Mambo Matano Ambayo Viongozi Bora Hufanya Kila Siku.
Karibu tena ndugu msomaji kwenye mtandao huu ambao umejikita kwenye kukujenga wewe kuwa kiongozi bora. Kwa siku za hivi karibuni hakujakuwa na makala mpya hapa kutokana na mambo yaliyoingiliana kidogo. Hata hivyo napenda nikukaribishe tena katika shule hii ya uongozi na kila jumapili utaendelea kupata makala za mambo ya uongozi.
Kama tulivyoona kwenye moja ya makala zilizopita kiongozi anatengenezwa na sio kuzaliwa. Ile dhana kwamba viongozi bora wanazaliwa sio kweli, bali viongozi bora hutengenezwa na mazingira waliyozaliwa na hata kukulia na pia elimu wanayoipata. Hivyo kama kuna mtu alikwambia wewe huwezi kuwa kiongozi kuanzia leo usikubali tena kauli hiyo.
Pia tuliona ni muhimu sana kila mtu kuwa kiongozi kwa sababu viongozi ndio wanaopata mafanikio makubwa kwenye jambo lolote linalofanyika na binadamu. Iwe kazi, biashara na hata familia, unapokuwa na tabia za uongozi bora unapata mafanikio makubwa zaidi.
Leo tutaona mambo matano ambayo viongozi bora hufanya kila siku, anza kufanya mambo haya ili uweze kuwa na uongozi bora kwenye jambo lolote unalofanya.
1. Kujifunza.
Viongozi bora hujifunza kila siku na hii huwasaidia kujua mambo mengi na hivyo kuwasaidia katika kufanya maamuzi. Kama hujifunzi kila siku ni vigumu sana kuwa kiongozi bora. Viongozi bora hujifunza kwa kujisomea na pia hujifunza kutokana na uzoefu wao na uzoefu wa watu wengine.
2. Kupangilia siku yao.
Viongozi bora hupangilia siku yao kabla hawajaianza. Hujua watafanya kitu gani na katika muda gani. Kupangilia siku humwezesha kiongozi bora kukamilisha majukumu yake muhimu na kuweza kuwa na matumizi mazuri ya muda.
3. Kugawa majukumu kwa wengine.
Viongozi bora wanajua hawawezi kufanya kila kitu wao wenyewe, hivyo kila siku hutafuta njia za kugawa majukumu kwa watu wengine. Hii huwawezesha viongozi kubaki na majukumu machache ya msingi ambayo huyatekeleza kwa ufanisi mkubwa. Ili kuwa kiongozi bora acha kung'ang'ania kufanya kila kitu mwenyewe.
4. Kutengeneza viongozi wengine.
Viongozi bora hutambua kwamba kutengeneza viongozi wengine ni jukumu lao. Hivyo kila siku wanatengeneza viongozi wengine kwa kuwa washauri wazuri wa watu waliochini yao ili waweze kujiongoza na kuongoza wengine.
5. Huwasiliana vyema.
Viongozi bora hufanya mawasiliano mazuri kila siku kwa sababu wanajua mawasiliano yanaweza kuwajenga au kuwabomoa kama viongozi. Mawasiliano haya bora huyafanya wakati wanakutana na wengine, wakati wanaendesha vikao au mikutano na hata wakati wanafanya mawasiliano kwa simu. Viongozi bora hujua ni lugha ipi ya kutumia ili kuweza kufikisha ujumbe na ujumbe huo uwe na ushawishi mkubwa.
Mpaka sasa wewe ni kiongozi kwa sababu umeonesha nia ya kujifunza zaidi sasa unaelekea kwenye uongozi bora. Ongeza mambo hayo matano kwenye maisha yako ya kila siku na utaona mafanikio makubwa ya uongozi.
Kama una maoni yoyote tafadhali tushirikishe kwenye sanduku la maoni hapo chini.
Usisahau kuweka email yako kwenye box hapo juu ili kupata makala mpya kwenye email yako kila zinapochapishwa.
Nakutakia kila la kheri katika uongozi wako.
TUKO PAMOJA.
8/24/2014 09:25:00 AM
|
|
This entry was posted on 8/24/2014 09:25:00 AM
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
0 comments:
Post a Comment