Kama Umewekeza Kwenye Majengo Yafahamu Magonjwa Sugu Yanayo Athiri Majengo.

Kama ilivyo kwa viumbe hai kuathiriwa na mazingira wanayoishi ndivyo ilivyo kwa viumbe visivyo hai ikiwemo majengo. Majengo huweza kuhimili mazingira kutokana na namna yalivyobuniwa na kujengwa katika mazingira yaliyopo. Hata ujenge majengo mazuri na makubwa kiasi gani, kama hayajabuniwa na kujengwa kutokana na mazingira husika majengo hayo huwa hatarini na watumiaji wa majengo hayo huwa kwenye majanga mazito kwa kujua au kwa kutokujua. Mbaya zaidi huwa hasara kwa mmiliki wa jengo husika. Kwa mujibu wa taaluma na ufahamu nilionao unaweza kujenga majengo mahali popote iwe ardhi tambalale, mabondeni, milimani, kando ya mito na hata baharini maadamu ikidhi ubunifu na ujenzi uzingatie mazingira husika. Kwenye makala zijazo nitaeleza hayo kwa ufasaha zaidi, lakini leo naomba uyafahamu magonjwa yanayoathiri majengo yako ili uweze kuyakinga na yadumu kwa muda mrefu kwa kuwa ujenzi ni uwekezaji na hugharimu fedha nyingi.




Nyufa
Nyufa ni uwazi unaosababishwa na utengano wa mihimili ya jengo uliokuwa muunganiko hapo awali. Nyufa zinapotokea kwenye jengo tambua kuwa jengo lako lipo katika tabu fulani, nyufa ni lugha kuu ya majengo kumjulisha mtumiaji kuwa lipo kwenye kashkashi. Nyufa husababishwa na matokeo mengi na utagundua tatizo kutokana na mwelekeo wa nyufa hizo na mahali ulipotokea. Kama nilivyoeleza hapo awali udhaifu wa majengo ni matokeo mabovu ya ubunifu na ujenzi kwa mazingira husika. Unachopaswa kufanya hapa ni kugundua tatizo na kuliweka sawa ndipo uzibe ufa. Watu wengi huishia kuziba ufa pasipo kushugulikia chanzo chake, kitendo hiki ni sawa na kuuficha ufa ili usiendelee kuuona machoni lakini tatizo linabaki palepale.
SOMA; Mambo Ya Kuzingatia Na Njia Bora Za Uwekezaji Wa Majengo Kwa Gharama Nafuu.
Kutitia kwa majengo
Ni kawaida kutitia kwa majengo lakini linapozidi kiwango huwa ni tatizo na hatari kwa watumiaji. Tatizo hili husababishwa na ukadiriaji hafifu wa tabia za udongo kwenye kiwanja cha jengo husika. Mara nyingi jengo hutitia kutokana na aina tofauti za udongo kwenye kiwanja kimoja au kimo cha msawazo wa msingi kuwa tofauti, pia ubunifu hafifu wa udongo kulingana na uzito wa jengo husika. Hatari kuu huwa kwenye majengo marefu na kwenye vyoo vya shimo. Cha kusikitisha mara zote serikali yetu huwajengea watoto wetu vyoo vya mashimo lukuki mashuleni jambo ambalo ni hatari kutokana na udhaifu wa muundo wa vyoo hivyo. Ni muhimu kutenganisha shimo na chumba cha choo kwa usalama wa watumiaji ili tusiendelee kupoteza watu na kufunga shule eti vyoo vimebomoka.
Majengo kupitisha maji
Maeneo mengi ya Tanzania yamezungukwa na vyanzo vya maji ambavyo ni bahari mito na maziwa hali inayosababisha ardhi yake kusharabu maji karibu majira yote ya mwaka na mbaya zaidi wakati wa mvua. Maeneo mengi ya pwani majengo mengi yameathiriwa na tatizo hili na hata limekuwa kero kwa wakazi na watumiaji wa majengo hayo. Majengo hupitisha maji kwa njia ya sakafu na kuta mithili ya chujio au chemchemu. Mara nyingi utagundua kwa kuona ardhi yake imetota maji wakati wote wa majira ya mwaka. Pia majengo mengi ya maeneo haya yanaoza na kutitia kwa haraka na hata mashimo ya vyoo vya maeneo hayo huinuka kwenda juu na siyo chini jambo ambalo ni hatari kwa afya za wakazi. Katika hali hii kuta na sakafu huoza kwa haraka kutokana na maji yaliyopo chini ya ardhi kuwa na kemikali mbalimbali zilizopo kwenye maji hayo. Katika mazingira haya lazima yatumike malighafi sahihi za kuzuia maji hasa wakati wa ujenzi.
SOMA; Kama Utashindwa Kufanya Chochote Utakachojifunza, Basi Fanya Hiki Kimoja Tu, Na Maisha Yako Yatagusa Wengine.
Kuoza kwa kuta
Moja ya masahibu yanayoyakumba majengo ni kuoza kwa kuta za tofali au chuma. Hali hii hutokana na unyevunyevu na kemikali mbalimbali kupitia maji kukaa kwa muda mrefu kwenye kuta hali inayoathiri ubora wakuta hizo. Pia hali hiyo husababishwa na kumea kwa mimea au kupanda maua kwenye viambaza vya kuta ambapo baadhi ya mimea hiyo kusababisha ukungu wa kijani kwenye kuta ambao huzalisha fangasi mbalimbali wanaokula kuta. Pia kitendo cha kumwagilia maua kwenye kuta huozesha kuta haraka. Kinga kuta zote zithiathiriwe na hali ya hewa na maji pale inapolazimu na Usiruhusu mimea kumea kwenye viambaza vya kuta.
Kuoza kwa paa
Unapaswa kutambua kuwa kila kilichoumbwa kina mwisho, ndivyo ilivyo hata kwenye majengo, kila aina ya malighafi iliyotumika hufika mwisho wake kwa wakati tofauti kulingana na ubora na namna yalivyotumika katika ujenzi. Kuoza kwa paa hutegemea ubora na aina ya malighafi zilizotumika bila kusahau na kimo cha mwinuko wa paa hilo. Paa huathiriwa na hali ya mazingira ya eneo husika, mfano paa zilizopo ukanda wa pwani huthiriwa na chumvichumvi zinazobebwa na mikondo ya upepo uvumao kutoka baharini hali inayosababisha paa kuoza haraka, pia hali ya mwinuko ukiwa mdogo husadia paa kuhifadhi takataka mbalimbali ikiwemo majani ya mimea, hali hii ya uchafu kukaa muda mrefu huozesha paa haraka. Unapaswa kuweka paa lenye ubora kulingana na mazingira halisi. Inasikitisha kuona hadi leo hii bado kuna nyumba za serikali zimeezekwa vigae vya asbestos ambavyo ni hatari na vimepigwa marufuku kwa matumizi ya binadamu.
Kusinyaa na kutanuka kwa milango na madirisha
Kuna shida sana hapa, watu wengi hujikuta wakiwalalamikia sana mafundi kuwa hawafai na wamewatia hasara. Kuna aina nyingi za malighafi zinazotumika kutengenezea milango na madirisha, kila aina ya malighafi hizo zina faida na hasara zake. Karibu aina zote za malighafi zina tabia ya kusinyaa na kutanuka kutokana na hali ya hewa (jotiridi) ya mazingira nyumba zilipo. Tumia mbao ngumu (treated hardwood) ili kuondokana na tatizo hili, usitumie mbao mbichi zitakusumbua sana siku zijazo. Kwa wale wanaotumia madirisha na milango ya vioo na aluminiam ni lazima wayapachike na kufitisha kwenye mbao na siyo moja kwa moja kwenye kuta ili kuruhusu hali ya kusinyaa na kutanuka, usipo fanya hivyo aluminiam hupinda na kuleta shida ya kufunga na kufungua. Pia kama unatumia madirisha haya ya vioo (sliding windows) ni lazima yawe makubwa ili kuruhusu hewa kuingia na kutoka kwa haraka kwa kuwa madirisha haya hufunguka nusu tu. Kumbuka kuweka vitasa sahihi kulingana na matumizi, Zingatia sana haya kwa kuwa kila unachoweka kwenye nyumba ni fedha hivyo usiache watu wafanye hovyohovyo tu, ni kero na hasara, wewe na wateja wako hamtafurahia mazingira ya nyumba hiyo.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888, Email: kimbenickas@yahoo.com

0 comments: