Wajue Watu Hawa Wanaokazana Kukurudisha Nyuma Na Jinsi Ya Kuwashinda.

Kuna watu katika jamii wapo kwa ajili ya kukufanya ushindwe, wapo kusubiri kuona ukiharibikiwa, wanafurahia kupata habari mbaya za kukuhusu, wanakaa kusubiri kuona kwamba umeshindwa kumaliza masomo yako, wanasubiri kuona kwamba hiyo biashara imekushinda, wanasubiri kusikia kuwa umefukuzwa kazi. Lakini tambua hawaishii kutamani hayo tu bali wengi huenda mbali zaidi kwa kuwafuata watu na kuwapa taarifa za mabaya yako hata kama si ya kweli, wengine hata wakisikia mtu anakuongelea vizuri au kukusifia watajitahidi kuonyesha kwamba wewe ni mbaya haustahili sifa hizo, wanaweza kukukosesha hata kazi au mambo mengi ya muhimu.
SOMA; Ukiendelea Na Maisha Haya Watu Watakunyanyasa Sana…
Lakini pia tambua watu hawa wanaweza kuwa ni watu wako wa karibu sana tu, watu wanaokufahamu vyema tu , hivyo wakati mwingine wanakuwa wana uhakika na wanachokisema au kukiongea mbele za watu, wanafurahia kuona mabaya yako yakijulikana nje, wanafurahi kuanika wazi udhaifu wako na wanapofanya hivyo wanasahau kwamba hakuna binadamu aliye mkamilifu, maana kila mwanadamu aliyezaliwa ana madhaifu yake na hata wao kwa kufanya hilo wanasahau kuwa wanaonyesha na kuweka wazi udhaifu wao pia, maana kama wanaweza fanya hayo kwako uliye mtu wao wa karibu je kwa asiye wa karibu hivyo wakati mwingine humfanya hata anayepokea habari hizo kushindwa kuwaamini hata kwa kufanya nao mambo mengine zaidi , maana tayari wanakuwa wameonekana si watu wema.
Kwa kutambua kuwa tuna watu wa aina hiyo, hutakiwi kuwafuatilia sana au kuacha kufanya yale unafanya na kuwaangalia hao na kuwasikiliza. Haijalishi watakuchafua kwa kiasi gani wewe endelea kufanya kile unafanya, ongeza bidii na maarifa katika kufanya hicho unafanya. Nadhani unaufahamu ule msemo unaosema kwamba mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe, hivyo tambua mpaka wakutakie hayo mabaya, mpaka wakufanyie yote hayo tambua kipo kitu cha ziada unacho ambacho wao hawana. Kuna kitu cha thamani wameona ndani yako na wanaona hawawezi kuwa nacho au wanaona kitakufaa sana maishani, hivyo wanatumia kila njia kukufanya ujione mnyonge au uache kufanya hilo jambo. Wanatafuta namna ya kukuhamisha hapo, wanatafuta namna ya kukupoteza ndugu yangu, huenda ni wivu tu unawasumbua , sasa kwanini ukubali au kuruhusu matatizo ya mwingine yakuzuie kuendelea na safari yako? Unajua kwanini unafanya hivyo, unajua kwanini upo hivyo, hiyo inatosha sana, usisubiri kuona kila mtu anakubali unachofanya, usitegemee hilo maana kwanza haliwezi kutokea katika dunia yetu hii, wengi wa watu wamezoea kuona kwamba kuna baadhi ya vitu haviwezi kufanywa na watu wa aina fulani, sasa mtu huyo akiona wewe unafanya hivyo vitu na wakati upo kwenye kundi la wasioweza unafikiri atakuunga mkono? Anaweza kukufanya ushindwe, ujiuone huwezi , anaweza kufanya upoteze dira kama utakuwa hujielewi, kama hujui nini unataka maishani mwako atakupoteza tu. Hivyo wewe kujielewa inakutosha sana.
SOMA; Kitu Pekee Unachoweza Kukidhibiti Kwenye Maisha Yako.
Amua kuishi wewe, kuishi maisha yako, kuishi ndoto yako usisikilize kelele zisizokuhusu, chagua kitu cha kuilisha akili yako, kaa na watu wenye mtazamo sahihi juu ya unachofanya watakupa moyo wa kusonga zaidi, hata pale ambapo huwezi watakutia moyo tu, watatamani kuona unafanikiwa, unaishi ndoto yako, mafanikio yako ni furaha kwao , hawa ndio watu unatakiwa kuwa nao, lakini hao wanaosubiri anguko lako, wanaosubiri uharibikiwe waache hivyo, wamechagua fungu hilo huwezi kuwabadilisha. Ila wanaweza kushangaa jinsi watakavyopoteza muda wao kusubiri anguko lako milele, maana ikiwa unajitambia haitatokea kamwe, maana kelele zao ni kama zinakufanya uzidi kufanikiwa tu maana wewe ndio kwanza unazidi kufanya kazi kwa bidii. Kataa kuwapa sababu ya kucheka, kataa kuwafanya waone walichoksiema kwako ni kweli kwa kukazana kuiishi ndoto yako.
Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu wa Tehama, lakini anaandika makala katika muda wake wa ziada kwa ajili kuelimisha jamii.
Ms.Beatrice Mwaijengo
+255755350772
bberrums@gmail.com

0 comments: