Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu EAT THAT FROG.

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu.  Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa EAT THA FROG. Kitabu kimeandikwa na mwandishi mashuhuri wa vitabu Brian Tracy. Mwandishi wa kitabu anaongelea kuhusu” KULA HUYO CHURA”, kwa kawaida hakuna mtu anayependa kula chura, lakini ukijizoesha kula chura, baada ya muda utazoea na utamla chura kirahisi zaidi. Mwandishi anafananisha Chura na shughuli, kazi au jukumu ambalo linaonekana ni gumu kufanya na ambalo ni rahisi kuahirisha. Mara nyingi majukumu tunayoahirisha ndiyo yenye kuleta matokeo makubwa katika maisha.

Karibu tujifunze mambo mengine

1.     Katika ulimwengu wa leo unalipwa kutokana na matokeo unayoyapata au kuyasababisha. Ukitaka kuongezwa mshahara basi kwanza ongeza matokeo kazini mwako.

2.     Mafanikio yanasababishwa na tabia. Tabia ndio zinavuta mafanikio. Tabia yakuweka vipaumbele,  kuepuka kuahirisha mambo na kushughulika na jambo lenye umuhimu ni ujuzi wa kiakili na kimwili. Tabia hii unaweza kujifunza kwa kufanyia mazoezi, kurudia rudia mpaka pale inapokua tabia ya kudumu. Ikishakua tabia ya kudumu inakua ni rahisi

3.     Asilimia 3 ya watu wazima ndio wenye malengo yaliyoandikwa. Na watu hawa wanafanikisha mambo mara 10 zaidi ya wale ambao hawajaandika malengo yao. Kamata kalamu na karatasi andika malengo yako.

4.     Hakuna njia ya mkato, kufanyia mazoezi ndio njia pekee inayoweza kumudu kutengeneza tabia na kuongeza ujuzi. Unaweza usione mabadiliko katika hatua za mwanzo, lakini ukiweza kudumisha mazoezi, lazima tu mabadiliko yatatokea.

5.     Kanuni yenye nguvu ya kuweka malengo na kuyafanikisha. Kanuni hiyo ina hatua saba. Hatua ya Kwanza: Amua ni nini hasa unataka. Watu wengi hawajui hasa ni nini wanataka, tafuta mahali palipotulia kaa kwa utulivu, jaribu kutafakari na kupambanua nini hasa unachotaka. Kama umeajiriwa pia njia ya kuweza kutimiza malengo ya kampuni, kaa chini na bosi wako, muulize hasa ni nini anachotegemea kutoka kwako.

6.     Hatua ya Pili: Andika mahali. Haitoshi kuamua ni nini unataka, nenda mbali zaidi andika mahali. Usipoandika malengo yako yanakua hayana nguvu, unapoandika chini unatengeneza kitu ambacho unaweza kukishika na kukiona.

7.     Hatua ya 3: Wekea malengo yako muda (deadline). Lengo linapokosa muda linakosa uharaka, na hatimaye kuendelea kuliahirisha, maana unaona bado hujachelewa kulifanya. Ila ukiliwekea muda, itakufanya ulitekeleze maana utaona muda unayoyoma.

8.     Hatua ya 4: Weka orodha yenye kila kitu ambacho unafikiri  utahitaji ili kufanikisha malengo yako. Orodha iwe pia na vitu utakavyotakiwa kufanya ili kufikia kule ulikopanga.

9.     Hatua ya 5: Orodha ya vitu utakavyohitaji kuvifanya, ipangilie kwenye mpango kazi. Unapopanga jua ni kipi kinapaswa kutangulia, kitakachofuata hadi kufikia kwenye malengo. Lazima mpango wako uwe kwenye mtiririko mzuri wa vipaumbele.

10.           Hatua ya 6: Anza utekelezaji mara moja. Mpango wa kawaida ambao unafanyiwa kazi ni mzuri zaidi, kuliko ule mpango ambao ni wa viwango vya juu lakini umebakia kwenye makaratasi.
Hatua ya 7:  Amua kufanya kitu kila siku. Hakikisha haipiti siku bila kufanya chochote chenye mchango kwenye malengo yako.

11.           Panga siku yako mapema. Ni vizuri kujenga tabia ya kuipangilia siku yako siku moja kabla.  Jitahidi usikubali kulala bila kuweka mpango wa siku inayofuata. Kila dakika unayotumia kupanga, unaokoa dakika 10 za utekelezaji. Itakuchukua dakika 10 hadi 12 kupanga siku yako inayofuata, lakini utaokoa hadi masaa 2 ya utekelezaji katika shughuli za siku inayofuata.

12.           Mara zote hakikisha unafanya shughuli ambazo zipo kwenye orodha ya mpango kazi wa siku. Usitekeleze shughuli iliyopo nje ya ulizopanga ikiwa ulizopanga hazijaisha, na kama ikikulazimu kufanya hivyo basi kwanza ijumuishe shughuli hiyo kwenye orodha kabla haujaifanya.

13.           Adui mkubwa ambaye tunapaswa kumshinda tunapokua kwenye njia ya mafanikio sio kukosa uwezo au kukosa fursa, bali ni hofu ya kushindwa na kukataliwa. Njia pekee ya kumshinda adui huyu hofu ni kufanya kile kitu unachokiogopa

14.           Kamwe usiache kujifunza. Maboresho binafsi na maboresho ya kitaaluma ni moja ya njia nzuri za kuukomboa muda. Maana unapokua bora wewe hata ufanyaji wa kazi unakua ni rahisi na kwa muda mfupi zaidi. Continuous learning is the minimum requirement for success in any field.

15.           Teknolojia inaweza kua rafiki yako mzuri au adui yako mbaya. Ukuaji wa teknolojia umesababisha watu wengi kupoteza muda mwingi, mitandao ya kijamii kwa sasa ndiyo inayoongoza kusababisha watu kuahirisha  mambo ya muhimu. Mbaya zaidi ni kwamba mitandao hii inalevya (addiction) yaani hata kama hupendi unajikuta tu ushaingia, facebook, whatsapp twiter, instagram, sijui na wapi kule. Lazima uweke mikakati kabambe ya kukabiliana na ulevi wa kwenye teknolojia hasa mitandao hii ya kijamii, maana wakati wewe unapoteza muda wako huko, wamiliki wa mitandao hiyo ndio wanaingiza pesa. Unapokua unafanya kazi hakikisha unaweka simu mbali na wewe mpaka umemaliza kazi, unaweza ukatenga muda maalumu wa kuangalia simu.

16.           Ukitaka kumla tembo, ukimkabili kwa kutaka kumla mzima mzima, utaona haiwezekani, laini ukimkata vipande vipande, na kuanza kimoja hadi kingine, utakuta tembo kaisha bila kujua. Hivyohivyo unapokua na jukumu kubwa, usilikabili kwa ujumla, ligawanye vipengele vipengele, halafu anza na kipengele kimoja baada ya kingine. Baada ya muda utakua umemaliza jukumu hilo.

17.           Watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya shughuli (activity) na Ufanikishaji (Accomplishment). Wanaongea tu, wanafanya vikao visivyoisha, na kutengeneza mipango mizuri sana, lakini cha kushangaza mwishowe ukifanyika uchambuzi au tathimini unakuta hakuna aliyefanya kazi hiyo na kupata matokeo yaliyotakikana.  Tatizo tunajiweka ‘bize’ na shughuli ila mwishowe ufanikishaji unakua mdogo. Amua leo kujikita katika ufanikishaji kuliko shughuli, maana shughuli kila mtu anaweza kufanya, ila kupata matokeo yaliyokusudiwa au hata zaidi yake ni wachache sana wanaoweza. Ila ukiamua unaweza.

18.           Tumia kanuni ya ABCDE. Unapopanga majukumu yako ya siku, unapoyaandika kwenye karatasi mbele ya shughuli husika weka alama A, au B au C, D au E. Majukumu yanayoangukia kwenye A ni yale ya muhimu sana, kuyafanya yataleta manufaa mazuri, na usipofanya yataleta madhara makubwa. Kama una shughuli za muhimu zaidi 1, unaweza kuandika A1, A2, A3 …..Usifanye jukumu la B kabla ya majukumu yote yaliyopo kwenye A hayajaisha.  Majukumu yanayoangukia kwenye B ni yale majukumu unayopaswa kuyafanya, ila ukiyafanya au usipoyafanya hayana madhara kivile. Majukumu yanayoangukia kwenye kundi C ni yale mabao haya umuhimu wowote, mfano kumpigia rafiki yako simu wakati wa kazi. Kundi D ni yale majukumu ambayo unaweza kumpatia mtu mwingine akafanya kwa niaba yako (Delegate). Kundi E ni la yale majukumu ambayo hupaswi wala kufanya, unaweza kuyaondoa yasifanyike kabisa (Eliminate)

19.           Sehemu ya kufanyia kazi iwe safi. Kama unafanyia kazi mezani hakikisha panakua safi kwanza. Sehemu unayofanyia kazi kama sio safi ni rahisi kuahirisha kufanya shughuli.  Sehemu safi akili inakua na utulivu na inafanya kazi kwa ufanisi zaidi.

20.           Tambua muda gani katika siku akili yako inakua katika uwezo wake wa juu, na kisha panga muda huo kufanya shughuli ya muhimu . Anza na shughuli ile ngumu zaidi, maana muda huo akili yako ndio inafanya kazi vizuri zaidi. Watu wengi wanakua na nguvu ya akili wakati wa asubuhi, baadhi ni mchana na wachache akili zao zinakua na nguvu zaidi jioni



Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

0 comments: