Usichague Watu Wa Kusikiliza, Kuna Jambo La Kujifunza Kwa Kila Mtu.



Ni mara nyingi wengi wetu tumekuwa tukichagua watu wa kuwasikiliza, tunadhani ni watu wa aina fulani tu tunaweza kukaa chini na kujifunza vitu vipya kutoka kwao.  Inaweza kuwa kuna ukweli fulani lakini katika maisha haya tunayoishi na watu wachache niliopata neema ya kuonana nao, nimeona kwa kila mtu lipo la kujifunza, lipo la maana natoka nalo la kunifaa katika safari yangu hii ya hapa duniani.
Pengine ni nyumbani unaona mtoto wako kwa kuwa ni mdogo hana lolote la maana la kukuambia, ndugu yangu hata kama haukukubali atakachosema ni vyema kama utatoa muda wako kumsikiliza, ni vizuri kama utampa nafasi ya kusema kile alichonacho moyoni. Msikilize tu hata kama anachoongea hakina maana masikioni mwako, japo wakati mwingine unaweza kuona kuwa hakina maana kwa kuwa wewe mwenyewe umejiwekea wigo wa kusikiliza, umejiwekea wigo wa kuelewa, lakini ikiwa utafungua moyo wako na ukawa tayari kupokea vitu vipya/kujifunza kutoka kwa wengine bila kuangalia hali ya anayekufundisha utaweza kupata vitu vingi vya thamani sana na maana kubwa ambavyo pengine unalipia ili kuvipata kutoka kwa watu ambao umejiwekea kuwa ndio wa maana.
Wengi wa watu wanaoishi na wasaidizi wa kazi majumbani wanawaona kama watu wasio na msaada kabisa au wasio na lolote la maana wanaloweza kujifunza kwao, huwa tunasahau kuwa watu wale wameweza chukua hatua hata kuweza kuacha familia zao kuja kuishi na sisi wasiotufahamu vyema ili waweze kujiingizia kipato na pengine waweze kutimiza ndoto zao maishani mwao. Ni wangapi tunashindwa kufanya baadhi ya mambo, mfano mtu anaweza kuona kuwa kule Sumbawanga kuna fursa ya kilimo na inaweza kumnufaisha mtu sana kwa haraka lakini badala ya kukomaa na hiyo fursa wengi tunakimbilia kuona ubaya wa lile eneo na kuupa ubaya ule maana na uzito kichwani mwetu mpaka kushindwa kufikia malengo yetu. Lakini kama utakaa chini na kumsikiliza huyo binti na kuweza kumhoji maswali kadhaa vipo vitu utajifunza, utagundua ipo sababu iliyomfanya awe hapo kwa sasa na ni wachache unakuta wanataka kukaa hapo kwa muda mrefu, japo mara nyingi tunakasirika wanapoondoka maana tunatamani wabaki kuwa wasaidizi majumbani mwetu daima. Tunakuwa wabinafsi na kusahau kuwa wana ndoto zao pia, tunasahau kuwa hata kila jambo lina majira yake, tunasahau kuja kama wamekuja kwetu leo basi tuweke na akilini kuwa kuna siku wataondoka, ni lazima tujipange kuwa tayari kuendelea na maisha hata baada ya wao kuondoka. Ni lazima mtu uwe na mbadala wa kwamba leo ikitokea hivi itakuwaje maana haijalishi unakutana na nini maishani ni lazima ufike unapotakiwa kufika.
Inawezekana pia akawa anaongea kitu ambacho hakikufurahishi masikioni mwako, lakini hata katika hicho naamini kipo utakachojifunza   usimpuuze, wakati mwingine huwa tunafundishwa hata uvumilivu kwa kuweza kusikiliza watu ambao kiuhalisia wanakera au kukwaza. Inakusaidia nawe wakati mwingine kabla ya kusema kitu kufikiria na kujiuliza kama kuna ulazima wa kusema hicho kitu na je kitaongeza nini kwa wanaokusikiliza? Ukiona hakifai hautazungumza maana haupo tayari kugeuka kero kwa wengine. Kuwa tayari kujifunza kwa yeyote, usimpuuze yeyote bali usiwe mwepesi wa kumeza kila unachosikia, sikiliza kwanza ndipo uweze kutambua kinachofaa na kisichofaa.

Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo, anapatikana kwa namba +255 755 350 772 au kwa barua pepe bberrums@gmail.com

0 comments: