katika kufikia mafanikio makubwa wachache wameweza na wengi wao kutofikia au kukua kwa taratibu. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa katika ujasiriamali kuna vitu ambavyo unatakiwa kuvifahamu na kuthubutu kuvifanya ili kupata mafanikio makubwa. Mambo ambayo yana tija kubwa ni mambo madogo madogo ila yana mchango mkubwa sana katika kufikia mafanikio makubwa.

Hizi ndio siri za mjasiriamali bora ambazo zitapelekea kufikia mafanikio makubwa

Kupenda kitu ambacho unakifanya

Kama unatoa huduma au kuuza bidhaa ni muhimu kuipenda na kuithamini huduma ambayo unaitoa ili uweze kuifanya kwa ubora na kukidhi mahitaji ya wateja wako. Ukipenda kitu ambacho unafanya ni rahisi kukifanya bila kuchoka hata kama unakutana na changamoto kwa kiasi gani. Ukipenda huduma unayoitoa utawapenda wateja wako na kuweza kutoa huduma bora.

SOMA; Wajasiriamali Wenye Mafanikio Hufanya Mambo Haya Matano Kila Siku.

Kuwa mvumilivu na kutokata tamaa

Hakuna jambo ambalo unaweza kulifanya kwa urahisi katika dunia ya leo ambayo imejaa changamoto nyingi na kukatishwa tamaa. Ukiwa mjasiriamali unatakiwa kuwa mvumilivu hasa pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo yako. Ukiwa katika ujasiriamali kuna kipindi unakutana changamoto nyingi ambazo usipokuwa makini unaweza kata tamaa ila changamoto hizi zinapima uwezo wako wa ustahimilivu na kupambana na changamoto. Ukiwa umefanikiwa kutatua changamoto hiyo ndivyo ambavyo utapiga hatua na kufikia mafanikio makubwa.

Kuwa na nidhamu ya pesa

Kama unahitaji kuwa mjasiriamali ambaye anakua kila siku nidhamu ya pesa ni muhimu sana katika msingi wa kukuza biashara yako. Matumizi yako yasizidi au yasiathiri ukuaji wa biashara yako. Ili uweze kukuza biashara yako ukawa na matumizi ya kiasi ambayo yatakuwa rafiki wa ukuaji wa biashara yako. Ili uweze kujua kama biashara yako inakua ni vizuri ukawa na kumbukumbu ya biashara yako kuhusu matumizi na mapato.

SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.

Kuanza kufanya biashara hata kwa mtaji mdogo

Watu wengi hasa wenye elimu hupenda kuanza kufanya biashara kwa mtaji mkubwa na kuona tatizo kubwa ambalo linafanya washindwe kujiajiri na kwa kutokuwa na mtaji wa kutosha. Kuna faida kubwa ya kuanza kuifanya biashara kwa mtaji mdogo huku ukiendelea kukua kwa taratibu faida hizo ni a) Unapata uwezo kusimamia biashara kwa madaraja yaani kuanzia chini b) Unapata uwezo wa kuzisimamia pesa c) Unapata uwezo mkubwa wa kupambana na changamoto

Kufanya kazi kwa Bidii na Ubunifu

Hakuna kitu ambacho unaweza fikia mafanikio makubwa kama hautofanya kazi kwa bidii. Unaweza kuwa na mtaji mkubwa kama hufanyi kazi kwa bidii na kwa ubunifu ni kazi bure. Mafanikio makubwa yanahitaji kujitoa na kufanya kazi kuliko ambavyo ulikuwa unafanya kazi mwanzo na ikiwezekana fanya kazi zaidi ya masaa ambayo ulikuwa unafanya mwanzo.

Huduma au bidhaa yako ilenge kuisaidia jamii

Ukitoa huduma ambayo itasaidia kutatua matatizo ya jamii husika ni rahisi kwako kuweza kuliteka soko na kuuza bidhaa yako au huduma katika kiwango cha juu. Kama huduma yako itatua tatizo katika jamii ni rahisi kupata wateja wengi na wewe mjasiriamali kuweza kufikia mafanikio makubwa. Biashara nyingi ambazo zimelenga kutatua matatizo ya jamii zinafanya vizuri katika soko na kuwa na ushindani mdogo kuliko bishara za kuiga toka kwa wengine.

SOMA; Huyu Ni Mjasiriamali Mwenye Hamasa Kubwa sana. Unaweza kujifunza kila kitu kutoka kwake.

Jifunze kila siku

Mjasiriamali unatakiwa kujifunza kuhusu biashara mpya au kujifunza zaidi kuhusu biashara ambayo unaifanya ili uweze kuwa bora zaidi na kuifanya kwa ubora. Katika kujifunza jifunze kwa vitu ambavyo vinalenga kuiboresha biashara yako ili uweze kupata mbinu mpya na kuwa bora zaidi. Kujifunza huku kutakufanya kufanya vitu kwa ubora na kuwa tofauti katika kutoa huduma na kuifanya biashara yako kuwa bora na kuvutia wateja wengi zaidi.

Mwandishi: Emmanuel Mahundi

Mawasiliano emmanuelmahundi@gmail.com au 0714 445510

Kwa kujifunza zaidi tembelea www.wekezamtanzania.blogspot.com

Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422. http://rumishaelnjau.wix.com/editor

0 comments: