Njia Nne Za Kuishi Na Watu Vizuri.
Ndugu msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU ni siku
nyingine tena nzuri aliyoipanga mwenyezi Mungu kutukutanisha pamoja katika makala
hii ili tuweze kujifunza pamoja. Wahenga walisema elimu ni kama bahari na haina
mwisho. Hakuna hata mtu mmoja ambaye ataweza kujua kila kitu mpaka kufikia
mwisho wa maisha yake kwani duniani na hata nje ya dunia kuna mambo mengi ya
kujifunza. Hii ni fursa nyingine ambayo unapata kuisikia sauti yangu ikiongea
na wewe kupitia maandishi haya. Ni matumaini yangu unaendelea kujifunza kila
siku na ndiyo maana huwa napata mrejesho (feedback) kutoka kwenu kupitia simu
na barua pepe. Niwashukuru sana kwani mnanipa nguvu ya kuendelea kuwapa makala
nzuri na za kufundisha. Pia usisite kutembelea mtandao wa Life Adventures kwa
mambo mengine mazuri kwako.
Baada ya utangulizi huu mfupi
nipende kuanza moja kwa moja kwa kueleza kuhusu maisha yetu ya hapa duniani. Ni
ukweli usiofichika kwamba kila mtu anahitaji watu. Huwezi kuishi bila watu.
Kuna wakati unakutana na mtu haelewani na asilimia kubwa ya watu na kujiuliza
tatizo ni nini, ni ule msemo kwamba ana damu ya kunguni au lah! Ukweli ni
kwamba kuna tabia huwa zinatatiza mahusiano baina ya watu. Baadhi ya tabia hizo
nimejaribu kuzieleza hapa chini. Twende sasa
1.
Usiwe mwepesi wa kukosoa, kulalamika au kulaumu
Ndugu msomaji wangu najua
utakubaliana na mimi kuwa hakuna binadamu aliyekamilika na kila mtu ana udhaifu wake. Kwa kujua hilo hata
wewe mkosoaji una mapungufu na madhaifu yako pengine makubwa kuliko yeye.
Usijaribu kutoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako na wakati huo kwako kuna
boriti. Usiwe wa kwanza kurusha jiwe kwa mwenzako kwa sababu tu makosa yake yamewekwa
hadharani ili hali ya kwako yakipata nafasi ya kujulikana utatamani ardhi
ipasuke uingie. Pia usiwe mtu wa kulalamika na kulaumu kwa kila kila kitu hata
ambayo wewe ndiye msababishi. Usiwe mtu wa kukashifu na kutoa maneno ya ovyo.
Beba msalaba wako mwenyewe na uupeleke Goligotha, acha kuhukumu, kukosoa na hata
kulaumu wengine. Amini usiamini hakuna mtu anayependa mtu mwenye tabia hizo na
mara nyingi watu wa hiyo huogopwa na kukwepwa kama ukoma. Kama mtu kakosea tafuta namna ya kumwambia
makosa yake naye kama ni muungwana atakuelewa.
2.
Toa pongezi za dhati
Kila mtu huhitaji pongezi pale
anapofanya kazi nzuri. Mathalani nimpongeze Makirita Amani, Deogratius Kessy, Esther
Ngullwa, Goodluck Moshi, Beatrice, Mahundi, Daudi na waandishi wengine wa
JIONGEZE UFAHAMU nitakuwa natoa pongezi za dhati kutoka moyoni. Kumbuka
ninaposema pongezi za dhati namaanisha zile pongezi ambazo kweli zinatoka
moyoni mwa mtu na si zile za kumvisha mtu sifa zisizofaa ambazo waswahili wana
msemo wao wa ‘’Kuvika kilemba cha ukoka’’ au ‘’kupaka mafuta kwa mgongo wa
chupa. Naamini waandishi hawa ni mahiri na hivyo hawataona kama nawasifia bure.
Pia usisahau kuwa pongezi za kinafiki hazisaidii ila kama umedhamiria kutoa
pongezi zitoe moyoni hata kama huyo mtu humkubali lakini jaribu kuikubali kazi
yake. Kwa jinsi hii utaweza kukaa na kila mtu na kuishi vizuri na watu na hata
kupunguza idadi ya maadui na kuongeza marafiki. Faida ya marafiki
nilishaiandika siku za nyuma, kama hujaisoma Makala hiyo usisite kutembelea Life
Adventures.
3.
Toa
msaada kwa watu wengine kufikia malengo yao
Kila mtu duniani ni msafiri na
katika safari yake anategemea kufika kituoni siku moja. Kwa kuwa njiani kuna
dhoruba nyingi huhitaji msaada wa watu wengine. Kama wewe ndiye uliyefikwa na
wajibu huo usisite kutoa msaada. Mtu anayesaidia wengine huwa na mahusiano
mazuri na watu na hata yeye kusaidiwa pale anapopata majanga. Kumbuka msaada
mzuri ni ule unaoutoa bila kutegemea malipo yoyote, na kama unataka kusaidia
basi msaidie yule ambaye unajua hana uwezo wala jinsi ya kukulipa. Hii itakupa
faraja na utajenga jina lako na wasifu wako kwa watu. Neno msaada lina maana
pana sana, linaanzia katika vitu mpaka hali. Kuanzia hela, ushauri, kufundisha,
kuelimisha na mambo yanayofanana na hayo.
4.
Toa faraja kwa watu
Kuwa mtu mwenye kufariji na kutia
moyo wengine. Usiwe mtu mwenye kukatisha tamaa watu wengine. Usiwe mtu wa kuumiza mioyo ya watu wengine,
usiwe mtu wa kunyooshewa vidole kila kona kwamba una hasara nyingi kuliko
faida. Kuna msemo unasema kama huwezi kuwapa faraja kwa watu basi usiwaumize.
Kama mtu amekuambia jambo na unaona huwezi kumshauri au kumpa faraja yoyote ni
bora umpe pole na ujiondokee zako na si kumuumiza kwa kumwambia maneno yenye
kujeruhi. Kumbuka kuwa ukisha sema neno halirudi tena kinywani, hivyo basi
fikiria kwanza kabla ya kuongea na pia jaribu kuvaa uhusika wa unayemwambia. Kumbuka
watu wengi wamekuwa wakijiua kila siku kwa kukosa faraja na maelfu wakiokolewa
kutoka kifo kwa faraja tu. Nenda na kauli mbiu hii ‘’Toa faraja, okoa maisha na
jenga undugu’’
Ni faraja yangu kuwa umefika mwisho
wa Makala hii, ni matumaini yangu kuwa utafanyia kazi kila nililoandika hapa
mtandaoni. Yatakuwa ni masikitiko kwangu kama umesoma mpaka hapa halafu
ukashindwa kubadilika kwani utakuwa umepoteza muda wako, muda wangu na hata gharama
zako kusoma Makala hii. Naamini wewe ni wa tofauti na utabadilika kuanzia sasa.
Nikutakie siku njema yenye
mafanikio tele.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes Unaweza kuwasiliana
na nae kwa kwa: simu: 0712 843030/0753 843030 e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com
kujifunza zaidi.
6/16/2015 07:30:00 AM
|
Labels:
MBINU ZA MAISHA
|
This entry was posted on 6/16/2015 07:30:00 AM
and is filed under
MBINU ZA MAISHA
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment