Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria.

Nina imani umeshawahi kusikia au kusoma historia za watu tofauti tofauti na mara nyingine ukawaza kuwa watu hao walikua jasiri sana. Kuna watu mbalimbali waliowahi kuendesha nchi, kufanya vitu vya utofauti ambavyo kwa hali ya kawaida sio kila mtu anaweza kufanya, watu waliochukua maamuzi magumu ambayo sio rahisi kufikiria kwanini waliamua kuchukua maamuzi magumu kiasi hicho. Inawezekana wakati wanafanya maamuzi hayo hata watu wa karibu yao yaani ndugu na marafiki hawakuungana nao kwakua maamuzi hayo yalikuwa ni magumu mno, hivyo waliwakataza kufanya maamuzi hayo. Ukiwasoma au kuwasikia watu hawa unakubali kuwa watu hawa walikuwa na ujasiri mno.

Inawezekana pia kwenye familia yako kuna mtu jasiri wa namna hii katika eneo fulani la maisha,je na wewe pia ungetamani kuwa jasiri? Endelea kusoma makala hii mpaka mwisho na ufanyie kazi yale unayoyasoma kwa umakini ili uweze kuwa na ujasiri wa kufanya jambo lolote unalodhani ni zuri na litakuwezesha wewe kukamilisha ndoto za maisha yako.

SOMA; SIRI YA 14 YA MAFANIKIO; Tengeneza Ujasiri Wa Kufanikiwa.

VITU VITAKAVYOKUSAIDIA KUJENGA UJASIRI

Nimeorodhesha vitu hivi katika namba lakini haina maana kuwa kitu namba moja ndio cha muhimu zaidi kuliko namba ya mwisho. Vyote ni muhimu kulingana na nini unahitaji.

1. Weka malengo.

Nina imani sio mara ya kwanza unasoma kitu kama hiki. Mara nyingi umesoma na kusikia watu wakikuambia uweke malengo ya maisha yako. Malengo ya muda mrefu, malengo ya muda wa kati na malengo ya muda mfupi.

Kwanini kuweka malengo kunasaidia kukupa ujasiri?

Ukiorodhesha malengo yako unakuwa unafahamu ni nini unatakiwa ufanye, au njia gani uanatakiwa upite ili kufanikisha lile ulilokusudia katika maisha yako. Na katika kutimiza malengo kuna wakati unatakiwa kufanya maamuzi magumu ambayo yatakuhitaji wewe kuwa na ujasiri ndani yako ili kuweza kuyafanya maamuzi hayo. Fanya maamuzi hayo na utimize lengo ulilokusudia .Kwa kufanya hivi utakuwa unajijengea ujasiri wa kufanya mambo mengine yaliyopo mbele yako hata kama ni makubwa kiasi gani.

SOMA; NENO LA LEO; Jinsi Ya Kuimarisha Ujasiri Wako.

2. F anya jambo moja baada ya jingine.

Ili uweze kuwa jasiri ni vizuri ufanye jambo moja kwa wakati. Kufanya jambo moja kwa wakati kunakupa urahisi wa kutafuta mbinu za kuweza kufanya jambo hilo. Ukiwa na mambo mengi kichwani unayohitaji kuyafanya na hauna mpangilio ufanye lipi kwanza, unaweza kufikia hatua ukachanganyikiwa na kuamua usifanye jambo lolote lile.

Unaona tu mbele yako kuna mambo mengi na wingi huo wa vitu vya kufanya unaweza kukuondolea ujasiri wa kukamilisha hata jambo moja. Ni vizuri kuandika katika karatasi unahitaji kufanya nini na uweke vitu hivyo katika vipaumbele kuwa unaanza na kipi na utafuatia kipi. Ukifanya vitu vyote kwa wakati mmoja utashindwa kukamilisha vyote, utajiona huwezi kufanya lolote na hivyo kukuondolea hata uthubutu kidogo ulipo ndani yako.

3. Pata taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya.

Ni vizuri kupata taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya ili upate ujasiri wa kufanya kitu hicho. Inawezekana kweli kitu unachotaka kukifanya kikawa ni kigumu, ukiwa na taarifa hizo unajiandaa tangu mwanzoni kwaajili ya kupambana na ugumu huo. Unatengeneza njia za kupana na ugumu huo. Unapata ujasiri wa kuendelea na lengo lako hata kama mambo yatakuwa magumu kwakua unafahamu kuwa ili kufanikisha lengo lako kunaugumu fulani inabidi uupitie. Hiyo inakupa ujasiri wa kupambana hadi kukamilisha kusudio lako.

Ukiwa hauna taarifa za kutosha juu ya kitu unachoenda kufanya, ukipata changamoto hata kama ndogo, au hata watu wakikukatisha tama, ni rahisi kuacha kufanya jambo ulilotaka kulifanya nakujiona huwezi kufanya jambo lolote kubwa katika maisha yako.

SOMA; UKURASA WA 60; Je Una Ujasiri Huu?

4. Maandalizi.

Ili kupata ujasiri wa kufanya jambo lolote lililopo mbele yako ni lazima kufanya maandalizi mapema.

Ukiwa na taarifa sahihi za kitu unachokwenda kukifanya ni rahisi kujua ni nini utahitaji, iwe ni vifaa au tabia fulani. Kwa mfano unahitaji kuwa mkulima mzuri wa kahawa na umepata raarifa sahihi kuhusu eneo kahawa zinapostawi, mtaji wake, soko na faida. Lakini pia umepata taarifa ni nini changamoto katika ulimaji wa kahawa. Basi maandalizi ya kutafuta eneo, mbegu, watu watakao kusaidia, jinsi ya kupambana na changamoto ulizoambiwa hufuatia. Kwa kufanya hivi unapata ujasiri wa kuendelea na kilimo chako huku ukitegemea matokeo mazuri mbeleni.

Asante sana kwa kuungangana nami katika makala hii ya leo. Tutaendelea kuangalia vitu vingine vitakavyokusaidia kujenga ujasiri wiki ijayo siku kama ya leo.

Nakutakia maisha yenye furaha.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110/ 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

0 comments: