Hii Ndio Siri Ya Kupata Marafiki Bora Watakaokuwezesha Kufikia Malengo Yako.

Habari za leo mpendwa msomaji wa mtandao huu wa JIONGEZE UFAHAMU. Karibu tena kwenye ijumaa nyingine ambayo kwa leo tunaangalia upande wa marafiki na mchango wao katika maisha yetu ya kila siku

Waswahili wanasema nioneshe rafiki zako nami nitakuambia tabia zako. Msemo huu ni wa kweli. Kila mtu ni shahidi wa usemi huu ingawa kuna baadhi hujifariji kwa kusema mimi nina rafiki jambazi lakini mimi si jambazi.

Ukweli ni kwamba tabia za watu ambao ni marafiki hufanana kwa kiwango kikubwa ingawa hazitafanana kwa asilimia mia moja kwakua kila mtu anatofautiana na mwingine kwa namna moja ama nyingine. Kwa mfano mtu anaweza kukutambulisha kwa rafiki yake na kusema ukimuona yeye umeniona mimi. Si kweli kuwa mtu mwingine anaweza kuwa wewe lakini kuna namna fulani au katika maeneo fulani(ambayo ni muhimu sana) mnaendana na sababu hiyo ndiyo iliyoleta ukaribu ndani yenu na kuwafanya muwe marafiki.

SOMA; Kanuni Sita(6) Muhimu Za Kushinda Tatizo Lolote Unalokutana Nalo.

clip_image002

URAFIKI NA MALENGO.

Mara nyingi marafiki zetu wamekua na sehemu kubwa sana ya kutufanya tufikie au tusifikie malengo yetu. Marafiki hawa tunaweza kuwa tumeonana nao mahali pa kazi,masomoni, mahali tunapoishi, sehemu za ibada. N.k

Marafiki wanafaida sana katika malengo yetu ikiwa ni kututia moyo pale tunapokata tamaa, kutushauri, kuturekebisha wakati tunapokosea, kutufariji, kushirikiana nao nyakati za huzuni na furaha na pia marafiki ndiyo hao wanaoweza kuwa mume au mke baadae. Kwa hiyo marafiki wanamchango mkubwa sana katika maisha yetu ya kila siku .

Kuna baadhi ya watu hushindwa kufikia malengo ya maisha yao waliyojiwekea kwasababu tu ya marafiki walionao. Marafiki hawa huwa ukuta wa wao kufanya mambo mazuri na makubwa wanayohitaji kuyafanya. Ni vizuri kuwa makini na kuchunguza vizuri kama maraki tulionao wana chembechembe za mambo ambayo tumeyapa kipaumbele. Kama una rafiki mlevi , mtembezi, anayependa kubishana, mvivu na wewe ukawa na tabia za tofauti na yeye basi urafiki wenu waweza kuingia doa au hapo lazima mmoja abadilike amfuate mwingine ili muweze kuongea lugha zinazofanana.

SOMA; Kitu Pekee Unachoweza Kuwa Na Uhakika Nacho…

Fikiria unapokuwa na ndoto za kufikia mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na uhuru wa kifedha, furaha, mahusiano yenye tija, familia nzuri,afya bora na kuwa muumini mzuri katika dini yako. Halafu ukatafuta rafiki ambaye yeye hatarajii kuboresha eneo lolote lile kama wewe unavyofikiri. Je atakuwa msaada au kikwazo cha wewe kufika pale unapohitaji? Mkiwa kama marafiki mtakuwa mnazungumza nini basi mkikaa pamoja. Kwakua kama unatarajia kuboresha eneo fulani ni vizuri ukawa karibu na mtu aliyefanikiwa katika eneo hilo au ambaye naye pia yuko katika safari ya kuboresha eneo hilo ili ule msukumo ulioko ndani yako usijeondolewa na watu wanokatisha tamaa.

Ni vizuri kufahamu mwelekeo na namna ambavyo rafiki yako anayachukulia maisha, mafanikio,na vipengele vingine ambavyo kwako wewe ni muhimu. Kwa kujua hivyo ni rahisi kumshirikisha rafiki yako ratiba yako ya siku na yeye kukushirikisha yake ili kusiwe na ugomvi na kila mmoja atambue na kuheshimu kitu rafiki yake anachokifanya na kujali muda pia.

SOMA; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015.

Hakikisha kuwa rafiki uliyenaye anakusaidia kufikia malengo yako na wewe pia unamsaidia kufikia malengo yake. Kama rafiki uliyenae ni kikwazo cha wewe kufika unapotaka basi ni vizuri ukaachana nae. Kuna wakati unafika ni lazima ufanye maamuzi magumu ili kuhakikisha kuwa unafikia ndoto zako. Usiachane nae kwa ugomvi. Fuata ratiba zako na umwambie kuhusu ratiba yako akishindwa kuendana na wewe basi yeye mwenyewe ataamua kuachana na wewe. Na hio itakuwa fursa nzuri kwako kuweza kuwa na rafiki ambaye mwelekeo wenu unaendana.

Pia kuna marafiki wengine wazuri sana ambao hawawezi kukuvunja moyo hata siku moja ambao ni vitabu vya uhamasishaji, makala mbalimbali, vitabu vya audio n.k.

Kumbuka watu wanaotuzunguka wana mchango mkubwa katika ukuaji wetu. Hivyo usijitenge kabisa na watu ila ufahamu namna bora ya kushirikiana nao bila kupoteza mwelekeo wako wa maisha.

Nakutakia utekelezaji mwema wa haya uliyojifunza.

Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

2 comments:

Unknown said...

Nimependa sana mafundisho mazur

GATSON said...

Nimependezwa sana na mafundisho