Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria. ( 2)

Ndugu msomaji karibu tena kwenye muendelezo wa makala hii ambayo itakusaidia kukupa ujasiri wa kufanya jambo lolote unalohitaji katika maisha yako. Wiki iliyopita tuliangalia baadhi ya vitu vitakavyosaidia kujenga ujasiri ambavyo ni kuweka malengo, kufanya jambo moja baada ya jingine,kupata taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya na maandalizi. Kwa maelezo zaidi soma makala ya wiki iliyopita. Tuendelee kuanagalia vitu vingine.

Kama hukusoma makala ya wiki iliyopita hii hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria.

5. Amini kuwa unaweza.

Hakuna jambo lolote lile unaloweza kufanya vizuri kama hata wewe mwenyewe huna imani kuwa unaweza kufanya. Imani ni kitu cha muhimu sana katika kila eneo ili kufikia malengo yako.Ukishindwa kujiamini mwenyewe basi hata watu wanaokuzunguka hawawezi kukuamini kwa lolote unalotarajia kulifanya. Ukishakuwa na wasiwasi ndani yako kwa lile unalohitaji kufanya ujasiri wote huondoka na nguvu ya kufanya jambo lolote lile hata liwe dogo huondoka.

Ukiwa na imani kuwa unaweza kufanya na kufikiri ni namna gani ufanye jambo lako , utaona akili yako ikifunguka na kukupa mbinu mbalimbali za kufanya kitu unachotaka kukifanya. Jiamini kuwa unauwezo wa kufanya mambo makubwa nutapata ujasiri wa kuyafanya mpaka wewe mwenyewe utashangaa kama ni wewe umefanya au ni mtu mwingine?

6. Kila unachogusa kufanya fanya kwa ubora wa hali ya juu.

Unapopanga kufanya kazi yoyote ile, iwe ndogo au kubwa mahali popote pale, hakikisha umeifanya vizuri sana. Ukifanya kazi kwa ubora unasikia amani ndani yako na hivyo kukupa ujasiri wa kufanya kazi nyingine huku ukiwa na imani kuwa nayo utaifanya vizuri.

Ninaimani kuna wakati uliwahi kufanya kitu kizuri na ulifanya kwa kukusudia kabisa kuwa unataka kukifanya vizuri kadiri unavyoweza. Hebu fikiria wakati ule baada ya kufanya tu kitu hicho ulijisikiaje. Ona ujasiri ulioupata ndani yako baada ya kukamilisha kitu kile. Je hauwezi kujipanga na kufanya mambo mengine makubwa unayofikiria kwa kuweka akili yako yote na kutoa muda kwa hayo mambo makubwa ambayo unafikiri yatakufikisha katika malengo yako? Kafanye unalotaka kufanya kwa ubora kabisa na utapata ujasiri wa kuendelea na mambo mengine.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Za Watu.

7. Usiogope kushindwa.

Kama kuna jambo kubwa linaloweza kumzuia mtu kuwa jasiri na kufanya vitu vikubwa basi uoga ni jambo kubwa moja wapo.

Hakuna mtu yeyote katika maisha yake ambaye hajawahi kushindwa hata mara moja. Watu wengi jasiri uliowahi kuwaona na unaowasikia wamepitia vipindi mbalimbali vya kushindwa pia. Walijipanga kufanya mambo fulani lakini kwa namna moja au nyingine hayakwenda vile wao walivyotarajia.

Inapotokea umeshindwa, usikate tamaa. Jifunze ni wapi vitu havikwenda vizuri na ujipange upya kwa mara nyingine uboreshe pale unapoona palikua na tatizo. Katika jambo lolote unalolifanya kama umefanya maandalizi mazuri kuna matokeo ya aina mbili yaani kushinda na kushindwa, lakini katika uoga na kutofanya, tokeo ni moja tu ambalo ni kushindwa. Je unachagua kuogopa na kujiondolea hata ujasiri kidogo ulionao au kujipanga vizuri na kufanya jambo unalotaka na kuhakikisha kuwa matokeo yake hayakukatishi tama lakini yanakuwa ni njia ya wewe kujifunza na kukufanya uwe jasiri wa kufanya vitu vikubwa zaidi ambavyo vitakusaidia kupata matokeo makubwa baadae?

8. Omba msaada.

Sio rahisi sana kufanya kila jambo wewe mwenyewe na ndio maana Mungu alituumba binadamu wengi. Kila mmoja husaidiwa au kumsaidia mwingine wakati fulani. Usiogope kuomba msaada wakati unapodhani unahitaji kusaidiwa. Fahamu kuwa unaweza kupata msaada wa nguvu kazi, ushauri, au msaada wa kifedha mahali fulani na kwa wakati fulani. Uwepo wa rasilimali zote unazohitaji ili kukamilisha jambo unalohitaji ni muhimu ili kupata ujasiri wa kufanya jambo hilo. Hivyo pale unapodhani kuwa unahitaji kitu fulani usisite kuomba msaada mahala ambapo unadhani utasaidiwa.

SOMA; NENO LA LEO; Haya Ndio Maafa Unayojitengenezea Mwenyewe.

9. Sikiliza ushauri lakini usifanyiwe maamuzi na mtu mwingine.

Watu jasiri ni wazuri sana katika kufanya maamuzi. Hii haimaanishi kuwa huwa hawapati ushauri kutoka kwa wengine. Kama unahitaji ushauri ni vizuri kusikiliza wengine wanakushauri nini lakini baada ya kusikiliza ushauri kaa chini uchambue mambo mazuri katika ushari ulioupata na uamue ni nini unahitaji kufanya. Kumbuka kuwa jambo lolote unalohitaji kulifanya baada ya matokeo wewe ndiye utaonekana katika nafasi ya kufanya na sio washauri wako wala waamuzi wako. Hivyo ni vizuri kusikiliza ushauri na kuamua wewe binafsi ni nini unataka ufanye.

Ukiamua wewe mwenyewe inakupa ujasiri wa kufanya jambo tena kwa wakati mwingine lakini ukiamuliwa unaweza kujikuta ukitupia lawama kwa watu wengine. Kumbuka kuwa katika jambo lolote unalotaka kulifanya wewe ndio mwamuzi wa mwisho.

10. Muombe Mungu wako.

Kutokana na imani yako muombe Mungu wako akupe ujasiri wa kufanya mambo makubwa ambayo unaimani kuwa unaweza kufanya na yataleta mabadiliko chanya katika jamii inayokuzunguka. Amini kuwa kama watu wengine wanaweza kuwa na ujasiri wa kufanya mambo makubwa basi wewe pia waweza kujifunza kutoka kwao na kujijengea ujasiri na kuweza kufanya zaidi ya unavyoweza kufikiri.

SOMA; UKURASA WA 77; Kama Watu Hawakupingi Unakosea Sana.

Nakutakia safari njema ya kujijengea ujasiri nikiwa na imani kuwa unakwenda kukamilisha malengo yako na kufanya zaidi na zaidi kwa kadiri ya utakavyoamua wewe.

Uwe na maisha yenye furaha.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

0 comments: