Hili Ndilo Kosa Kubwa Tunalokwenda Kufanya Watanzania 2015.
Mwaka 2015 ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu sana na watanzania wengi umekaribia kabisa kufika. Huu ni mwaka ambao uchaguzi mkuu wa nchi yetu utakwenda kufanyika na hivyo wananchi kupata nafasi ya kuchagua diwani, mbunge na raisi ambaye tunaona anatufaa.
Mwaka 2015 umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu kwa sababu wananchi wengi tumeaminishwa na kuamini kwamba baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 na chama tawala kuondoka madarakani maisha yetu yatakuwa mazuri sana. Ni imani nzuri sana ambayo tumekuwa nayo hasa ukizingatia hali ya nchi kiuchumi ipo chini sana ukilinganisha na rasilimali tulizonazo.
Pamoja na kuwa na imani hii nzuri, kuna kosa kubwa sana ambalo watanzania tutakwenda kulifanya mwaka huo 2015. Kosa hili litatugharimu tena miaka mingine mitano au hata zaidi ya hapo kama hatutaendelea kujifunza.
Kosa hili kubwa ni kutokuwa na vigezo vya kiongozi tunayemtaka sisi wananchi. Na kwa kukosa vigezo hivi tutarudia makosa ambayo tuliyafanya nyuma kwa kuchagua watu kutokana na umaarufu wao. Kutokana na kuangalia umaarufu tumechagua viongozi wengi ambao wameishia kutuangusha na kushindwa kutimiza ahadi zao wenyewe.
Ni lazima sisi kama wananchi bila hata ya kuambiwa na wanasiasa, tuwe na vigezo vya aina ya kiongozi tunayemtaka. Na hii ni kuanzia udiwani, ubunge na uraisi. Lazima sisi tuwe na vigezo vyetu kisha wale watakaojitokeza kuomba nafasi hizo tuwachuje kwa kutumia vigezo vyetu.
Ilivyo sasa ni kwamba wananchi hatuna vigezo vyetu, ila tunatumia vigezo vya wagombea watakavyotuletea na hivyo tunaweza kulinganisha baina ya mgombea na mgombea na kuamua kumchagua mmoja wao. Hapa ina maana kama wagombea wote ni wabovu tutamchagua ambaye ni ahueni. Na hapa ni kwa sehemu ndogo, shemu kubwa itatumia kigezo cha umaarufu.
Ni kigezo hiki cha umaarufu ambacho kinawafanya watu sasa hivi kuitisha mikutano ya waandishi kila kukicha kutangaza nia zao za kugombea uongozi. Ni kigezo hiki cha umaarufu ambacho kinawafanya watu kuzunguka huku na kule kutoa misaada ili waonekane wanajali sana.
Sasa watanzania tuache kufanya kosa hili ambalo litaendelea kugharimu maisha yetu.
Katika makala zijazo tutazungumzia ni vigezo gani tunaweza kuvitumia katika kila nafasi ya uongozi ili tuweze kupata viongozi bora.
Tanzania ni nchi yetu sote, unapopata ujumbe huu wajulishe na wenzako wote unaowafahamu ili tuweze kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu.
Usisahau kuweka email yako ili upate makala hizi moja kwa moja kwenye email yako.
TUKO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment