Jinsi Unavyoweza Kutumia Changamoto Kama Fursa Ya Kujifunza Zaidi.
Kuna wakati katika maisha tunakutana na changamoto ambazo zinatulazimisha kuacha au kusimama kabisa kuishi ndoto zetu au kuzitimiza.
Ndugu yangu huenda kweli unapitia kitu ambacho ukikiangalia unaona ni kweli hutakiwi kuendelea na mambo mengine, pengine kwa kuwa hauna uwezo tena na nguvu za kufanya hayo mambo, lakini hata katika hali hiyo kipo unachoweza kujifunza, kipo unachoweza kufanya kama tu utaamua kubadili namna unavyoangalia mambo na kuyachukulia. Unaweza tumia hiyo changamoto kama fursa ya kupata au kujifunza mambo mengine hata kwa watu wengine unaokutana kutokana na changamoto hiyo. Usiiangakie changamoto hiyo tu mpaka ukashindwa kupata kile ulitakiwa upate hapo, bali hakikisha unapata kile ulikusudiwa kukipata kwenye changamoto hiyo, hakikisha unaelewa somo, hakikisha unapotoka hapo unakuwa ni mtu mwingine , unakuwa umejifunza kitu, unakuwa una kitu kipya cha kujifunza au hata kushirikisha wengine. Hata kama ni tatizo kubwa kiasi gani bado lipo unaloweza kujifunza hapo kama tu utaamua kubadili namna unavyotazama mambo ndugu yangu.
SOMA; Najua Umeshasikia Hili Mara Nyingi, Sio Vibaya Ukasikia Tena Na Leo.
Unaweza kuwa unaumwa , umelala kitandani huwezi lakini bado unaweza kujifunza hata kwa kulala kwako pale maana bado unakuwa na uwezo wa kufikiri na kutafakari mambo na pengine hata kuona jinsi mambo yanavyoenda. Unaweza jifunza hata kwa kuangalia wale wanakuhudumia au wanaokuja kukutembelea jinsi wanavyochukulia hali yako, lipo unaloweza kujifunza pale ndugu, maana mfano ukiangalia wewe ndiye unayeumwa na pengine unaelewa zaidi maumivu unayopitia, unaelewa zaidi hali unayoipitia lakini mtu mwingine anaweza jidai au dhani kwamba kwa kuwa alishawahi ona mtu mwenye tatizo kama lako basi atafikiri anayaelewa hata maumivu yako, kwa kuwa analinganisha na ya yule huyu unatakiwa kumwelewa na kwenda naye kama alivyo. Mwingine atajidai ni mtaalamu zaidi ya daktari hivyo anaweza akatumika kukuchanganya zaidi badala ya kuwa pale kukufariji, mwingine atakuja pale kuona jinsi gani unaumwa na apate cha kwenda ijuza jamii au naye aonekane alikuja na anakujali lakini kumbe lengo ni apate tu cha kwenda kuongea kwa watu. Lakini mwingine ni kweli anajali, anakupenda anaumizwa na hali unayopitia anatamani kuona ukiinuka,ukisimama tena na kuendelea na harakati za maisha huyu ni mtu mwema kwako, ni ndugu/rafiki mwema anakupenda kweli, anakutakia mema na huyu anakufanya hata wewe usiangalie kile unapitia na kujifunza hata kwa huyu kwa namna anachukulia hali yako na kwa upendo anakuonyesha katika wakati huu, anakufanya uone kama una deni kwake na jamii kwa ujumla kwa namna amekubeba katika hali unayopitia, katika jamii hawa ni wachache sanaa.
SOMA; Hiki Ndio Kitakachotokea Miaka 100 Ijayo..
Lakini wakati mwingine unapokuwa kwenye changamoto au niseme mitihani ya maisha inaweza kuwa wanaokuzunguka ndio wanakatishwa tamaa zaidi na hali unayopitia hivyo badala ya wewe kutaka au kutegemea kuhurumiwa zaidi unaweza geuka msaada kwao kwa kuwafariji, kuwatia moyo kuwafanya wasikate tamaa, waamini kwamba inawezekana kuinuka tena, inawezekana kusimama tena na hata isipowezekana wanatakiwa kukubali kuwa haijalishi nini kinatokea , haijalishi wanakutana na nini maisha huwa ni lazima yaendelee, kuwafanya wasiwe watu wa kukata tamaa, kuwafanya hata katikati ya huzuni waweze kuona sababu ya kucheka, sababu ya kufurahi, wasiangalie ukubwa wa kile wanapitia , wasiangalie pale wanapitishwa bali wahakikishe wanaelewa kwanini wanapita pale, lengo haswa ni nini? Wahakikishe wameelewa lengo la kupita pale, wahakikishe wameelewa somo sawasawa ili liwafae katika maisha yao.
SOMA; Siku Ya Furaha, Kifo Cha Furaha…
Wanatakiwa wajifunze kuwa kusikitika, kuumia, kulalamika juu ya hali fulani ngumu unayopitia haiwezi kubadili kitu , haiwezi badili ukweli bali wanatakiwa kujifunza kukabiliana na hali zilizopo wakiwa na mtazamo sahihi , wanatakiwa kuwa watu wa kushukuru hata katika magumu, unaweza kuona pengine unahangaika kutafuta kazi wakati umesoma na ukaumia sana , kumbuka kuna mwingine hata hiyo elimu hakupata neema ya kuipata, hivyo acha kulalamika na kusikitika kama kweli umesoma tumia hiyo elimu kuweka maisha sawa, Jifunze kumshukuru Mungu kwa kuangalia vile amekujaalia, kwa kuangalia vile unavyo sasa, mshukuru hata kwa nyakati ngumu unazopitia maana angeweza angezuia, lakini karuhusu kwa kuwa anajua unaweza kuhimili, unaweza ukijiamini.
Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo, anapatikana kwa namba +255 755 350 772 au kwa bberrums@gmail.com, unaweza pia kumsoma zaidi kwenye http://jitambueunani.blogspot.com
5/14/2015 07:17:00 AM
|
Labels:
MBINU ZA MAISHA
|
This entry was posted on 5/14/2015 07:17:00 AM
and is filed under
MBINU ZA MAISHA
.
You can follow any responses to this entry through
the RSS 2.0 feed.
You can leave a response,
or trackback from your own site.
0 comments:
Post a Comment