Kama Umeajiriwa Na Hujaanza Kufanya Hili Jua Kuwa Unapotea.

Kupata ajira imekuwa ndoto ya watu wengi na mafanikio kama sehemu tu ya maisha yao. Kama umeajiriwa na umekuwa ukitamani kuajiriwa nakupa pongezi kwani umefikia baadhi ya malengo yako. Watu wengi katika kada mbalimbali, wenye elimu na wasio na elimu wamekuwa wakitamani kuajiriwa na kuwekeza nguvu kubwa katika hilo. Sisemi kwamba wamekosea wala sisemi kwamba wamepatia kwani yote yanaweza kuwa sahihi kwa mtazamo wa muhusika. Lakini kama umeajiriwa au una mpango wa kuajiriwa ni muhimu zaidi kujua kuwa kufanikiwa ama kutofanikiwa kupo mikononi mwako mwenyewe na si kwa serikali wala mwajiri wako. Watu wamekuwa wakitafuta ajira nzuri na yenye kutoa pesa nyingi ili waweze kukidhi mahitaji yao lakini hata baada ya kupata ajira hizo bado tatizo la fedha lipo kwao.

clip_image002

Robert Kiyosaki katika mfululizo wa vitabu vyake vya Richdad, Poordad, anasema kuwa tatizo siyo pesa bali tatizo kubwa ni elimu kuhusu pesa (Financial education). Kwa leo sitajadili kuhusu hili bali nitajadili kidogo jambo linalofana na hilo japo kwa mbali kidogo. Watu wengi walioajiriwa wamekuwa wakitumia nguvu na akili nyingi katika kuwaletea watu wengine utajiri huku wenyewe wakibaki masikini ama watu wa hali ya kati katika maisha yao yote ya utumishi na hata baada ya utumishi na kuishia kutegemea mafao baada ya kustaafu. Wengi pia wamekuwa wakiingia kwenye ajira na kujiahidi kutoka katika ajira na kujiajiri lakini wanakuwa watumishi maishani mwao kwani hawakuwa na dira na mwelekeo wa kuweza kuwatoa huko kwani hujikuta wameshaingia katika mtego wa panya na kujishindwa kujinasua. Hutamani kutoka lakini woga wa kupata pesa unawashikilia. Naamini unajua methali hii ‘’mbio za sakafuni huishia ukingoni’’ndizo mbio ambazo walioajiriwa wengi wamekuwa wakizikimbia, mbio ambazo mwisho wake sote tunaujua kuwa ni kutosonga mbele na wengine kutumbukia katika lindi la madeni kila uchao.

SOMA; Tofauti ya mtazamo Kati ya Mtu wa Hali ya kati na Mtu wa hali Juu.

Naomba sasa nirudi katika lengo halisi la makala hii, kama umeajiriwa ni muda sasa wa kuanza kufanya mambo yako (mind your own business). Mbali na ajira ya kila siku ambayo umekuwa ukiifanya kupata kipato kila baada ya muda fulani mathalan siku, wiki na mwezi ni muda sasa wa wewe kutenga muda wa kufanya shughuli zako mwenyewe za kukufikisha katika kilele cha mafanikio. Tafuta kitu ambacho unaweza kukifanya mbali na ajira yako ya kila siku ili uweze kujiongezea kipato. Mishahara imekuwa haijitoshelezi na ndio maana migomo na ari ndogo makazini haiishi. Hivyo basi kuendelea kulalamika kuwa mshahara ni mdogo bila kufanya juhudi za kuongeza kipato hakutakusaidia lolote.

Unaweza ukaanza kufanya shughuli zako mwenyewe baada ya muda wako wa kazi kuisha unaporejea kutoka kazini. Wakati huu ambapo mradi au biashara yako inakua inahitaji usimamizi wako mkubwa ili iweze kusimama. Kwa muda huu si vizuri kuwaachia watu biashara yako waisimamie bila wewe kuwepo ili kuweza kuikuza zaidi. Wakati huu pia uwe na nidhamu ya fedha ili kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima. Ikiwezekana usitumie kipato chochote unachopata kwenye mradi wako ama biashara yako kwa muda wa hata miezi sita ili ikue na utazame pia kuhusu mwenendo wake. Naomba nikushauri kitu kimoja unapoamua kujifanyia shughuli zako, kama una familia na unategemea ajira yako ikupatie kipato sikushauri uache kazi unayoifanya mapema mpaka biashara yako itakaposimama kama lengo lako ni kujiajiri na kuacha kazi. Kama utaamua kuendelea na kazi baada ya shughuli zakokusimama kuacha kazi na kurudi kusimamia miradi yako itakuwa juu yako mwenyewe kulingana na utashi wako.

SOMA; Dalili Kwamba Unaweza Kufikia Mafanikio Makubwa.

Watu wengi wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua za kuweza kujitegemea na si kutegemea ajira kutokana na woga na kushindwa kufanya maamuzi magumu kwa maisha yao. Kumbuka haya maisha ni yako na hakuna wa kukufanyia maamuzi. Watu wamekuwa wakishindwa kufanya biashara kwa kuogopa madhara (taking risk) na kuamua kuwa kama walivyo. Nikuambie kuwa hakuna mafanikio ya haraka na yasiyokuwa na hatari. Hata katika kusoma kuna hatari zake, muda wowote unaweza kufeli na kila kitu ulichofanya kuwa historia. Unapoanguka hupaswi kukaa chini na kuanza kulia bali kunyanyuka na kusonga mbele huku ukijifunza kutokana na makosa yako. Nikupe mfano katika elimu, katika darasa la watu mia labda walifanikiwa kufaulu sitini kuingia elimu ya sekondari huku arobaini wakishindwa na kurudi mtaani kuendelea na maisha mengine. Kufika sekondari ishirini wanafanikiwa kupata alama za kuendelea na kidato cha tano huku arobaini wakibaki nyuma na wengine kwenda katika vyuo vya kati. Baada ya safari ya miaka miwili ya elimu ya sekondari ya juu wanafaulu kumi na mbili kati ya waliochaguliwa kidato cha tano ambapo kumi kati yao kwenda vyuo vikuu na wawili kwenda vyo vya kati. Kumbuka kuwa watatu hawakufanikiwa kusonga mbele na hivyo kurudi mtaani kupambana na maisha mapya. Baada ya kufika vyuo vikuu saba kati ya wale kumi wanafanikiwa kupata shahada zao na watatu kati yao wakishindwa safari na wao kuungana na hao wengine walioshindwa kuanzia shule ya msingi. Kwa mfano huu nikuambie kuwa kukabiliana na hatari ndio njia nzuri zaidi kuliko kuogopa kujaribu kutimiza ndoto zako kwa kufanya jambo litakalokuletea mafanikio. Kama wale wote walishindwa kuanzia shule ya msingi na hata sekondari waliweza kufanya uwekezaji ni dhahiri kuwa hata wale waliosoma watakuwa wameachwa nyuma. Kwa mfano huu naamini umeelewa kuwa wanaofikia mafanikio makubwa ni wachache sana, naamini na wewe ni mmojawapo. Mwisho basi kwa wewe unayetaka kufanya biashara au mradi fanya tu, usitishwe na hali iliyopo, tafuta kitakachokufanya uwe tofauti na wengine na utaona mafanikio.

Kabla ya kuhitimisha nipende kuzungumzia kuhusu muda. Kila mtu ana muda sawa na kila mtu katika hii dunia na ni bidhaa pekee ambayo kila mtu anayo katika kiasi sawa yaani saa 24 kila siku. Hivyo basi jitahidi kuutumia muda wako kwa faida na si kwa hasara. Kumbuka muda ndio maisha yako. Muda ulionao unakutosha sana kama utaamua kuupangilia. Kama ukitoka kazini punguza mijadala isiyo na tija, punguza kufuatilia mitandao ya kijamii, punguza kuhudhuria sehemu za starehe kama baada hasa baada ya kazi na utumie muda huo kujijenga. Kumbuka hukuja duniani kulipa bili bali kuishi na kufurahia kila siku yako ya maisha. Kama hutafanya shughuli zako (minding yourown business), utakuwa mlipaji wa bili daima na hutafurahia maisha yako.

Mwisho kabisa nikutakie usomaji mwema na mafanikio mema nategemea kukuona katika kilele cha ubora.

Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes ambae ni mjasirimali na mhamasishaji.

Unaweza kuwasiliana na naye kwa: simu: 0712 843030/0753 843030

e-mail:nmyohanes@gmail.com

Pia unaweza kutembelea blogu yake: www.lifeadventurestz.blogspot.comkujifunza zaidi

0 comments: