Sababu Mbili Kwa Nini Tanzania Ni Nchi Masikini.

Kwa nini Tanzania ni nchi masikini? Pamoja na rasilimali nyingi tulizonazo, mlima mrefu, mbuga za wanyama, madini na hata ardhi kubwa kwa nini tunaendelea kuwa masikini?
Hili ni swali gumu sana maana hata raisi wa nchi mheshimiwa Jakaya Kikwete alikiri kwamba hajui kwa nini nchi yetu ni masikini. Sasa leo nataka tujadiliane nini kinatufanya tuendelee kuwa kati ya nchi masikini sana duniani licha ya rasilimali nyingi tulizonazo.
Katika moja ya vitabu vyake Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika kwamba ili tuendelee tunahitaji vitu vinne. Vitu hivyo ni WATU, ARDHI, SIASA SAFI na UONGOZI BORA. Katika vitu hivi vinne kuna viwili ambavyo tunavyo vya kutosha na viwili ambavyo tumekosa na ndio maana tunaendelea kuwa masikini.


Vitu viwili tulivyonavyo.

Katika vitu hivi vinne tunavyohitaji ili kuendelea, viwili tayari tunavyo, vitu hivyo ni;
1. Ardhi. Tunayo ardhi kubwa sana ya kutosha. Sehemu kubwa ya ardhi ya tanazania bado haijatumika kabisa. Na sehemu kubwa ya ardhi yetu ina rutuba na hivyo inafaa kwa kilimo cha kila aina. Nenda katika kila mkoa utakuta kuna mazao fulani yanayokubali sana. Hata maeneo ya katikati ya nchi ambayo yana asili ya ukame bado kuna mazai yanakubali vizuri.
Lakini ardhi hii sasa iko hatarini kutoweka kutokana na ukosefu mwingine tutakaouona baadae.
2. Watu. Katika sensa ya mwaka 2012 tanzania ina watu zaidi ya milioni 45. Na wengi katika watu hawa ni vijana. Kwa watu wote hawa tulionao, kama wangeweza kutumiaka vizuri tungeweza kufikia maendeleo makubwa sana.

Vitu viwili ambavyo tumekosa.

1. Siasa safi. Kila nchi duniani inaendeshwa kwa siasa. Tanzania tuliwahi kuwa na siasa ya UJAMAA NA KUJITEGEMEA, ambayo ilikwenda vizuri sana mpaka pale ilipouliwa, tumewahi pia kuwa na SIASA NI KILIMO ambapo kilimo kilipewa kipaumbele kwa sababu ndio sehemu kubwa ya wananchi wanategemea kilimo. Lakini nayo haikudumu muda mrefu. Tuliwahi pia kuwa na SIASA YA UWEKEZAJI NA UBINAFSISHAJI ambapo tulishuhudia mashirika ya umma yakipewa watu binafsi na wengi wao kutoka nje ya nchi. Sasa hivi sina hakika tunaendeshwa na siasa gani.
Tumekosa siasa safi na ndio maana tumeshindwa kutumia rasilimali zetu na hata watu wengi tulionao kuweza kufikia maendeleo kama taifa.
2. Uongozi bora. Hili ndio tatizo kubwa sana na ndio linazaa matatizo mengine yote. Tumekosa uongozi bora ambao unaweza kuwatengeneza na kuwatumia watu tulionao kuweza kufikia mafanikio. Tumekosa uongozi bora ambao utatengeneza siasa safi ambayo itatuwezesha kutumia watu wetu na rasilimali zetu vizuri.
Tunao watu wengi ambao wanashikilia nafasi za uongozi ila wamekosa sifa za uongozi. Watu hawa ndio wanafanya maamuzi mabovu na hivyo kutufanya tuendelee kuwa masikini.
Hii ndio sababu kubwa iliyonifanya niwe naandika kuhusu uongozi kwenye blog hii kila siku ya jumapili. Kama umekosa kusoma makala za uongozi zilizopita, bonyeza maandishi haya ili uweze kuzisoma.

Tufanye nini ili kuondoka kwenye umasikini huu?

Kwa kuwa tumeshajua mambo mawili muhimu tunayokosa ili kufikia maendeleo na kwa kuwa tumeshajua ukosefu wa uongozi bora ndio tatizo kubwa zaidi nashauri sisi wananchi tuchukue hatua ya kujua na kuchagua viongozi bora. Na nashauri hasa vijana tujifunze sana kuhusu uongozi na kisha tugombee nafasi mbalimbali za uongozi ili tuweze kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu.
Kukaa tu na kulalamika kila siku hakutakuwa na msaada kwetu binafsi na hata kwa vizazi vijavyo. Kuna chaguzi zinakuja mwaka huu na mwaka ujao, tutumie nafasi hii kujua ni viongozi wapi wanaotufaa na wapi wasiotufaa. Tukiendelea kufanya makosa haya katika uchaguzi wa viongozi tutaendelea kuwa masikini siku zote.
TANZANIA NI NCHI YETU SOTE, TUSHIRIKIANE KUIJENGA.

0 comments: