Haya Ndio Makundi Matatu Ya Watu, Je Wewe Upo Katika Kundi Lipi?



Kuna watu wa aina mbalimbali ambao huwa tunaonana nao na kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kila siku. Watu hawa tunaonana nao barabarani, ndugu katika familia, wafanyakazi wenzetu, waumini wenzetu, marafiki na majirani pia.
Watu hawa haijalishi jinsia ya kiume au ya kike, umri wao au rangi zao, wamegawanyika katika makundi matatu.
Wale wanaoona au wanaosikia unachofanya lakini wasielewe, wale wanasikia unachosema au wanaoona unachofanya wakakukatisha tamaa, na wale wanaoona nakusikia unachofanya wakakutia moyo.
WASIOELEWA
Hawa husikia unachofanya na huwa hawana maoni yoyote juu ya kile kinachoendelea. Hawawezi kukubishia wala kukuunga mkono. Wao husubiri tu kuona hatua inayofuatia. Inawezekana kabisa huwaza juu ya kushinda au kushindwa kwako. Lakini hawawezi kutoa maoni yoyote zaidi ya kusubiri kuona tukio linalofuatia.
WANAOKATISHA TAMAA
Hawa kwa namna moja au nyingine huelewa kile unachofanya , lakini mara nyingi watakuambia maneno ambayo hayakupi moyo wa kuendelea kufanya kile unachokusudia kufanya. Wao hutoa mifano ya watu walioshindwa katika jambo ambalo unalifanya na kukuogopesha kabisa. Mara nyingi watu hawa huwa hawajafinikiwa pia. Hivyo sifa ya watu hawa ni kwamba wao pia hawafamu njia au mbinu zinazoweza kukusaidia kufanikiwa katika kitu unachokifanya, hivyo ushauri watakaokupa unatokana na uzoefu walionao katika vitu walivyowahi kufanya
Mara nyingi watu hawa huamini kuwa wale waliofanikiwa katika eneo hilo walikuwa na bahati au wana uwezo fulani hivi ambao wamepewa na Mungu hivyo si rahisi mtu mwingine kufanikiwa kama wale wenye uwezo huo. Imani yao hiyo ni njia ya wao kujilinda ili kuonyesha kuwa katika juhudi zao hakuna makosa waliyoyafanya ila kuna nguvu tu za ajabu ambazo wengine wanazo na wao hawana ndio zilizotofautisha kufanikiwa kwa wengine na kushindwa kwao.
Ukiwasikiliza na kuwaamini watu hawa lazima utafanana nao na hautaweza kufanya mambo makubwa kwa imani kuwa kuna aina ya watu wamezaliwa kufanya mambo makubwa na wanabahati hiyo.
WANAOTIA MOYO
Watu hawa hukupa mawazo ya matumaini katika jambo ambalo unakusudia kulifanya. Wao hukuelekeza pale unapokosea na kukupa moyo kuongeza juhudi zaidi. Huwa wakweli kama kuna kitu ambacho hufanyi vizuri watakuambia na kukuelekeza namna ya kukiboresha. Au wanaweza kuona kitu ambacho ungefanya vizuri zaidi na wakakuambia kutokana na vipaji walivyoona ndani yako.
Watu hawa mara nyingi huwa ni wale wenye mafanikio na ukikaa na watu hawa kutokana na ushauri wao na mawazo yao utajikuta ukifanana nao na wewe pia kuwa na mafanikio kwani hakuna wakati watakuvunja moyo.
NINI UNATAKIWA UFANYE
Ingawa kuna aina hizi za watu ni vizuri kuamua wewe ungependa kuwa katika kundi gani. Kundi zuri ni hili la kutia moyo kwani kwa kufanya hivi hata wewe mwenyewe huwezi kujikatisha tamaa. Kama unakatisha tama wengine ni vigumu hata wewe kujipa moyo pale mambo yanapokuwa magumu.  Ni vigumu kuendelea mbele hata pale unapokutana na changamoto ndogo.
Ni vizuri kuwa karibu na watu wanaotia moyo na wenye ndoto za kufanikiwa lakini cha kwanza ni wewe kuwa na mawazo chanya , kuwa mvumilivu na kujipa moyo ili kufikia kiwango kile unachotaka katika eneo lolote lile. Kwa kufanya hivyo sio rahisi mtu mwingine akakurudisha nyuma hata kama changamoto zitakuwa nyingi kiasi gani.

Nakutakia utekelezaji mwema wa haya uliyojifunza.
Kama una swali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com





0 comments: