Jinsi Ya Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Za Watu.

Hofu ya kuongea mbele za watu ni hofu kubwa inayotawala katika maisha ya watu wengi sana duniani. Inasemekana kuwa zaidi ya robo tatu ya watu wote duniani hukabiliwa na hofu hii. Kuna watu hofu hii ni kubwa hata kuliko hofu ya kifo. Dalili za hofu hii ni kama kutetemeka, kutoka jasho mikononi na mfadhaiko. Hofu si kitu zaidi ya hali ya kiakili (state of mind) ya kuogopa kitu ambacho mara nyingi hakipo au hakiwezi kutokea. Katika maisha yetu hakuna jinsi ambayo tutaweza kukwepa kuongea mbele za watu, hivyo basi penda ama tusipende yatupasa na kutulazimu kujifunza kuongea mbele za watu. Hofu hii ina madhara makubwa hasa katika fani zetu na maisha yetu ya kila siku. Kuna njia kadhaa za kujijengea uwezo na kuondoa hofu hii, ambazo ni:

1. Kujiandaa vyema

Mojawapo ya njia ya kuepusha hofu hii ni kujiandaa vyema kwa kitu ambacho utakiwasilisha mbele ya hadhira. Kujua vizuri mada husika kutakupunguzia hofu kwa kiasi kikubwa. Pia hakikisha kwamba vifaa ambavyo utavitumia kuwasilisha mada yako mfano kompyuta, projekta n.k vinafanya kazi vyema na unajua kuvitumia. Kutokufanya kazi kwa vifaa hivi kutakufanya kuwa na mfadhaiko (panic) ambao mwishowe huleta hofu.

SOMA; Hizi ndio Hofu mbili ulizozaliwa nazo, nyingine ni uongo.

2. Fanyia mazoezi unachotaka kuwasilisha

Ili uweze kufanya vyema katika nyanja yoyote kama michezo na masomo yakubidi ufanye mazoezi ya kutosha ili uweze kumudu. Vivyo hivyo katika kuongea ama kuhutubia, andika yanayopasa kuwasilishwa na fanyia mazoezi ili uweze kujibu swali lolote ambalo litaulizwa. Ila wakati wa kuwasilisha si vyema kusoma kila kitu ulichoandika bali tumia tu kama mwongozo wako. Hii itakusaidia sana kuondoa hofu na kuweza kuimarika.

3. Ondoa hofu ya kukataliwa

Hofu ya kukataliwa inatawala vichwa vya watu wengi sana. Hii ni kwa sababu hakuna mtu anayependa kukataliwa. Kama nilivyosema mwanzo kuwa hofu si kitu zaidi ya hali ya kiakili uliyojijengea mwenyewe ambayo pia waweza kuiondoa ukitaka. Watu wamekuwa wakihofia kuhusu kuchukiwa kwa mada zao, mwonekano na vitu vinavyofanana na hivyo. Kumbuka umati uliokusanyika umekusanyika kwa ajili yako, hivyo wewe ni wa thamani mbele yao.

SOMA; Adui Yako Anaanzia Hapo Ulipo Na Anaanza hivi.

4. Lenga kutimiza ulichopanga

Inashauriwa kulenga katika yale uliyopanga. Ongea katika lugha inayoeleweka na punguza misamiati migumu ili uweze kuvutia wasikilizaji. Usiongee haraka haraka na weka msisitizo kwa kurudia mambo ya msingi.

5. Fanya mazoezi mbele ya kioo kikubwa

Wataalamu wanashauri kufanya mazoezi mbele ya kioo kikubwa ili uweze kujitazama mwonekano wako kwa ujumla na jinsi unavyowasilisha mada yako. Hii itakusaidia kuweza kujiamini kwani utachukulia kama upo mbele ya hadhira. Kwa njia hii utajigundua udhaifu na ubora wako hivyo kuurekebisha.

6. Rekodi na usikilize sauti yako

Watu wengi huchukukia sauti zao na jinsi wanavyoongea. Hivyo basi jijengee tabia ya kujirekodi na kusikiliza sauti yako ili uweze kuizoea. Pia kama una uwezo jirekodi video pale unapowasilisha mada. Itakusaidia kujua sehemu ya kurekebisha na pia jua kwamba huwezi kufanya kitu usichokipenda, hivyo zoea sauti yako na namna yako ya kuongea (voice flow).

SOMA; NENO LA LEO; Kitu Kimoja Kitakachokujengea Kujiamini Na Kujithamini.

7. Fanyia kazi upumuaji wako (breathing) na mazoezi mepesi

Ongeza uwezo wa kupumua kwa kufanya mazoezi ya viungo (physical exercises). Pumua katika hali ya taratibu pale unapowasilisha mada yako. Inashauriwa pia kupumua kwa nguvu pale unapokabiliwa na hofu, lakini si vizuri kufanya hivyo mbele za watu. Mazoezi mepesi ya viungo kabla ya kuhutubia yataongeza mzunguko wa damu na oksijeni katika ubongo wako.

8. Wasilisha mada yako mbele ya mtu mwingine

Mojawapo ya njia nzuri ya kukabiliana na hofu hii ni kuwasilisha mada yako mbele ya rafiki yako/zako, ndugu na jamaa pia. Hakikisha mtu huyo ni yule unaemuamini. Mwambie mtu huyo/watu hao udhaifu wako na uwe mkweli mara zote. Watakusikiliza, kukuuliza maswali, kukukosoa na hata kukurekebisha. Tegemea kuwa hiyo ndiyo hadhira yako na chochote watakachokirejesha ni sawa na ambavyo hadhira yako itafanya.

9. Tafuta muelekezaji wako (Mentor)

Hakuna mtu ambaye amefanikiwa sana kwa kufanya kila kitu peke yake. Ukigundua tatizo lako, mtafute mtu ambaye unajua ana uwezo huo na umwambie akuelekeze. Wakati mwingine itakulazimu kwenda darasani kujifunza kama kutakuwa na madarasa ya namna hiyo.

SOMA; SIRI YA 35 YA MAFANIKIO; Jinsi Ya Kujijengea Kujiamini.

10. Wasilisha mada unayoipenda/ Penda unachokiwasilisha

Kuwasilisha unachokipenda itakufanya ukione cha muhimu na utapenda kuwashirikisha. Kitu unachokipenda utakiwasilisha kwa umakini, kwa moyo, hamasa na kwa akili yako pia. Hivyo basi utakuwa umeondokana na hofu hii kwa asilimia kubwa sana.

11. Jifunze misamiati mingi

Ili uweze kuzungumza vizuri ni lazima uijue vyema lugha husika. Kuwa na misamiati mingi ya neno moja itakusaidia kuwasilisha mada yako bila kulazimika kukariri neno kwa neno hiyvo kutotakiwa kuogopa kulisahau neno husika. Kutokuwa na misamiati kutafanya wasikilizaji kuchukulia kwamba hujui unachowasilisha mbele yao. Cha muhimu ni kuilewa mada/ hotuba yako kabla hujaiwasilisha.

12. Relax na usiogope jinsi wasikilizaji wako watakavyokuchulia

Hakikisha akili yako haijasongwa na mawazo wakati unawasilisha maada yako au unaongea mbele za watu kwani hii itakusababisha kutoongea vizuri, kusahau na hata kuchanganya mambo. Pia kuwa huru kuwasilisha unachowasilisha bila kuogopa watu kwani siku zote hutaweza kuridhisha kila mtu. Kuna ambao watafurahi, watakereka na wengine watakuwa wanawasiliana kwa simu. Usiwatilie maanani sana kwani watakufanya ushindwe kuendelea vyema.

SOMA; SIRI YA 24 YA MAFANIKIO; Fanya Licha Ya Kuwa Na Hofu.

13. Usiongee haraka haraka

Kuongea haraka haraka kutakufanya uishiwe na pumzi mapema. Hii itakufanya mwishowe ufadhaike (panic) na ushindwe kuendelea. Hii inaweza pia kuwafanya wanaokusiliza wakereke na kushindwa kuendelea kukusikiliza kwa umakini. Pia unashauriwa kukielewa unachowasilisha ili isikulazimu kusoma mada/hotuba yako neno kwa neno

14. Kuwa na maji karibu

Ni muhimu kuwa na maji safi ya kunywa ili uweze kulainisha koo pale unapohisi kukaukiwa na maji au kuhisi koo linakaba. Ni muhimu yawe kwenye chombo ambacho ni rahisi kutumia, mfano glasi. Mbali na maji, hushauriwi kutumia vinywaji vyenye sukari kwani vitakufanya kupungukiwa na maji wakati unaongea. Pia usitumie vinywaji vyenye caffeine maana vitaongeza kasi ya mapigo ya moyo na kusababisha mfadhaiko wa mwili na akili.

Asante kwa kusoma Makala hii

Makala hii imeandikwa na ; Nickson Yohanes

Mwandishi ni mjasiriamali na mhamasishaji

Unaweza kuwasiliana nae kwa;

Simu: 0712-843030/0753-843030

E-mail: nmyohanes@gmail.com

Pia unaweza kutembelea blog yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com

0 comments: