Uongozi Ni Watu, Na Sio Vinginevyo.
Kama nikikuuliza swali ni nani muhimu kati ya kiongozi na mwananchi anayeongozwa?
Kwa hali ya kawaida na mazoea tuliyonayo sisi, unaweza kufikiri kiongozi ni bora zaidi ya mwananchi. Lakini huu sio ukweli hata kidogo.
Sio ukweli kwa sababu bila ya mwananchi anayeongozwa hakuna kiongozi, kiongozi ni mwakilishi wa wale waliompa nafasi ya kuwawakilisha. Sasa inakuwaje mtu huyu aliyepewa nafasi awe bora zaidi ya wale waliompa nafasi hiyo?
Kuna utamaduni ama mazoea mabaya ambayo yamejengeka kwenye jamii yetu yanayowafanya viongozi kujiona ni bora kuliko wale wanaowaongoza. Au kujiona ni muhimu zaidi ya wale ambao wamewapa nafasi ya kuwawakilisha.
Haya ni mazoea mabaya sana ambayo yalipata nafasi kutokana na watu wengi kutokuwa na uelewa mzuri kwenye mambo ya uongozi. Ila kwa sasa asilimia kubwa ya watu wana uelewa mzuri sana juu ya wajibu wao na wajibu wa viongozi wao.
Hivyo kwa kizazi kipya cha viongozi ni vyema tukafahamu huu mtazamo wa zamani wa uongozi umekufa na hautoweza kukusaidia. Wewe kama kiongozi unayejitengeneza jua watu ni muhimu kama ulivyo wewe kiongozi. Watu wana nafasi kubwa sana kwenye mafanikio ya uongozi wako.
Ule utamaduni wa viongozi kutaka kupata huduma bora kwa sababu wao ni viongozi hauwezi kukujenga na kukupa mafanikio. Kwa kusema hivi pia sisemi kiongozi apate huduma mbovu ili aonekane yuko na wananchi. Bali kiongozi ahakikishe wananchi wanapata huduma bora kama anazopata yeye.
Lakini hili halitokei kwa sababu baada ya kiongozi kupata huduma bora anasahau kwamba wananchi wanapata huduma mbovu. Na hata akiambiwa haoni uzito sana kwa sababu huduma hizo mbovu hazimuumizi moja kwa moja.
Ni mara ngapi tumeona mtu akiwa na uchungu sana kabla ya kuwa kiongozi ila anapokuwa kiongozi anasahau yale aliyokuwa anayalalamikia? Wanasema madaraka matamu, ila usianguke kwenye shimo hili. Jua watu unaowaongoza ni muhimu sana kama ulivyo wewe na baada ya kujua hili hakikisha unafanya kila juhudi kulinda umuhimu wao.
Karibu katika darasa letu la uongozi ambapo kila jumapili unapata makala nzuri inayohusu uongozi. Tembelea mtandao huu kila mara ili kujifunza mengi zaidi. Karibu tujenge kizazi kipya cha uongozi ambao utaleta tija kwenye nchi yetu Tanzania.
7/27/2014 08:28:00 AM
|
Labels:
UONGOZI
|
This entry was posted on 7/27/2014 08:28:00 AM
and is filed under
UONGOZI
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
0 comments:
Post a Comment