Kama Hutengenezi Hiki Mahali Ulipo Hustahili Kulipwa Chochote.
Ndugu
msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU salamu. Karibu katika makala yangu ya leo. Napenda
kutumia wasaa huu kuzungumza na wewe japo kwa ufupi kuhusu maisha. Katika
maisha tumekuwa tukifanya mambo mengi sana, mengine yana faida lakini mengine
mengi ni ya hasara sana kwetu hasa ukizingatia kwamba muda tulio nao hapa
duniani ni mfupi sana na umehesabiwa na aliyetuumba, hivyo katika kila unachofanya
ni vyema sana ukautumia muda wako vizuri kwani hutaweza kamwe kupata nyongeza
ya japo saa moja kwa siku ili yafike 25.
Ndugu
msomaji nikiandika hapa najua unasoma kwa sababu kuna kitu cha muhimu ambacho
najua utakwenda kukipata. Unajua unapofanya kitu chochote katika dunia hii kuna
malipo ambayo kwa kiasi kikubwa unayategemea ambayo yanaweza kuwa katika vitu
au isiwe katika vitu (material and non-material things). Kwa wengi mategemeo
haya yamekuwa yakiwasukuma kufanya kazi na kupata hicho wanachokitarajia. Kama
ni mfanyakazi unategemea upate mshahara na marupurupu na kama ni mfanyabiashara
unategemea kupata faida. Lakini hata kama wewe ni mwanafunzi nawe unahitaji
kufaulu katika hatima ya masomo yako. Najua na naelewa vyema kuwa hakuna mtu
atakayekupa hayo yote kama hakuna ulichokifanya.
Ndugu
msomaji huwezi kulipwa kwa sababu wewe unafanya kazi saa nyingi kwa siku,
huwezi kulipwa kwa sababu wewe una elimu kubwa wala huwezi kulipwa kwa sababu
wewe ni mtanashati au mrembo sana. Utalipwa tu kama umefanya jambo lenye thamani. Kama hutatengeneza thamani
yoyote kazini, shuleni, biasharani au popote pale ambapo wewe unapaswa kuwapo
basi hustahili kulipwa chochote na wakati mwingine unastahili adhabu. Thamani
utakayoitengeneza katika kile unachokifanya itatoa mchango katika nyanja za
maisha ambazo wewe umezisimamia. Mchango wako katika sehemu ndio pia ambao
utakupa furaha na kukuongezea uwezo wa kujiamini. Huwezi kujiamini kama
hujatekeleza yale ambayo unapaswa wewe kuyafanya.
Ili uweze
kutengeneza thamani katika kile ambacho unakifanya ni lazima kwanza uutumie
vyema muda wako katika kufanya yale yenye thamani kubwa kwako kwanza kabla ya yale
yenye thamani ndogo na pia kufanya jambo moja kwa wakati mmoja na sio kushika
mambo elfu kwa wakati mmoja. Ukweli ni kwamba utafanya yote lakini hakuna hata
moja ambalo utalifanya kwa ubora wake na hivyo kuondoa thamani yake. Kuwa yule mtu
ambaye akikosekana sehemu kwa muda mfupi umuhimu wake unaweza kuonekana na
thamani yake yaweze pia kuonekana. Kama ulipo hauna thamani ni muda wa wewe
kujiongezea thamani au uondoke kwani hakuna utofauti wa wewe kuwepo ama kutokuwepo.
Ninaposema fanya jambo moja kwa wakati mmoja (focus) namaanisha kuwa fanya kile
unachokikusudia kukifanya tu na si vinginevyo. Mathalani upo kazini lakini
unachokifanya ni kupiga soga, kutembelea mitandao ya kijamii na kutega tega
kazi kiasi kwamba kufikia muda wa kuondoka unakuwa umetumia chini ya asilimia
sabini katika kazi na kuwa na mzigo wa kuufanya unaporudi nyumbani. Kwa wale
washabiki wa mpira wanajua thamani ya mchezaji haitokani na chenga anazopiga au
kasi yake uwanjani bali idadi na uwezo wake wa kufunga magoli. Kumbuka katika
mpira wa miguu chenye thamani ni magoli ambayo ndiyo huleta ushindi.
Labda nikupe
mfano mdogo, wewe ni meneja masoko wa kampuni fulani na unaona mwenendo wa
kampuni sio mzuri katika mauzo unaweza kubuni mbinu mpya na kuongeza mauzo.
Katika hili umetengeneza thamani na wewe umeongeza thamani yako pia. Kwa maana
hiyo unaweza kumfuata bosi wako na kumwambia akuongeze mshahara naye bila shaka
atakubali kulingana na faida unazoleta.
Ni wakati wa
wewe kukaa chini sasa na kutafakari kuhusu thamani yako sehemu uliyopo. Ongeza
thamani yako na wewe pia utafaidika. Usikae kulalamika kuwa mshahara
hauongezewi wakati bosi wako haoni unachokifanya. Usitegemee kufanya jambo lile
lile kwa namna ile ile na utegemee kuongeza thamani bali badili namna unavyoenenda
nawe utaona mafanikio.
Mwisho
nirudie kwa kusema kuwa thamani yako mahali ulipo haitokani na kiasi gani muda
unaokaa kazini, kiwango cha elimu ulicho nacho, uzuri, au uwezo wako bali kitu
kimoja tu ambacho ni thamani unayotengeneza.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes
Unaweza kuwasiliana na nae kwa: simu: 0712
843030/0753 843030
e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.
6/10/2015 07:20:00 AM
|
Labels:
MBINU ZA MAFANIKIO
|
This entry was posted on 6/10/2015 07:20:00 AM
and is filed under
MBINU ZA MAFANIKIO
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment