Maazimio Matano Muhimu Ya Fedha Kwa Kila Kijana Kuweka Mwaka Huu 2015.

Bado tupo kwenye msimu wa mwaka mpya na huu ni wakati muhimu wa kuweka maazimio na malengo mbalimbali ili kuboresha maisha yetu zaidi.

Huenda tayari umeshaweka malengo na mipango yako ya mwaka 2015, leo tutakumbushana mambo machache ambayo ni ya muhimu sana kuyajumuisha kwenye malengo yako ya mwaka huu 2015.

Kama bado hujaweka malengo mpaka leo bado hujachelewa, unaweza kukaa chini leo na kuandika malengo yako kwenye karatasi na kuanza kuyafanyia kazi.

Kama huna mpango wa kuweka malengo kabisa kwa mwaka huu pole…

100_7560 ED1

Yafuatayo ni maazimio muhimu kuweka kwenye malengo yako ya kifedha kwa mwaka huu 2015;

1. Weka akiba zaidi ya ulivyoweka mwaka jana.

Kama mwaka jana ilikuwa unaweka akiba, mwaka huu ongeza kiwango cha akiba unachoweka. Kama huna utaratibu wakujiwekea akiba kabisa anza na kuweka pembeni asilimia 10 ya kile unachopata. Ukipata elfu kumi, weka elfu moja pembeni. Ukipata laki moja weka elfu kumi pembeni. Baada ya muda mfupi utaona mabadiliko makubwa ya kifedha kwenye maisha yako.

2. Punguza madeni yako.

Madeni ni mzigo, madeni ni utumwa, mtu anayekudai anaweza kunyanyasa utu wako muda wowote. Mwaka huu weka azimio la kupunguza madeni yako na kama ikiwezekana lipa yote kabisa. Kaa chini na wale wanaokudai na wape pendekezo la njia rahisi kwako kuwalipa kisha anza kuwalipa. Utanunua uhuru wako ulioupoteza.

3. Tengeneza, badilisha bajeti yako.

Ni muhimu sana kuishi kwa bajeti, kama mpaka sasa huna bajeti tafadhali sana tengeneza bajeti yako leo. Amua ni kiasi gani utakachoishi nacho kwa siku, wiki na hatimaye mwezi. Na jitahidi sanakuishi kwa kiasi hiko, usinunue vitu kwa tamaa tu, nunu kile ulichopanga kwenye bajeti. Kama umepanga mwezi huu hununui nguo, usishawishike kununua nguo hata ukikutana nayo nzuri kiasi gani, nguo nzuri huwa haziishi. Siku ambayo bajeti yako inaruhusu utapata nzuri kuliko uliyokutana nayo.

4. Jifunze kuhusu uwekezaji.

Bila shaka uwekezaji ni somo gumu sana kwa vijana. Wengi hawapendi kusikia kitu hiki na huona ni kitu kinachohitaji elimu kubwa. Ukweli ni kwamba uwekezaji ni rahisi na ni njia rahisi kwako kukuza kipato chako. Kuna aina nyingi za uwekezaji, kuna uwekezaji wa kununua mali, uwekezaji wa fedha na kadhalika. Unaweza kuanza kujifunza hapa hapa kwa kubonyeza maandishi haya

Soma; Hivi ndivyo unavyoweza kutajirika kwa kuanza na shilingi elfu moja.

5. Jijengee nidhamu ya fedha.

Kama hutakuwa na nidhamu ya fedha, yote tuliyojadili hapo juu hayataweza kukusaidia. Mara zote tumia pungufu ya unachokipata, yaani matumizi yako yasizidi mapato yako. Na pia kwenye kuweka akiba weka akiba na inayobaki ndio ufanye matumizi. Ukifanya matumizi ili inayobaki ndio uweke akiba hutabakiwa na kitu.

Wewe kama kijana ni muhimu sana kwako kujijengea misingi imara ya kifedha na kiuchumi. Weka maazimio hayo matano muhimu mwaka huu 2015 na anza kuyafanyia kazi.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322

0 comments: