Jinsi Ya Kuondokana Na Hofu Ya Kupata Ajali.



Habari za leo msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU. Ni imani yangu kuwa ulikua na wiki nzuri. Ni mwisho wa wiki ambapo tunakutana tena ili kujiongezea maarifa ya maisha.
Leo tutaangalia suala la ajali za vyombo vya usafiri.
Katika miezi ya karibuni kumekuwa na ajali za mara kwa mara za vyombo vya usafiri hasa mabasi. Maisha ya watu wengi yamepotea na watu wamepata ulemavu pia, ikiwa ni pamoja na kuumia kwa baadhi ya wasafiri. Watu hawa inawezekana ni ndugu zetu wa karibu, marafiki na hata majirani zetu. Niwape pole wale ambao kwa namna moja au nyingine waliguswa na matukio haya. Lakini pole kwa Watanzania wote kwakua tumepoteza nguvu kazi kwa taifa letu.
Inawezekana hata wewe msomaji ni mmojawapo wa watu ambao wamewahi kupata ajali katika chombo chochote kile cha usafiri, naomba upokee pole yangu pia. Kupata ajali husababisha hofu kwa mhusika na hivyo kumfanya kila mara akitaka kusafiri akose raha. Wakati mwingine ukiwa safarini unakuwa na wasiwasi wa hali ya juu mpaka unapomaliza safari, kutokana na hofu uliyonayo kichwa kinakuuma kupita kiasi.
Unaweza kuondokana na hofu ya kupata ajali kwa kufanya haya yafuatayo
1.     HAKIKISHA UNATUMIA USAFIRI IMARA
Ni vizuri kutumia usafiri ambao hata wewe mwenyewe unakuwa na amani moyoni kuutumia. Kama utakosa amani kwa mwonekano wa gari tu basi ujue kama ukipanda hata likikwepa jiwe tu lazima roho yako itaruka na kukukosesha amani. Sasa kama unasafiri safari ndefu mpaka unafika hofu inakuwa imeongezeka maradufu.
Kwa utaratibu wetu watanzania hata kama wewe ni mgeni mahali fulani na unahitaji usafiri watu hufahamu sifa za magari. Unaweza kuwauliza watu unaowaamini katika eneo hilo gari lipi ni imara na lipi ni bovu lakini. Kuwa makini usiwaulize wapiga debe kwakua watakudanganya.

2.     USISHABIKIE MWENDO KASI
Madereva wengi sana hupenda kuendesha magari kwa mwendo wa kasi sana. Mara nyingi abiria huwa mashabiki na kuwafanya madereva kuendesha magari kwa vurugu sana. Usijaribu kushabikia mwendo wa kasi kwani ni rahisi kupata ajali kama mwendo wa gari sio mzuri lakini pia madhara ya gari linalopata ajali kwa kua na mwendo wa kasi ni makubwa kuliko gari ambalo liko katika mwendo wa kawaida.

3.     USIWAZE MAWAZO HASI
Jitahidi kuwaza mawazo chanya kila wakati. Usifikirie kupata ajali kila mara unaposafiri. Mara nyingi unaloliwaza ndilo linalotokea. Waswahili wana usemi wao kuwa ”aliwazalo mjinga ndilo limtokealo” Jitahidi usiwaze mawazo hasi katika akili yako. Fikiria ni mara ngapi umekuwa na wasiwasi wa kupata ajali na hakuna lililotokea zaidi ya wewe kufika salama. Kuwaza mawazo hasi hakuwezi leta unafuu wowote au kusitisha lile lililopangwa kutokea. Kama umekuwa na wasiwasi kutokana na mwendo kasi basi toa taarifa mahali panapohusika. Na jambo zuri ni kwamba katika vyombo vya usafiri wameweka namba za mawasiliano kama kutakuwa na tatizo lolote katika chombo cha usafiri ulichopo.

4.     MUNGU ANAJAMBO ANATAKA UJIFUNZE KATIKA KILA LITOKEALO.
Kuna  baadhi ya vitu vingi vinatokea katika maisha yetu hata kama tutachukua tahadhari kiasi gani moja ya vitu hivyo ni ajali. Katika kila litokealo basi usijilaumu na usijute. Kuna kitu Mungu anataka kukufundisha kwakua kama kuna kitu Mungu amepanga kitokee huwezi kuzuia. Unaweza kupoteza baadhi ya viungo au kupoteza ndugu wa karibu. Inasikitisha sana na ni inaleta uchungu mno. Kuwa na hofu, kuwa na majonzi wakati wote na kushindwa kuendelea na maisha mengine hakusaidii zaidi ya kukupa uchungu zaidi. Ni vizuri kukubali hali  iliyotokea na kuendelea tena na maisha ya kila siku.

5.     KUFA NI LAZIMA
Inawezekana kauli hii ya KUFA NI LAZIMA imekushitua kidogo. Lakini ukweli ni kwamba kama tulizaliwa basi lazima siku moja tutakufa. Kila mmoja ana namna yake ambayo Mungu amempangia kifo chake lakini pia yeye anafahamu ni siku gani ya mwisho sisi kuwepo hapa duniani. Tunatofautiana nyakati za kuaga dunia na namna ambavyo tunaiga dunia hii. Hivyo kwa kufahamu hili basi ni vyema kujiandaa wakati wote, lakini kuendelea kutimiza majukumu yetu ili siku ikifika tuwe tumekamilisha yale tuliyopaswa kuyafanya hapa duniani.

Ni imani yangu kuwa haya uliyoyasoma yatasaidia kuondoa hofu ya kupata ajali ambayo inakuzonga. Au hata kumshirikisha mtu mwingine mwenye hofu ya namna hii ili umsaidie kuwa makini lakini awe na amani pindi anapokuwa akisafiri.
Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO:  0767 900 110 / 0714 900 110

0 comments: