Mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu 85 INSPIRING WAYS TO MARKET YOUR SMALL BUSINESS. (Njia 85 za kutangaza biashara yako)

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu.  Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa 85 INSPIRING WAYS TO MARKET YOUR SMALL BUSINESS.  Kitabu kimeandikwa na mwandishi  anayejulikana  kama Jackie Jarvis. Kitabu hiki kinaangazia njia 85 ambazo unaweza kuitangaza biashara yako ndogo ikawa moja ya biashara kubwa ulimwenguni. Kama una biashara ndogo basi jitahidi ukisome maana yapo mambo mengi sana ya kujifunza.

Karibu tujifunze

1.     Kuna Njia tatu kuu za kukuza biashara ambazo ni (a) kupata wateja wapya  (b) Kuongeza kiwango cha matumizi cha wateja (Kuuza zaidi). Mfano kama mteja hua anafanya manunuzi ya 20,000 basi jitahidi kuongeza thamani hadi aweze kuongeza na kufikia manunuzi ya 40,000 au zaidi. (c) Kuongeza marudio (frequency) ya kufanya biashara na wewe. Mfano kama wateja wako wanafanya biashara na wewe mara 2 kwa mwezi, unatakiwa kuongeza juhudi kufanya wateja waongeze marudio pengine kufika mara 4 au 5 kwa mwezi.

2.     Itazame biashara yako kwa jicho la mteja. Kama unataka kuwashawishi wateja wako ili wafanye biashara na wewe ni lazima uweze kuwaelewa na kua na mahusiano mazuri na wateja. Unapoitazama biashara yako kwa jicho la mteja utaweza kuiona kwa mtazamo tofauti. Hebu jaribu kuvaa kiatu cha mteja wako, itazame biashara yako ukiwa umevaa miwani ya mteja, unaona nini? je unaona kitu tofauti? Unapaswa uone tofauti. Wamiliki wengi wa biashara wanashindwa kua na mtazamo huu, maana wanaishia kuitazama biashara kwa jicho la mmiliki wa biashara. Ukifanya hivi utashindwa kutambua mahitaji ya mteja, lakini ukitazama kwa jicho la mteja, utajua ni nini hasa mteja anahitaji.


3.     Uwezo wako na ujuzi ulionao ni wa kipekee kwako, na vinaweza kua sehemu kubwa ya kukutofautisha wewe na wengine na pia ndivyo vinavyojenga thamani ya ushauri utakao wapa wateja wako. Uwezo na ujuzi ulionao ni sehemu ya historia yako, historia iliyojenga biashara uliyonayo leo. Unaweza kuwa umetumia miaka kadhaa kujenga ujuzi ulionao, unaweza kua umetumia miaka mingi kupata uzoefu ulionao. Lakini si rahisi kwa wateja kutambua hayo, kama wanafahamu ni sawa ila swali ni je wataona thamani zaidi katika kile unachowapa? Je uzoefu wako na ujuzi wako vina mchango katika thamani wanayotaka kuipata?

4.     Jiamini mwenyewe kabla hujaaminiwa. Imani binafsi ni kule kujiamini katika ujuzi na uzoefu ulionao. Ni ile sauti ya ndani inayosema NAWEZA KUFANYA HILI. Kujiamini haina maana kwamba umekamilika, au kwamba hauna mapungufu au madhaifu la hasha. Kujiamini mwenyewe ni kule kukubaliana na madhaifu uliyonayo, lakini kwa upande mwingine ukitazama uwezo ulionao na kuweza kuutumia kufanya vizuri kufunika madhaifu yako.


5.     Unapoongeza bei ya huduma au bidhaa yako, kwanza angalia ni thamani gani utakayoiongeza kwenye huduma yako ili kuhalalisha ongezeko la bei. Ukitaka kudumisha wateja wako pindi uongezapo bei ya huduma au bidhaa yako ni lazima kuongezeka huko kwa bei kuambatane na ongezeko la thamani kwa mteja. Think value before price.

6.     Kua mbunifu mara zote. Ubunifu katika biashara ni kule kua na uwezo wa kuja na njia za kufanya vitu kwa utofauti. Ni kule kufikiri nje ya mipaka ya kawaida, au kufikiri nje ya sheria zilizopo. Pia kua mbunifu ni kule kufikri nje ya boksi ambapo wengi wamo humo ndani.

7.     Watambue washindani wako wa kibiashara. Usikae kama upo kwenye kisiwa peke yako. Hakikisha unawatambua washindani wako wa kibiashara, tambua uwezo wao kibiashara, pia tambua udhaifu wao ambao wewe utaweza kuutumia kujinadi zaidi, kwa kuboresha lile eneo ambalo mshindani wako ameshindwa.


8.     Chagua njia bora zaidi za kunadi biashara yako. Njia bora ni zile ambazo zinakuwezesha kulenga watu sahihi kwa ujumbe sahihi na kuweza kupata mapato makubwa kutoka kwenye uwekezaji ulioufanya. Tumia chombo sahihi kuinadi biashara yako. Kwanza tambua ni wateja gani unaowalenga ndio ujue ni chombo kipi kitawafikia kirahisi. Mfano unawalenga watu wa vijijini halafu unatangaza kwenye mtandao (online marketing), hii itakua sio sahihi maana wahusika hawana uwezo wa kupata hizo taarifa kupia mitandao.


9.     Jenga utaratibu wa kuwasiliana na wateja wako ulionao. Kuwadumisha wateja wako ili waendelee kufanya biashara na wewe inategemea sana na jinsi unavyowasiliana na kuhusiana nao. Kuwasiliana nao mara kwa mara kutafanya waone unawajali hata pale wanapokua hawajaja kununua kitu kwako. Unaweza kutumia njia mbalimbali kuwasiliana na wateja wako, kama vile barua pepe, ukaribisho wa kwenye tukio lolote, unaweza kuwatumia zawadi za kadi kama kadi za Christmas, maulid, pasaka n.k

10.           Jenga mahusiano ya kuaminiana/uaminifu na wateja wako. Mahusiano ya uaminifu ndio yanayojenga uti wa mgongo wa biashara iliyofanikiwa.  Katika ulimwengu wa leo ambapo kuna machaguo mengi sana, watu wanawasaidia wale wanaowaamini zaidi. Ukikosa kuaminiwa ndio mwanzo wa kudidimia kwa biashara yako. Chunga sana imani ambayo wateja wako wanayo kwako. Maana imani hii inajengwa kwa muda mrefu, lakini inaweza kutoka ndani ya dakika chache. Trust can take a long time to build and an instant to break.

11.           Vitu vinavyojenga imani/uaminifu kwenye mahusiano ya kibiashara ni kama kuonyesha heshima kwa watu, kuuliza maswali na kusikiliza watu kwa makini, kua mkweli hata kama kufanya hivyo kutasababisha usiuze bidhaa zako, kutoa kile ulichoahidi, pia kama umeshindwa kutoa kama ulivyoahidi hakikisha wahusika wanapata taarifa mapema n.k

12.           Pitia upya mahitaji ya wateja wako. Unatakiwa kufahamu kwamba sababu iliyofanya mtu akawa mteja wako kwa mara ya kwanza, sio sababu hiyohiyo itakayoendelea kumfanya aendelee kua mteja wako katika kipindi kijacho.  Wateja wako waliopo wana mahitaji yanayobadilikabadilika, hivyo wanahitaji uelewa na mawasiliano endelevu. Ulivyokua ukimuelewa mteja fulani mwaka jana ni tofauti na mwaka huu, kwa hiyo usitegemee kumhudumia kama mwaka jana. Lazima uwe na utaratibu wa kupitia mahitaji yao mara kwa mara, usiseme “ huyu najua tu anachotaka, mahitaji yake nayajua” wateja hawapendi wahudumiwe kimazoea, wanatamani kila siku waonekane wapya, wahudumiwe kwa mbinu mpya. Maana mahitaji yao ndiyo yanayoashiria mahitaji ya soko kwa wakati huo.

13.           Elimisha wateja. Elimu kwa wateja kunawapa wateja fursa ya kujifunza zaidi kuhusu bidhaa au huduma unayotoa. Vile wateja wanaelewa thamani wanayopata kwako ndivyo itakavyokua rahisi kwao kununua. Kuelimisha wateja ni moja ya njia nzuri sana za kupata wateja wapya.  Elimu kwa wateja inaweza kua hatua ya mwanzo katika mchakato wa kufanikisha mauzo. Maana wanunuzi wengi wanatenga muda kutafuta taarifa kabla ya kuwa tayari kuchagua ni kwa nani wanunue.

14.           Sehemu ya faida rudisha kwa jamii. Hii itakufanya kua karibu zaidi na wateja wako, maana watu wengi wanapenda kua karibu na watu wanaosaidia wengine. Pia kusaidia jamii kwa utoaji ni nguzo muhimu sana ya kiroho ya biashara yako. Hakuna aliyetoa akafilisika, tunaona kina Bill Gates kila kukicha wanatoa mabilioni ya pesa kusaidia masikini na wasiojiweza, lakini ndio kwanza utajiri wao unaongezeka.

15.           Hamasisha timu yako. Wafanyakazi wanapokua wamehamasika wanafanya kazi vizuri zaidi na hivyo kupelekea kupata zaidi. Kwa mmiliki wa biashara ni muhimu kua kiongozi zaidi kuliko kua meneja.  Jifunze jinsi ya kuongoza watu, jinsi ya kuwahamasisha wafanyakazi wako wawe na nguvu kila mara ili kuongeza ufanisi kwenye kazi.


16.           Pima mapato yanayotokana na utangazaji wa biashara yako. Ukiona hakuna tofauti ya mapato baada ya kutangaza biashara yako, basi sitisha halafu jipange upya kutafuta njia sahihi ya utangazaji wa biashara hiyo. Maana utangazaji wa biashara unatumia fedha, sasa kama hakuna mapato ya ziada yanayopatikana baada ya kutangaza ni dhahiri kwamba unapata hasara, hivyo ni muhimu sana kupima matokeo ya utangazaji hasa kwenye mapato.

17.           Tengeneza dhamana (guarantee). Dhamana ni ofa unayoitoa kwa mteja, ili kupunguza au kuondoa ile hatari (risk) ya kimtazamo ambayo imekua ikimfanya asite kununua. Dhamana inasaidia kuondoa hofu kwa mteja ya kufanya manunuzi. Dhamana zinaweza kua za aina tofauti. Mfano unaweza kuweka dhamana ya matokeo ya bidhaa unayouza. Mfano kama unauza dawa ya kupunguza uzito, unaweza kumhakikishia mteja kwamba akitumia ndani ya wiki moja na asipoona matokeo yeyote atarudishiwa fedha yake. Hii itampa ujasiri wa kununua maana atajihisi hapotezi fedha na yuko upande salama maana amepewa uhakika. Lakini pia dhamana ni rahisi kutumika kama njia ya kunadi biashara yako. Maana huyo mteja ni rahisi kumwambia mwenzake kuhusu dhamana inayotolewa kwako.

18.           Yafanyie kazi malalamiko ya wateja. Malalamiko ni kule kujieleza kwa wateja kwa kutoridhika na huduma waliyopata. Kumbuka wateja wana machaguo mawili  wanapokua hawajaridhika na huduma au bidhaa yako, moja ni aidha waongee (walalamike) au waondoke kabisa waende kwingine. Kama wataondoka ujue hutapata fursa ya kutoa suluhisho la tatizo na wala hutajua ni nini tatizo maana hawajasema wameondoka kimyakimya. Watu wengi hawapendi kulalamika kwako moja kwa moja hata kama hawajaridhika na huduma yako, sababu ya kutokusema inaweza kuwa pengine hawataki kukusumbua, au hawajui waanze vipi, hivyo wanachofanya ni kuwaambia watu wengine, ambapo taarifa hii inaweza kuwafikia hadi watu 20. Hivyo ukipata malalamiko ya wateja unachotakiwa ni kuyachukulia kwa mtazamo chanya na kufanya marekebisho husika haraka kadri inavyowezekana.

19.           Rahisisha jinsi wateja watakavyo nunua kutoka kwako. Kwa sasa watu wengi wako bize, na biashara zinazoweza kufanikiwa ni zile tu ambazo mchakato wa kununua ni mfupi. Ukiwa na urasimu mwingi hutapata wateja labda uwe ni wewe pekee unayetoa huduma hiyo, na hata hivyo hutafika mbali. Kwa jinsi utakavyorahisisha mfumo wa manunuzi, utaendelea kudumisha wateja na pia utavutia wengine wapya.


20.           Wafanye wateja wako wawe wenye furaha wakati wote. Kama wateja watakua wanakufurahia wewe pamoja na biashara yako, ni kwamba wataendelea kubakia waaminifu na wataendelea kununua kutoka kwako. Sio hivyo tu bali watawashauri na wengine waje kununua kwako, hivyo wateja watazidi kuongezeka. Hata pale utakapoongeza bei ya huduma sio rahisi kuondoka maana tayari wanafurahia thamani wanayoipata kutoka kwako.

Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

0 comments: