Makundi Matatu (3) Ambayo Hayawezi Kufikia Mafanikio.

Ni haki ya kila mtu hapa duniani kufikia mafanikio makubwa katika nyanja yoyote ile ya maisha kama vile kijamii, kiuchumi, kimwili na kadhalika. Na ili kuwa na mafanikio yoyote lazima uamue. Katika makala yetu ya leo tutajifunza makundi matatu ya watu ambayo ni vigumu sana kwao sana kufikia mafanikio yoyote yale.

HAWAWEZI

Makundi hayo ni kama yafuatayo;

1. Kundi Ambalo Hawataki au Hawahitaji Mafanikio

Mtu mwenyewe au watu wenyewe hawataki au hawahitaji mafanikio au hawana utayari wa kuwa na mafanikio. Kundi hili huwa wanajilinda sana kwa nafsi zao, ni watu ambao ni wagumu na siyo rahisi kuingilika na wana maneno mengi sana ya kujihami kiasi ambacho hawawezi kuvamiwa ovyo.

Kundi hili hawapendi kuingia katika matatizo, hawaishiwi sababu na wanaamini kuwa ukiingia katika mafanikio ni lazima ujiingize katika matatizo. Ni watu ambao hawataki kujifunza, kusumbuliwa ,wanachelewa sana kuamka na kulala upesi, hata akifanya kitu hapendi kukosolewa na wanakuwa wakali sana wanapoulizwa na ukiwaambia waongeze mwendo wako tayari kugeuza na kurudi nyuma au kutafuta njia nyingine ili wasiongozane na wewe na kusumbuliwa katika safari hiyo.

Hivyo basi, watu hawa wameridhika na hali zao za maisha wanaishi kwa imani. Wako tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza katika maisha yao na watu hawa au kundi hili ni vigumu kufikia mafanikio au utajiri.

SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.

2. Kundi Lisilopenda Kujiingiza Katika Hatari

Kundi hili lina mawazo na imani kuwa unapojiingiza katika mafanikio au kuwa na utajiri umejiingiza katika hatari , kuwa katika hali ya kuvamiwavamiwa na majambazi wakati wote au kuingiliwa na wezi kauli yao kuu wanasema ‘’ Hali niliyonayo inatosha sitaki kujiingiza katika hatari’’

Watu hawa ni watafutaji na wanenaji wazuri sana wa kutoa habari za watu ambao wamepatwa na mikasa mikubwa kutokana na utajiri au kutafuta utajiri . Watu hawa hawana ile hali ya kutamani kuwa na mafanikio au utajiri na ndani mwao hali hiyo haipo kabisa.

Hata wakiwa wana uwezo au kipato ndani yao hawana ile tabia ya kuwaza na kutamani mambo makubwa ya mafanikio au utajri watu hawa ifikapo uzeeni hali yao huwa mbaya sana kwa sababu pale mwanzo hakutaka kujiingiza katika hatari ili apate mafanikio.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.

3. Kundi Ambalo Lina Tabia ya Wasiwasi (Hofu na Woga ) Ndani Mwao

Kuna baadhi ya watu ambao ndani mwao wana ile hali ya woga na hofu, ile hali ya kuogopa kila wakati na kila kitu. Ukiwa na hofu huwezi kuthubutu na kuingia katika uwanja wa mapambano kutafuta mafanikio ili upate utajiri .

Kundi hili wana hofu ya shinikizo la mahangaiko. Hawataki na wanaogopa kushikwa na ile hali ya mahangaiko wanajuwa kuwa ili kuingia katika mafanikio kuna hali inayojitokeza bila kutazamia mahangaiko. Ni lazima upambane na uhangaike huku na huku na baadaye mafanikio yatatokea lakini wao wanaendelea kuogopa hali hiyo ya mahangaiko ingawaje hawana chochote kinachowawezesha katika maisha.

Wanaogopa kuteseka, wanaogopa ile hali ya kutowajibika, mafanikio au hali yoyote ya utajiri haiji bila ya kujitesa .

Kwahiyo, katika haya makundi tuliyojifunza leo yapo sana katika jamii yetu iliyotuzunguka. Kama wewe ni miongoni mwa haya makundi matatu tuliyojifunza leo achana na ondoka kabisa katika hali hiyo na chukua hatua leo ya kukufikisha katika kilele cha mafanikio.

Makala hii imendikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

0 comments: